Ahahahaha!! Mbona
Kiranga anaonekana mstaarabu!
Nimesoma huu uzi tangu awali, nafikiri jana, kwa kuwa nimekuwa tagged, na pia kwa kuwa napenda kuchangia habari za kusafiri sehemu tofauti duniani.
Nimepata shida sana kuujibu kutokana na misimamo yangu ya kifalsafa inayopingana na jambo la msingi kabisa la maudhui ya uzi huu. Rushwa.Hadaa.Kutofuata utaratibu.Kutumia fedha vibaya.
Nlitaka kuanza kujibu, nikaahirisha kwa kuogopa kutoa maoni ambayo kwa Kiingereza yanaitwa "blaming the victim", na sasa nimekuwa tagged mara ya pili. Hivyo naona ni wakati muafaka kujibu.
Kwanza kabisa nataka kusema kwamba, nina mshikamano na watu wote ambao wakiona sehemu moja haiwatoshi kujiendeleza mambo yao, wana haki ya kutalii , kusoma, kufanya kazi, biashara au kutembelea tu sehemu nyingine ya dunia. Hii kwangu ni haki ya msingi kabisa ya watu wote wenye uwezo na nia nzuri. Mimi mwenyewe ni mfano wa watu hao waliosafiri na kuanza maisha sehemu nyingine duniani.
Pili, mimi nataka niseme kwamba, napenda sana kuishi ndani ya sheria, na nataka sehemu yoyote ninayoshurutishika kuvunja sheria, sheria yenyewe ionekane kuwa ni ya kidhalimu na kuifuatilia kunavunja maadili makubwa zaidi. Hapa unaweza kuweka mifano kama ya sheria za ubaguzi wa rangi za enzi ya ukaburu Afrika Kusini au Marekani, na sheria za kikoloni zilizopinga watu kujitawala wenyewe.
Miaka yote zaidi ya ishiri niliyoishi ughaibuni, kosa kubwa kabisa nililofanya ni kwamba siku moja nilisahau kuondoa gari langu upande mmoja wa barabara uliokuwa unasafishwa, nikapata adhabu ya faini kwa kuwa sikuondoa gari upande huo. Na nililipa $35 kwa kosa hilo mara moja mtandaoni.Hilo ndilo kosa moja na pekee lililo katika rekodi yangu kwa muda wote huu. Naheshimu sana kuishi nje ya sheria mpaka muhasibu wangu alikuwa ananiambia kwamba tunaweza kupata "tax returns" zaidi kwa kubadili mambo madogo tu kwenye taarifa zangu za kodi, ambayo hayawezi kujulikana na mamlaka za kiserikali na yatanizidishia pesa sana, lakini nilikuwa nakataa, kwa sababu sijazoea kuishi kwa ujanja ujanja wa njia za panya.
Tatu, naheshimu sana taifa la Tanzania na nataka kuwa sehemu ya watu wanaopeleka mbele juhudi za kuondoa mawazo ya kuchochea rushwa, kufanya mambo kwa njia za panya na mkatomkato, na kiujumla kutofuatilia utaratibu uliowekwa.
Nimepata tabu sana kutoa msaada katika jambo ambalo linaonekana kuwa linakwendana na hadaa kama si jinai kabisa.
Nilitaka kusema kwa nini watu wanataka kusafiri muda huu wa mlipuko mkubwa wa ugonjwa wa Covid-19, lakini inawezekana safari zikawepo na haja ya kutulia ninayoiona mimi ikawa si sawa na ya mwingine.
Lakini pia, kama mtu ana shida ya kumfanya atake kusafiri kwenda nje, kwa nini hafuati matakwa ya visa yaliyowekwa na nchi hizo na kusafiri kihalali kama tulivyosafiri wengine? Kwa nini aanze kwa kutaka kutoa rushwa kwa kitu ambacho ukiwa umekamilisha masharti unakipata kwa visa fee ndogo tu? Mbona Watanzania wenye sababu nzuri na uwezo wanasafiri kila siku bila kutoa rushwa?
Ni kwamba huyu mwenzetu ni muoga/mvivu tu anataka kutumia fedha kama fimbo ya kutatua matatizo yote? Yani, anaweza kutimiza masharti, ila ni muoga/ mvivu tu, anataka kurahisisha mamabo kwa fedha? Kama ni hivyo, mimi nina matatizo na watu wanaotaka kutumia fedha kuruka utaratibu na siwezi kumsaidia.
Au ni kwamba huyu mtu anataka kusafiri kwenda nchi za nje bila ya kuweza kutimiza masharti yanayotakiwa? Kama ni hivyo, mimi pia nina matatizo na watu wanaotaka kusafiri kwenda nchi za nje huku hawajafikisha masharti yanayotakiwa, pengine hawana pa kufikia, hawana mpango wa kazi, hawana kitu kinachoeleweka wanachoenda kufanya, wanajiweka katika nafasi kubwa ya kukutwa na matatizo au hata kufa.
