Pinda: Ikilazimu JWTZ itakwenda Zimbabwe
na Salehe Mohamed na Rachel Chizoza, Dodoma
KITENDAWILI cha hali ya usalama nchini Zimbabwe kinaweza kuilazimisha Tanzania kupeleka nchini humo vikosi vya majeshi yake ya kulinda amani iwapo itaombwa kufanya hivyo na Umoja wa Afrika (AU) au Jumuiya ya Maendeleo ya Nchi za Kusini mwa Afrika (SADC).
Kauli hiyo ilitolewa bungeni jana na Waziri Mkuu, Mizengo Pinda, alipokuwa akijibu maswali ya papo kwa hapo aliyokuwa akiulizwa na wabunge katika utaratibu mpya ambao ulianza kufanyika jana. Hilo litakuwa likifanyika kila Alhamisi.
Mbunge wa Kigoma Kaskazini, Zitto Kabwe (CHADEMA), ndiye aliyeuliza maswali kuhusu msimamo wa Tanzania kuhusu kusuasua kutangazwa kwa matokeo ya uchaguzi nchini Zimbambwe.
Mbali ya hilo, Zitto alitaka kujua iwapo Tanzania itakuwa tayari kupeleka majeshi ya kumuondoa kiongozi ambaye hatakubaliana na matokeo ya uchaguzi kama ilivyofanya Comoro.
Chama kinachotawala nchini Zimbabwe ni rafiki mkubwa wa chama chako Mheshimiwa Waziri Mkuu. Je, serikali itakuwa tayari kupeleka majeshi huko kama mtu hatakubaliana na matokeo? alihoji Zitto.
Katika majibu yake, Pinda alisema kwa hivi sasa wanasubiri kuona hali ya mambo inavyokwenda nchini Zimbabwe, kwani hadi sasa matokeo ya uchaguzi wa rais bado hayajatangazwa.
Suala la Zimbabwe halipendezi hata kidogo na ni kitendawili kwa dunia nzima
lakini pia hatuwezi kujiingiza mahali ambapo hatujaombwa kufanya chochote, maana tukijiingiza tunaweza kuulizwa, nani kawaita, alisema Pinda.
Alisema jambo la msingi ambalo Tanzania inapenda kuona ni matokeo ya uchaguzi yanatangazwa na mshindi anapatikana kulingana na kura alizopigiwa na wananchi. Alisema SADC inakutana kesho na ndiyo kiungo kikubwa cha jambo hilo, na kama itashindwa kulitolea maamuzi, linaweza likapelekwa AU, ambayo ndiyo chombo kikubwa barani Afrika kufanya maamuzi.
Zimbambwe ni miongoni mwa marafiki wakubwa wa Tanzania kihistoria na katika harakati za kudai uhuru, Tanzania iliisaidia sana Zimbabwe kama zilivyo nchi nyingine kusini mwa Afrika.
Hata hivyo, katika miaka ya hivi karibuni, nchi hiyo imekabiliwa na matatizo makubwa ya kisiasa, kiuchumi na kijamii, hasa baada ya Rais wake Robert Mugabe, kuingia katika mgogoro na mataifa makubwa kutokana na sera zake.
Taifa hilo lilifanya uchaguzi wake wiki mbili zilizopita na hadi sasa matokeo yake hayajatangazwa bila kutolewa sababu ya msingi, huku mpinzani mkuu wa rais wa sasa, Morgan Tsvangirai, wa Chama cha MDC, akidai kuwa hizo ni mbinu za kutaka kubadilisha matokeo ambayo yeye ameshajitangaza kuwa mshindi.
Aidha, katika kile kinachoonekana kumpigia debe Waziri Mkuu, muda mfupi baada ya kipindi hicho cha maswali kumalizika, Spika wa Bunge Samuel Sitta, alisema Tanzania imepata kiongozi anayefaa, ambaye ameonyesha kumudu vilivyo nafasi hiyo.
Alisema Mungu anajua kuchagua kiongozi anayefaa kwa taifa la Tanzania, na lazima ijivunie kwa kuwa na aina hiyo ya kiongozi ambaye amepata madaraka muda mfupi uliopita, lakini ameonyesha kuifanya kazi yake hiyo vizuri.
Sifa hizo alimmwagia alipokuwa akifunga kipindi hicho kipya cha maswali na majibu ya papo kwa hapo kwa Waziri Mkuu, kilichoanzishwa kwa lengo la kuwapa fursa wabunge kupata nafasi ya kuuliza na kujibiwa moja kwa moja kutoka kwa Waziri Mkuu, Mizengo Pinda.
Kweli Mungu huchagua viongozi wake, na kweli Tanzania tumepata PM (Waziri Mkuu) anayefaa, kwani tumemuona jinsi alivyojibu maswali vizuri katika awamu yake ya kwanza ya kujibu mambo hapo kwa hapo, alisema Sitta.
Source: Tanzania Daima.