SoC01 Ombwe la uongozi litaendelea kukita mizizi iwapo sifa hizi za ndani hazitahuishwa

SoC01 Ombwe la uongozi litaendelea kukita mizizi iwapo sifa hizi za ndani hazitahuishwa

Stories of Change - 2021 Competition

colesh

New Member
Joined
Jul 28, 2021
Posts
1
Reaction score
1
Wapendwa salam, amani iwe kwenu.

Mwaka 2007 nilitamani sana kuwa kiongozi mahali fulani.Nikiri kuwa ndani ya nafsi yangu kwa dhati nilidhamiria kuitenda kazi ile kwa bidii,uaminifu na moyo wa kujituma. Kwa kuwa nafasi ile ilikuwa ni ya kupigiwa kura kulikuwa na 100% ya kushinda au kushindwa. Nilipiga magoti kumsihi Mungu anipe nafasi hiyo.Mungu ni mwema nilipata nafasi ile, tena kwa kura nyingi sana.Katika kipindi cha awali nilifanya kazi ile kwa bidii ila si kwa kiwango ambacho nilidhamiria hapo awali. Baada ya muda kitambo tabia ya ukifutu,dharau,majivuno,kiburi na kila aina ya tabia isiyofaa kwa kiongozi vilinitawala.Wengi walio nipigia kura walifadhaika sana,walijaribu kunionya lakini ilishindikana.Uongozi wangu ulitamalaki uvuli wa chuki,fitina,makundi,utengano na mengine yenye kufanana na hayo.Katika kipindi changu chote kulikuwa na ombwe kubwa katika uongozi .Hatimaye awamu yangu ilitamatika.

Zimwi la uongozi wangu mbaya liliniandama miaka kenda.Kila awamu niligombea nikiambulia patupu.Nilijuta na kufedheheka sana. Nilimuomba Mungu sana na wakati mwingine nilifunga nikimsihi Mungu anipe nafasi tena. Kipindi hiki nilijiwekea kipimo iwapo Mungu atakuwa amenichagua mwenyewe basi ajidhihirishe.Siku ya uchaguzi ilipowadia muda wa uchaguzi ulipangwa kuwa saa kumi za jioni.Kwa hali isiyo ya kawaida nilipatwa na usingizi mzito na nikaamua kujipumzisha.Niliposhtuka ilikuwa tayari imefika saa kumi na mbili na nusu.Nilikurupuka haraka kuelekea kilipokuwa chumba cha uchaguzi.Kwa kifupi uchaguzi ulikuwa umekwishafanyika.Huku moyo wangu ukitanda wingu la fadhaa huku nikitweta, nikajua nimeikosa nafasi. Kwa kuwa tulikuwa na kikao usiku wa siku hiyo nilihudhuria kwa unyonge sana.Nilipoingia chumba cha mkutano nilishangaa kusikia kila mtu akanipa hongera.Nilipigwa na butwaa nisielewe nini kimetokea.Kumbe nilipigiwa kura bila ya mimi kuwepo.Cha kushangaza zaidi nilipigiwa kura zote nikikosa kura moja ambayo ni yangu mwenyewe.Nilimshukuru sana Mungu na nikajiapiza kufanya kazi kwa moyo mkuu na kutorudia makosa ya awali.

Kwa kuwa asili yangu ya ndani haikua imehuisha tabia na sifa za uongozi bora,taratibu utusitusi wa zile tabia za 2007 zilianza kujirudia zikaota,zikachipuka na kuota mizizi na kuzaa matunda ya uovu na machukizo.Awamu hii nilijiinua zaidi.Sikushaurika wala kusikia.Niliumiza na kujeruhi mioyo ya watu niliowaongoza.Hawakuamini kama ningewatendea mabaya kwa namna walivyojenga matarajio makubwa sana juu yangu.Walitegemea mapambazuko ya kiungozi ambayo mbegu yake ilikauka na kufa bila kumea.

