SoC01 Ponografia na Vijana

SoC01 Ponografia na Vijana

Stories of Change - 2021 Competition

Bdt

New Member
Joined
Jul 30, 2021
Posts
2
Reaction score
3
Kwa kawaida ponografia si jambo geni kwa mtu yeyote mwenye uwezo wa kuingia mtandaoni mara kwa mara lakini kwa ufupi, ponografia ni uwakilishi wa ngono kwa njia ya picha, vitabu, vinyago, sanamu pia na video ambao una nia ya kuchochea hisia za kimapenzi kwa mtumiaji.

Aina ya ponografia ambayo ni maarufu sana kwetu ni ile ya vitabu na video, ambapo mwanzoni ilikua ni rahisi kumtambua mtu ambae anaangalia video za ngono kwa sababu zilikua zipo kwenye mfumo wa diski ndogo(CD), lakini siku hizi sio rahisi kabisa kumtambua mtu ambae anaangalia video za ngono kwani mambo yamerahisishwa, mtu yeyote mwenye kifaa cha mawasiliano chenye uwezo wa kuingia mtandaoni bila kujali umri anaweza kujikuta amekuwa mraibu wa video za ngono al maarufu kama X-videos.

Vijana wengi ambao ndio wapo kwenye hatua ya kubalehe, ambao wengi wao ni wanafunzi na wenye uwezo wa kumiliki simu zenye uwezo wa intaneti, hujaribu kutafuta majibu ya maswali yao kuhusu tendo la ndoa katika simu zao na mwisho hujikuta wanaangalia video za ngono na kuwa waraibu, na ubaya ni kwamba wakishaona hilo limeshakua ni tatizo na wanapojaribu kuomba msaada kwa marafiki zao ambao nao wapo kwenye umri huohuo wa kubalehe huishia kupata majibu kwamba hilo ni jambo la kawaida na ikifika muda litaisha bila hata kuwapa njia ya kujiondoa kwenye tatizo hilo.

Na hata hivyo hili huwa halionekani kuwa kama ni tatizo ambalo linawakumba vijana wengi kwani,
1/ watu hawa huangalia video hizo kwa usiri mkubwa na huwa wanafahamu jinsi ya kufuta na kuficha ushahidi.
2/ Hata wakijulikana huonekana tuu ni la kawaida na ni moja ya mambo katika hatua za ukuaji na ikifika wakati atajielewa na kuacha.
3/watu hawajui kuwa kuna matokeo hasi ya kuwa muangaliaji hodari wa video za ngono na huona tuu ni njia mojawapo ya kujifurahisha.

William struthers (profesa wa saikolojia kutoka marekani) amewahi kusema kuwa "ponografia inadhuru ufanyaji kazi wa ubongo wa mwanadamu na ina madhara endelevu kwenye kufikiri na maisha kiujumla". Pia Dokta Trish Leigh (mwanasayansi wa neva) baada ya tafiti zake alikuja kusema "Ponografia inaathiri mtu anavyoyatatua matatizo yake".Na ukweli ni kwamba hawa wote sio waafrika na tafiti zao hawakuzifanyia huku kwetu lakini hii haimaanishi kwamba majibu waliyokuja nayo hayana ukweli kwetu kwani japo tunatofauti kubwa sana lakini mifumo ya miili yetu wote ni sawaa.

DOPAMINE

Kitu chochote ambacho kinasababisha mtu kuwa mraibu hucheza na dopamine na huirubuni na kuifanya iwe silaha ya kumuangusha mhusika bila hata yeye kujitambua.

Kwa uchache dopamine (ambayo hupatikana kwenye sehemu inayotambulika kama reward centre kwenye ubongo) ni kama kemikali ambayo huachiliwa kwenye ubongo ili kuupa mwili hamu ya kufanya vitu ambavyo ubongo hudhani kwamba vina faida kwa maendeleo ya mwili au huwa vinamridhisha tu mhusika kila anapovifanya mfano kula, kucheza, kusoma vitabu, kuangalia filamu, kufanya mapenzi, kunywa pombe na hata kuangalia video za ngono.

