Iran kwa sasa inaonekana kama nchi inayosema:
“Ni afadhali nikabiliane na Uncle Sam kuliko nimguse Israel.”
Marekani ikishambulia, Iran nayo hujibu kwa kushambulia kambi za Marekani katika ukanda huo. Lakini inapofika kwa Israel, hapo ndipo miguu inakuwa mizito. Hadi sasa hawajathubutu kwenda mbali.
Sababu ni rahisi: Iran inaamini Marekani bado ni taifa la mazungumzo. Mashambulizi yakipamba moto kidogo tu, si ajabu ukamsikia Trump akisema:
“Tukae mezani tuzungumze.”
Ukiachana na hayo, Trump kabanwa na chama pinzani Wademocrat ambao wanapambana kumpunguzia uwezo wa kuanzisha au kupanua vita bila idhini ya Bunge. Kwa hiyo, kila shambulio analoidhinisha halipimwi kwa uwezo wa kijeshi, bali pia kwa gharama za kisiasa. Pia uchaguzi wa wabunge wa majimbo wa mwezi Novemba unakaribia, Trump kabanwa akijua kwamba mashambuliz mazito yanaweza kukigharimu chama chake.
Lakini Israel? Hao hawana muda mwingi wa meza, hotuba wala maonyo marefu. Wakiamua kuanza, wanaanza moja kwa moja.
Mara kadhaa Trump amekuwa akiwaomba Israel waache mashambulizi mfano vita ya mwaka jana wakiwa wanaenda kumla kicha Ayatollah, Israel wamekuwa wakitii kwa kujua siasa za Marekani zilivyombana Trump, lakini kwa hali ya sasa wametamka Iran akiwagusa hakuna wa kuingilia ni mpaka mbungi iishe.
Vita ya siku 12 ya mwaka jana ilionyesha hilo. Viongozi wengi wakuu walilengwa, na walipokuwa wakikaribia kumfikia Ayatollah, Trump aliingilia kati na kuwaambia warudishe ndege.
Na vita ya mwaka huu ilipoanza, Israel walirudi pale pale walipoishia—kwa Ayatollah.
Mbungi ilipigwa bega kwa bega na Marekani. Ni Marekani ambao ndege zao zilishambuliwa mara kwa mara, hadi kufikia operesheni ya kumuokoa rubani wao aliyekuwa akitafutwa kwa dau kubwa.
Lakini Israel?
Hakuna ndege yao wala rubani wao aliyepata changamoto ya aina hiyo.
Kwa kifupi, Iran inaweza kucheza mchezo wa kurushiana makombora na Uncle Sam kwa sababu inaamini mwisho wa mchezo huo kuna meza ya mazungumzo.
Lakini kwa Israel, wanajua mchezo unaweza kuisha kabla hata meza haijaandaliwa.
Hadi sasa Israel inaendelea kuisambaratisha Hezbollah na kutwaa ngome zake nchini Lebanon. Ingawa Hezbollah ni mkono wa Iran, utawala wa Iran hawajaonyesha ujasiri uleule inaouonyesha inapojibu mashambulizi ya Marekani, imeishia kutoa vitisho na malalamiko.
Iran inaujua ukweli mmoja mchungu, ikithubutu kurusha hata kijiti kuelekea Israel, haitakutana na onyo, hotuba wala mwaliko wa kukaa mezani. Itakutana na jibu la moja kwa moja lenye gharama kubwa. Israel ya sasa imechoshwa kuamriwa na Trump kusimamisha mashambulizi. Safari hii msimamo wao uko wazi, hakuna kazi ya nusu, wameapa kumaliza kazi.