Mkandara,
Asante, maneno hayo ni ya Masanja mie nimemnukuu tu.
Nilimjibu Masanja kabla sijasoma yote tuliyoletewa na Asha.
Yaliyomo kwenye Orodha ya ITIKADI NA SERA ZA CHADEMA ni mengi na mema Sijui kama kuna cha kuongeza maana kero zote zimeguswa.
Swali, utekelezaji wa orodha hiyo ndefu utakuwaje? Ni dhahiri itabidi mambo yafanyike hatua kwa hatua. Tunaanza na hatua gani na tunamalizia na ipi?
Mwisho wa bandiko la Asha kuna msisitizo kwamba TUNACHOHITAJI TANZANIA SIO UZURI WA SERA TU, TUNAHITAJI VIONGOZI WAZURI WATAOONGOZA TAIFA NA KWA MUJIBU WA MATAKWA YA UMMA-AMBAYO NI SERA ZA KWELI ZINAZOJALI WATU BADALA YA MAWAZO YAO BINAFSI WANAYOYAPA BARAKA KWA KUYAITA SERA ZA CHAMA.
Tunarudi kwenye hoja yangu ambayo naamini ilifanya Masanja ahamaki na kuita watu punguani, akitaka tujiunge tu maana CCM wameshindwa!
Asha anasema: Ili tuweze kukidhi matarajio ya wananchi chini ya uongozi wa CHADEMA tunahitaji Viongozi Wazuri.
Kama hivyo ndivyo, ni wazi ndani ya miaka 2 CHADEMA itabidi wafanye kazi ya ziada ya kutafuta na kupata viongozi wazuri wa kutosha wanaotarajiwa kuifanya hiyo kazi kubwa ya kuibadili nchi. Vinginevyo, tusijeanza kuwazomea na kuwapopoa mawe akina Zitto kwa frustrations watakazotupa!
Halikadhalika, kama wasemavyo Waswahili Shughuli ni Watu, watu watakaotakiwa kufanikisha Sera za CHADEMA ni sisi Watanzania wote katika sehemu yeyote tuliyopo iwe shambani, ofisini, viwandani, kwenye biashara zetu ama jikoni. Je CHADEMA na Watanzania wazalendo tutatumia mbinu gani kubadili mawazo na mwelekeo wa baadhi ya viongozi na Watanzania waliokengeuka?
Kwa maoni yangu, bado KILIMO ndicho uti wa mgongo wa maendeleo ya Watanzania walio wengi. Kwa hiyo, ni vyema kabla ya jingine lolote, CHADEMA Kielekeze nguvu zake kwa wakulima vijijini. Endapo tutawapa uongozi, basi Mabilioni atakayotoa Rais wangu mtarajiwa MMwanakijiji kwa wananchi wake yote yaelekezwe kwenye sekta ya Kilimo. Wakulima vijijini wasaidiwe kwa hali na mali ili waweze kujikwamua kutoka hapo walipo.
Napiga picha na kuwaona wamachinga na akina jobless wakiondoka mjini taratibu kufuata mabilioni yatakayoelekezwa vijijini. Kwa maana hiyo, hata kama si wote watakaorudi vijijini lakini wapo watakaoshawishika kufanya hivyo. Na hao watakaokwenda kupokea mabilioni ya Rais wetu wawekewe vizingiti vya makusudi wasiweze kurudi tena mijini!
Kazi ya kubadili utendaji ndani ya Jeshi la Polisi, Usalama wa Taifa, TAKUKURU, Madaktari, Manesi, Makarani, Mahakimu uchwala wapenda rushwa, n.k. itategemea Ukali wa kiongozi ama viongozi wa juu wa Serikali.
Sie wa mwaka 47 tunakumbuka viongozi wa watumishi serikalini kama akina Mzee Benard Mulokozi aliyewahi kuwa Katibu Mkuu ofisi ya Waziri Mkuu na baadaye Utumishi, alivyokuwa strict, hakucheka wala hakuwa na mchezo na mtumishi yeyote yule Wizarani kwake. Nani angelithubutu kuomba chai kwa mgeni aliyetaka huduma ama aliyetaka kuonana na afisa yeyote yule? Katibu Mkuu gani sasa hivi anayeweza kusimama kwenye gate la kuingilia ofisini ili kuwabana watumishi wachelewaji?
Siku hizi ni jambo la kawaida jijini Dar es Salaam kwa watumishi wa Serikali kufika ofisini saa 3 asubuhi badala ya saa 1.30 ana 2.00 kwa madai kwamba usafiri ni shida. Enzi za Mzee Mulokozi unaambiwa kama unataka kazi amka saa 10 ili uwahi kufika ofisini kwa wakati. Hao wachelewaji, wakiingia ofisini jambo la kwanza ni kuchukua birika na kuanza kuchemsha maji ya chai. Chai inaweza kunywewa kwa muda wa saa nzima huku watu wakitia stori. Kwa hiyo, hadi mtu aketi kitini kufanya kazi ni saa 5.00 mchana. Saa 7 au nane atatoka kwenda canteen kula lunch na kabla ya saa 9.30 kufika huondoka kwenda kuwahi usafiri wa kurudi nyumbani!
Mzee Mulokozi alikuwa na tabia ya kupita kila ofisi bila taarifa kuangalia kwamba kila mtumishi yuko mezani kwake anafanya kazi anayopaswa kufanya. Soga za yaliyotokea saloon ama disco weekend zilikuwa hazina nafasi maana hujui siku wala saa ambayo Katibu Mkuu ataamua kufanya round zake! Leo hii, utakuta Katibu Mkuu au hata Waziri, kaketi juu ya meza ya Sekretari anatia stori! CHADEMA kazi ya kubadili watu mnayo!
Ni rahisi sana kuketi chini na kuweka sera na mikakati ya utekelezaji kwenye karatasi. Tatizo liko kwenye namna ya kutekeleza yaliyo kwenye karatasi. Wapo wanaosifu kwamba Siasa ya Ujamaa na Kujitegemea ilikuwa nzuri lakini utekelezaji ulikuwa mbovu katika kipindi ambacho uzalendo viongozi na wa wananchi ulikuwa hautiliwi shaka sana. Sembuse sasa? Hivi sasa wananchi wanategemea sana misaada na ufadhili na hakuna maadili yoyote ya kiutendaji yanayofuatwa.
Kazi ni ngumu, lakini kama kweli CHADEMA ama chama chochote kina nia ya dhati ya kutaka kuwaletea wananchi maendeleo yanayohitajika lazima kuwe na mipango mahususi ya kubadilisha fikra na kufufua uzalendo miongoni mwa wananchi wa nyanja zote.
Operesheni Sangara ikusanye wanachama lakini pia ianze kukusanya watakaokuwa viongozi wa kuweza kubadili fikra za wananchi zilizodumaa na kutekeleza yaliyomo kwenye orodha ndefu ya itikadi na Sera za CHADEMA.