SI KWELI Ofisi ya CCM Kinondoni yavunjwa na Wananchi kisa Mkataba wa DP World

SI KWELI Ofisi ya CCM Kinondoni yavunjwa na Wananchi kisa Mkataba wa DP World

Baada ya kuitathmini taarifa hii, tumebaini kuwa si ya kweli.
Mdau wa JamiiForums ameweka Chapisho lenye kichwa cha habari "CCM kimeanza kuumana" akimaanisha kuwa hali imeanza kubadilika kwenye Chama cha Mapinduzi baada ya Serikali inayoongozwa na Chama hicho kusaini Mkataba na kampuni ya DP World kuhusu uwekezaji kwenye Bandari ya Dar es Salaam.

Hali hii imesababisha kuvunjwa kwa mojawapo ya Ofisi za Chama hicho iliyopo Kinondoni.




pic-ccm.png

Ukweli wa suala hili upoje?
 
Tunachokijua
Juni 10, 2023, Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania lilipitisha Azimio la kuunga Mkono Mkataba wa Uwekezaji wa Bandari kati ya Tanzania na kampuni ya DP World ya Dubai.

Pendekezo hili lenye lengo la kuanzisha Ushirikiano wa Kiuchumi na Kijamii katika uendelezaji wa Maeneo ya Bandari Nchini lilisomwa na Waziri wa ujenzi na Uchukuzi, Prof. Makame Mnyaa Mbarawa ambapo pamoja na mambo mengine alidai kuwa Serikali iliamua kutia saini ushirikiano ili kuongeza ufanisi Bandarini, ambapo ndio lango kuu la uchumi.

Mjadala kuhusu uwekezaji wa kampuni ya DP World
Suala hili limeleta mjadala mkubwa nchini. Aidha, wananchi mbalimbali kwa nyakati tofauti wameshiriki kutoa maoni yao kuhusu suala hili akiwemo Mgombea urais wa CHADEMA (2020) Tundu Lissu, Profesa Issa Shivji na Balozi Mstaafu Dkt. Slaa.

Juni 19, 2023 yalifanyika maandamano yanayopinga uwekezaji huu na Julai 3, 2023, Mahakama Kuu kanda ya Mbeya ilianza kusikiliza Shauri lililofunguliwa na Wanasheria Boniface Mwabukusi na mwenzake wakitaka Mahakama iweke zuio kwa kampuni ya DP World kuhusu uwekezaji wake nchini hadi pale ambapo kesi ya msingi itakapomalizika.

Video inayososambaa sasa kwenye mitandao ya kijamii ambayo imewekwa pia na mdau wa JamiiForums inahusishwa pia na kutokuridhika kwa wananchi juu ya mkataba huu.

Uhusiano wa video hii na Mkataba wa DP World
Julai 7, 2023, Mdau wa JamiiForums aliweka video hii ikiambatana na maneno yanayosema "Bandari, bandari Bandari".

Mdau mwingine aliweka pia video hiyohiyo. Aidha, aliambatanisha maneno yanayosema "Utavuna ulichopanda. Wananchi Hawaielewi CCM". Video hii inayoonekana kutolewa kwenye Mtandao wa TikTok imehaririwa na kuwekewa maneno yanayosomeka hivi;

"Huku Mawakili wakipambana Mahakamani kupinga Mkataba haramu wa kuuza Bandari zetu, wananchi tupambane huku mtaani"

Chapisho hili limeleta mgawanyiko wa mawazo miongoni mwa wachangiaji, baadhi wakifafanua kuwa imekuwepo tangu zamani, haina uhusiano na yanayoendelea sasa na wengine wakikubali na kupongeza hatua hii.

Mathalani, mchangiaji mmoja anasema;

"Safi kabisaa..
Tuipinge laana hii CCM."


Uchunguzi wa JamiiForums umebaini kuwa video hii ilichukuliwa siku za nyuma na haina uhusiano na yanayoendelea sasa.

Video husika iliwahi pia kuwekwa kwenye Mtandao wa Twitter na Mtumiaji anayefahamika kwa jina la Maria Sarungi Tsehai, oktoba 11, 2022 saa 2:23 usiku.

Pia, JamiiForums imezungumza na watu wanaokaa kinondoni wanaoifahamu Ofisi hii ambao wamethibitisha kuwa tukio hili kufanyika mwaka 2022.

Sababu za kuvunjwa kwa Ofisi
Mdau wa CCM mwenye ufahamu mkubwa kuhusu suala hili ambaye hakutaka jina lake liweke wazi amebainisha kuwa Ofisi hii ilikuwa inapatikana nyuma ya Msikiti wa Mtambani Manyanya, Kinondoni na mojawapo ya sababu za kuvunjwa kwake ni kujengwa kwenye eneo lenye mgogoro ambapo wamiliki halali wa eneo baada ya madai yao kukubaliwa kwenye ngazi ya Wilaya waliamua kuivunja.

Ufafanuzi huu unafanana na mchango wa mtumiaji wa Twitter anayefahamika kwa Jina la Pompiduu alioutoa wakati akichangia chapisho la Maria Sarungi Tsehai. Alisema;

"Hizi zilikua ni ofisi za CCM Kinondoni mjini, walivamia eneo hilo, wenye plot wameshinda kesi,na wameamuru wawalipia fidia kikundi hicho cha kina mama (Tusirudi nyuma)"

Hata hivyo, Mdau huyo amebainisha kuwa baadhi ya wahusika wa tukio hili walikamatwa na kushtakiwa mahakamani kwa kuchukua uamzi kabla kesi haijafika mwisho ambapo hadi sasa kesi hiyo inaendelea.

JamiiForums inathibitisha kutokea kwa tukio hili mwaka 2022, lakini madai ya kuhusishwa na Sakata linaloendelea sasa kuhusu Bandari hayana ukweli.
Mbona kinachoonekana kuvunjwa hapo kwenye video siyo ofisi,ni kama jiwe la msingi la wakereketwa,hebu fafanua vizuri.
 
Habari hii inapotoshwa,hii sehemu ilivunjwa muda tu mbona kabla hata ya sakata hili la dp
Na sababu ya kuvunjwa ni kuna watu walidai hilo eneo ni lao

Ova
 
Back
Top Bottom