Elias Msuya
Platinum Member
- Dec 23, 2011
- 267
- 1,014
Akihitimisha mjadala wa Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa mwaka 2025/26 Juni 24 bungeni jijini Dodoma, Waziri wa Fedha, Dk Mwigulu Nchemba alifafanunua kuhusu deni la Taifa akisema wanakosoa deni hilo kupanda wasijikite kwenye wingi wa fedha, bali waangalie matumizi.
Dk Maigulu alisema kinachoitofautisha Tanzania na mataifa mengine ni nidhamu ya fedha zilizokopwa, kwani zipo nchi zinazoingia kwenye matatizo ya madeni kwa sababu ya kukosa nidhamu ya matumizi ya fedha walizokopa kwa kutozingatia mapato na mikopo unayochukua.
Alitoa mifano ya matumizi ya fedha za mikopo kuwa ni pamoja na ujenzi wa barabara akiitaja inayotoka Dodoma kwenda Arusha akisema imepunguza mzunguko wa kwenda Morogoro na Tanga.
Kwa mujibu wa taarifa za Serikali, Deni la Taifa sasa lilifikia Sh107.7 trilioni kutoka Sh91.7 trilioni katika kipindi kama hicho mwaka 2024, sawa na ongezeko la asilimia 14.9. Kati ya hizo, deni la ndani ni Sh34.25 trilioni na lile la nje likiwa dola za Marekani 26.67 bilioni.
Deni hilo limeongezeka kutoka Sh60.9 trilioni, Aprili 2021, hivyo ni kama ongezeko la Sh46.8 trilioni kwa kipindi cha miaka minne.
Sasa tukiangalia matumizi kama anavyotaka Waziri Mwigulu, wala hakuna ubishi kwamba kuna miradi mingi ya maendeleo inaendelea nchini.
Soma Pia: Mwigulu afafanua utofauti wa deni la Serikali na deni la Taifa
Ipo miradi mikubwa ya kimkakati kama ujenzi wa mradi wa umeme wa Julius Nyerere Hydroelectric Power unaoelekea kukamilika, madaraka kama la Magufuli lililozinduliwa na Rais Samia Suluhu Hassan hivi karibuni, ujenzi wa reli ya kisasa na ununuzi wa ndege na miradi ya barabara.
Upotevu wa fedha
Pamoja na miradi hiyo, kuna upotevu wa fedha ambao kila mwaka Mdhibiti na Mkaguzi wa Hesabu za Serikali (CAG) amekuwa akiuzungumzia. Huo Dk Mwigulu hauzungumzii.
Uchambuzi wa ripoti ya CAG ya mwaka 2023/24 uliofanywa na Chama cha ACT Wazalendo hivi karibuni, umebainisha upotevu wa fedha zinazofikia Sh2.56 trilioni.
Ripoti hiyo imebainisha ubadhirifu wa fedha za umma unaofikia Sh1.116 trilioni, ambapo ubadhirifu katika Serikali Kuu ni 141.95 bilioni, ubadhirifu katika uiradi ya maendeleo ni Sh190 bilioni, ubadhirifu katika Serikali za Mitaa- Sh134.36 bilioni, ubadhirifu katika mashirika ya umma –Sh650.02 bilioni.
Katika ubadhirifu huo, ripoti ya CAG inaonesha ya kwamba takribani Sh506 bilioni pekee ya ubadhirifu unatokana na matumizi yasiyo na tija na ukusanyaji wa mapato nje ya mfumo wa kielektroniki.
Ripoti ya CAG inaendelea kubaini kwamba, jumla ya kiasi cha Sh1.446 trilioni kinatokana na upotevu wa fedha za umma; ambapo Sh1.34 trilioni pekee zinatokana na madeni ya mapato yasiyokusanywa [ada, faini na gharama za huduma] na hivyo kuwa sehemu ya fedha za umma zinazopotea.
Sasa pamoja na kukopa na kukusanya kodi, bado kuna upotevu wa fedha zote hizi, watu wataacha kulalamikia kukua kwa deni la Taifa? Nani amechukuliwa hatua kwa upotevu wa fedha za umma?
Hayo yote Dk Mwigulu hayazungumzii, bali anazungumzia miradi michache inayofadhiliwa na mikopo.
Mbali na upotevu wa mapato, kuna matumizi mabaya ya fedha za umma, ikiwemo ununuzi wa magari ya kifahari kwa viongozi.
Hilo limeshasemwa sana, lakini Serikali imeziba masikio na ndio kwanza imejikita kufanya anasa kwa kununua magari ya kifahari kila uchao.
Kwa mfano kwa mwaka wa fedha wa 2025/26, Ofisi ya Rais - TAMISEMI imepanga kutumia Sh204.90 bilioni kwa ajili ya ununuzi wa magari ya viongozi wa mikoa, wilaya na halmashauri na ujenzi, ukarabati na ukamilishaji wa miundombinu ya mikoa, wilaya, halmashauri na tarafa ikiwemo majengo ya utawala, ikulu ndogo na makazi ya viongozi.
