Ongea na kamanda yawafikia wananchi wa HAI na kutaka utatuzi migogoro ya wakulima na wafugaji

Ongea na kamanda yawafikia wananchi wa HAI na kutaka utatuzi migogoro ya wakulima na wafugaji

Ndagullachrles

JF-Expert Member
Joined
Jun 20, 2023
Posts
256
Reaction score
259
Kutoka Dawati la Habari Polisi Kilimanjaro


Wananchi wa Kijiji cha Chekimaji, Kata ya Masama Rundugai, Wilaya ya Hai, wameibua changamoto mbalimbali zinazohusu migogoro kati ya wakulima na wafugaji, matumizi ya dawa za kulevya na vilevi haramu, pamoja na uhalifu, huku wakiiomba Serikali na Jeshi la Polisi kuimarisha usimamizi na kuchukua hatua za kisheria dhidi ya vitendo vinavyo hatarisha amani na usalama katika jamii.

Changamoto hizo ziliwasilishwa Oktoba 29, 2026, katika mkutano wa kampeni ya Ongea na Kamanda uliofanyika katika Ofisi ya Kijiji cha Chekimaji, ukiongozwa na Mkuu wa Polisi Wilaya ya Hai SSP Suzana Kidiku, akishirikiana na Mkuu wa Polisi Jamii Wilaya ya Hai (DCEO), SP Elishafra, Mkuu wa Polisi Jamii Kata ya Masama Rundugai (WCEO), INSP Robert, pamoja na CPL Bahati kutoka Dawati la Jinsia na Watoto.

Katika mkutano huo, wananchi walieleza kuwa baadhi ya wafugaji wamekuwa wakiingiza mifugo katika mashamba ya wakulima, kuharibu mazao na kusababisha migogoro inayofikia hatua ya kupigana na kujeruhiana. Aidha, walieleza kuwa baadhi ya wafugaji wanaotoka maeneo ya nje ya Wilaya ya Hai, ikiwemo Kiteto na Sanya Station, huingiza mifugo katika mashamba ya wananchi na kuondoka baada ya kulisha mifugo hiyo.

Wananchi pia walipendekeza kutengwa kwa maeneo maalumu ya malisho ya mifugo, kusajili wafugaji na kujua idadi halisi ya mifugo yao kabla ya kuruhusu wafugaji wapya kuingia na kuishi katika kijiji hicho, ili kuweka utaratibu unaozingatia haki na maslahi ya pande zote.
Katika changamoto nyingine, wananchi walieleza kuwepo kwa biashara ya bangi, mirungi na gongo katika baadhi ya vijiwe na vibanda vya pembezoni. Pia waliibua hoja kuhusu tukio la shambulio la kudhuru mwili na tukio la kulawiti mtoto, wakitaka kufahamu hatua zilizofikiwa katika ufuatiliaji wa matukio hayo.

Aidha, wananchi walieleza changamoto za matumizi na usimamizi wa mashine ya kuvunia mpunga (combine), huku wakisisitiza umuhimu wa wakulima na wafugaji kuishi kwa amani, kupendana na kupata huduma sawa bila ubaguzi. Walisisitiza pia umuhimu wa viongozi wa kijiji kufahamu idadi halisi ya wafugaji na mifugo kabla ya kumpokea mfugaji mpya.

Akijibu kero hizo, SSP Suzana Kidiku alieleza kuwa Jeshi la Polisi kwa kushirikiana na Serikali ya Kijiji limeweka mikakati ya kudhibiti migogoro ya wakulima na wafugaji, ikiwemo kuzuia mifugo kuingizwa kwenye mashamba ya wananchi kinyume cha utaratibu na kuwabaini wafugaji wanaoingia kutoka maeneo ya nje bila kufuata taratibu zilizowekwa.

Aidha, uongozi wa kijiji umeelekezwa kuhakikisha wafugaji wanasajiliwa na idadi ya mifugo yao inatambuliwa kabla ya kuruhusu wafugaji wapya kuingia katika kijiji hicho, ili kuweka usimamizi mzuri wa shughuli za ufugaji.

Kuhusu matukio ya uhalifu yaliyoripotiwa, viongozi wa Jeshi la Polisi walieleza kuwa shambulio la kudhuru mwili na tukio la kulawiti mtoto vimechukuliwa kwa uzito na vinaendelea kufuatiliwa kwa mujibu wa taratibu za kisheria, kwa lengo la kuwabaini wahusika na kuwachukulia hatua stahiki. Wananchi pia walielimishwa kuhusu taratibu za dhamana kwa watuhumiwa pale wanapokidhi vigezo vya kisheria.

Katika kukabiliana na biashara ya dawa za kulevya na vilevi haramu, Jeshi la Polisi limeelekeza kuimarishwa kwa doria na operesheni katika maeneo ya vijiwe na vibanda vinavyotajwa kuhusishwa na biashara ya bangi, mirungi na gongo, ili kuwabaini na kuwachukulia hatua wanaojihusisha na vitendo hivyo.

Sambamba na hilo, wazazi wameonywa dhidi ya kuwapa watoto wadogo jukumu la kuchunga makundi makubwa ya mifugo ambayo hawawezi kuyadhibiti, wakisisitizwa kulinda haki na usalama wa watoto.

Kwa upande wao, Mkuu wa Polisi Wilaya ya Hai na Mkuu wa Polisi Jamii Wilaya ya Hai wamesisitiza umuhimu wa wakulima na wafugaji kuishi kwa amani, kuheshimiana na kutumia vikao halali vya kijiji kutatua changamoto zao badala ya kujichukulia sheria mkononi.

Kampeni ya Ongea na Kamanda inaendelea kuwa jukwaa muhimu la wananchi kuwasilisha maoni na changamoto zao kwa Jeshi la Polisi na Serikali, ili zipatiwe ufumbuzi kwa kushirikiana na kuimarisha amani na usalama katika jamii

IMG-20261030-WA0225.jpg
IMG-20261030-WA0224.jpg
IMG-20261030-WA0228.jpg
IMG-20261030-WA0231.jpg
IMG-20261030-WA0233.jpg
IMG-20261030-WA0232.jpg
IMG-20261030-WA0230.jpg
IMG-20261030-WA0227.jpg
IMG-20261030-WA0229.jpg
IMG-20261030-WA0234.jpg
IMG-20261030-WA0235.jpg
 
Back
Top Bottom