Kwenye mkutano wa 76 wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa (UN), Rais Xi Jinping wa China alitoa Pendekezo la Maendeleo ya Dunia (GDI) likiwa na wito wa kuleta maafikiano kuhusu kufuata maendeleo, kuhimiza ukuaji wa pamoja na kusaidia kuharakisha utekelezaji wa ajenda ya Umoja wa mataifa ya mwaka 2030 ya kufikia maendeleo endelevu.
Tangu pendekezo hilo lilipotolewa hadi sasa, hatua kwa hatua limeanza kupokelewa kwa dhati, mifumo yake ya utekelezaji inazidi kueleweka, na ushirikiano wa kivitendo chini ya mfumo wa pendekezo hilo vimeanza kuonekana taratibu, na hivyo kuleta suluhisho la China la kupunguza pengo la maendeleo katika nchi za Kusini na kaskazini, na kujenga dunia bora kwa pamoja.
Mhadhiri mwandamizi katika Idara ya Sayansi ya Siasa, Chuo Kikuu cha Dar es salaam Dr. Ng’wanza Kamata, anapongeza pendekezo hilo na kuliona kuwa ni mwendelezo wa moyo wa Mkutano wa Bandung uliofanyika mwaka 1955, lakini ni pendekezo ambalo limejikita kwenye mahitaji ya sasa ya kiuchumi.
“Kwanza linahimiza nchi kuwa na uhuru wa kujuamulia njia ipi ya maendeleo wanayoitaka, lakini mbali na uhuru tunatakiwa kuangalia hali halisi ya sasa. Tukiangalia mgawanyo wa nguvu ya dunia kwa sasa, tunachoweza kuona ni kuwa bado nchi za magharibi ziko juu kijeshi, lakini kiuchumi nchi za magharibi hazina ukiritimba tena kama zamani. Kuna nchi za kusini kwa sasa ziko juu kiuchumi kuliko baadhi ya za magharibi, kwa mfano China na India sasa zimekuwa nchi zenye uchumi mkubwa kuliko nchi nyingi za magharibi. Hali hii inatoa unafuu kwa nchi nyingi za Afrika, ambazo zinaweza kuwa na nafasi ya kufanya machaguo. Kama kukiwa na ncha moja ya nguvu ya kijeshi na kiuchumi, ncha hiyo inaweza kuamrisha, lakini kama kuna nchi nyingi nchi za Afrika zinapata fursa ya kuwa na machaguo”
Licha ya kuakisi moyo wa mkutano wa Bandung, Pendekezo la Maendeleo ya Dunia (GDI) linaendana kabisa na mahitaji ya sasa ya dunia, na linakwenda sambamba na malengo ya maendeleo endelevu ya mwaka 2030 ya Umoja wa mataifa. Hata hivyo ni ukweli usiofichika kuwa mfumo wa uchumi wa dunia bado si wa haki kwa nchi za dunia ya tatu, hasa nchi za Afrika. China imekuwa ikichukua hatua mbalimbali kujaribu kuzishika mkono nchi za Afrika kujiletea maendeleo, kumekuwepo na mifano mbalimbali ya miradi inayoitwa miradi "midogo lakini mizuri" iliyo chini ya ushirikiano wa China-Afrika, ikiwa ni pamoja na ile ya uzalishaji wa chakula, nishati safi na nishati mpya kwa gharama nafuu, na hadi karakana za Luban, zinazotoa mafunzo ya ufundi kazi kwa vijana wengi wa Afrika.
Dr. Kamata pia anaona kuimarika kwa China kumekuwa na manufaa makubwa kwa nchi za Afrika na nchi za kusini zenye nia ya kujiletea maendeleo. Ametolea mfano kuwa zamani teknolojia zilikuwa zimehodhiwa na nchi za magharibi, ilikuwa vigumu sana kwa nchi za Afrika na nchi nyingine za kusini kupata teknolojia hizo. Lakini sasa, kupitia China, nchi za Afrika na nchi nyingine za dunia ya tatu zinaweza kupata teknolojia hizo kutoka China kwa gharama nafuu na kujiletea maendeleo.
Kwenye upande wa soko, Dr. Kamata pia amesema kuinuka kiuchumi na kiteknolojia kwa China, kumeifanya China iwe soko kubwa la maliasili na malighafi. Hali hii pia imezipa nchi za Afrika chaguo la mahali pa kuuza malighafi zake, na sio kama ilivyokuwa zamani ambapo soko la malighafi lilidhibitiwa na nchi za magharibi. Hali hii sasa inatoa fursa zaidi kwa nchi za Afrika kujiendeleza kwa kuuza maliasili zake kwa nchi mbalimbali duniani.