Mohamed Said
JF-Expert Member
- Nov 2, 2008
- 23,526
- 34,057
View: https://www.instagram.com/reel/DLVrV_LKwvP/?igsh=ZjFkYzMzMDQzZg==
Nimeangalia hii Makinikia aliyoweka Muhidin Issa Michuzi.
Nimemwona Jomo Kenyatta na Julius Nyerere kwenye Land Rover wakienda kwenye mkutano wa hadhara kuhutubia wananchi.
Hii ilikuwa mwaka wa 1961 Kenya bado haijapata uhuru wake.
Makinikia hii imenikumbusha mambo katika historia ya Tanganyika na Kenya wakati wa kupambana na ukoloni wa Muingereza.
Nitayaweka hapa machache kama nilivyoandika katika kitabu cha Abdul Sykes ili wale ambao hawaijui historia hii wapate kuifahamu lau kwa uchache:
Abdul Sykes na Jomo Kenyatta 1950
Mwaka 1950, Abdulwahid alisafiri kwenda Nairobi kukutana na Jomo Kenyatta ili kuanzisha uhusiano na Kenya African Union (KAU).
Abdulwahid alifunga safari hii wakati wa mashindano ya kandanda ya Kombe la Gossage.
Haya yalikuwa mashindano ya kila mwaka ambayo nchi tatu za Afrika ya Mashariki pamoja na Zanzibar zilikuwa zikishiriki.
Huenda Abdulwahid alichagua wakati huu mahsusi ili kuficha dhamiri ya safari yake.
Kama mtu labda angetaka kujua sababu ya safari yake ingewezekana kwa urahisi kabisa kuelezwa kuwa alisafiri kwenda Nairobi kutazama mashindano ya Gossage.
Abdulwahid alifikia Railway Hotel na alikwenda kuonana na Kenyatta usiku akifuatana na rafiki yake mpenzi kutoka Zanzibar, mmoja wa wacheza mpira katika timu ya Zanzibar.
Abdulwahid na rafiki yake walikwenda nje kidogo ya Nairobi kwenye nyumba moja iliyokuwa imegubikwa na giza na kuzungukwa na walinzi wa Mau Mau.
Abdulwahid alikuwa anatarajiwa.
Kenyatta alipofahamishwa kuwa Abdulwahid amefika na yupo nje, alitoka kumlaki.
Kenyatta alikuwa akimfahamu Ally Sykes tangu mwaka wa 1946.
Inawezekana kuwa kazi ya Abdulwahid ilirahisishwa na uhusiano huu wa Kenyatta na mdogo wake.
Mzanzibari huyu aliyemsindikiza Abdulwahid alikutana na Kenyatta na wakapeana mikono.
Baada ya kutambulishwa Kenyatta, Abdulwahid, Fred Kubai, Bildad Kaggia na Kungu Karumba waliingia kwenye chumba kingine ambako mkutano ulifanyika.
Mzanzibari, rafiki yake Abdulwahid alibakia nje na mlinzi.
(Mzanzibari huyu ambae sikumtaja jina lake katika kitabu ni Ahmed Rashaad Ali na sikumtaja kwa kuwa nyakati natafiti kitabu hiki watu walikuwa wanaogopa kueleza historia iliyokuwa kinyume na historia rasmi ya uhuru iliyokuwa inaanza na Julius Nyerere na kumalizikia na Julius Nyerere hivyo Mzee Rashaad aliniomba nisimtaje).
Hapo juu ni taarifa ya kikachero ya Special Branch ikimueleza Abdulwahid Sykes na chini kushoto ni Jomo Kenyatta na kulia ni Ahmed Rashaad Ali.
Kitabu cha Abdul Sykes kina historia ya pekee katika harakati ya kupigania uhuru wa Tanganyika.