Kwamba nilianza vizuri na kumaliza vibaya, hayo ni maoni yako, mimi ninaandika kilicho moyoni mwangu bila nia ya kumfurahisha au kumkweza yeyote. Lazima mjifunze kuvumilia kauli za wenzenu hata kama zinakinzana na unacho amini, na ndio maana leo hii huko kwenu mnafukuza waziri kwa bastola na kukamata wasanii kama akina Nay maana hamtaki kuvumilia kuskliza kauli pinzani na imani zenu.
Kwa nchi iliyo na chembechembe za chuki dhidi ya wageni, lazima uhakikishe unawalinda watoto wako hata kama wana uraia. Wayahudi walikua na uraia wa Ujerumani wakati Hitler ana wasaka, Wahindi walikua na uraia wa Uganda wakati Amin anawafanyia unyama, mifano ipo mingi tu. Hivyo ukibarikiwa kupata mtoto baada ya ndoa na mwanamke kwenye nchi ya kihivyo, hakikisha mwanao umemrejesha kwenu, tena akiwa bado mdogo, malezi, dini, itikadi, elimu na kila kitu zifanyie kwenu na atakushukuru sana katika ukubwa wake wakati vurugu za ubaguzi zinaanza.
Leo hii kulingana na hizi taarifa hapa, mtu alizaliwa Tanzania hata kabla nchi haijapata uhuru, mnamfurusha kwamba aende kwao ghafla, tena kwa kushtukiza, jameni kwao wapi. Haya ndio yanatokea kule Afrika Kusini, japo kule yanafanywa na raia wenye chuki na sio serikali.
Sijui kama ipo siku mtakuja elewa kwamba Kenya ndio ndugu zenu wa karibu, kama nilivyosema awali, tuna mpaka mrefu baina yetu, tunaongea lugha moja, tuna makabila ambayo yana ndugu pande zote mbili. Wazungu wakati wanagawana Afrika kama shamba la bibi, walikuja wakachora mpaka baina ya Wajaluo, Wakuria, Wadigo, Wamaasai n.k. na kuwaambia wa huku waitwe Wakenya na wa kule waitwe Watanzania, unakuta mtu ana mjomba upande wa pili na shangazi upande wa huku.
Mimi hapa Mkikuyu, najaribu kuwaza jinsi ningekua namwona Mkikuyu wa Tanzania upande wa pili kisa mzungu kachora mpaka baina yetu. Anyway tuliyakuta, na itabidi tuishi yalivyo kimya bila sauti au nia ya kuyabadilisha. Lakini naomba sana Kenya isije kujitoa ufahamu na kuwafurusha ndugu zetu Watanzania waliojaa huku kwa maelfu, itaniuma balaa japo sitakua na uwezo wala cha kufanya kuzuia.