Zitto akwama bungeni
[Source Tanzania Daima]
na Sauli Giliard, Dodoma
MBUNGE wa Kigoma Kaskazini, Zitto Kabwe (CHADEMA), jana alikumbana na wakati mgumu baada ya wabunge kugoma kuunga mkono hoja yake ya kutaka kuwazuia wabunge kuwamo katika bodi za mashirika ya umma.
Zitto alitaka yafanyike marekebisho katika muswada wa korosho uliowasilishwa jana bungeni na Waziri wa Kilimo, Chakula na Ushirika, Stephen Wasira, ambapo alibainisha kuwa ni vema kipengele cha kuwazuia wabunge kikajumuishwa.
Alisema kuna umuhimu mkubwa kwa wanasiasa kutoingizwa katika bodi za mashirika ya umma, ikiwamo korosho, ili kuepusha migongano ya kimasilahi.
Pendekezo hilo aliliwasilisha jana asubuhi, lakini jioni wakati wa uhitimishaji, wabunge hawakumuunga mkono, hali iliyofanya kutupwa kwa marekebisho hayo.
Katika utetezi wa kutaka kukubalika kwa hoja yake, Zitto alibainisha kuwa katika Bunge kuna wabunge 322, lakini waliomo kwenye mashirika hayo ni 35 tu, ambao wengine wamekuwa wakizunguka katika bodi zaidi ya moja.
Alisema madhara ya wanasiasa kuwamo katika bodi hizo kuna sababisha mgongano wa kimasilahi wakati wanapofanya maamuzi kadhaa katika mashirika ya umma, jambo ambalo kimsingi linaathiri ufanisi wa chombo husika.
Kuna umuhimu wa wanasiasa kuondolewa katika bodi hizi. Huwa tunapopita katika mashirika ya umma tunapata matatizo makubwa kwa Kamati yetu ya Ukaguzi wa Mahesabu ya Mashirika ya Umma, alilieleza Bunge.
Zitto alisema Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), Ludovick Utoah, alishawahi kupendekeza jambo hilo ili kuleta ufanisi katika mashirika hayo.
Hili jambo si geni, ni ukweli usiopingika kuwa kuwapo kwa wabunge katika bodi za mashirika ya umma kwa namna moja au nyingine kunashusha uwajibikaji wa mashirika hayo, alisema Zitto.
Pamoja na utetezi huo, bado Zitto hakuweza kupata uungwaji mkono wa wabunge.
Mwenyekiti wa Bunge, Job Ndugai, ambaye alikuwa akiendesha kikao hicho cha jioni, alimtaka Zitto akubaliane na matokeo, kwa kuwa hoja yake haikuungwa mkono na wabunge.
Mheshimiwa Zitto, ulitoa hoja ya kuwapo kwa marekebisho katika muswada wa korosho lakini kutokana na kutoungwa mkono na wabunge, pendekezo hilo haliwezi kuwa halali, alisema Ndugai.
Awali, Zitto alibainisha kuwa anashangazwa na muswada huo mpya kutoweka bayana kuhusu suala hilo ambalo kwa muda mrefu limekuwa likisababisha mkanganyiko wa utendaji kazi, hasa unapofika wakati wa kufanya maamuzi yenye kuiwajibisha bodi ya shirika Fulani.
muswada huo utakaounda bodi ya korosho na kufuta ile ya mwaka 1984, alipingana na kipengele kinacholilinda soko badala ya mkulima wa korosho.
Katika hilo, alibainisha kwamba, soko huwa linajilinda lenyewe na kushauri wakulima walindwe kwa kuwa katika soko, kuna wafanyabiashara wakubwa wenye nguvu za kuwanyonya wakulima wadogo.
Zitto alisema, licha ya takwimu kuonyesha kwamba, msimu uliopita pekee, korosho za thamani ya dola milioni 40 ziliuzwa nje na kuchangia pato kubwa la taifa, bado sekta hiyo haipewi kipaumbele kama zilivyo sekta nyingine na kutolea mfano ile ya madini.
Naye Mbunge wa Mtwara, Mohamed Sinai alitaka afya za wakulima zipewe kipaumbele katika sheria hiyo mpya inayotarajiwa kutungwa endapo mswada utapita, ikiwa ni pamoja na kuwalazimisha wenye viwanda vya kubangua korosho kuwapima mara kwa mara wafanyakazi wao.
Alisema, moshi unaotoka katika viwanda huwaathiri wafanyakazi hao mapafu huku mafuta yakiwaharibu ngozi licha ya kupewa ujira mdogo usioendana na kazi nzito wanayoifanya.
Moshi wa korosho unawaharibu mapafu, mafuta yanaharibu ngozi yao, wafanyakazi wanatakiwa wapimwe afya zao, alisisitiza mbunge huyo.
MY TAKE:
Ni obvious kuwa First priority ya Wabunge wetu wa CCM ni ulaji na sio kuwatetea wapiga kura waliowapeleka pale. Kila mwaka posho za waheshimiwa wetu zinaongezeka bila kujali hali ya mwanachi wa kawaida ikoje. Mimi naimba kila siku kwamba dawa yake ni kuwa na chama cha upinzani chenye nguvu at any cost bungeni. Nachoshwa sana na huu upumbavu wa kutuvuga kwamba wewe ni mpambanaji unakosoa madudu ya serikali kwelikweli, unapiga kelele kwenye luninga mpaka mishipa inakutoka halafu unamalizia kwa kuunga mkono mia kwa mia hoja ya kijinga. Watanzania amkeni. "Sidanganyiki" ndio iwe kauli yetu 2010.
.