TANROADS YATANGA BARABARA SITA ZA PPP KUUNGANISHA MIKOA YA DAR, PWANI, DODOMA, SINGIDA NA TANGA KM 969.
Katika hatua nyingine kubwa ya kuharakisha maendeleo ya miundombinu na kuimarisha ukuaji wa uchumi wa Taifa, Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS) umetangaza fursa za uwekezaji katika miradi sita mikubwa ya barabara yenye urefu wa kilomita 969 kupitia mfumo wa Ubia kati ya Sekta ya Umma na Sekta Binafsi (PPP).
Tangazo hilo la kimataifa la kutafuta wawekezaji wa ndani na nje ya nchi kwa ajili ya kubuni, kujenga, kugharamia, kuendesha, kutunza na hatimaye kukabidhi miradi hiyo kwa Serikali kupitia mfumo wa Design, Build, Finance, Operate, Maintain and Transfer (DBFOMT), linaendelea kudhihirisha dhamira ya Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan ya kutumia nguvu ya sekta binafsi kuharakisha utekelezaji wa miradi mikubwa ya maendeleo.
Hatua hiyo pia inaakisi mafanikio ya mageuzi makubwa yanayosimamiwa na Kituo cha Ubia kati ya Sekta ya Umma na Sekta Binafsi (PPPC) chini ya Mkurugenzi Mtendaji David Kafulila, ambaye amekuwa mstari wa mbele kuhamasisha ushiriki wa sekta binafsi katika uwekezaji wa miundombinu na huduma za kijamii nchini.
Miradi iliyowekwa mezani kwa wawekezaji ni pamoja na upanuzi wa Barabara ya Morogoro–Dodoma yenye urefu wa kilomita 260 kuwa njia nne, Barabara ya Handeni–Kiberashi–Chemba–Kwamtoro–Singida yenye kilomita 384, upanuzi wa Barabara ya Chalinze–Segera–Tanga yenye kilomita 246 kuwa njia nne pamoja na ujenzi wa Kitonga Escarpment Bypass yenye kilomita 27.
Miradi mingine ni Dar es Salaam Port–Kibaha Expressway yenye kilomita 42 na Dar es Salaam CBD–Julius Nyerere International Airport Expressway yenye kilomita 10.
Kwa mujibu wa TANROADS, miradi hiyo inalenga kupunguza msongamano wa magari, kuboresha usafirishaji wa watu na mizigo, kuongeza ushindani wa uchumi wa Tanzania na kuimarisha nafasi ya nchi kama kitovu cha biashara na usafirishaji katika ukanda wa Afrika Mashariki na Kati.
Kwa ujumla, miradi hiyo ina urefu wa kilomita 969. Kwa makadirio ya wastani ambapo kilomita moja ya barabara inaweza kugharimu takribani Dola za Marekani milioni moja, miradi hiyo inaweza kuvutia uwekezaji wa karibu Dola za Marekani milioni 969, sawa na zaidi ya Shilingi trilioni 2.6 kwa viwango vya sasa vya ubadilishaji fedha. Hii inaonesha ukubwa wa fursa za uwekezaji zinazofunguliwa kupitia mfumo wa PPP na mchango wake katika kuchochea ukuaji wa uchumi wa Taifa.
Wataalamu wa uchumi wanaeleza kuwa utekelezaji wa miradi hiyo kupitia mfumo wa PPP utawezesha kuvutwa kwa mitaji mikubwa ya sekta binafsi bila kuongeza mzigo mkubwa kwa Serikali, huku ukifungua maelfu ya ajira na kuchochea ukuaji wa sekta mbalimbali za uzalishaji.
Katika nyakati tofauti, Mkurugenzi Mtendaji wa PPPC, David Kafulila, amesisitiza kuwa PPP ni nyenzo muhimu ya kuifikisha Tanzania kwenye uchumi wa dola trilioni moja ifikapo mwaka 2050 kwa kuvutia uwekezaji mkubwa wa ndani na nje, kuongeza tija katika utekelezaji wa miradi na kuharakisha maendeleo ya Taifa.
Jitihada hizo zinaendana na maelekezo na dira ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan ya kujenga uchumi shindani unaotegemea ushirikiano wa karibu kati ya Serikali na sekta binafsi. Kupitia mageuzi mbalimbali yaliyofanywa katika sheria, kanuni na mifumo ya uwekezaji, Tanzania imeendelea kujijengea mazingira bora zaidi ya biashara na uwekezaji.
Kutangazwa kwa miradi hii sita ya barabara kunatajwa kuwa hatua nyingine muhimu katika utekelezaji wa Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050 na mkakati wa Serikali wa kuifanya Tanzania kuwa kitovu cha biashara, usafirishaji na uwekezaji katika Afrika.
Kwa hakika, hatua hii inaonesha namna PPPC chini ya David Kafulila, kwa kushirikiana na Wizara ya Fedha na taasisi nyingine za Serikali chini ya uongozi wa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, wanavyoendelea kufungua ukurasa mpya wa uwekezaji wa kimkakati utakaosaidia kuibadilisha Tanzania kiuchumi kwa vizazi vya sasa na vijavyo.