Tuchukulie mfano wa mtu mwenye njaa, mtu akiwa na njaa dopamine ambayo inakua imeachiliwa kwa muda huo huwa ni ya kiwango cha juu na hii humsukuma mtu kutafuta chakula akiwa na hamu kubwa, Iwapo mtu huyu atasikia harufu nzuri ya chakula dopamine yake itaongezeka na kumpa hamu maradufu, atakapopata chakula na kuanza kula hamu yake hupungua na hata kuisha. Lakini kuna uwezekano kwamba mtu huyu huyu ambaye kwa sasa amesharidhika kula akipewa chakula kingine au kitu kingine chochote cha kula ambacho ni pendwa kwake atakula tena japo si kama ambavyo alikula mwanzo. Na hii ni kwa sababu dopamine hupenda vitu vipya na huupa mwili hali ya kutegemea matokeo mapya na mazuri zaidi hivyo huachiliwa tena ili kumpa tena hamu mhusika.

Dopamine hiihii hufanya kazi kwenye ponografia kama inavyofanya kazi mtu akiwa na njaa, na pia humfanya muangaliaji atoke video ya kwanza na kwenda ya pili na kuendelea kwa sababu dopamine inaendelea kuachiliwa ikimfanya mtu ategemee matokeo tofauti ma mazuri zaidi ambayo yatamfurahisha mhusika kwa muda huo.

Ni kama vile dopamine huuambia ubongo hiki unachokifanya ni kizuri kwa sababu kinakupa raha kila unapokifanya, na ubongo (ambao hauoni tofauti ya matokeo ya kujiburudisha mwenyewe kihisia kwa kuangalia video na kufanya mapenzi) hulikumbuka jambo hilo ukishilikiana na glutamate, na kulipendekeza jambo hilo iwapo tu mhusika atakuwa peke yake au ameona jambo linalohusiana na ngono katika kuishi kwake, hata kama lina madhara mbeleni na hutoa sababu ya ushawishi ili kulifanya (mfano si leo tuu, leo ndio mwisho, sio dhambi kwa sababu najiridhisha mwenyewe, nikiamua nitaacha sijaamua bado) hata kama kuna shaka (mfano sio vizuri au ni dhambi) na hapo ndipo uraibu wa video za ngono unapoanzia.

Sasa mtu anaeangalia video za ngono kwa muda mrefu huchechemua sana hiyo reward system na mwisho wake ili apate raha ile aliyokua anaipata mwanzo basi itambidi aangalie video nyingi zaidi na zenye utofauti na pengine zenye kutumia mabavu.(Na ndio maana mwisho wake wengi wao hujikuta wakiangalia video za kwenda mtungoni na za ubakaji).

Matokeo
(Matokeo ambayo yanaelezwa hapa chini mengi ni yale ambayo huwakuta vijana ambao ndio kwanza ni wanafunzi hasa wa elimu za sekondari ambao hawana wenza na hata kama wanao hawawezi kushiriki nao tendo na huwa na hofu ya kuweka wazi kwa watu wao wa karibu na hivyo kubaki nalo mioyoni mwao tuu)

1/Kukosa uvumilivu hasa kwenye mambo ambayo yanachukua muda kufanikiwa.Mara nyingi wanapofanya jambo wanategemea lifanikiwe hata kama wamelifanya kwa muda mfupi tuu na hii inaweza kuwa hata kwenye masomo yao kwani wanategemea wafaulu iwapi wamewekeza nguvu kidogo sana. Na hii ni kwasababu ameshazoesha ubongo kupokea raha kwa kutumia nguvu kidogo, kutafuta tuu video mtandaoni wakati kiuhalisia tendo hili huchukua hatua kadhaa(kumpata mtu, kumfahamu, kuanza nae mahusiano, kukubaliana kuhusu tendo na kulifanya).

2/Viungo vya uzazi kutofanya kazi kiukamilifu wakati wa tendo. Sababu mojawapo ya jambo hili ni video za ngono kwani mhusika anakuwa ameshazoea kujiridhisha kihisia anapoona miili na staili ambazo kiuhalisia ni vigumu kupata mtu wa aina ile na manjonjo ya video za ngono ni tofauti na kile anachokiona mbele yake hivyo inakuwa vigumu kwa mtu huyu kuchechuka.

3/Mawazo na huzuni. Hii itatokea pale ambapo mtu huyu atajaribu kuachana na mambo ya video za ngono lakini bado anajikuta anashindwa kujizuia na kuangalia tena na tena.

