Tafakari ujumbe wa Pengo na uchukue atua
Nimeutafakari ujumbe wa pengo,kwa bahati mbaya au nzuri nina tofautiana naye sana. Natofautiana naye si kwa maudhui ya kile alichokisema bali kwa dhamira ya yale aliyoyasema. Sio pengo tu, viongozi wote wa dini kwa ujumla wamekuwa wanatuchanganya. Mfano ni viongozi hao wa dini wanajua wazi kuwa katiba yetu ina utata na hakuna haki. Ni wangapi wamewahi kusema kuhusu hilo. Viongozi wetu wa dini wanajua kuwa mfumo wa uchaguzi una matatizo hasa katika haki[level field] ni wangapi wamesema kuhusu hilo. Unapowaambia waumini wachague kiongozi safi bila kuchukua khanga huku ukijua kuwa kuna wizi wa kura na hukemei, hii ni nini kama si woga au unafiki.
Viongozi wa dini wanajua wazi kuwa haki haitendeki, wakulima wanaponyan'ganywa ardhi yao na kigogo mmoja tu, wangapi wameongelea hilo!
Viongozi wa dini wanajua kuwa kuna wizi wa kodi za wananchi na kikundi kidogo cha watu, mbona hawajakemea hadharani licha ya kuongea kwa mafumbo. Viongozi hao hao wanaona jinsi akina mama na watoto wanavyoteseka huko vijijini ili hali kodi zao zina nunua mashangingi, mbona wamekaa kimya. Ni hao hao kwa kutumia dini zao wanaingiza magari bila kulipia kodi na kuyauza, je ujasiri wa kuwakemea wagawa khanga wanaupata wapi.
Kiongozi Askofu mmoja aliwahi kumwalika Rais mmoja mstaafu na kuwaambia wananchi rais huyo ni msafi amefanya mengi juu ya uchumi. Kiongozi huyo anazijua tuhuma za wizi ambazo zipo wazi dhidi ya kiongozi huyo, lakini kwa kutaka milioni 5 za mchango akamsafisha mbele ya waumini wake. Sasa kiongozi huyu ataniambia niache kuchukua khanga kwa kumumini kwa lipi. Ninakemea vikali tabia za kuchukua khanga na kofia au 20,000 kuuza kura, lakini dhamira yangu lazima iambatane na matendo. Hawa viongozi hawana hilo.
Taifa lilipogubikwa na kashfa za wizi wa hali ya juu, viongozi wa dini zote walikaa kimya na kuwaachia akina ''Kubenea'', sasa leo wanatambua umuhimu wa viongozi wasio wala rushwa, swali ni je walifanya nini kutetea haki za mamilioni ya watanzania yaliyotafunwa kwa kupitia mikataba feki kama richmond,? au labda wizi wa kalamu ni dhambi ndogo kuliko kuvunja banda la kuku!
Nina jumuisha kwa kusema, alichosema Kadinali Pengo ni sahihi kabisa, lakini yeye na viongozi wa dini zote na madhehebu yote hawajasimamaia yale wanayoyajua, ni vipi leo watufundishe kile wasichoweza kukisimamia.? Ningewaomba wakae kimya watuachie mapambano ya khanga, kofia na bahasha za 20,000 sisi wapiga mayowe kwasababu tunaamini mayowe yetu yatasikika kwa mungu na wadhalimu wanaotutia umasikini siku zao zinakarabia, inaweza isiwe leo au kesho lakini tunaona pambazuko la matumaini mema.
Nitamsiiliza Dr Slaa kwasababu yeye amethubutu kusimama si mara moja au mbili kukemea maovu kwa dhamira yake,kwahiyo akiniambia anaichukia rushwa ninamwelewa zaidi kuliko yule anayenishawishi niichukie rushwa huku akiwabeba wala rushwa kwa namna flani ilimradi tu mambo yake au yao yaende vizuri.