Kuongoka na kuokoka katika Ukristu
Maneno kuongoka na kuokoka huchanganya baadhi ya watu, wakiwemo Wakristu. Baadhi yao hutumia neno kuokoka badala ya kuongoka, na vivyo hivyo kuongoka badala ya kuokoka.
Kuongoka ni nini?
Kuongoka ni kugeuka/kugeuza nia. Ni kuacha itikadi fulani, mfano kwa Waislamu neno hili hujulikana kama kusilimu. Lakini kwa Wakristu neno hili linajulikana kama kuongoka. Mtu anaweza akawa amechukua hatua ya kufanya hivi ama kwa ajili ya kuolewa au kwa ajili ya shida au jambo jingine. Huyu anaweza kuwa ametoka kwenye ukristo kuelekea uislam au ametoka kwenye uislamu kuelekea ukristo, bado neno halibadiliki. Linabaki vile vile kuwa ameongoka.
Sasa kwa kuwa amegeuka, mtu huyu anakuwa hajaokoka, bali ameamua tu kuacha njia moja na kugeukia nyingine. Na ndiyo maana utaona kwenye Biblia kumeandikwa wakahubiri habari ya kuongoka kwao kwa mataifa. Ina maana wakahubiri habari ya kugeuka kwao. Naweza kusema kuwa hawa watu waliamua kuacha njia moja na kugeukia njia nyingine. Matendo ya Mitume 15:3: “Basi, wakisafirishwa na kanisa, wakapita kati ya nchi ya Foinike na Samaria, wakitangaza habari za kuongoka kwao mataifa; wakawafurahisha ndugu sana.
Kwa maneno mengine kuhusu kuongoka, Biblia inaposema mtu ni mwongofu inamaanisha kuwa ni mtu aliyegeuka na kuacha mienendo aliyokuwa anaiendea hapo mwanzo.
Mathayo 18.3 “akasema, Amin, nawaambia, msipoongoka na kuwa kama vitoto, hamtaingia kamwe katika ufalme wa mbinguni”.
Hapo Bwana alikuwa anamaanisha msipogeuka na kuwa kama vitoto, yaani wasipogeuzwa fikra zao na kuwa kama watoto wadogo hawawezi kuingia katika ufalme wa mbinguni. Kadhalika, Marko 4: 11: “Akawaambia, ninyi mmejaliwa kuijua siri ya ufalme wa Mungu, bali kwa wale walio nje yote hufanywa kwa mifano,
12 ili wakitazama watazame, wasione; na wakisikia wasikie, wasielewe; wasije wakaongoka, na kusamehewa.”
Tunaona hapo Bwana alimaanisha wale watu wasije wakageuka na kuacha njia zao mbaya, ambapo kama wakifanya hivyo Mungu atawasemehe, na kuwaachilia neema ya kusamehewa dhambi zao. Pia, katika 1Timotheo 3.6: “Wala asiwe mtu aliyeongoka karibu, asije akajivuna akaanguka katika hukumu ya ibilisi.”
Hapo Mtume Paulo aliposema mtu aliyeongoka hivi karibuni, alimaanisha kuwa mtu yule aliyegeuka na kuacha njia zake mbovu, hivi karibuni, asije akapewa kazi kama ya uaskofu kwa sababu mtu kama huyo bado hajaweza kuijua imani vizuri, na kuweza kuzitambua hila za shetani kwani bado ni mchanga wa imani.
Kwenye vifungu vingine utaliona jambo hilo pia: Mathayo 13:15, Luka 22:32.
Kuokoka ni nini?
Kuokoka ni kutolewa kutoka kwenye utumwa wa dhambi, ili nguvu ya dhambi isikutawale tena, uweze kuishi maisha matakatifu.
