UMOJA, UHURU, UADILIFU
Qauli ya Umoja wa Wazalendo
Kukhusu Maelezo ya Mhishimiwa Waziri Mkuu
Bwana Pinda juu ya huu wenyekuitwa muungano
Kwa hishima tunaleta hapa yale yalioandikwa kwenye gazeti la MWANANCHI la Ijumaa, taarikh 24 July, 2009 kukhusu maelezo ya Mhishimiwa Waziri Mkuu, Bwana Mizengo Pinda juu ya huu wenyekuitwa muungano. Maelezo yetu, sisi Umoja wa Wazalendo; tumeyabainisha kwa khati za italic.
Pinda: Vunjeni tu Muungano muone
ASEMA UKIVUNJIKA UPANDE MMOJA UTASAGA MENO
Habel Chidawali, Dodoma
WAZIRI Mkuu Mizengo Pinda ameonya uwezekano wa Muungano kati ya Tanzania Bara na Zanzibar kuvunjika endapo malumbano kuhusu gesi asilia na mafuta yalioanza sasa yataendelea na kuonya kwamba baada ya hatua hiyo upande mmoja utapata shida. Wazee wetu wanasema: Aliezama hachelei kutota. Sisi Wazanzibari kwa hivi kuvamiwa Dola yetu ya Zanzibar siku ile ya Januari 11, 1964 na kutiwa chini ya ukoloni wa Tanganyika; siku ile ya April 24, 1964 ni kupotezewa kila chetu, ndipo tulipozamishwa; kwahivyobasi sisi Wazanzibari si wenye kuchelea kutota, madhali tushazama.
Pinda alitoa onyo hilo bungeni jana, wakati tayari viongozi wawili wa ngazi ya juu ya Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar (SMZ) walishatoa msimamo rasmi wa kutaka suala la mafuta na gesi asilia liondolewe katika orodha ya mambo ya Muungano. Si suala la kutaka lifanywe, ni suala lenye kutekelezwa.
Viongozi hao ni Waziri wa Maji, Ujenzi, Nishati na Ardhi, Mansour Yusuf Himid ambaye alitoa msimamo wake wakati akiwasilisha makadirio ya mapato na matumizi ya bajeti ya wizara hiyo kwa mwaka 2009/2010 katika Baraza la Wawakilishi Mjini Zanzibar. Inapasa ifahamike kwamba huu si msimamo wa Mhishimiwa Mansor binafasi yake, huu ni msimamo rasmi wa Sirikali ya Zanzibar uliokubaliwa na Baraza la Wawakilishi na Baraza la Mawaziri na kutolewa na yeye Mhishimiwa Mansour kwa vile hili suala linakhusiana na wizara yake. Wazanzibari kwa khatuwa ya kuthibitisha huu msimamo wa Sirikali ya Zanzibar, na msimamo wa Wazanzibari wote kwa jumla ndio ikapangwa kufanywa maandamano kuungamkono suala hili. Maandamano haya yalikuwa yahudhuriwe na Wazanzibari kutoka kila pembe, mashamba na mjini. Inaaminika na wengi kwamba ni amri ya Bara ndio kuzuiliwa maandamano haya, wakikhofia kudhihiri mshikamano wa Wazanzibari katika kuhami haki na milki zao.
Naye Naib Waziri Kiongozi Zanzibar, Ali Shamhuna, amewahi kutoa kauli kama hiyo akidai kuwa suala la mafuta ni la Zanzibar peke yake, Bara hawahusiki nalo. Hapana shaka mali ya Zanzibar ni kwa Wazanzibari.
Pinda alitaka Watanzania kuangalia jambo hili ili kujua nani ataathirika zaidi endapo jambo hilo litafanyika. Wazanzibari kimsingi hawaoni kuwepo nguvu za hoja katika kulizingatia suala hili katika hoja ya kuathirika kwa kuvunjika huu wenyekuitwa muungano. Hoja yetu ni kama tulivyoeleza hapo juu, yaani; aliezama hachelei kutota. Kurejea Dola Huru ya Zanzibar ni haki ya maumbile.