Au ni kwamba huyu mtu ana sababu mbaya, biashara haramu kama ya madawa ya kulevya, ugaidi, etc., na anaogopa kufuatilia mlolongo uliowekwa wa kupata visa, anataka kutumia njia za mkato ili mambo yake haramu yasigunduliwe? Hilo nalo mimi ninajiweka mbali nalo na siwezi kumsaidia mtu.
Mimi sina tatizo la kumsaidia mtu kusafiri, hususan upande wa Marekani. Maana huku ndiko niliko.Tena naweza kumsaidia mtu mpaka barua ya mualiko na akafikia nyumbani kwangu asilale hoteli. Kuna Mzee mmoja Profesa wa Chuo Kikuu alitaka kuja Marekani nikamuandikia hivyo barua ya mualiko akaja Marekani.Mtu mzima na heshima zake. Hata hapo ubalozi wa Marekani walivyomuangalia huyu Profesa wa Chuo Kikuu anaenda Marekani, na huyu anayemualika mtu wetu Marekani tunamjua nyendo zake siku nyingi hana kosa la hata speeding ticket na anatengeneza mkwanja wa maana kila mwaka ana kwake, hawezi kushindwa kumkarimu huyu Profesa, hawakuwa na shida. Walimpa visa.
Ila, nitakuwa mjinga nikimsaidia mtu simjui, sijui anataka kusafiri kwa sababu gani, na sijui amejikita kufanya nini. Nikimsaidia halafu kesho akikutwa na kesi ya ugaidi au madawa ya kulevya nikasema "huyu simjui, nilikutana naye online tu nikamsaidia", wakati naonekana nimempa msaada mkubwa sana, watu watanielewa kweli? Au wataniona mpango wangu na yeye ni mmoja?
Kibongobongo hili ni jambo rahisi tu kusaidiana bila kujuana, lakini huku tunavyoishi hakuna kitu kama hicho. Siku moja nilikuwa kwenye treni natoka mji wangu naenda mji wa state ya pili, sasa nikawa nimesahau kuweka full charge kwenye simu, nakaribia kufika ninakoenda.Natakiwa niwapigie simu wenyeji wangu waje kunichukua train station.Nikakuta simu haina charge. Nikamuomba mtu wa pembeni yangu, kijana Mmarekani mweusi, nikamwambia "kaka, nakuomba simu yako mara moja niwapigie wenyeji wangu waje kunipokea train station, kwani simu yangu imekwisha chaji".
Niliona ni ombi dogo tu. Kibongobongo.
Yule jamaa alinijibu kwamba yeye hawezi kunipa simu yake, kwa sababu alisema "I am flying under the radar".
Yani inaonekana alishapata matatizo na vyombo vya sheria, au anaogopa sana kupata matatizo na vyombo vya sheria, kiasi kwamba, anaogopa hata kumpa mtu baki simu yake apige, kwa sababu, ikitokea tu simu yake imeonekana kupiga kwenye network mbaya kama ya wauza madawa ya kulevya au magaidi, anaweza kupata tabu sana
Hayo ndiyo maisha tunayoishi huku. Na kipindi cha nyuma tumesaidia sana wasafiri wa Kitanzania. Kuna watu walikuwa wanakuja US hata hatuwajui tunakaa nao, wengine wameenda Canada, wengine mpaka leo tumejenga undugu.
Lakini, hapa kati, lazima niseme ukweli, biashara ya ngada imeharibu sana trust kati yetu Watanzania. Mtu kumsaidia mtu, hata kumpa hela tu, inabidi umjue, ama sivyo umpe hela cash ambayo haina track record.Kwa sababu unaweza kumsaidia mtu kwa roho nzuri tu, akapata matatizo, watu wakaangalia nani yupo kwenye mtandao wake wa kumsaidia.
Kuna mtu kapata kesi mpaka karudishwa Tanzania kwa kisa cha kumnunulia Mtanzania tiketi ya ndege tu, tena ile ya "ebwana mimi sina credit card ninunulie tiketi nakulipa hela yako cash hapa". Ikaonekana huyu amefanya biashara ya ngada, wewe umemnunulia tiketi, mna lenu moja mnajuana nyie. Wkamuunganishia na mambo mengine ya uongo na kweli, wakamrudisha Bongo.
Hivyo, mimi watu legit, hususan ninaowajua mwenyewe, sina tatizo kuwasaidia.
Ila hizi habari za kukutana mitandaoni tu, sanasana kama hujui process nitakuambia tu process ni hii, kinachoptakiwa ni passport na bank statement na sababu ya kusafiri na barua ya kazi au chuo au mualiko au reservation ya hoteli etc, mambo ambayo yote unaweza kuyapata online.
Waswahili walisema, mtaka nyingi nasaba, hupata mwingi msiba.
Nishaona watu wakipata tabu sana kwa kuendekeza tabia za Kibongobongo za kusaidia "watu wasiojulikana".
Huo ndio msimamo wangu kuhusu hili jambo.