Ndugu zangu ninapoandika makala hii ni miaka kumi na tano imepita tangu uongozi wangu ulipokoma.Katika kipindi hiki chote nimekuwa nikitafakari sana juu ya sababu kubwa zilizonifanya nishindwe kuwa kiongozi bora.Ukweli ni kwamba kabla ya kuchaguliwa nilikua na kiu kali na nia thabiti ya kufanya mapinduzi ya kiutawala na kuleta uongozi wenye tija. Ndugu zangu kila kosa huja na funzo ndani yake.Katika kipindi hiki cha miaka kumi na tano nimejifunza kuwa uongozi bora hautokani na sifa za nje pekee kama kuwa na lugha ya ushawishi, sura yenye mvuto, kimo,muonekano wa upole n.k.Sifa hizi za nje hazitoshi hata kidogo kukufanya uwe kiongozi bora bali sifa bainifu za ndani ndio humjenga kiongozi bora. Matendo ya kiongozi yeyote ni akisi ya sifa zake za ndani.

Ni dhahiri shahiri Nchi yetu katika kipindi cha miaka 60 ya uhuru tumepita katika tawala (awamu) tano na hivi sasa tukiwa ya sita.Katika awamu zote hizi,kila awamu kuna somo tumejifunza.Kwa maoni yangu binafsi vigezo tunavyotumia kuwachagua viongozi kwa kiasi kikubwa vimeaksi sifa za NJE na katika ufinyu sana tumezingatia sifa za ndani.Sote tu mashuhuda katika awamu zote tano na hivi sasa ya sita tumeshuhudia pasi na shaka ukiukwaji mkubwa wa miiko ya uongozi,tabia za ukifutu,rushwa,ufisadi,matumizi mabaya ya madaraka ,uongo, na uzandiki .Vitendo hivi vimekuwa kansa na vimekomaa na kuwa sehemu ya maisha ya uongozi.

Mwalimu na mchungaji Dr. Peter Mitimingi akimnukuu John.C.Maxwell katika kitabu chake cha TOFAUTI YA UONGOZI NA UTAWALA alisema“Kitu kisicho fanyika katika ukamilifu wake,hakikufanyika kabisa”. Hii inajidhihirisha pia kwa kiongozi yeyote iwapo atakosa sifa yeyote muhimu basi tegemea dosari nyingi katika uongozi wake.Hapo awali nilipata kutaja sifa bainifu za kiongozi bora. Sifa hizi ni za nje na ndani. Katika makala hii nitaangazia zaidi sifa kuu nne za ndani ambazo kwa kiasi kikubwa sana ndio zinaakisi uwepo wa kiongozi bora.

Kuwa na katiba bora,bunge,mahakama na mifumo mingine ya kiutawala kwa uwepo wake ni hakika kuwa baadhi ya mambo yatadhibitiwa kwa nguvu ya mifumo hii. Lakini ni kwa nasibu sana mifumo hii inaweza kujenga uongozi bora. Sote ni mashahidi kuna nchi ambazo kwa ubora wa katiba na mifumo yake ya kiserikali imesemekana kuwa bora na thabiti lakini bado mambo kama ubadhirifu wa fedha,rushwa,ufisadi,Ugatuzi mbaya wa madaraka,wizi na ukandamizaji wa demokrasia bado vimeendelea kutamalaki katika nchi hizo.Hii inadhihirisha kuwa zipo sifa nyingine zaidi zinazojenga uwepo wa uongozi bora.

Ukisoma na kutafakari kwa utulivu ahadi kumi za MwanaTANU utabaini kuwa zilijikita sana katika kumjenga mwanachama mzalendo ambapo kimsingi matunda yake ni kujenga kiongozi aliyebora.Ni ukweli usio na mashaka kuwa nchi yetu imekua chini cha chama kimoja ambacho kiitakadi na miiko yake imejikita katika kumjenga kiongozi aliye bora. Lakini kwa kipindi cha zaidi ya miaka sitini ya uongozi wa chama hiki mambo kama ubadhirifu wa fedha,rushwa,ufisadi,Ugatuzi mbaya wa madaraka,wizi na ukandamizaji wa demokrasia vimetamalaki kwa kiasi kikubwa karibu kila awamu ya uongozi.Katika tafakuri yangu nimebaini kuwa kwa kiasi kikubwa sehemu ya upatikaji wa viongozi wa chama hiki ulichakatwa na kughubikwa na sifa za nje kuliko za ndani.