Baada ya dhambi kuingia duniani, hakuna tena mwanadamu hata mmoja ambaye angeweza tena kuwa mtakatifu duniani, ili aweze kwenda Mbinguni. Hata kama kungekuwa na uwezekano wa kuishi bila kutenda dhambi, bado ile hali ya dhambi tuliyozaliwa nayo ilitosha kutuweka katika hali ya hukumu. Dhambi ya wazazi wetu Adamu na Hawa ilitosha tu kutufanya wanadamu wote tuwe wadhambi na hivyo kuhitaji mwokozi/wokovu. Hakuna mtu angezaliwa asihitaji wokovu kisa hajawahi kutenda dhambi.
Warumi 5:12-19 inasema: Kwa hiyo, kama kwa mtu mmoja dhambi iliingia ulimwenguni, na kwa dhambi hiyo mauti; na hivyo mauti ikawafikia watu wote kwa sababu wote wamefanya dhambi; walakini mauti ilitawala tangu Adamu mpaka Musa, nayo iliwatawala hata wao wasiofanya dhambi ifananayo na kosa la Adamu aliye mfano wake yeye atakayekuja.
Lakini karama ile haikuwa kama lile kosa; kwa maana ikiwa kwa kukosa kwake yule mmoja wengi walikufa, zaidi sana neema ya Mungu, na kipawa kilicho katika neema yake mwanadamu mmoja Yesu Kristo kimezidi kwa ajili ya wale wengi.
Wala kadiri ya yule mtu mmoja aliyefanya dhambi si kadiri ya kile kipawa; kwa maana hukumu ilikuja kwa njia ya mtu mmoja ikaleta adhabu; bali karama ya neema ilikuja kwa ajili ya makosa mengi, ikaleta kuhesabiwa haki.
Kwa maana ikiwa kwa mtu mmoja kukosa, mauti ilitawala kwa sababu ya yule mmoja, zaidi sana wao wapokeao wingi wa neema, na kile kipawa cha haki, watatawala katika uzima kwa yule mmoja, Yesu Kristo.
Basi tena, kama kwa kosa moja watu wote walihukumiwa adhabu, kadhalika kwa tendo moja la haki watu wote walihesabiwa haki yenye uzima.
Kwa sababu kama kwa kuasi kwake mtu mmoja, watu wengi waliingizwa katika hali ya wenye dhambi, kadhalika kwa kutii kwake mmoja watu wengi wameingizwa katika hali ya wenye haki.
Ili tuondokane na hali hii, na tufanikiwe kwenda Mbinguni, ilikuwa ni lazima kuzaliwa mara ya pili.
Mtu mpaka awe ameokoka ni lazima kwanza awe amehusishwa na anayemwokoa mwenyewe, yaani mwokozi. Katika ukristo huwezi kusema umeokoka mwenyewe kama Yesu Kristo hajayageuza maisha yako, kama maisha yako hayajahusianishwa na Kristo moja kwa moja.
Biblia inasema katika Warumi 10:9: “Kwa sababu, ukimkiri Yesu kwa kinywa chako ya kuwa ni Bwana, na kuamini moyoni mwako ya kuwa Mungu alimfufua katika wafu, utaokoka.
10 "Kwa maana kwa moyo mtu huamini hata kupata haki, na kwa kinywa hukiri hata kupata wokovu”.
Na pia inasema: “aaminiye na kubatizwa “ataokoka”; asiyeamini, atahukumiwa.(Marko 16:16)”. Suala la kuokoka ni jambo la kuingia moja kwa moja katika mahusiano ya karibu na yule anayekuokoa.
Kama ndivyo basi tunamkirije Kristo?.
Tunamkiri Kristo kwa maisha yetu na matendo yetu kuonyesha kuwa ni kweli Kristo alikufa, na kufufuka pamoja na sisi. Kwanza, kwa kubatizwa katika jina la Yesu Kristo kama maandiko yasemavyo pindi tu tuaminipo kama ishara ya kuamini kuwa alikufa akafufuka pamoja na sisi, kuuonyesha ulimwengu tumekuwa milki halali ya Bwana. Pili ni kukubali kuishi maisha yanayomkiri Kristo kila siku.
