SoC01 Njia nzuri za kupunguza ajali za bodaboda

SoC01 Njia nzuri za kupunguza ajali za bodaboda

Stories of Change - 2021 Competition

DustBin

JF-Expert Member
Joined
Jun 3, 2021
Posts
609
Reaction score
604
Kwa miaka ya hivi karibuni kumekuwa na ongezeko kubwa la matumizi ya pikipiki kama njia ya usafirishaji kuanzia mijini hadi vijijini hapa kwetu Tanzania. Matumizi ya pikipiki maarufu kama Bodaboda yamepunguza adha na changamoto ya usafiri kwa kiasi kikubwa sana hasa katika maeneo ambayo miundombinu ya usafirishaji kwa njia ya gari ni finyu. Na hata katika miji mikubwa bodaboda zimekua msaada mkubwa sana katika kuepukana na msongamano wa magari unaosababisha foleni hasa kwenye makutano ya barabara zenye taa za barabarani.

Hata hivyo hakuna kizuri kisicho na kasoro, ongezeko la bodaboda limeongeza idadi ya vifo na vilema watokanao na ajali za bodaboda. Kwa hakika ajali za boda boda zimekua nyingi sana kiasi huwezi mkuta mtu isipokua mdogo wake, au mwane, au baba yake au rafiki yake amewahi kupata ajali ya bodaboda. Watu wengi wamepata ulemavu wa viungo kutokana na ajali za bodaboda, ukienda hospitali kwenye wodi ya mifupa ukifanya sensa utagundua kundi kubwa la wagonjwa ni wahanga wa ajali za bodaboda.

Ili kupunguza madhila haya nimefikiria kama njia zifuatazo zitatumika ipasavyo na kuzingatiwa huwenda tukadhibiti janga hili;-

  1. Kila dereva bodaboda lazima awe na leseni ya udereva.
    Nimegundua madereva bodaboda wengi hawana leseni za udereva, hii ni kutokana kwanza hawajapata mafunzo ya udereva hivyo hata sheria za matumizi ya barabara hawazijui. Madereva wengi wa bodaboda wamejifunza mtaani pikipiki hata wengine hawajaijua vizuri tayari wanaingia barabarani kubeba abiria, hili linaongeza ajali zilizowezekana kuzuiliwa. Kwa hiyo serikali iweke mkazo kwenye hili na sheria isimamiwe kwamba kila mwendesha bodaboda lazima kwanza awe amepata mafunzo ya udereva, na kisha awe na leseni ya udereva.

  2. Kuwe na mafunzo ya udereva, sheria za barabarani kwa madereva bodaboda mara kwa mara.
    Serikali inaweza kuweka utaratibu japo kwa kulipia gharama kidogo ili kila baada ya miezi kadhaa inafanya mafunzo kwa madereva bodaboda kwa kuzingatia vyama vyao/makundi yao. Zoezi hilo linaweza kusimamiwa na askari wa usalama barabarani au hata mashirika binafsi yanayojishugulisha na masuala ya usafirishaji au ulinzi na usalama. Haya mafunzo au semina zinaweza kutumika kuwajengea uwezo madereva bodaboda au kuwaelimisha kama kuna mabadiliko ya sheria za barabarani nk. Mafunzo hayo yanaweza kufanyika kila baada ya miezi minne au mitano kutokana na mahitaji.
    Hili litawezekana endapo kila dereva bodaboda atajisajili kwenye kikundi chake/kijiwe chake, hivyo mafunzo yatafanyika kwa makundi yao. Lakini pia kuwahamasisha madereva bodaboda kuunda makundi yatakayotambuliwa na idara husika ya usalama barabarani kutasaidia kupunguza kesi za unyang’anyi na mauaji yanayofanywa kwa madereva bodaboda. Kwani kila dereva bodaboda atatambulika katika sehemu husika, naikiwezekana wapatiwe vitambulisho maalumu na wawekwe kwenye kanzi data (data base)

  3. Kuwe na (kamera) tochi ya kung’amua mwendo kasi wa pikipiki na kuwekwe ukomo wa mwendo kasi kwa baadhi ya maeneo kama ilivyo kwa magari.
    Kama ilivyo kwa magari kupigwa kamera maarufu kama tochi, na kuwekewa vipunguza mwendo (ving’amuzi) vivyo hivyo napendekeza kwa badoboda iwe hivyo. Nimeona maeneo mengi sana madereva bodaboda wakiendesha bodaboda zao kwa mwenda wa hatari na hali ya kuwa wapo katika maeneo ya makazi ya watu ambayo watoto hucheza pembezoni mwa makazi yao au hata karibu na barabarani, lakini pia kuna wanaotembea kwa miguu.