1627546840125.png

Picha kwa hisani ya mtandao.

SIFA KUU NNE ZA NDANI ZA KIONGOZI BORA.

Katika makala hii dhima kuu ni kujenga picha kuwa pamoja na katiba bora na mifumo mingine ya kiserikali,Uwepo wa itikadi kali, sheria,kanuni na hata miiko ya kiuongozi.Ombwe la uongozi litaendelea kukita mizizi iwapo sifa hizi za ndani hazitahuishwa. Sifa hizi ni zifutazo;

Mosi,kiu kali ya kutenda haki. Neno haki kwa tafsiri ya kamusi ya kiswahili sanifu lina maana ya ‘jambo ambalo mtu anastahiki au kitu anachostahili kuwa nacho.Kwa tafsiri ya kamusi ya kisheria neno haki lina maana ‘kile mtu anachostahili kuwa nacho au kile anachoruhusiwa kufanya, au kile anachostahili kupokea kutoka kwa wengine kwa mujibu wa sheria’.Kwa tafsiri hii tunaweza kuona kuwa sheria ndio msingi wa haki, sheria ndio inasema kile unachostahili kuwa nacho au unachoruhusiwa kufanya au unachotakiwa kupata kutoka kwa wengine. Kwa maana pana zaidi tunaweza kusema haki ni maslahi ya mtu ambayo yanatambuliwa na kulindwa na sheria.Kiongozi bora ana kiu ya kutenda haki. Utendajiwa haki haudhibitiwi na mazingira ya aina yeyote wala unasaba ulipo baina ya mtenda na mtendewa haki.

Pili,uaminifu.Mtu aliye mwaminifu ni yule ambaye anatenda sawasawa na maagizo, sheria na taratibu zilizowekwa.Ikiwa ni mtu aliyeajiriwa katika kazi za nyumbani au ya serikali anafanya kazi ipasavyo,si mwizi, mpokea rushwa,mdhulumaji na wala si mwenye hila.Ukiona unapungua au kutia shaka kwa namna yeyote katika kutenda sawasawa jua kuwa wewe HUNA sifa za ndani zitakazokufanya uwe kiongozi bora.

Tatu, upendo wa kweli .Vitabu vyote vya dini vinaeleza nguvu iliyoko ndani ya upendo. Penye upendo kuna kusamehe, kuvumilia, kufadhili, kustakabali na sifa nyingine zinazofanana na hizi.Kiongozi bora anatakiwa kuhifadhi na kudumisha upendo kwa wale anaowaongoza.Katika ukristo upendo ni mojawapo ya amri kuu.Sifa hii pia ni kuu kwa kiongozi yeyote aliye bora. Kipimo chake cha ubora wake kinadhihirika na kiasi cha upendo wake kwa wale anaowaongoza.

Nne.Hofu ya Mungu.Katika dunia pamoja na kuwepo mifumo mingi ya kuendesha na kusimamia amali na ustawi wa maisha ya binadamu lakini kuna mahali inafika mifumo na ujuzi wa binadamu unafika tamati, hivyo kutegemea nguvu iliyo juu ya uwezo wake.Jamii yetu inaamini uwepo wa Mungu aliyemuumba wa vitu vyote vinanyoonekana na visivyoonekana. Kiongozi yeyote mwenye kutambua uweza wa Mungu hana budi kuwa na hofu naye hasa pale anapokua katika utekelezaji wa majukumu yake.

HITIMISHO
Kama mbegu imeavyo kutoka katika kuoza, kuchipuka na hadi kuzaa matunda ndivyo sifa hizi za kiongozi bora zinavyokomaa. Sifa hizi za ndani zinajengwa na dhamira ya kweli, muda, rasilimali watu na mazingira kwa ujumla. Mbegu za sifa hizi zikakuzwa kutokea utotoni hadi unapokua mtu mzima. Ni vyema sifa hizi kuzingatiwa kuanzia ngazi ya familia hadi Taifa. Sifa hizi hazina njia ya mkato bali ni mchakato mrefu, unaohitaji kujizatiti na kujitoa kwa dhati.​
 
Upvote 1
Back
Top Bottom