Paroko Na Polisi Watoa Wito Wa Kukabiliana Na Migogoro Ya Ndoa Malinyi

Paroko Na Polisi Watoa Wito Wa Kukabiliana Na Migogoro Ya Ndoa Malinyi

Roving Journalist

JF Roving Journalist
Joined
Apr 18, 2017
Posts
5,352
Reaction score
15,876
m .jpeg
Paroko wa Parokia ya Shirika la Roho Mtakatifu, Kilosa Mpepo, Padri Nikas Kiuko, amewaomba waumini wa Parokia hiyo kuikataa migogoro ya ndoa inayoweza kusababisha vitendo vya ukatili na unyanyasaji, majeraha na hata vifo kwa wanandoa.

Wito huo umetolewa wakati wa adhimisho la Misa Takatifu ya kuwaombea wanandoa katika Parokia hiyo, ambapo wanandoa wamepata fursa ya kurudia ahadi zao za ndoa na elimu iliyotolewa kwa waumini hao na Jeshi la Polisi Mkoani Morogoro.
WhatsApp Image 2026-10-17 at 11.56.48n.jpeg
WhatsApp Image 2026-10-17 at 11.56.49kk.jpeg
Padri Kiuko amesisitiza umuhimu wa wanandoa kutokubali migogoro kuwa sehemu ya maisha yao, badala yake kutafuta suluhisho kupitia maombi, mazungumzo na ushauri wa kitaalamu, ikiwemo huduma za wataalamu wa afya ya akili na saikolojia, ili kusaidia kuponya majeraha ya kihisia na kuimarisha mahusiano ya kifamilia.

Kwa upande wake, Mkuu wa Polisi Jamii Mkoa wa Morogoro, Kamishna Msaidizi wa Polisi (ACP) Samweli Kijanga, amemshukuru Paroko kwa ushirikiano wake na Jeshi la Polisi katika kutoa elimu kwa jamii huku, akiwataka waumini kuzingatia misingi ya kiroho na mafundisho ya viongozi wa dini ili kudumisha upendo, mshikamano na amani ndani ya ndoa na familia zao.

Naye Mkuu wa Polisi Jamii Wilaya ya Malinyi, Mrakibu wa Polisi (SP) Shangwe Mlela, amewakumbusha wananchi kuhusu zoezi la kusalimisha silaha haramu na kuwataka kutumia muda uliobaki kusalimisha silaha hizo katika mamlaka husika, kwa lengo la kuimarisha usalama katika jamii.

Kwa upande wake, Sister Jesca Musimbi wa Shirika la Kitawa la Wadogo wa Roho Mtakatifu, ameishukuru Jeshi la Polisi Mkoa wa Morogoro kwa kutoa elimu kwa waumini huku akiweka wazi kuwa elimu hiyo imekuwa darasa muhimu kwake na uzoefu wa kipekee, huku akibainisha kuwa ameguswa na namna vyombo vya usalama nchini Tanzania vinavyoshirikiana na jamii katika kutoa elimu na kuimarisha usalama.

Elimu hiyo ni sehemu ya jitihada za kuimarisha ushirikiano kati ya Jeshi la Polisi, viongozi wa dini na wananchi katika kukabiliana na vitendo vya ukatili, kuimarisha usalama na kujenga familia zenye amani na mshikamano.
 
Back
Top Bottom