PENIELA SEASON 3
EPISODE 2
MTUNZI : PATRICK.CK
ILIPOISHIA SEHEMU ILIYOPITA
“ Stop the car !!!..akasema Jason kwa ukali
“ Unataka kushuka? Akauliza Mathew
“ Mathew simamisha gari nishuke !!!..akasema Jason .Mathew hakujibu kitu akaendesha gari hadi katika kituo cha daladala kilichokuwa karibu akasimamisha gari na Jason akashuka kwa hasira na kuubamiza mlango na kutamka neno ambalo Mathew hakulisikia vizuri.Mathew hakumjali akaingiza gari barabarani na kuendelea na safari yake
“ stupid !!..akasema Mathew
“ Katika maisha yangu yote ndani ya kazi hii nimekutana na watu wengi makatili lakini si kama John Mwaulaya.Mtu huyu aliiteketeza familia yangu bila huruma na ametoa roho za watu wengi.Hata hivyo siku zake zinahesabika .Nitarudi tena kwake kwa mara nyingine na hii itakuwa ni zamu yangu.Picha za moto ule mkubwa ulioiteketeza familia yangu bado haijafutika kichwani kwangu.Nitamuua John taratibu sana na kwa mateso makali ” akawaza Mathew huku akiuma meno kwa hasira
ENDELEA……………………..
Hatimaye baada ya jitihada kubwa Dr Edwin na Dr Alex wakisaidiana na Dr Martini walifanikiwa kuirejesha hali ya John Mwaulaya katika hali yake ya kawaida.Mapigo ya moyo yalirejea katika hali ya kawaida japokuwa bado John bado hakuwa na fahamu.
“ Ouh ahsante Mungu ! akasema Dr Edwin baada ya mashine inayoonyesha mwenendo wa mapigo ya moyo kuanza kuonyesha kwamba sasa yalianza kwenda kawaida.Kwa takribani dakika mbili wote walibaki kimya wakimtazama John.Dr alex akamuita Edwin pembeni wakaongea kwa zaidi ya dakika kumi huku wakielekezana jambo fulani halafu wakamfuata Martin
“ Martin tunahitaji kuonana na Peniela” akasema Dr Alex.Martin akatoka na baada ya dakika tatu akarejea akiwa ameongozana na Peniela na Josh
“ Dr Alex vipi hali ya John? Akauliza Peniela kwa wasi wasi.Dr Alex akamshika mkono na kumketisha sofani
“ Peniela hali ya John mwaulaya siwezi kusema ni nzuri kwa sasa japokuwa mapigo ya moyo yamerejea katika hali yake ya kawaida.Inaonekana alipatwa na mstuko mkubwa na ndiyo maana hali yake ilibadilika ghafla.Tumejitahidi kwa kila tulivyoweza na tumefanikiwa kuyarejesha mapigo ya moyo katika hali yake ya kawaida.Pamoja na hayo ninaomba niwe muwazi kwako kwamba tatizo la John linaonekana ni kubwa tofauti na tulivyokuwa tunafikiria.” Akasema Dr Alex na kuzidi kumuogopesha peniela
“ Dr Alex mmegundua nini kinamsumbua John? Akauliza Peniela
“ Ni mapema sana kutamka chochote kwa sasa hadi hapo uchunguzi wa kina utakapofanyika.Kwa sasa kuna kitu tunahitaji “
