Umati mkubwa wa wakazi wa mji wa Mwanza na vitongoji vyake wakiongozwa na viongozi na wafuasi wa Chadema, jana walifurika katika uwanja wa Magomeni Kirumba, kumsikiliza mgombea urais kupitia chama hicho, Dk. Slaa, saa chache baada ya askari polisi wa Kikosi cha Kutuliza Ghasia (FFU) kuwatawanya katika uwanja wa Furahisha, ulioko mjini hapa.
Watu hao walianza kumiminika kama mvua uwanjani hapo, kuanzia saa 7:00 nchana na hadi kufika saa 10:00 jioni, ulifurika kiasi ambacho hakukuwa na nafasi ya mtu kuweza kusimama katika eneo la uwanja huo.
Hali hiyo iliwafanya baadhi ya watu kulazimika kupanda juu ya miti na wengine kusikiliza hotuba ya mgombea huyo wa urais wakiwa wamesimama eneo la mbali ya uwanja huo.
Hata hivyo, wakati hali ikiwa hivyo, hakukuwa na ulinzi wa polisi, baada ya askari wa jeshi hilo kushindwa kukaribia eneo la mkutano kwa ajili ya kuweka ulinzi kama ilivyo kwaida.
Hali hiyo ilizua hofu kubwa muda wote wa mkutano juu ya usalama wa watu waliokuwapo uwanjani hapo.
Kutokana na hali hiyo, Mratibu wa Kampeni za Dk. Slaa, Suzan Kiwanga, aliwataka walinzi wa chama kuimarisha ulinzi.
Dk. Slaa aliwasili uwanjani hapo saa 11:52 jioni na kushangiliwa kwa sauti kubwa na umati wa watu waliofurika.
Mara baada ya kuwasili na kushuhudia umati huo, Dk. Slaa alishindwa kujizuia na kujikuta akitamka: Kwa wingi huu mnanifanya nitokwe na machozi.
Aliwashukuru wananchi hao kwa mahudhurio makubwa waliyoyaonyesha kwake na kusema: Kwa mapenzi mliyonionyesha nitawatumikia kwa uaminifu.
Aidha, aliwapa pole watu waliojeruhiwa katika mashambulizi ya mabomu ya kutoa machozi yaliyofanywa na FFU katika uwanja wa Furahisha.
Akihutubia mkutano huo, Dk. Slaa alisema katika kufanya maamuzi magumu kuhusu kufuta kodi ya serikali katika vifaa vya ujenzi, hatatazama nchi za Afrika Mashariki, kama anavyotaka Waziri wa Ushirikiano wa Afrika Mashriki, Dk. Diodurus Kamala kwa vile maamuzi atakayochukua ni kwa ajili ya maslahi ya Watanzania.
Nasema sitakuwa na woga katika kufanya maamuzi kwa ajili ya maslahi ya Watanzania, alisema Dk. Slaa.
Nipashe