Alisema hayo alipokuwa akijibu swali la Mbunge wa Nzega, Lukas Selelii aliyetaka kujua sababu za viongozi wa juu akiwamo Rais Jakaya Kikwete kuwa kimya kuhusu jambo hilo ambalo linaonekana kuuweka Muungano katika hali tete. Akijibu swali hilo, Pinda wakati akijibu maswali ya papo kwa hapo bungeni jana, alieleza wasiwasi wake kuhusu jambo hilo akisema kuwa likitokea lazima kuna upande ambao utaathirika, bila ya kutaja ni upande gani. Kama kuna uwezekano jambo la mafuta na gesi asilia kuondolewa katika Katiba ya Muungano ambako liliingizwa mwaka 1968 itakuwa ni jambo la heri, lakini sio kuvunja Muungano, alisema Inapasa ifahamike kwamba kulingana na misingi ya Umoja wa Wazalendo, suala la mafuta na jengine lolote lile lenye kukhusiana na huu wenyekuitwa muungano ni matawi ya mti uliooza, kwahivyobasi; madhali mti umeoza haitarajiwi matawi kuwa na uhai. Vilevile, ni imani ya Umoja wa Wazalendo kwamba linalojengeka juu ya haramu ni haramu, hivi ni kwamba huu wenyekuitwa muungano umejengeka juu ya haramu haramu ya kuvamiwa Dola huru ya Zanzibar kwahivyobasi; kila lenye kujengeka juu ya huu wenyekuitwa muungano ni haramu. na kuongeza: Tumekuwa tukipata tabu sana na kusumbuliwa na kauli zinazotolewa na baadhi ya wenzetu. Mara tunaambiwa kuwa ni wezi wa mchana, wakati mwingine tunaambiwa kuwa ni wakoloni
. Suala la kuambiwa Tanganyika ni wakoloni wa Zanzibar hilo halina shaka, ni ndivyo kabisa. Si tu ni wakoloni, bali ni wavamizi wa Dola huru ya Zanzibar, ni wakoloni kuliko wakoloni Waingereza walioondoka. Wakati wa wakoloni Waingereza Zanzibar iliendelea kuwa Dola Kaamili, lakini kwa ukoloni wa Tanganyika imepotezwa Dola ya Zanzibar kwa huu wenyekuitwa muungano. Kheri ya mkoloni Muingereza kuliko mkoloni Tanganyika. Ahaa jambo hili linanisikitisha sana
., ipo siku muungano utavunjika na ikifika hatua hiyo, nina hakika upande mmoja wa muungano utaathirika. Ilipovimiwa Dola ya Zanzibar, ilikuwa na kila uwezo na nguvu kamili za kidola; haikuwa masikini au faqiri wa lolote lile. Zanzibar juu ya kuwa imedhiliwa na kufukarishwa katika hiki kipindi cha miaka arubaini na tano ya utawala wa Tanganyika, mpaka leo Zanzibar inao uwezo kaamili wa kujiendesha katika hali ya salama, amani na kila mafanikio na maendeleo, muhimu ni kutoka chini ya huu ukoloni wa Tanganyika na kurejea kuwa Dola Huru Kaamili kama ilivyokuwa kabla ya huu wenyekuitwa muungano.
Katika swali lake Selelii alimtaka Waziri Mkuu aeleze ukimya wa viongozi wa juu akiwemo Rais wa Jamhuri pamoja na Rais wa Zanzibar kuhusu jambo la mafuta ambalo linaonekana kuuweka Muungano katika hali tete. Zanzibar, wananchi na Sirikali yao, suala hili la mafuta wamelibainisha wazi kabisa kama vile ilivyoelezwa na Mhishimiwa Mansour katika Baraza la Wawakilishi (Bunge la Zanzibar). Mheshimiwa Waziri Mkuu, kumekuwa na maneno ambayo yanaonekana kuuchokonoa Muungano kutoka kwa baadhi ya wabunge pamoja na Baraza la Mapinduzi Zanzibar ambapo sote tuliapa kuulinda na Katiba yake; lakini viongozi wa juu mmekuwa kimya sana, hamuoni kuwa hivi ni viashiria vya kuvunja Muungano?alihoji Selelii. Kama tulivyosema hapo juu, na tunavyosema daima; kwamba lenye kujengeka juu ya haramu ni haramu, kwahivyobasi, kuapa kulinda haramu ni haramu; kwahivyobasi, kiapo hiki ni haramu.
Akijibu swali hilo, Pinda alitumia baadhi ya maneno ambayo yalitolewa katika hotuba ya Rais Jakaya Kikwete Juni 26, mwaka huu akisema: Hata rais alishasema na kukemea juu ya jambo hilo. Pinda aliongeza: Rais alishasema kuwa mafuta hayajapatikana na huenda yasipatikane kabisa. Ikiwa hii ndio hali, basi kwa nini mayowe yote haya? Kiongozi wa nchi alionya juu ya malumbano hayo na kuagiza kuwa yaachwe mara moja. Alifafanua kuwa ilishaundwa tume ya wataalamu kutoka nje ili kuangalia uwezekano wa namna bora ya kuzishauri serikali mbili juu ya kugawana pato litakalotokana na mafuta na kwamba, tume ilishawasilisha taarifa yake ndani ya serikali tangu Juni 23 mwaka huu. Alisema tume iliyoundwa ambayo iko chini ya ofisi ya Makamu wa Rais inafanya utaratibu mzuri wa kuangalia masilahi kwa pande zote mbili ndani ya Muungano ili kutoa nafasi sawa. Imeshaundwa tume ya wataalamu kuzishauri sirikali mbili juu ya kugawana pato litakalotokana na mafuta. Maelezo haya ni kinyume kabisa na maelezo hayo hapo juu kuwa mafuta huenda yasipatikane kabisa.