“ Kitu gani Alex? Sema chochote “
“ Kutokana na hali ya John ilivyo kwa sasa anatakiwa afanyiwe uchunguzi mkubwa sana katika mfumo wake wote wa fahamu.Kwa vifaa tulivyo navyo hapa zoezi hilo haliwezi kufanikiwa kwa hiyo tunahitaji kupata hospitali yenye vifaa ambavyo tunaweza tukafanya uchunguzi wa kina na kubaini kile kinachomsumbua John hospitali yenye usalama mkubwa kwani matibabu ya John yanatakiwa yawe ni siri kubwa” akasema Dr Alex
“ Hospitali itapatikana bila wasi wasi .Naomba dakika mbili nifanye mawasiliano ” akasema Peniela na kutoka mle chumbani akachukua simu yake na kumpigia daktari mkuu wa hospitali ile kubwa yenye aliyosaidiwa na Dr Joshua na kumtaarifu kwamba angempeleka John muda si mrefu kutokana na hali yake kuzidi kuwa mbaya.Baada ya kuwasiliana akarejea tena chumbani
“ Gari la wagonjwa litafika hapa muda si mrefu kwa hiyo tuanze kumuandaa mgonjwa.Tunampeleka katika hospitali kubwa ambayo huwatibu viongozi wakuu wa serikali na hata rais mwenyewe hutibiwa hapo.Kuna vifaa vyote mnavyovihitaji na hata usalama wake ni mkubwa sana” akasema Peniela
“ Josh gari la wagonjwa litafika hapa muda si mrefu nenda kawasubiri nje uwapokee.Dr Alex,Edwin na Martini tuanze kumuandaa mgonjwa” akaamuru Peniela
Gari la wagonjwa lilifika kwa haraka na John Mwaulaya akachukuliwa na kuwahishwa hospitali.Ndani ya gari hilo walipanda Dr Alex ,Dr Edwin na Martin.Peniela na Josh wao walifuata nyuma kwa gari la Peniela.Mara tu alipofikishwa hospitali John akapokelewa na bila kupoteza muda madaktari wa hospitali ile wakisaidiana na akina Dr Edwin wakaanza taratibu za kumfanyia uchunguzi wa kina .Madaktari katika hospitali ile walijitahidi kwa kila wawezavyo kutoa huduma za kiwango cha juu kwa John wakijua ni ndugu wa rais.
Kwa kuwa hakufahamu uchunguzi ule ungechukua muda gani , Peniela akaamua aondoke akaendelee na majukumu mengine kwani alikuwa na miadi na Anitha .Walipanga waonane ili aweze kumkabidhi vifaa maalum ambavyo vitawasaidia katika kumfuatilia Dr Kigomba.
“ Josh utaendelea kukaa hapa na kufuatilia kila kinachoendelea.mimi ninatoka kidogo nina miadi ya muhimu na mtu.Utanifahamisha kila kinachoendelea hapa” akasema Peniela na kuondoka zake
********
Mathew aliwasili nyumbani kwake akashuka garini na kumkuta jaji Elibariki peke yake sebuleni wakasalimiana
“ Anitha yuko wapi? Akauliza Mathew
“ Aliondoka hapa muda si mrefu na kusema kwamba anakwenda kuonana na Peniela kwa ajili ya kumpatia vifaa vile vya kusaidia kumfuatilia Dr Kigomba.”
