Damaso
JF-Expert Member
- Jul 18, 2018
- 3,978
- 6,739
Ni asubuhi umeamka zako na unajiandaa kwa ajili ya kwenda kazini ila ghafla unasikia sauti yenye ukali mlangoni kwako ikikutaka utoke nje, unaamua kufungua unakutana na mtu ambaye amevaa jeans na jezi ya Man United pamoja na kofia nyeusi ya New York. Anajitambulisha kuwa yeye ni afisa wa Polisi kutoka Kituo cha jirani hapo na hana hata kitambulisho na anahitaji uongozane naye muende kituo kwa sababu kuna kesi anahitaji kukuhoji.
Ile unamuelekeza kuwa akusubirie upate kuweka mambo sawa, huyu mtu anayedai kuwa ni polisi anachomoa pocket knife na kukutishia kuwa unataka uondoke naye. Najiuliza kama ni wewe utakubali kuondoka naye au utamfundisha na kujilinda kikatiba? Binafsi atachagua anipeleke huko akanihoji nikiwa maiti au yeye abakie maiti ndani kwangu.
Hakuna ambaye kwa sasa ana imani tena na jeshi la Polisi wala huruma, matendo ya maafisa hawa yamefanya jamii iwaone watu wa tofauti kabsa, sio kwa ubaya ila wanafuata maagizo ambayo mengine sio maagizo yenye maana za msingi kabsa. Polisi na akili zako timamu kabsa unamshambulia kwa silaha mtu ambaye hana wembe wala pini? Na unasema kuwa unatuliza ghasia?
Kuna baadhi ya maagizo yamekuwa yakiwafanya watu ndani ya jamii wawe na mioyo migumu. Jambo baya kama vifo au ulemavu kwa afisa wa polisi basi ni sherehe kubwa sana kwa wananchi na wanamshukuru Mungu.
Nikupe mfano, Umetoka usiku kwenye starehe zako ukaona Askari polisi amevamiwa na kupigwa na vibaka kisha kuwekwa kwenye kichaka akiwa hoi bin taabani, ukimtazama yule askari unamfahamu vyema kabsa na ni moja ya wale maaskari wababe, SWALI, je utatoa msaada wa kumsaidia na kutoa taarifa kwenye kituo cha polisi kuwa kuna askari amekutana na vibaka na kujeruhiwa?
Je wakikugeuzia kibao kwamba wewe ni mmoja wa wale vijana waliomjeruhi askari wao, ni nani atakusaidia? Nafahamu kwa hali ilivyo, watu wengi watamuacha pale pale huyo askari yeye na Mungu wake.
Maafisa usalama nao ni watu ambao tunaishi nao ndani ya jamii, tunaishi na wazazi wao, watoto wao na ndugu zao, tunakwenda kwenye sherehe zao za harusi, vipaimara, send off, lakini pia tunahusika kwenye kuwafariji kwenye misiba na nyakati ngumu kama ugonjwa au ulemavu, ni moja ya sehemu ya jamii yetu tunaishi nao.
Ila ajabu, wanajisahau sana na kuona wao wapo mbingu tofauti na ile ambayo tunaishi sisi, wanaishi kana kwamba wao sio sehemu ya jamii kabsa. Hivi huwa wanakwenda Makanisani na misikitini kweli au ndo wapagani!? Jumapili mnakwenda kanisani kufanya nini, Ijumaa mnakwenda kufanya nini?
Sio kitu kizuri kusikia kuwa askari fulani nyumba yake imepata hitilafu ya umeme na kutetekea huku majirani wakikataa kutoa msaada wa kuzima moto, kiubinadamu ni suala ambalo sio jema ila kwa upande mwingine mioyo ya watu hujisikia vizuri wakiona askari na maafisa usalama wakipata uchungu sawia na ule wanaoupata wananchi na familia zao.
Rai yangu, IGP pamoja na wasaidizi wako na maafisa polisi wafundishe kuwa na utu haswa linapokuja suala la kuishi na wanajamii. Andaeni semina na warsha mbalimbali na waalikeni wataalamu wa saikolojia wapate kuwafundisha maaskari kuwa jamii wanaoishi inajifunza kuhusu matendo yao, wakumbushe kuwa “Muosha ipo siku ataoshwa”, leo wanafurahi kuona maumivu ya wanafamilia wa Savita ila wakisikia vijana wao wamekutana na kadhia hii ya Savita, basi watahuzunika sana.
Mkitaka kufahamu kuwa wananchi kwa sasa hawana tena huruma wala mioyo ya huzuni kwenye misiba, tazama taarifa kuhusu askari wa Kikosi cha Valantia (KVZ) Haji Machano Mohamed, ukitembelea ukurasa wa Facebook wa Millard Ayo pamoja na Ukurasa wa EATV, utakutana na comments za watu zikisifia kabsa na kuridhika kusikia taarifa za mtu kupoteza maisha. Taarifa za kifo cha A/INSP Eliuterius Hyera, ambaye alikuwa Mkuu wa Kituo Kidogo cha Polisi Chiungutwa wilayani Masasi Mkoani Mtwara.
Yaani ukitegemea kukutana na jumbe za watu za pole ndo kwanza watu wanashukuru kuona kumbe na Maafisa Polisi nao wanaweza kupoteza maisha. Yaani tunategemea kuona watu wakitoa pole ila ndo kwanza unakutana na nukuu ya kauli ya Rais Samia kuwa Kifo ni Kifo tu.
Hivi kweli tumepoteza utu kiasi cha kwamba Polisi wanaona ni sawa kupoteza maisha ya mtu ili tu wapate kuonekana wanachapa kazi kwa kiongozi fulani? Yaani maisha ya Akwilina yalikuwa ni sadaka kwa askari ambao walipokea maagizo kutoka kwa Kamanda Lazaro Mambosasa? Hivi Biswalo Mganga unajisikiaje ulipoamua kufunga jalada la kesi ya Akwilina kwa kigezo cha Jeshi la Polisi linapotumia nguvu kuzuia maandamano au vurugu na kusababisha mauaji, haliwezi kushtakiwa.
Familia yako inakuchukuliaje ukiwa kama Baba na kuamua kuzima kesi ya binti ambaye kwao walimtazama kama sehemu ya msingi wa familia. Yaani polisi sita ambao walikuwa wanatakiwa wahojiwe, wewe Biswalo Mganga kwa utashi wako tu ukaamua kufunga jalada la kesi na kuwaeleza wananchi kauli isiyo na mashiko. Shame on you Biswalo Mganga na Lazaro Mambosasa.
Maafisa polisi kumbukeni mnaishi na watu, na wanawatazama ipo siku ingawa siombei lakini mtaanza kuona kuna mikosi na vifo vya ajabu ndani ya familia zenu, msianze kuuliza fahamu kuwa nature ya maisha huwa haidanganyi, law of nature ipo kazini ikishirikiana na karma. Kama watu watashindwa kuwashughulikia na kuwaonesha namna nzuri ya maisha ipo siku mtakutana na vitu vizito.
Maagizo yapo ila fahamuni kuwa mnaishi na watu, sabuni, chumvi na vocha utaenda kununua kwa Mangi, Ukipata hitilafu ya umeme utamuita Side akusaidie, septic tank limejaa maji machafu utamuita Eze pamoja na wenzake waje kukusaidia kuzibua.
MAISHA NI KUSAIDIANA PAMOJA NA KUISHI KWA WEMA! JIFUNZENI WEMA!