Roving Journalist
JF Roving Journalist
- Apr 18, 2017
- 3,984
- 13,760
Mkurugenzi Mtendaji wa MOI, Prof. Abel Makubi, leo Julai 12, 2023 amefanya kikao na madaktari bingwa/Bobezi wa MOI ili kujadili kwa pamoja namna ya kuboresha huduma kwa wagonjwa, suala la huduma kwa wateja, uwajibikaji wenye matokeo , kuwa na mtazamo chanya pamoja na kuongeza na kuifanya Taasisi iweze kupata fedha za kutosha kununua vifaa na dawa ili kuondoa mahangaiko kwa Wananchi.
Kikao hiki ni muendelezo wa vikao baina ya Prof. Makubi na makundi mbalimbali ya watumishi wa MOI vyenye lengo la kupata maoni, ushauri na changamoto ili kuleta mageuzi makubwa katika Taasisi ya MOI ambayo sasa ina miaka 26 tangia kuanzishwa kwake.
Prof. Makubi amewaomba ushirikiano wa dhati madaktari bingwa ili kuleta mageuzi makubwa katika utoaji huduma za kibingwa za Mifupa, Ubongo, Mgongo na mishipa ya fahamu hapa nchini.
“Niwaombe madaktari bingwa na wasomi wenzangu, kila mtu abadilike na kujielekeza kwenye muelekeo huu wa menejimenti unaolenga kuleta matokeo chanya, kuongeza uwajibikaji; sioni sababu ya kwanini tubaki hapa tulipo nashauri twende haraka tuboreshe huduma, mazingira ,vifaa na dawa viwepo vya kutosha; naamini uwezo huo tunao” Alisema Prof. Makubi
“Katika kipindi cha mwaka mmoja na nusu tujipange kukamilisha ujenzi wa jengo jipya kisasa la kuona wagonjwa wa nje (OPD) ambalo litakuwa na vyumba vya kliniki vya kutosha na vyenye hadhi ya kimataifa ili wagonjwa wengi zaidi kutoka Tanzania na mataifa mengine wapate huduma” Alisema Prof. Makubi.
Kwa upande wao Madaktari bingwa wa MOI wamemuahidi Prof. Makubi kuongeza uwajibikaji, kufanya kazi kwa bidiii, kuwa na ‘Sense of ownership’ kwa taasisi ili kuboresha huduma kwa wagonjwa pamoja na kuifanya taasisi iweze kumudu gharama za mahitaji ya msingi ya kutolea huduma.