Pale uponyaji unapohitaji sindano tu, matibabu ya akyupancha ya China yaleta nafuu kwa wagonjwa wa Zanzibar

Pale uponyaji unapohitaji sindano tu, matibabu ya akyupancha ya China yaleta nafuu kwa wagonjwa wa Zanzibar

ldleo

JF-Expert Member
Joined
Jan 9, 2010
Posts
1,310
Reaction score
1,265
微信图片_20250515151315.png


Kwa Mtanzania Hassan Jumbe mwenye umri wa miaka 26, matatizo ya kukosa usingizi siku zote wakati usiku ilikuwa ni maumivu na mfadhaiko mkubwa kwake.

Usiku mmoja baada ya mwingine, maumivu makali ya kichwa yasiyoisha yalimwandama mfanyakazi huyu mbichi wa ujenzi, na kumfanya ashindwe kupumzika na kuzingatia. Ingawa alijaribu kila njia kuanzia dawa za magharibi hadi dawa za mitishamba, lakini zote hazikufua dafu na kushindwa kumpatia afueni.

Baadaye, rafiki yake mmoja alimwambia kuhusu matibabu ya akyupancha katika Hospitali ya Mnazi Mmoja, ambapo madaktari kutoka China walitumia sindano laini za fedha kupunguza maumivu. Akiwa na mashaka kidogo Jumbe aliamua kwenda kujaribu matibabu hayo kutokana na kuchoka na maumivu makali.

Hospitali ya Mnazi Mmoja ndio kituo kikuu cha huduma za afya ya umma katika mkoa wa Mjini Magharibi, Unguja, mahali walipo timu ya madaktari wa China.

"Mwanzoni nilidhani labda ni mzaha tu. Sindano inaponya maumivu ya kichwa, kweli?" Jumbe aliiambia Xinhua katika mahojiano ya hivi majuzi.

"Lakini baada ya kupatiwa huduma mara ya kwanza, nilihisi unafuu. Hadi ilipofikia mara ya tatu, maumivu ya kichwa yalikuwa karibu kuisha kabisa," alikumbuka, akisugua eneo kwenye mwili wake ambalo liliwahi kuingizwa sindano. "Yaani haikuwa matibabu pekee. Madaktari wako makini sana, na wana subira kubwa. Unahisi kabisa kwamba wanajali kwelikweli."

Jumbe ni miongoni mwa wagonjwa zaidi ya 120,000 waliopona kwa kupatiwa tiba jadi ya Kichina (TCM) visiwani Zanzibar, ambapo timu za madaktari wa China zimekuwa zikitoa huduma tangu mwaka 1964.

Kwa miongo kadhaa, zaidi ya madaktari 30 wa matibabu ya jadi ya Kichina wamefanya kazi kwa zamu katika kisiwa hicho, wakitoa tiba ya akyupancha, tuina yaani matibabu ya ukandaji, na tiba asilia.

Ndani ya kliniki ya kawaida katika Hospitali ya Mnazi Mmoja, Li Dengke, daktari wa matibabu ya jadi kutoka Mkoa wa Jiangsu, China, alifanya kitendo kwa usahihi. Mikono yake iliyotulia iliingiza sindano moja moja, huku sauti yake tulivu ikiwatuliza wagonjwa wenye wasiwasi. Kwake yeye, matibabu ya jadi sio tu yanahusiana na mbinu, bali uelewa wa kina wa mwili wa binadamu na mazungumzo ya kimyakimya kati ya tabibu na mgonjwa.

"Nimeona wagonjwa wakija na maumivu makali na kuondoka wakiwa na ahueni, lakini ni zaidi ya hapo," Li alisema. "Kila sindano inabeba huduma. Na kila mguso unatoa ujumbe."

Fatma Ally Abdallah, muuguzi mwenye umri wa miaka 30, alitazama kwa makini huku mikono yake ikiwa imetulia wakati alipokuwa akimtayarisha mgonjwa anayefuata. Hakuwa tena mtazamaji tu. Tangu mwaka 2021, amekuwa akijifunza mbinu za matibabu ya jadi ya China chini ya uongozi wa madaktari wa China. Kile kilichoanza kama udadisi tu sasa kimegeuka na kuwa ujuzi anaotumia kwa kujiamini.

"Mwanzoni, ilionekana ni ngumu sana. Lakini madaktari wa China walikuwa na subira. Walinifundisha akyupancha, walielezea mfumo wa meridian, na hata kuniongoza katika kuchagua vituo vya matibabu mwilini, kurekebisha sindano kwa mgonjwa anayesumbuliwa na maumivu ya sehemu ya chini ya mgongo. Sasa ninaweza kufanya akyupancha mimi peke yangu." Alisema.

Chen Wei, kiongozi wa timu ya 34 ya madaktari wa China Zanzibar, alieleza kuwa kazi yao ni kutibu na kufundisha.

"Tunazingatia mambo mawili. Kwanza, tunatoa mafunzo rasmi ambapo madaktari na wauguzi wazawa hujifunza mbinu za matibabu ya jadi, kwa dharia na vitendo. Pili, tunawahimiza kufanya mazoezi kwa wagonjwa wenyewe, ili kuwajengea ujasiri na ujuzi," alisema.

Hivi sasa, madaktari na wauguzi kadhaa wazawa wana uwezo wa kufanya wenyewe matibabu ya msingi ya jadi. Wanatumia tuina, kusimamia tiba ya vikombe, na kuwaelezea dhana za matibabu ya jadi kwa wagonjwa wanaotaka kujua.

Akitazama nje ya dirisha la kliniki linalopigwa na mvua, Chen alikumbushia safari ya timu ya matibabu ya China akisema kwa upole "Sio tu kuhusiana na sindano, bali ni kuhusu mioyo wanayogusa."
 
Back
Top Bottom