Mukasha akasikiliza tena na kuvua zile spika. “ Ahsante Irene.Fuatilia kibali cha mzazi wako wizarani kila kitu kitakuwa tayari.Kuhusu hiki ulichokifanya usiwe na wasi wasi kila kitu kitakua salama.” Akasema Mukasha akatoka nje ya kile chumba akaeleka ofisni kwake kichwa kikionekana kujawa mawazo.Alikumbuka maongezi aliyoyasikia simuni kati ya rais na Janet mwamsole. “ It’s about Monica” “ Monica amefanya nini? “ Ninawasi wasi na usalama wake” Maongezi haya ya Ernest na Janet yakajirudia kichwani kwake kama wimbo “Monica yupi ambaye Janet ana wasiwasi na usalama wake? Kwa nini amueleze Ernest” akaendelea kuwaza Mukasha “ Hapa kuna jambo kubwa limejificha .Nikiendelea kuwachunguza Ernest na Janet kuna kitu nitakifahamu.Nitahakikisha ninamfahamu huyo Monica ambaye Janet anadai yuko kwenye hatari.” Akawaza Mukasha
*************************
Rais wa jamhuri ya muungano wa Tanzania Ernest Mkasa aliwasili Kobwe hospitali ambako amelazwa Austin.Aliposhuka garini akamuita Evans na kumueleza kwamba amtafute Janet yuko pale hospitali na akimpata ampeleke katika mgahawa amsubiri hapo.Rais akapokewa na daktari mkuu aliyeshuka haraka baada ya kupata taarifa za ujio wa rais.Walielekea katika chumba alimo lazwa Austin.Rais akawasalimu walinzi waliokuwa nje ya chumba kile na kuingia chumbani.Austin alikuwa amekaa kitandani akizungumza na Amarachi.Baada ya kusalimiana na rais,Amarachi na daktari wakatoka wakamuacha rais akiwa na Austin “ Nimefarijika sana kukuona ukiwa katika hali hii Austin.Jana nilipopewa taarifa za kilichotokea nilipatwa na mstuko mkubwa na nikajua tayari mwisho wa mapambano umefika.Nawashukuru sana rafiki zako Job na Amarachi ambao walifanya juhudi kubwa kuhakikisha unafika hapa na kupatiwa matibabu kwa haraka.Mungu yuko upande wetu na tutashinda vita hii licha ya vikwazo vingi. Unajisikiaje sasa hivi? “Najisikia vizuri mzee.Maendeleo yangu mazuri sana.Nasikia maumivu sehemu zile zenye majeraha lakini ni maumivu ya kawaida ambayo hayawezi kunizuia kufanya kazi zangu.Mzee nahitaji kutoka hapa hospitali.Nahitaji kurejea nyumbani.Mapambano lazima yaendelee na muda huu ninaokaa hapa hospitali wenzetu wanaendelea kujipanga.Mzee hatutakiwi kuwapa nafasi hawa jamaa” akasema Austin “ Hapana Austin.Unatakiwa uendelee kukaa hapa hospitali hadi hapo utakapopona kabisa.Wewe ndiye pekee ninayekutegemea kuongoza mapambano haya kwa hiyo unatakiwa uwe na afya njema” akasema Rais “ Mheshimiwa rais naomba sana uwaeleze madaktari waniruhusu nitoke hapa hospitali.Dr Marcelo yuko pale nyumbani atanihudumia.” “ Austin nakushauri endelea kupumzika kijana wangu.Kazi zote zitasimama hadi pale utakapopona kabisa.Kukitokea kazi ya dharura Job na Amarachi watafanya ila tafadhali endelea kupata matibabu” Austin akamtazama rais na kusema “ Mr President I’m fine.Please let me out of here.Kuna kazi ambazo haziwezi kusubiri hadi nipone.Tunatakiwa kuwahoji Boaz na mwanae .Nahitaji kumfahamu Maria ni nani kwani kwa hiki alichokifanya ni wazi si Maria Yule ambaye nimekuwa naye kwa miaka kadhaa nikiamini ndiye hasa mwanamke wa maisha yangu.She’s very dangerous than we all know.Amarachi ameniambia kwamba Job tayari amekueleza kila kitu kuhusu Wilson Mukasha.” “ Ndiyo amenieleza .Nimestuka sana.Iliniwia ugumu kuamini