4/Ufanyaji kazi wa mhusika huwa ni wa hali ya chini kwa sababu anashindwa kuwa makini kwenye kazi kwani ubongo wake umejaa ngono tuu na huzifikilia hata mahali ambapo hazihitajiki.

5/Kutoridhika na baadhi ya saizi ya viungo vyao au wenza wao mfano makalio, uume au matiti.

6/Kutojiamini kwenye mambo kadhaa hata kwenye tendo lenyewe kwani hujaribu kujifananisha na wale aliowaona kwenye video bila kufikiri kuwa wengine ile ni kazi yao hivyo wanapaswa kuwa wabunifu ipasavyo ili wapate madili mengine.

7/Kupoteza muda na

8/ Kupungua kwa uwezo wa kukumbuka. Silaha mojawapo itakayomfanya mwanafunzi afaulu akiwa shuleni ni uwezo wake wa kukumbuka hivyo basi, kama kuna ambaye anaichezea silaha yake hii anaweza pia kushindwa kuendelea na masomo.

9/ Kuhalalisha vitu ambavyo si halali. Mahusiano kadhaa yapo kwenye mzozo kwani kuna vitu ambavyo mwenza huwa anatamani avipate kutoka kwa mwenzie ambavyo si halali kidini wala kisayansi lakini anatamani avifanye kwa sababu labda ameona kwenye video zake kuwa ni raha sana kulifanya au kasimuliwa (mfano kwenda mtungoni),hili pia linaweza kuwa moja ya tokea la video za ngono kwani jambo likishakuwa ni halali na la kuvutia kwenye kichwa cha mtu ni rahisi sana kulifanya kwenye dunia ya kawaida na kushawishi wengine pia walifanye bila kujali madhara kwake au kwa mwenza wake.

CHA KUFANYA ILI KUACHANA NA VIDEO ZA NGONO NA PONOGRAFIA KIUJUMLA

Mtu hatofahamu kuwa amekuwa mraibu wa video za ngono mpaka pale atakapoamua kwamba hatoangalia tena, lakini akajikuta bado anaendelea kudumbukia kwenye shimo lilelile.

Zifuatazo ni njia ambazo zinaweza kumsaidia mtu ambae anapambana kuachana na ponografia:

-Mhusika atafute sababu ambayo itamfanya aache kufikilia kuangalia video za ngono iwapo wazo hilo litamjia kwa mfano labda kuna adhabu za kidini au hata tokeo la video za ngono ambalo hataki tena kulipitia.

-Kama kuna chochote ambacho kinahusu ponografia ambacho kimewahi kuhifadhiwa kwenye kifaa cha mawasiliano cha mhusika kinatakiwa kifutwe.

-Vishawishi ambavyo humfanya mhusika arudi kuangalia video za ngono vinatakiwa vitambuliwe na vidhibitiwe mfano kujitenge na kuangalia picha za nusu utupu

-Mhusika awe wazi, amshirikishe mtu ambae atakua na busara ya kumsikiliza na kujaribu kumsaidia na hata kama hatopokea msaada basi atakua ametua sehemu ya mzigo.

-Ule muda ambao mara nyingi mhusika hujikuta akiangalia video za ngono utafutiwe ratiba nyingine na ijulikane kabla ya muda huo ni kipi cha kufanya ili muda ukiwadia asianze kubabaika na kurudi kwenye ponografia tena.

-Kama kuna uwezekano wa kuwa na app ambazo huzuia tovuti za ngono pia ni vyema zaidi.

-Weka kumbukumbu. Haitakuwa rahisi kuacha kuangalia lakini iwapo mwenendo utaonekana basi itakuwa rahisi kujitahidi mafanikio yawe zaidi. Kwa mfano mhusika mara ya kwanza aliweza kukaa siku tatu bila kuangalia, basi akilifahamu hilo wakati ujao atajitahidi azidishe siku nyingine.

KUACHA PONOGRAFIA HAKUTATATUA MATATIZO YOTE LAKINI NI MWANZO MZURI NA UNAVYOZIDI KUJUA NDIVYO UNAVYOZIDI KUKUA
 
Upvote 6
Back
Top Bottom