Picha: Mpigapicha Wetu
Profesa Rwekaza Mukandala
JANA ilitimu miaka 28 kamili tangu kuzama kwa meli ya Mv Bukoba' katika Ziwa Victoria, Profesa Rwekaza Mukandala akiibua hoja mpya ikiwamo miili ya abiria kuelea kwa muda mfupi kwenye maji kunakotoa ishara walikunywa mafuta kabla ya kufariki dunia.
Vilevile, msomi huyo amesema meli hiyo ilizama kutokana na uzembe, haikusajiliwa licha ya kufanya kazi kwa miaka 17 huku nahodha wa meli hiyo akijiokoa kwanza na kutelekeza abiria wake.
Prof. Mukanadala aliyasema hayo jana, mkoani Dar es Salaam, katika Mhadhara wa Uprofesa uliofanyika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM) na kuhudhuriwa na wanazuoni pamoja na Mkuu wa chuo hicho, Rais mstaafu Jakaya Kikwete.
Akiwasilisha mada kwa takribani saa moja na nusu, Prof. Mukandala alisema: "Tume ya Jaji Kisanga ilitaja upungufu ya meli. Kati yake, ni meli kuongozwa na manahodha wasio na ujuzi, kujaza mzigo hasa ndizi na abiria zaidi ya 400, mara mbili ya kiwango kilichostahili."
Prof. Mukandala alisema Taasisi ya Maji ya Dermark iliwahi kufanya utafiti na kushauri meli hiyo iwe na matangi yaliyojaa maji muda wote ili kuweka uwiano wenye usawa kutokana na kasoro za meli tangu ilipoundwa na wahandisi wasio na ujuzi.
"Mnusurika maarufu anapinga maelezo kuhusu ubovu wa chombo. Rushwa na uendeshaji duni wa chombo, kutofanyiwa matengenezo kulichangia meli kuzama. Meli hii ilikuwa ikitembea upande na ikiserereka majini," alisema mwanazuoni huyo.
Prof. Mukandala alieleza kuwa inaaminika kwamba binadamu akizama huibuka baada ya siku kadhaa. Lakini mnusurika mmoja alisema wakati anajiokoa alizingirwa na mikungu ya ndizi na miili ya watu. Inawezekana walipigwa na shoti ya umeme au walikunywa mafuta.
Alisema pamoja na tukio hilo kutokea, likiwa ni miongoni mwa yaliyo makubwa nchini na kimataifa, baada ya miaka 15, ajali nyingine ya meli ikatokea, Mv Islander ikazama Bahari ya Hindi na kupoteza maisha ya takribani watu 1,000.
Prof. Mukandala alisema meli hiyo ilianza kazi mwaka 1979, ikiwa na kasoro kadhaa ambazo zilifanya isisajiliwe, akiutaja ubeberu kuwa chanzo cha meli kuzama.
"Serikali iliamua kutumia mkopo kununua meli kutoka Serikali ya Ubelgiji iliyoikopesha faranga za Kibelgiji milioni 500 wenye riba ya asilimia 8.3 kwa kipindi cha miaka saba.
"Ununuzi mzuri wa huduma ni ule wa kutangaza kwa ushindani, serikali haikufuata mchakato wa ununuzi uliozoeleka na mkopo ulikuwa wa pingu wenye masharti magumu sana.
"Serikali ya Ubelgiji iliteua kampuni ya ununuzi, kampuni ya MS Belgium Shipping ilikuwa ni kati ya muungano wa kampuni tatu zilizopata zabuni hiyo.
Shirika la Reli (msimamizi wa wakati huo) lilieleza aina ya meli inayohitajika," alisema.
Profesa Mukandala alisema kuwa meli hiyo licha ya kufanyiwa majaribio kadhaa, ilibaki kazini ikiwa na kasoro ingawa hakuna hatua zilizochukuliwa, hivyo kuhatarisha uhai wa wasafiri.
Alisema Shirika la Reli Tanzania halikuwa na muda wa kupitia na kusoma vifungu vya mkataba wa ununuzi. Waziri wa Mawasiliano na Uchukuzi wakati huo aliagiza mkataba utiwe saini haraka.
"Inaonesha naye waziri alipewa maagizo na Rais ambaye ana madaraka makubwa, akisema linatekelezwa. Tume ya Jaji Kisanga ilisema masharti yalikuwa magumu sana," alisema.
Prof. Mukandala alisema ujenzi wa meli wa meli ulifanyika Tanzania na watu 63 ambao tume ilibaini hawakuwa na ujuzi chini ya msimamizi mmoja kutoka Ubelgiji.
Alisema kuwa Julai 27, 1979, meli ilikabidhiwa kwa Rais Julius Nyerere na kuanza kazi mwezi uliofuata. Mamlaka zote tatu; dola, Shirika la Reli hazikuchukua hatua baada ya meli kubaini kuwa na kasoro.
"Ili kukabiliana na kasoro hizo, ilibidi ibebe maji katika matangi muda wote. Uokoaji ulikuwa na kasoro wakati ajali ilipotokea.
Hakukuwa na mtaalamu wa uzamiaji hata mmoja, maboya 'kiduchu' licha ya meli kuchukua takriban saa nne. Meli ya Titanic ilizama ndani ya saa tatu lakini watu wengi waliokolewa," alisema.
Prof. Mukandala alisema, "tunajifunza kwamba madaraka ya Rais ni makubwa, kuna haja ya kuwa na mjadala kuwapo Katiba Mpya. Rais Nyerere aliruhusu hili, meli inunuliwe.
"Kuna wakati meli ilijaa maji na kuelemea upande mmoja, lilitolewa tangazo la ununuzi ili kuepusha rushwa katika mchakato wa mradi wowote."
Credit: NIPASHE