Kumekuwa na hoja kwamba, bajeti ya ununuzi wa magari ya viongozi yaweza kupunguzwa kwa kuacha kununua magari ya kifahari ambayo mengine hugharibu hadi Sh500 milioni kwa kiongozi mmoja tu.
Mbali na kununua magari mapya ya gharama nafuu, Serikali inaweza ikarekebisha sheria ya ununuzi ikaruhusu ununuzi wa magari ya mitumba, ambayo kwa watu binafsi wamekuwa wakiyatumia kwa ufanisi mkubwa.
Kumekuwa na mifano ya nchi nyingine za Afrika na hata Ulaya, ambako viongozi wananunuliwa magari ya bei nafuu na hata nchi nyingine, viongozi hawanunuliwi magari bali wanakopeshwa na wanayalipia na kuyafanyia matengenezo wenyewe.
Kwa nini Tanzania tusifikie huko ili kubana matumizi ya Serikali?
Dk Mwigulu anasema fedha za mikopo haziendi kwenye matumizi ya kawaida, lakini kama tu kwenye ununuzi wa magari ya kifahari ambayo yananunuliwa kila mwaka, mabilioni ya fedha yanatumika, hiyo miradi ya maendeleo itakamilika lini?
Sio dhambi mtu kuendeshwa kwenye gari la kifahari linalofikia Sh500 milioni, lakini alinunue mwenyewe na alikarabati mwenyewe. Kwa nini Serikali itumie fedha nyingi kuhudumia viongozi kuliko kuhudumia wananchi waliowachagua?
Kingine ni mishahara na marupurupu ya wabunge wa Bunge la Jamhuri ya Muungano. Japo huwa hayawekwi wazi, lakini baadhi ya waliokuwa wabunge wanasimulia malipo manono wanayolipwa.
Kwa mfano, hivi kuna mantiki gani ya kumlipa mbunge mshahara na posho mbalimbali zinazofikia zaidi ya Sh15 milioni kwa mwezi, huku daktari anayehudumia Watanzania akiambulia mshahara wa Sh2 milioni kwa mwezi?
Huyu daktari amesoma miaka minne, amehangaika ili athibitike kuwa na viwango, lakini mshahara wake ndio huo. Matokeo yake sasa madaktari wa Serikali wanafanya kazi za nje katika hospitali za binafsi ili kufidia ukali wa maisha.
Lakini mbunge, tena wengine wameishia tu darasa la saba na kidato cha nne, ndio wanavuma mamilioni ya fedha kwa kuwa wabunge tu? Hii inaingia akilini kweli? Huo sio upotevu wa fedha za umma? Kwa nini tunaifanya siasa kuwa uwanja wa kujitajirisha?
Hali hii ndio imefanya siasa kuwa kama biashara na wanataaluma wengi sasa wanakimbilia kwenye siasa ili watajirike.
Kwa maoni yangu, Bunge ni kichaka cha upotevu wa fedha za umma, vinginevyo mishahara na marupurupu yao yaangaliwe upya.
Ukifuatilia nchi zilizoendelea ambazo ndio zinatupa misaada hiyo, siasa sio eneo la kutajirika. Ubunge kwao ni kama kazi ya kujitolea na kunakuwa na usawa wa kipato kwa taaluma zote.
Eneo lingine linalopoteza mapato ni misamaha ya kodi kwa wawekezaji na utoroshwaji wa fedha kwenda nje ya nchi.
Pamoja na kuvutia wawekezaji, misamaha hiyo na ulegevu wa sharia zetu unachangia upotevu wa mapato.
Haya ndio mambo yanayofanya wananchi waalamikie ongezeko la deni la Taifa na wanalalamika kwa sababu wanalipa kodi, halafu kuna maelfu ya vijana hawana ajira, hawana uhakika hata wa mlo mmoja kwa siku, hawawezi kuelewa ukisema matumizi ni mazuri.
Lazima mikopo na madeni ya Serikali yaakisi yaakisi maisha ya watu wa kawaida.
Deni linaweza likawa dogo na likawa himilivu, lakini matokeo yake hayaonekani kwa urahisi kwa wananchi.
Hata deni la Taifa lingekuwa limefika Sh150 trilioni, lakini kunakuwa na uwajibikaji wa hali ya juu, barabara za mitaani zipitike, maji yaonekane, umeme uwe wa uhakika.
Fikiria tu hapa Dar es Salaam, jiji la biashara, lakini barabara za mitaani hazipitiki, maji ya shida, usafiri ni mgumu, foleni kila mahali. Kuna mtu ataelewa ukisema tuna nidhamu ya matumizi ya mikopo?
Hivyo, Serikali itafute mikakati thabiti ya kukabiliana na upotevu wa mapato kwa kuongeza ukali wa sgeria kwa wabadhirifu wa fedha hizo.
Pia Serikali ipunguze matumizi ya anasa kwa viongozi ili fedha hizo ziende kwenye miradi ya maendeleo.