  4. Sheria ya viwango vya kubeba mizigo kwenye vyombo vya moto isimamiwe ipasavyo.
    Bila shaka kuna kanuni inayoelekeza kila chombo cha moto kubeba mzigo unaoendana na uwezo wake. Napendekeza hizo kanuni zisimamiwe na wahusika, na kama hazipo basi zitungwe ili kupunguza ajali zisizo za lazima. Kuna badhi ya madereva bodaboda hubeba mzigo mkubwa usioendana na uwezo wa vyombo vyao hivyo kusababisha kuelemewa na kushindwa kudhibiti chombo kikiwa barabarani. Mifano mizuri ni wale wenzetu wa mkoa wa Pwani wanaosafirisha magunia ya mkaa, na mzigo wa magogo kwa kutumia pikipiki, unakuta mzigo ni mkubwa sana ukilinganisha na uwezo wa pikipiki yenyewe.
    Sambamba na hili kuna utaratibu wa kubeba abiria Zaidi ya mmoja (mishikaki) nao udhibitiwe na iwekwe adhabu ya kulipa faini kwa atakaekamatwa na kosa hilo. Unakuta bodaboda ina abiria wanne na dereva wa tano, na wapo na mwendo kasi mno, hivi hawa wakipata ajali kuna usalama hapo? Nani wa kulaumiwa?

  5. Kwa wakati wa usiku madereva bodaboda wavae mavazi yenye viakisi mwanga (reflectors) ili waweze kutambuliwa kwa wepesi na waendesha magari.
    Hili nalielekeza kwa madereva wenyewe, kwa usalama wenu mkiwa katika barabara zinazopita magari hasa kwa wakati wa usiku mjitahidi mvae hayo mavazi yatawasaidia sana kutambuliwa na wanaoendesha magari hivyo kuwakwepa na kuepusha ajali. Changamoto kubwa ni kwamba madereva wengi wanapoambiwa kuhusu kuvaa sare fulani huwa wzito sana kutekeleza hata kama jambo hilo ni kwa maslahi yao wenyewe. Enyi madereva bodaboda akili za kuambiwa changanya na zako, usalama wako upo mikononi mwako, vaa reflectors kwa faida yako na kizazi chako, epusha ajali.

  6. Kuvaa kofia za usalama (helmets)
    Suala la kuvaa kofia za usalama limekua ni changamoto kwa madereva bodaboda wengi. Wengi wao huona ni ushamba kuvaa kofia hizo, ni madereva wachache sana wanaozivaa kwa ajili ya usalama wao. Wengine huvaa kwa ajili ya kupishana na askari wa barabarani na wakishapita walipo askari huzivua, kana kwamba wanavaa kwa ajili ya askari. Hili ni tatizo kubwa, sio kwamba kofia zinapunguza ajali hapana..! Lakini zinapunguza maafa ya ajali. Mtu alieanguka na bodaboda na hali amevaa kofia huwa na unafuu ukilinganisha na majeraha atakayoyapata yule asiyevaa kofia katika kichwa chake. Hivyo tukiachana na sheria, suala la kuvaa kofia nalileta kwako binafsi wewe dereva bodaboda, jali maisha yako vaa kofia ukiwa unaendesha bodaboda.

  7. Katika miji mikubwa kutengwe maeneo/mitaa maalumu ambayo bodaboda zisiruhusiwe kupita hasa maeneo yenye mikusanyiko wa watu wengi kama sokoni na madukani.
    Kwenye baadhi ya mitaa kuwekwe utaratibu wa kutoingia bodaboda kutokana na wingi wa watu waendao kwa miguu. Na kuwe na miji ya mfano ambayo bodaboda watakua na barabara zao ndogo za kupita tofauti na barabara zipitazo magari, na waendao kwa miguu, hasa kwenye barabara zinazoelekea kwenye maeneo ya mikusanyiko ya watu kama vile mjini, kituo cha mabasi, sokoni au madukani.

HITIMISHO

Ajali za barabarani ni majanga yanayotokea kwa kutokusudia, lakini wakati mwingine hutokea kwa uzembe wa waendesha vyombo vya barabarani. Endapo tutazingatia kanuni na sheria za barabarani tunaweza kupunguza kwa kiasi kikubwa ajali hizi. Serikali ndio yenye jukumu la kusimamia utekelezwaji wa kanuni na sheria zilizowekwa. Watendaji wa serikali wanatakiwa kusimama kidete katika kuhakikisha waendesha vyombo vya barabarani hasa madereva bodaboda ambao ndio msingi wa bandiko langu, wanafuata na kuzingatia sheria, kanuni, taratibu na miongozo wanayopewa wakiwa barabarani. Nachukua fursa hii pia kuipongeza serikali yetu kwa kufanikiwa kupunguza idadi ya vifo vitokanavyo na ajali za barabarani kuanzia mwaka 2015 hadi mwaka 2020.


DustBin
 
Upvote 0
Back
Top Bottom