Juma Issihaka
New Member
- Sep 25, 2019
- 3
- 3
Nyumba iliyo karibu kusombwa na Bahari, kijiji cha Mdimni wilayani Mkuranga.
Na Mwandishi Wetu
Maisha ya wakazi wa Kijiji cha Mdimni kilichopo wilayani Mkuranga katika Mkoa wa Pwani, yapo shakani kufuatia sehemu kubwa ya ardhi yake kughubikwa na athari zilizokithiri za mabadiliko ya tabianchi.
Kwa mujibu wa wakazi hao, takribani eneo la Kilometa 100 walilokuwa wakilitumia kwa shughuli mbalimbali ikiwemo kilimo na makazi limesombwa na sehemu ya fukwe ya Bahari ya Hindi.
Mohammed Kisuguru ni miongoni mwa wakazi wa kijiji hicho, anasema hali hiyo imedhoofisha uzalishaji wa zao la mpunga kijijini hapo kwani eneo lililosombwa na bahari lilitumika katika shughuli za kilimo cha zao hilo.
Anasema hali hiyo ilianza taratibu tangu miaka ya 1978, wakati huo akiwa na umri mdogo, ilishuhudiwa bahari ikitanuka kwa maana ya kusogea eneo la nchi kavu siku hadi siku.
Kisuguru anabainisha kwa wakati huo, haikutambulika moja kwa moja kuwa jambo hilo huenda likaleta athari kijijini hapo, iliaminika kwamba ni kawaida ya bahari kupwa na kujaa maji wakati fulani.
Anaeleza kinachowatia mashaka zaidi ni kwamba bado hali hiyo inaendelea na imeshafika hadi katika baadhi ya makazi ya watu.
Kwa mujibu wa Kisuguru, baadhi ya wakazi wa kijiji hicho wamekuwa wakihama kutoka kwenye makazi yao mara tu waonapo dalili ya ujio wa bahari hiyo.
“Huwa tunagundua dalili za ujio wa bahari hii kwenye makazi yetu kwa kuanza kuenea kwa mbegu za mikoko katika maeneo yetu, hivyo tukiona hayo yameanza haraka sana tunahama na kusogea eneo la mbali kidogo
“Tupo kwenye hali ngumu kwa sababu tunaamini utafika wakati itabidi tuhamie kijiji cha jirani maana hali inaendelea na tumeshindwa kuizuia,” anasema.
Anafafanua miaka ya 1977 eneo hilo lilikuwa mashuhuri kwa kilimo cha mpunga lakini kwa sasa halifai tena kutokana na kuingia chumvi ya bahari iliyosababisha kukosekana kwa rutuba ya udongo.
Kisuguru, anaishauri serikali na mamlaka zake kuwa na utaratibu wa kutembelea Vijiji mbalimbali ili kubaini changamoto vinavyokumbana nazo na huenda zikasababisha athari kwa taifa zima.
Kadhalika Kisuguru, anasema kinachoaminika na wanakijiji hao ni kwamba hali hiyo imesababishwa na ukataji wa miti bahari uliopitiliza.
Anasema katika fukwe hiyo, watu kutoka ndani na nje ya kijiji hicho walizuka na kuanza shughuli za ukataji wa mikoko kwa magendo hali ambayo kwa kiasi kikubwa inaaminiwa kusababisha janga hilo.
Anasisitiza kwa hali iliyopo sasa, tegemeo lao ni msaada wa serikali kubuni mbinu ya kukabiliana na kinachojitokeza.
"Tatizo mamlaka kama NEMC (Baraza la Usimamizi na Hifadhi wa Mazingira), wanaishia mijini hawafiki huku kutupa elimu ya jinsi ya kuishi na kuendana na mazingira," anaeleza.
WATAALAMU WA MAZINGIRA
Rebecca Muna, ambaye ni Mwanaharakati wa Mabadiliko ya tabianchi, anasema hali hiyo husababishwa na uwepo wa joto la kupitiliza Duniani.
Anasema kwa kawaida joto hilo husababishwa na shughuli mbalimbali zinazopelekea kuzalishwa kwa gesi joto nyingi, ambayo ndio chanzo cha kutokea kwa athari za mabadiliko ya tabianchi.
Anafafanua kuwa bahari kuingia kwenye eneo la nchi kavu ni jambo ambalo moja kwa moja linasababishwa na kuongezeka kwa kina cha bahari.
Kwa mujibu wa Rebecca, watu wengi huelewa tofauti juu ya dhana ya kuongezeka kwa kina cha bahari, wakiamini kuwa ni kitendo cha bahari kuchimbika chini ilhali sio tafsiri halisi.
Anabainisha kuongezeka kwa kina cha bahari katika muktadha huo, ni kupanuka kwake ambapo husababishwa na kujaa kupitiliza hivyo maji husambaa baada ya kuzidi kina cha bahari kilichopo.
