Makete. Takribani watoto wanne kati ya 10 wenye umri wa miaka 10 hadi 14 mkoani Njombe hawajafikia kiwango cha chini cha umahiri katika kusoma, huku watatu kati ya 10 wakikabiliwa na changamoto katika kuhesabu.
Takwimu hizo zimeelezwa wakati wa kufungwa kwa mafunzo ya walimu na wawezeshaji wa Mradi wa Kijiji Changu (My Village Project) Awamu ya IV, unaotekelezwa na Uwezo Tanzania kwa kushirikiana na Serikali ya Mkoa wa Njombe na halmashauri zake.
Kwa mujibu wa taarifa zilizotolewa katika hafla hiyo iliyofanyika Makete Septemba 17, 2026, takribani watoto sita kati ya 10 wanafikia kiwango cha chini cha umahiri katika kusoma, huku saba kati ya 10 wakifikia kiwango hicho katika kuhesabu.
Hata hivyo, watoto sita kati ya 10 pekee ndio wanaofikia kiwango kinachotarajiwa wanapopimwa kwa pamoja katika stadi za kusoma na kuhesabu, maana yake watoto wanne kati ya 10 wanakosa angalau moja ya stadi hizo mbili za msingi.
Kutokana na hali hiyo, Uwezo Tanzania imesema Mradi wa Kijiji Changu unalenga kutumia tathmini kubaini kiwango halisi cha ujifunzaji wa kila mtoto na kutoa msaada unaolingana na mahitaji yake.
Mkurugenzi Mkuu wa Uwezo Tanzania, Baraka Mgohamwende, amesema changamoto si kuhakikisha watoto wanakwenda shule pekee, bali kuhakikisha wanafunzi walioko shuleni wanajifunza.
Amesema kupitia Mbinu ya Jifunze, walimu wanapaswa kutambua mtoto yuko katika kiwango gani cha ujifunzaji, kubaini anapokwama na kutumia matokeo ya tathmini kumsaidia kuongeza umahiri wake katika Kusoma, Kuandika na Kuhesabu (KKK).
Mafunzo hayo yamewahusisha zaidi ya walimu 100, walimu wakuu 50 pamoja na maafisa elimu na maafisa taaluma kutoka halmashauri za Mkoa wa Njombe, kwa lengo la kuwajengea uwezo wa kutumia zana za tathmini, kupanga ujifunzaji kulingana na kiwango cha mtoto na kufuatilia maendeleo yake.
Kwa mujibu wa taarifa hiyo, hadi mwaka 2026 Mradi wa Kijiji Changu umewafikia watoto 168,599 kutoka shule 286 katika mikoa sita na kata 489, huku ukihusisha walimu wa awali 807 na wazazi 189,000.
Mradi huo pia umewezesha ugawaji wa vitabu kwa watoto 15,000 kupitia maktaba za shule, wakati kupitia mafunzo ya mwaka huu unatarajia kuwafikia watoto 5,000 mkoani Njombe.
Awamu ya nne ya mradi imepanua wigo zaidi ya KKK kwa kujumuisha stadi za maisha na maadili, zikiwemo uwezo wa kuwasiliana, kushirikiana, kutatua changamoto, kufanya maamuzi na kujiamini.
Mkuu wa Wilaya ya Makete, Kisa Gwakisa Kasongwa, aliyemwakilisha Mkuu wa Mkoa wa Njombe katika hafla hiyo, amesema mafanikio ya mradi hayawezi kubebwa na walimu pekee, bali yanahitaji ushiriki wa wazazi, viongozi na jamii kwa ujumla.
Amesema wazazi wanapaswa kuacha kujiuliza tu kama mtoto ameenda shule na badala yake kujiuliza kama mtoto huyo anajifunza.
Soma pia:
Uwezo Tanzania yazindua Mradi wa Kijiji Changu awamu ya IV Njombe
Kwa mujibu wa Uwezo Tanzania, Mbinu ya Jifunze inatambua kuwa watoto walioko darasa moja wanaweza kuwa katika viwango tofauti vya ujifunzaji, hivyo msaada unatakiwa kuanzia katika kiwango ambacho mtoto yupo na maendeleo yake kufuatiliwa mara kwa mara.
Mradi huo umeanza pia kuhusisha jamii katika ujifunzaji, kwa kuwataka wazazi, viongozi wa jamii, walimu, wawezeshaji na Serikali za Mitaa kushirikiana kuhakikisha watoto wanapata mazingira yanayowawezesha kujifunza na kusonga mbele.
Uwezo Tanzania imetoa wito kwa mikoa mingine yenye changamoto katika KKK kujifunza kutoka Njombe na kutumia Mbinu ya Jifunze, ikitaja Rukwa, Simiyu, Manyara, Morogoro, Kigoma, Tabora, Lindi, Shinyanga, Mtwara, Songwe na Geita.
Mafunzo ya Awamu ya IV yamefungwa rasmi Makete, huku viongozi wakisisitiza kuwa mafanikio ya mradi hayapaswi kupimwa kwa idadi ya walimu waliopewa mafunzo pekee, bali kwa maendeleo yatakayoonekana katika ujifunzaji wa watoto.