“ Ok good.Kuna habari yoyote mpya? Akauliza Mathew
“ Hakuna habari yoyote mpya Mathew.Mimi niko humu ndani na sijui ni kitu gani kinachoendelea huko nje kwa hiyo nategemea sana kupata habari na taarifa toka kwako.Kwema huko utokako? Akauliza jaji Elibariki.Mathew akachukua glasi ya maji akanywa halafu akaketi sofani akavuta pumzi ndefu na kusema
“ Ulikuwa sahihi jaji Elibariki,kuna mambo mengi ambayo Peniela hakuwa akiyafahamu kuhusiana na wazazi wake.John lied to her.Lakini nashukuru leo tumeufahamu ukweli wote.Peniela amefahamu kila kitu kuhusiana na historia ya maisha yake na kuhusu wazazi wake.” Akasema Mathew na kumsimulia jaji Elibariki kila kitu kilichotokea.Hii ilikuwa ni habari iliyomstua sana jaji Elibariki
“ Masikini Peniela.Sipati picha maumivu aliyonayo sasa baada ya kuufahamu ukweli kuhusiana na wazazi wake.Hata mimi nimeumizwa sana na jambo hili. Peniela needs someone to comfort her right now.Huyu John mwaulaya ni shetani mkubwa.Amemuumiza sana mwanamke ninayempenda kwa moyo wangu wote.Hana hata chembe ya ubinadamu huyu mtu na laiti kama ningekuwa karibu yake ningeweza kumfanya jambo lolote baya” akasema jaji Elibariki kwa hasira
“ Ni kweli inauma sana jaji Elibariki.John Mwaulaya ni mtu katili na ameumiza watu wengi sana .Picha ya moto ule mkubwa ukiiteketeza nyumba yangu ambayo ndani yake ilikuwamo familia yangu bado haijafutika kichwani kwangu” akasema Mathew halafu akainuka na kwenda ukutani kulikokuwa na picha kubwa iliyowaonyesha watu wawili mwanamke na mwanaume wakiwa katika tabasamu kubwa.Picha hii ikamkumbusha mbali sana Mathew ,hizi zilikuwa ni siku za furaha alipokuwa na mke wake aliyempenda sana
“ Get ready John.Your days are numbered.Kipimo kile kile ulichokitumia kuiteketeza familia yangu ndicho hicho nitakachokitumia kuhakikisha kwamba unakufa kwa mateso makali sana” akasema Mathew kwa sauti ndogo
“ Kwa hiyo nini kinaendelea hivi sasa Mathew? Huyu John tunamfanya nini? akauliza jaji Elibariki
“ Just relax judge.I’ll handle this ,don’t worry” akajibu Mathew halafu akaelekea katika ofisi yake
“ Sasa ni wakati wa kuufahamu ukweli wa kile kilichomo katika zile nyaraka zilizopoteza uhai wa Edson na wenzake nyaraka ambazo zina thamani ya mabilioni ya fedha.” Akawaza Mathew huku akiiwasha kompyuta yake na kuitafuta barua pepe kutoka kwa Yash.Barua pepe hiyo iliandikwa hivi
“ Mathew,nimechelewa kidogo kurudisha majibu ya kile ulichoniomba nikusaidie kukifanyia uchunguzi.Hii ni kutokana na jambo lenyewe kuwa kubwa tofauti na nilivyokuwa nikilifikiria.Ilinilazimu kuwashirikisha jopo la mabingwa wa sayansi ili kwa pamoja waweze kutambua kilichoandikwa katika zile karatasi.Baada ya uchunguzi wa kina imebainika kwamba kilichoandikwa katika karatasi zile ni kanuni ya kutengeneza kirusi hatari sana ambacho kinaweza kufanya maangamizi makubwa endapo kitatumika kama silaha.Hiki kitu kimetustua sana sote.Wamenihoji sana wakitaka kujua mahala nilikozipata karatasi zile hatari na ni mwanasayansi gani aliyeandika kanuni zile lakini sikuwaeleza chochote kwa kuhofia kuingilia uchunguzi wako lakini Mathew ukae ukijua kwamba yeyote uliyemkuta na karatasi hizi ni mtu hatari sana na lengo lake si zuri hata kidogo.Yeyote uliyemkuta na karatasi hizi anatakiwa ashikiliwe kwa nguvu zote ili aweze kutoa maelezo ya kina kuhusiana na karatasi zile.Nimekuwekea pia viambatanisho kadhaa ili uweze kupata picha halisi ya nini kinaweza kutokea endapo kirusi hicho kikiweza kutengenezwa kwa kutumia kanuni hizo.Mathew jambo hili ni hatari sana kwa usalama wa nchi yako na dunia kwa ujumla kwani sifahamu mtu aliyekuwa na karatasi hizi alikuwa na malengo gani ila ninachokuomba jitahidi kufanya kila kinachowezekana kuzuia kirusi hiki kisitengezwe na kama tayari kimetengenezwa fanya kila uwezavyo kuhakikisha kwamba kinapatikana mahala kilipo kabla ya kuleta maangamizi makubwa.Binafsi niko tayari kukupa msaada wa namna yoyote ile utakaouhitaji muda wowote .Najua kwa sasa uko katika uchunguzi wako na mimi sihitaji kuingilia jambo unalolichunguza ila narudia tena kukuomba kwamba jambo hili ni hatari kwa nchi yako na dunia kwa ujumla kwa hiyo jitahidi kwa kila utakavyoweza kuhakikisha kwamba wale wote wenye lengo ovu hawafanikiwi lengo lao.Ninategemea kupewa tena taarifa nyingine kutoka kwa wanasayansi ambao bado wanaendelea kufanyia uchunguzi kanuni zile kwa kina zaidi na mara tu nikiipokea taarifa hiyo nitakutaarifu mara moja.”
