Naomba tushirikiane kujadili Ibara yote ya 66 ya Katiba ya Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania (1977 as amended from time to time)
SEHEMU YA PILI
WABUNGE, WILAYA YA UCHAGUZI NA UCHAGUZI WA WABUNGE
Wajumbe wa Bunge
Ibara ya 66.
Ibara ndogo ya (1),
Bila ya kuathiri masharti mengine ya ibara hii, kutakuwa na aina zifuatazo za Wabunge, yaani-
(a) Wabunge waliochaguliwa kuwakilisha majimbo ya uchaguzi;
(b) Wabunge wanawake wa idadi inayoongezeka, kuanzia asilimia ishirini ya Wabunge waliotajwa katika aya ya (a), (c ) na (d), itakayotajwa mara kwa mara na Tume ya Uchaguzi kwa taarifa iliyochapishwa katika Gazeti la Serikali baada ya kupata kibali cha Rais, watakaochaguliwa na vyama vya siasa vinavyowakilishwa Bungeni, kwa mujibu wa ibara ya 78, na kwa kuzingatia masharti ya uwiano wa uwakilishi baina ya vyama hivyo;
(c) Wabunge watano waliochaguliwa na Baraza la Wawakilishi kutoka miongoni mwa wajumbe wake; (d) Mwanasheria Mkuu;
(e) Wabunge wasiozidi kumi walioteuliwa na Rais kutoka miongoni mwa watu wenye sifa kwa mujibu wa ibara ya 67, isipokuwa sifa iliyotajwa katika ibara ya 67(1)(b).
Ibara ndogo ya (2),
Rais na Makamu wa Rais kila mmojawao hatakuwa Mbunge.
Ibara ndogo ya (3),
Endapo Mkuu wa Mkoa atachaguliwa kuwa Mbunge anayewakilisha wilaya ya uchaguzi au endapo Mbunge anayewakilisha wilaya ya uchaguzi atateuliwa kuwa Mkuu wa Mkoa, Bunge litahesabiwa kuwa lina idadi ya Wabunge inayohitajika na shughuli zake zitakuwa halali ingawaje idadi ya jumla ya kawaida ya Wabunge kwa mujibu wa masharti ya ibara hii, itakuwa imepungua kutokana na uchaguzi huo wa Mkuu wa Mkoa au uteuzi huo wa Mbunge anayewakilisha wilaya ya uchaguzi.