Hapo ndio mtu anakuwa tayari kuingia gharama zo zote ikiwemo kuwa tayari kutengwa, kuchukiwa, kuachwa, kudharauliwa kwa ajili ya Kristo, kwa ajili ya kumfuata Kristo. Sasa hapo ndipo mtu amemkiri Kristo. Na wokovu kwake ni jambo la lazima.
Fananisha maneno hayo na vifungu hivi Bwana Yesu alivyowaambia makutano:
Mathayo 10:32: “Basi, kila mtu atakayenikiri mbele ya watu, nami nitamkiri mbele za Baba yangu aliye mbinguni.
33 Bali mtu ye yote atakayenikana mbele ya watu, nami nitamkana mbele za Baba yangu aliye mbinguni.
34 Msidhani ya kuwa nimekuja kuleta amani duniani; la! Sikuja kuleta amani, bali upanga.
35 Kwa maana nalikuja kumfitini mtu na babaye, na binti na mamaye, na mkwe na mkwe mtu; 36 na adui za mtu ni wale wa nyumbani mwake.
37 Apendaye baba au mama kuliko mimi, hanistahili; wala apendaye mwana au binti kuliko mimi, hanistahili.
Ni vizuri kufahamu kuwa wapo watu wanaosema kuwa tukiwa hapa duniani hatuwezi kuokoka mpaka tutakapokwenda mbinguni. Biblia inasema 2 Wakoritho 6: 2: “Wakati uliokubalika nalikusikia, Siku ya wokovu nalikusaidia; tazama, wakati uliokubalika ndiyo sasa; tazama siku ya wokovu ni sasa”.
Siku ya wokovu ni sasa.
Tunaokolewa tukiwa hapa duniani. Hivyo mtu anaweza kusema nimeokoka ikiwa kweli amezingatia vigezo vyote vilivyotolewa na huyo amwokoaye.
Raha ya wokovu inaanzia hapa hapa duniani pindi tu pale mtu anapomwamini Yesu Kristo, matunda ya wokovu yanaanzia duniani, mbinguni ni kukamilishwa tu.
Kuokoka maana yake ni kupokea rohoni mwako mambo haya matatu: msamaha wa dhambi, utakaso, na kuhesabiwa haki.
Ina maana kuwa kama unakuwa umeongoka,
mambo haya unakuwa huyapati, kwa sababu kuongoka hakupo ndani. Na hauwezi kuhesabiwa haki wala huwezi kupata huo msamaha wa dhambi na utakaso. Hauwezi kufanyika ndani yako kwa sababu tendo hili halihusiani na kuokoka, bali unakuwa umegeuka tu.
Kwa kuhitimisha, tunaweza kusema mtu aliyeongoka ni tofauti na aliyeokoka. Japo aliyeokoka tayari alishaongoka, lakini aliyeongoka haitupi uhakika kuwa ameokoka, kwa sababu neno lenyewe kuongoka ni kugeuka na siyo kuokolewa.
Kuongoka hauzaliwi bali unakuwa umefanya maamuzi ya kubadili jambo moja kulielekea jingine, ambapo huwezi kupata nafasi ya kuitwa Mwana wa Mungu, kwa sababu unakuwa haujampokea Yesu kwa sababu Biblia inasema “Bali wote waliompokea aliwapa uwezo wa kufanyika Wana, na Ndio wale wanaoliamini jina lake”.
Ukiongoka unakuwa umekuja kwa masilahi yako na si kwa kumpokea Yesu. Na kwa hali hiii watu wengi wameongoka (wamegeuka) huku wakidhani kuwa wameokoka. Wapo watu wana miaka mingi makanisani mwao, lakini bado hawajaokoka.
Maandiko katika Marko 16:16 yanasema: “Aaminiye na kubatizwa ataokoka; asiyeamini, atahukumiwa”. Sharti la kuokoka lazima uamini kisha ubatizwe. Kwa maana nyingine ni kwamba kama umeamini na hujabatizwa ni kwamba wewe umeongoka, yaani umegeuka tu, na hujaokoka. Kama unataka kuokoka sharti ubatizwe ili uokoke.