Hivyo ndivyo ilivyosomeka barua pepe ile kutoka kwa Yash kijana anayefanya kazi katika shirika la kijasusi la Israel Mossad .Mathew akairudia tena kwa mara ya pili kuisoma barua pepe ile pamoja na viambatanisho vyake vyote kwa lengo la kuwa na uelewa mpana sana kuhusiana na kile alichokisema Yash .Alipomaliza kusoma akavua shati na kubakiwa na fulana ya ndani,alihisi joto kali
“ Anything wrong Mathew?
Sauti ya jaji Elibariki ikamstua Mathew.Kwa muda wa dakika kadhaa Elibariki alikuwa amesimama mlangoni akimtazama Mathew bila ya yeye kuwa na habari.
“ Ouh ! Elibariki.Karibu” akasema Mathew
“ Nimesimama mlangoni kwa dakika zaidi ya kumi .Akili yako yote umeihamisha katika hicho unachokisoma katika kompyuta yako. Is Eeverything ok Mathew? Akauliza jaji Elibariki.Mathew akamfanyia ishara avute kiti aketi,akamtazama kwa sekunde kadhaa na kusema
“ Eli,kila uchao jambo hili linazidi kuwa kubwa na kuchukua sura mpya.” Akasema Mathew
“ Kazi ya kwanza uliyoniomba nikufanyie ilikuwa ni kuchunguza kuhusiana na kifo cha Edson .Tumekwisha fahamu ni kwa nini Edson aliuawa lakini yameibuka mambo mengine makubwa.Katika uchunguzi huo tumefanikiwa kugundua mambo kadhaa makubwa kiasi cha kutulazimu tuendelee kuyachimba hadi mzizi wake.Tumefanikiwa kuzipata karatasi ambazo zilisababisha kifo cha Edson na wenzake na kama utakumbuka karatasi zile ziliandikwa lugha ya kisayansi kiasi kwamba sote tulishindwa kuelewa nini kilichokuwa kimeandikwa.Ilinilazimu kuomba msaada toka kwa washirika wangu .Ninaye rafiki yangu mmoja anaitwa Yash yeye anafanya kazi katika shirika la ujasusi la Isrel Mossad na ni mtaalamu sana wa masuala ya silaha za kibaolojia.Pamoja na utaalamu wake katika sayansi lakini alishindwa kutambua kilichoandikwa ikamlazimu kuwashirikisha wanasayansi wakubwa.Kwa kushirikiana na jopo la wanasayansi wakubwa wamezifanyia utafiti karatasi zile na kugundua kilichoandikwa na leo hii Yash amenitumia majibu ndiyo maana nilikuwa nimeelekeza akili yangu yote huko nikiisoma taarifa yake.” Akasema Mathew
“ Wow ! That’s good news.Amegundua nini? Akauliza jaji Elibariki.Mathew akavuta pumzi ndefu na kusema
“ Katika uchunguzi wao wamegundua kwamba kilichoandikwa katika karatasi zile ni kanuni za kutengeneza kirusi hatari ambacho kinaweza kusababisha maangamizi makubwa endapo kitatumika kama silaha iwapo kitatua katika mikono isiyo salama.Kwa mujibu wa Yash,kirusi hicho ni hatari mno iwapo tayari kimetengenezwa au kikitengenezwa.” Akasema Mathew
“ Ouh Mungu wangu !!!...” jaji Elibariki akastuka sana.Kikapita kimya kifupi .
