Chanzo: Gazeti la Raia Mwema, imeandikwa na Ayub Rioba
SAFU hii ya Fikra Mbadala ilisimama tangu katikati ya mwaka jana wakati nikiwa masomoni. Halikuwa kusudio langu kuacha kuandika lakini iliniwia vigumu kufanya mambo mawili makubwa kwa wakati mmoja: kuandika safu na kuandika tasnifu. Nikakumbuka methali ya Mtaka Yote, Hukosa Yote. Nikachagua moja.
Wakati nikirejea leo hii ninawiwa na shauku ya kuwatakia kila la kheri wasomaji wa safu hii na gazeti la Raia Mwema kwa ujumla huku nikiwakumbusha kwamba kama ilivyokuwa huko nyuma, nitaendelea kudodosa fikra mbadala zinazoweza kukabili changamoto kubwa na muhimu katika maisha yetu kama watu na kama taifa.
Na madhali ninasisitiza katika kudadisi na kudodosa fikra mbadala, maana yake ni kwamba nitaendelea pia kuhoji fikra mazoea ambazo kwa muda mrefu zimetufunganisha na urithi wa ufukara na faraka na wakati mwingine kutufanya watu dhalili machoni pa binadamu wengine wa dunia hii.
Kama nilivyokwishabainisha siku zilizopita, kuhoji mazoea si jambo rahisi. Hata pale inapokuwa kwamba anayehoji yuko sahihi, mara nyingi walevi wa fikra mazoea humtazama yeye kama hayawani au kiumbe aliyechanganyikiwa.
Na historia, kama nilivyokwishakubainisha huko nyuma, inatufundisha kwamba walevi wa fikra mazoea siku zote hugoma kabisa kusikiliza fikra mbadala kwa kuamini kwamba kile wanachofikiri, wanachokijua na wanachokitenda ndicho Alfa na Omega.
Kwamba ndio ukweli wote kuhusu ubinadamu na kuhusu dunia. Kwamba hivyo ndivyo mambo yanavyotakiwa kuwa. Kwamba namna yoyote ile ya kufikiri, kujua au kutenda tofauti na fikra mazoea ni uasi unaotakiwa kuepukwa kwa juhudi zote.
Nilikwishajadili pia jinsi walevi mazoea wa enzi hizo walivyowahukumu kifo waumini wa fikra mbadala (Kumbuka Socrates na Galileo na hata Steve Biko miaka ya karibuni) kwa sababu tu walijaribu kuonyesha ukweli tofauti na mapokeo yaliyokuwa yamejikita katika fikra mazoea.
Safu hii itaendelea kuhoji bila ukomo. Lakini pia jambo la pili - na la msingi pia - safu hii itaendelea kukumbushia historia yetu sisi kama binadamu (hasa Bara la Afrika) tulikotoka, tulikopitia na tulipofikishwa leo. Kujua historia ni muhimu mno kwa binadamu yeyote anayehitaji kujitambua.
Na haitoshi kabisa kuijua tu historia kupitia miwani ya wageni waliotufanya watumwa, wakatutawala kimabavu na kuendelea kutuchezea shere hata baada ya miaka 50 ya uhuru.
Tunahitaji kuanza kufikiri zaidi, kutafiti zaidi, kujadili zaidi, kutafakari zaidi juu ya uwepo wetu sisi duniani. Haitoshi tu kwetu sisi, kwa mfano, kupaza sauti kila siku kuhusu dhana zinazotumiwa na binadamu wengine kana kwamba wao na sisi tuko sawa.
Haitoshi, kwa mfano, kwetu sisi kuanza kushadidia haki za binadamu, usawa wa binadamu kana kwamba na sisi pia ni binadamu wa daraja moja kama Wazungu, Waasia na wengine wenye rangi tofauti na yetu.
Kujifurahisha huku tunakokufanya kwa mazoea, eti na sisi ni binadamu kamili kama hao wengine, ndiko kunakoleta mkanganyiko mkubwa wa kimantiki katika michakato mingi tunayoibua – hasa tunayoletewa na wageni - inayokuwa na malengo ya kutuletea maendeleo (nitaijadili zaidi dhana ya maendeleo huko mbele).
Ninachojaribu kukisema hapa ni rahisi tu. Kwamba kimantiki endapo mtu mweusi anatangaza kwamba yeye ni binadamu kamili kama wengine, basi analazimika kufikiri, kujua na kutenda kama wale binadamu (ambao mpaka sasa wanajipambanua kama kipimo cha ukamilifu kifikra).
Haiwezekani huyu mtu mweusi akajiita binadamu kamili lakini akafikiri kama kuku, akawa na maarifa kama ya kuku, na wakati huo huo akajaribu kutenda kwa kuiga wale binadamu wengine wanavyotenda.
Matokeo yake ni mkanganyiko mkubwa unaotokana na ukweli kwamba yeye anaigiza kama binadamu kamili lakini anafikiri kama kuku, anajikuta na maarifa kama ya kuku na hata uwezo wake wa kuiga unakuwa unalingana na ule wa kuku.
Lakini bado eti hataki kabisa kujiita kuku-mtu, au basi mtu-kuku. Analazimisha aitwe mtu au binadamu. Na anaweza kupigana kwa hasira pale atakapoitwa – kwa maneno – mtu-kuku.
Lakini hajali kabisa kwamba fikra zake (za kikuku), maarifa yake (ya kikuku) na hata baadhi ya matendo yake (ya kikuku) vinamtambulisha kwa ufasaha zaidi kuhusu hadhi yake ya Ukuku-mtu.
Na ndipo linapokuja swali jingine la kimantiki. Kwamba je, ile tu maumbile ya huyu mtu mweusi kufanana na ya wale binadamu wengine (ambao ni kipimo cha ukamilifu) kunamfanya kuwa binadamu kamili? Je, kufanana tu kwa maumbile kunatosha kumfanya huyu mtu mweusi alazimishe kwamba na yeye basi ni binadamu kamili?
Je, ni katika kutembea kwake kwa miguu miwili huku akitumia mikono kwa shughuli nyingine ndipo anapata uhalali wa kuwa (au kuitwa) binadamu kamili? Je, pale Sokwe anapotembea kwa miguu miwili na kutumia mikono kwa shughuli nyingine naye pia anakuwa amepata uhalali wa kuitwa binadamu kamili? Au Kangaroo wa kule Australia ambaye ana ustadi mkubwa wa kutembelea miguu miwili anaweza kupata uhalali wa kuitwa binadamu?
Mantiki inashawishi kwamba sifa kubwa inayompambanua binadamu kamili na hayawani wengine ni kule kufikiri kwake, ambako humwezesha kutaka kujua zaidi na kujikuta akikusanya maarifa zaidi na ujuzi zaidi unaomsaidia katika kupambana na changamoto za kuishi kwake katika namna ambazo hayawani wengine hawawezi.