Polisi nchini Uganda wamesema wamemkamata mwanaharakati maarufu wa haki za binadamu, hatua inayokuja wakati serikali ya Rais wa muda mrefu Yoweri Museveni ikiendelea kuimarisha ukandamizaji dhidi ya wapinzani na sauti za upinzani, kuelekea uchaguzi mkuu wa Januari 15, 2026
Kukamatwa kwa Sarah Bireete, mkuu wa shirika la haki za binadamu na mchambuzi wa mara kwa mara wa masuala ya serikali kwenye redio na televisheni za ndani, kumethibitishwa na polisi kupitia chapisho kwenye mtandao wa kijamii wa X siku ya Jumanne. Polisi walisema, “Yupo chini ya ulinzi wa polisi. Atapandishwa kizimbani kwa wakati muafaka,” bila kueleza ni lini atafikishwa mahakamani au mashtaka anayokabiliwa nayo.
Bireete ni mwanasheria na Mkurugenzi Mtendaji wa Kituo cha Utawala wa Kikatiba (Centre for Constitutional Governance – CCG). Amekuwa akiikosoa serikali mara kwa mara kuhusu masuala mbalimbali, ikiwemo madai ya upinzani juu ya kukamatwa kinyume cha sheria na mateso dhidi ya wafuasi wao.
Jitihada za kuwasiliana na CCG kwa ajili ya maoni hazikufanikiwa mara moja.
Uchaguzi wa Januari unamkutanisha Rais Museveni, mwenye umri wa miaka 81 na aliyeko madarakani tangu mwaka 1986, dhidi ya msanii wa muziki aliyegeuka mwanasiasa, Bobi Wine.
Bobi Wine, 43, pamoja na chama chake cha National Unity Platform (NUP), wanasema mamia ya wanachama wao wamekamatwa mwaka huu, wakiwemo waliokamatwa wakati wa kampeni. Wanasema hatua hizo zinalenga kuwatisha wafuasi wao na kudhoofisha morali ya chama.
Mwezi uliopita, Kamishna Mkuu wa Umoja wa Mataifa wa Haki za Binadamu, Volker Türk, pia alilaani kile alichokitaja kuwa “kuongezeka kwa ukandamizaji” dhidi ya upinzani nchini Uganda, akisema kuwa angalau wafuasi 550 wa NUP walikuwa wamekamatwa mwaka huu.
Source: Reuters