“ Kwa taarifa hii ya Yash,tayari tumeanza kupata picha ni kwanini karatasi hizi zilitaka kuuzwa kwa thamani kubwa sana.Kumbuka mtu ambaye anatajwa kutaka kununua karatasi hizi alitaka kuzinunua kwa mabilioni ya fedha.Ilitia shaka kidogo kwa mtu kutaka kununua karatasi kwa fedha nyingi kiasi kile kumbe alifahamu kilichoandikwa katika karatasi hizo.” Akasema Mathew
“ mambo yanazidi kuwa makubwa.Sikutegemea kabisa kama suala hili lingekuwa kubwa kiasi hiki.Ni nani aliyetaka kununua karatasi hizo kwa fedha nyingi kiasi hicho na alitaka kuzipeleka wapi? Do you know him? Akauliza jaji Elibariki
“ Tayari tunamfahamu mtu aliyetaka kuzinunua karatasi hizo.Anaita Habib Soud ni tajiri toka nchini Saudi Arabia.Bado hatujui ni kwa nini alizihitaji karatasi zile na kwa sasa inabidi tumfanyie uchunguzi mkubwa sana huyu mtu ili tufahamu nini hasa lilikuwa lengo lake la kutaka karatasi zile .Yawezekana akawa na mafungamano na makundi ya kigaidi na yawezekana akawa alihitaji karatasi zile kwa ajili ya kutengeneza kirusi ambacho wangekitumia katika mashambulio ya kigaidi.Tutafahamu haya yote baada ya kufanya uchunguzi wa kina.Pamoja na hayo bado kuna maswali ya kujiuliza mfano Ni nani aliyeandika kanuni zile? Ni wazi hazikujiandika zenyewe lazima kuna mtu ambaye aliziandika,kama ni hivyo ni nani basi aliyeandika? Tutanatakiwa tulitafutie majibu swali hili.Pili karatasi zile zilifikaje katika ikulu yetu na kuhifadhiwa pale? Tatu ,kama nyaraka zile zilihifadhiwa ikulu basi ni lazima kuna mtu au watu waliokuwa wakifahamu mahala zilipo na katika hao wachache lazima kuna mmoja wao aliyevujisha siri na kupelekea kuibiwa. Kwa unyeti wake karatasi hizi lazima zilikuwa zikihifadhiwa sehemu ya siri sana ambako si rahisi kwa mtu kama Edson kufahamu kwa hiyo ninapata picha kwamba Edson lazima alielekezwa mahala zilipo na akaziiba.Kama ni hivyo mtu huyo ni nani? Tunatakiwa kumfahamu pia.Kingine kikubwa ambacho tunatakiwa tukifahamu ni je kirusi hicho tayari kimekwisha tengenezwa au bado? Kama tayari kimekwisha tengenezwa kiko wapi? Kama bado lazima tufute kabisa mipango yote ya kukitengeneza kwa kuwatia nguvuni wale wote wanaohusika katika suala hili.Lazima tulichimbe jambo hili hadi mzizi wake na hakuna hata mmoja ambaye anahusika na suala hilo atabaki salama.” Akasema Mathew
“ Mathew nimekosa neno la kusema lakini ni wazi nimestushwa mno na taarifa hii” akasema jaji Elibariki
“ Hii ni taarifa ambayo hata mimi imenistua mno .Wakati ninaisoma taarifa hii mwili ulikuwa unanitetemeka.Sikuamini kama jambo hili linaweza kuwa kubwa kiasi hiki.Hapa nilipo ninahis joto kali sana na ndiyo maana unaniona nimevua hadi shati.Si kwamba nimeogopa ila nimestuka tu kwani ni mara ya kwanza kwa kitu kama hiki kupatikana hapa nchini kwetu.Pamoja na ukubwa wa jambo lenyewe lakini lazima tutalichimba hadi mzizi wake na kuhakikisha tunazizuia njama zote ovu .Tutafahamu karatasi hizi zimetoka wapi, nani kaandika na zilifikaje ikulu na nini lilikuwa lengo la Yule aliyetaka kuzinunua.” Akasema Mathew halafu akasita kidogo na kusema