Hata hivyo, akijibu swali lingine lililohusu Muungano, Waziri Mkuu alionekana kuwa na hasira baada ya kujibu swali lililohusu Katiba ya Muungano ambalo alilijibu kwa mkato tena kwa hasira. Mhishimiwa Waziri Mkuu, hasira hizi ni za nini? Kwa nini kuwacha nguvu za hoja na kuingia kwenye hoja za nguvu, yaani vitisho na hasira? Swali hilo liliulizwa na Yahya Issa mbunge wa Chwaka (CCM) aliyetakakujua juu ya Zanzibar kuingizwa katika ushirikiano wa Kimataifa. Issa alisema kuwa kutokuingizwa Zanzibar katika ushirikiano wa Kimataifa ni njia moja wapo ya kuinyanyasa Zanzibar kwa kuwa jambo hilo halipo ndani ya Katiba, hivyo upande huo wa pili wa nchi ni kama unakandamizwa. Akijibu swali hilo, Pinda alisema Katiba ya Muungano ndio mwakilishi wa nchi ya Zanzibar pia, hivyo upande huo wa pili wa Zanzibar utaendelea kuwakilishwa na Waziri wa Ushirikiano wa Kimataifa siku zote. Mkitaka mjaribu muone kama kuna urahisi katika jambo hilo,alijibu Pinda kwa mkato. Mhishimiwa Waziri Mkuu, hapana shaka ni vyema kutumia busara katika utekelezaji wa dhamana; inatarajiwa mfano mwema.
Wakati huo huo, Kiongozi wa kambi ya upinzani bungeni, Hamad Rashid Mohamed amepinga majibu ya Pinda, akidai kuwa chokochoko za Muungano zilianza tangu wakati wa hayati Karume na Mwalimu Nyerere. Kwa hakika si chokochoko, bali ni madai ya Wazanzibari ya kutaka kurejea Dola Huru Kaamili ya Zanzibar na kutokana na ukoloni wa Tanganyika. Alisema katiba ya Muungano ndiyo kikwazo kikubwa kwa kuwa iliongezwa vipengele ambavyo havikuwepo awali. Mzizi wa ukoloni huu wa Tanganyika juu ya Zanzibar ni zile Articles of Union, 1964, ambazo zimeipoteza Dola Huru ya Zanzibar kwa kisingizio cha huu wenyekuitwa muungano. Kuongezwa kwa vipengele hivyo kulitokana na Katiba ya muda ambayo ilikuwa imepanga kuwa kabla ya mwaka kumalizika, baada ya muungano, kuwe na katiba ya kudumu, lakini haikutekelezwa badala yake ikakamilishwa baada ya miaka saba, alisema Rashidi. Aliyataja mambo yaliyoongezwa katika kipindi hicho kuwa ni pamoja na suala la mafuta ambalo mwanzo halikuwepo.
Aliongeza kuwa jambo lingine linaloyumbisha Muungano ni pamoja na kuondolewa kwa wadhifa wa Rais wa Zanzibar katika nafasi ya makamu wa rais wa Muungano. Alisema hakuna usawa wa kimasilahi kwa nchi hizo mbili kutokana na upande mmoja kupata masilahi zaidi ya upande wa pili.
Sio kupata maslahi zaidi, bali ni kujipa maslahi zaidi. Umoja wa Wazalendo unasisitiza juu ya msingi wa imani yake, kwamba kilichojengeka juu ya haramu ni haramu. Katika msingi hii, na kupotezwa Dola ya Zanzibar ndio Umoja wa Wazalendo kuendelea kuwania kwa kila njia na hali za amani kurejea Dola Huru Kaamili ya Zanzibar kama ilivyokuwa kabla ya huu wenyekuitwa muungano.
Tunamuomba Mwenyezi Mungu Mtukufu, Subhaanahu wa Taáala atujaalie kila kheri na atuepushe na kila shari, Aamyn.
Wa Billahi Tawfiiq
Umoja wa Wazalendo
Zanzibar
July 24, 2009