“Unaweza kujiuliza bahari inajaa maji yanatoka wapi, hii ndio kama nilivyoeleza kuwa uzalishaji wa gesi joto uliopitiliza husababisha kuwepo kwa joto kuzidi kiwango Duniani, hali hii inakwenda kuyeyusha barafu zilizopo kwani tunatambua kuwa kuna baadhi ya visiwa vimezungukwa na barafu na hata baadhi ya nchi,
“Inapotokea barafu zikayeyuka moja kwa moja zinakwenda kujaza vyanzo vya maji ambavyo ni bahari na kwa sababu maji hayo yatakuwa sio yale yaliyokuwepo kila siku kwenye bahari hiyo, maana yake yatasababisha kina kuongezeka na hatimaye bahari kutapika ndipo yanakwenda kwenye maeneo ya nchi kavu,” anasema.
Anasema kitendo cha bahari kuingia eneo la nchi kavu, kinaathiri shughuli nyingi za uzalishaji kikiwemo kilimo, kwani panapoingia maji ya bahari rutuba ya udongo hupotea na kuifanya ardhi hiyo kutohimili ustawi wa zao lolote.
Anashauri namna pekee ya kudhibiti kutokea kwa hali hiyo ni kupunguza shughuli zinazozalisha gesi joto kwa wingi au kubadili teknolojia za shughuli hizo ili kuleta uhimili.
Rebecca ambaye pia ni Mkurugenzi wa Asasi ya Kiraia inayoshughulika na kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi (FORUMCC), anaongeza uhamasishaji jamii kutumia nishati jadidifu ni jambo jingine muhimu kukabiliana na hali hiyo.
Anasema pamoja na juhudi zinazofanywa na wadau kubadili matumizi ya nishati ili kuleta ustawi wa mazingira ni muhimu kwa jamii, asasi za kiraia na wadau wengine kutilia maanani mapambano dhidi ya athari za mabadiliko ya tabianchi kwani ni janga kubwa linaloleta athari nyingi na katika sekta mbalimbali.
Naye Ofisa kutoka taasisi ya Mpango wa Usafi na Utunzaji wa Mazingira (TCCI), Godwin Mahendeka, anasema hali hiyo ni tishio kwa maeneo mengi nchini.
Anasema hali hiyo huwa inajitokeza pia hata katika sehemu ya Ziwa Victoria na kusababisha kuingia kwa maji katika maeneo yasiyo rasmi.
Kwa mujibu wa Mahendeka, hicho ni kiashiria cha moja kwa moja cha athari za mabadiliko ya tabianchi ambayo kutokea kwake hutokana na mambo mengi ikiwemo uharibifu wa mazingira.
Anasema taasisi hiyo imekuwa ikifanya shughuli za usafishaji bahari, upandaji wa miti na kuihamasisha jamii kuendana na dhana ya utunzaji wa mazingira ikiwa ndio msingi imara wa kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi.
Anaongeza kuwa nguvu ya asasi za kiraia, serikali na wataalamu wa mazingira ni muhimu katika kujenga uelewa wa jamii ili ibadili fikra na mitazamo ya maisha ya kale hadi kufanya shughuli zao kwa kuzingatia uhifadhi na utunzaji wa mazingira.
NEMC WATOA NENO
Mkurugenzi Mkuu wa Baraza la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC), Dk. Samuel Gwamaka, anasema jukumu la baraza hilo ni kuhakikisha uhifadhi na utunzaji wa mazingira kupitia kuielimisha jamii.
Anasema kwa hali kama hiyo, baraza linawajibika kwa kutoa elimu kwa jamii ya eneo husika, juu ya namna ya kuleta ustawi lakini hakuna uwezekano wa kurejesha hali ya zamani.
“Kinachofanywa ni kuielimisha jamii ya eneo husika kwani itakapokuwa na uelewa ndipo wataimarisha ustawi, mara nyingi matokeo ya athari za mabadiliko ya tabianchi au uharibifu wa mazingira hutokana na uelewa duni wa jamii juu ya kudhibiti hali hiyo,” anasema.
Naye Bwenda Bainga, Ofisa Kilimo Wilaya ya Kibiti mkoani Pwani, anasema athari za mabadiliko ya tabianchi ni hatari kwa shughuli za kilimo.
Anasema uwepo wa hali hiyo ndiyo sababu ya kuanza kwa matumizi ya mbolea kwa ajili ya kuoteshea, kukuza na kustawishia mazao.
Kadhalika Bainga, anasema kabla ya kukithiri kwa athari hizo, ardhi ya Tanzania haikuwa na uhitaji wa matumizi ya mbolea kwa ajili ya kuzalishia mazao, kwani ilijitosheleza kwa rutuba.
Anasema ni muhimu kwa wadau wa sekta ya kilimo kuzingatia utekelezaji wa shughuli zao kwa kuhifadhi mazingira kwani sekta ya mazingira na kilimo zina uhusiano mkubwa katika uzalishaji.
Upvote
2