“ Kuna wazo limenijia.Suala hili haliwezi kuwa na mahusiano na lile suala tunaloendelea kulichunguza kuhusiana na package ambayo Dr Joshua anataka kuiuza? Mpaka sasa hakuna yeyote ambaye anafahamu chochote kuhusiana na kilichomo ndani ya package hiyo .Dr Joshua yuko tayari kufanya chochote kile kuhakikisha kwamba mpango wake unafanikiwa na hii inaonyesha uthamani mkubwa wa package hiyo. Lakini hata hivyo ni mapema sana kusema chochote.Kila kitu kitajulikana baada ya uchunguzi.” Akasema Mathew na kuinama chini akafikiri kwa sekunde kadhaa halafu akasema
“ Katika nyakati hizi ninamkumbuka sana Noah.Alikuwa ni mtu mwenye msaada mkubwa sana kwangu na katika wakati huu angenisaidia sana.” Akasema Mathew
“ Mathew tafadhali usinikumbushe kuhusu Noah.Picha ya usiku ule bado haijafutika haijafutika kichwani kwangu.Kama si yeye tayari ningekwisha kuwa marehemu sasa lakini Noah aliyatoa maisha yake kwa ajili yangu.Nina deni kubwa sana kwake na namna pekee ya kuweza kulipa deni hilo ni kuwapata wale wote waliosababisha kifo chake.I don’t know how I’m going to do this but I promise you we’re in this together.” Akasema jaji Elibariki kwa hisia kali sana.
“ Samahani Elibariki kwa kukukumbusha kuhusu Noah.He was a good guy.Binafsi nimefanya naye kazi kwa muda mrefu and that’s why it’ll take a long time to forget him. Hata hivyo hakijaharibika kitu na tutaifanya kazi hii mpaka mwisho.Niko mimi ,Anitha pamoja na wewe.Tunaweza kuifanya kazi hii.Anitha ni mtu ambaye atatusaidia sana katika suala hili.Ni mtaalamu mkubwa sana wa teknolojia na ni mwepesi sana katika kufikiri na kuchambua mambo.Binafsi ninapokuwa naye katika kazi Fulani basi huwa sifikirii kushindwa hata kidogo katika jambo lolote na hata katika hili nina hakika tutafanikiwa tu” akasema Mathew halafu akachukua simu na kumpigia Anitha
“ Hallow Mathew ,uko wapi? Akauliza Anitha baada ya kupokea simu
“ Tayari nimerejea nyumbani.Wewe uko wapi? Akauliza Mathew
“ Niko njiani ninarejea nyumbani.Nimetoka kuonana na Peniela na tayari nimemkabidhi vile vifaa na jioni ya leo atakapokutana na Dr Kigomba tutaanza kupata kila taarifa toka kwa Dr Kigomba.” Akasema Anitha
“ Good job Anitha.Ninakusubiri hapa nyumbani.Kuna suala zito linalotukabili”
“ Kuna jambo jipya ? akauliza Anitha kwa wasi wasi kidogo
“ Si jipya sana lakini ni mwendelezo wa kile ambacho tumekuwa tunaendelea nacho” akasema Mathew
“ Sawa Mathew .Niko njiani ninakuja sasa hivi” akajibu Anitha na kukata simu
TUKUTANE SEHEMU IJAYO…………………………