Pombe ni kitu ambacho hakikubaliki kabisa kwa baadhi ya madhehebu ya dini, na wanaotumia huwa wanajifichaficha, pombe ni bidhaa ambayo ikikukolea kuacha ni tabu kweli kweli.
Sikiliza hii. Bibie mmoja alikuwa akikasirishwa na tabia ya mumewe kulewa tena kila siku, kila anapomsihi aache pombe ilikuwa ni ugomvi mkubwa, siku moja alimuomba atakaporudi arudi na kitoweo cha nyama kwani tangu Christmas ya mwaka uliopita hawajawahi kula nyama tena hapo nyumbani, jamaa aliafiki kwani yeye huwa akila akiwa baa.
Kabla ya kurudi jamaa alipitia butcher na kununua nyama lakini alionelea apitie baa japo apate moja mbili. Waliendelea kunywa na rafiki zake huku akimuomba mchoma mishikaki akate japo kidogo ile nyama ya kupeleka nyumbani, waliendelea kidogo kidogo mpaka yote ikaisha.
Saa za kurudi jamaa alirudi akiwa chakali, na mkewe alimfungulia na kwa bahati mbaya jamaa alitapika sebuleni, na vipande vya nyama vilionekana dhahiri. Mkewe hakutaka shari akamkokota mpaka chumbani akamlaza vizuri na kumfunika. Jamaa akachapa usingizi. Mkewe akarudi kupiga deki matapishi na kuokota vipande vyote vya nyama na kuvihifadhi kwenye bakuli.
Asubuhi mkewe aliamka mapema na kusonga ugali nakuandaa meza likiwemo bakuli la nyama aliyoitapika jamaa usiku akafunika vizuri kwa KAWA. Jamaa alipoamka na kuoga alikaribishwa mezani, hamadi! alipofunua bakuli alikumbana na nyama yenye harufu ya matapishi ya kilevi akapandisha hasira na kufoka '' umepata wapi nyama hii?'' Mkewe kwa kujiamini na sauti ya upendo akajibu ''Ulituletea jana mume wangu, mimi na watoto tulishakula ya kwetu usiku''
Jamaa alifedheheka sana, na akaamua toka siku hiyo pombe basi na kila akipata pesa mboga nzuri ikiwemo nyama ililiwa nyumbani kwake sio mpaka siku ya Christmas. Wana JF leteni mikasa iliyosababisha watu fulani kuacha kabisa pombe. Ijumaa njema na wikiendi njema.