lakini kwa vile ninakuamini siwezi kukataa Mukasha kujihusisha na mambo hayo.Nimesikitika kwani Mukasha ni mmoja kati ya watu niliowaamini na kuwategemea sana.Kama yeye yuko hivi basi hakuna katika watu wanaonizunguka aliye msafi.Wote wameoza.” Akasema rais “Mambo yote uliyoelezwa na Job ni ya kweli kabisa mheshimiwa rais.Wilson Mukasha si mtu wa kumuamini hata kidogo na hafai kupewa madaraka yoyote achilia mbali uwaziri mkuu.Tunaendelea kutafuta ushahidi ili kuwasilisha kwako kukuhakikishia kwamba Mukasha hafai” akasema Austin “ Hakuna haja ya kutafuta ushahidi Austin.I believe you.Tusipoteze muda katika kumchimba Mukasha bali tujielekeze zaidi katika masuala yetu ya msingi.Mukasha ninajua namna nitakavyomshughulikia mimi mwenyewe” “ Ahsante sana mheshimiwa rais kwa kuniamini.Hata hivyo bado tunatakiwa kuufahamu mtandao wake wote .Tunataka pi kumuhoji Boaz.Huyu ndiye anayemtafuta Marcelo “ Boaz ?!! akashangaa rais “ Ndiyo mzee.Boaz ndiye anayemtafuta Marcelo usiku na mchana na amenipa mimi kazi hiyo ya kumtafuta kwa hiyo kuna mambo mengi ambayo tunahitaji kuyafahamu kutoka kwake.Ukiacha hayo kuna lingine kubwa.Tayari nimeipata sampuli ya nywele ya Monica .Tunatakiwa kuchukua na sampuli yako ya nywele tayari kwa kipimo cha vinasaba” Bila kujali kama Austin ana majeraha rais akamkumbatia kwa furaha hadi pale Austin alipolalamika kuhisi maumivu. “I’m sorry Austin.Nimepatwa na furaha ya ajabu sana kwa hiki ulichoniambia.Umewezaje kuipata nywele hiyo?Monica amefahamu chochote? “ Mzee ulihitaji kupata sampuli na tayari imepatikana.Namna nilivyoipata hayo ni masuala yangu.Kitu cha msingi tunahitaji tupate na sampuli yako halafu tufanye utaratibu wa kupeleka sampuli hizo nje ya nchi kwa kipimo.Sintakueleza kwa sasa ni hospitali ipi tunapeleka sampuli hizo lakini ni hospitali ninayoiamini sana.Mheshimiwa rais nadhani mpaka hapo utakubaliana nami kwamba kuna ulazima mkubwa wa kutoka hapa hospitali na kwenda nyumbani ili nikasimamie mambo haya yote.” Akasema Austin.Rais akamtazama kwa makini halafu akauliza “Are you sure you’ll be ok? “ Yes I’m sure.Dr Marcelo yupo na atanihudumia.Endapo kutatokea tatizo lolote kubwa nitarejea hospitali mara moja” “ Sawa Austin .Nitawaomba madaktari wakuruhusu utoke ila tafadhali endapo kuna tatizo lolote unitaarifu mara moja” “ nashukuru mzee.Kuna jambo lingine ambalo nataka kukujulisha.Nimehama katika ile nyumba uliyonipa niishi.Nimehamia katika nyumba ya Job.Ni nyumba nzuri na yenye usalama mkubwa sana lakini hii haimaanishi kwamba ile nyumba sintoitumia.Bado tutaendelea kuitumia hadi hapo operesheni hii itakapomalizika.Muda wowote kama kutakuwa na ulazima wa kuonana basi tutakutana pale katika ile nyumba yako.” “ Sina tatizo na hilo Austin.Chochote unachoona kinafaa mimi sina kipingamizi” akasema rais “ Thank you” “ Can I see that sample? Akauliza rais.Austin akaufunua mto na kutoa pakiti ndogo ya nailoni akampa rais ambaye aliitazama huku akitasamu na kufumba macho “ Ee Mungu naomba jambo hili liwe la kweli na Monica awe ni mwanangu” akaomba kimya kimya kisha akamrudishia Austin ile pakiti “Austin ahsante sana.Natakiwa na mimi nitoe nywele yangu” akasema na kunyofoa nywele kichwani akaziweka katika pakiti nyingine ya nailoni “ Kila kitu kimekamilika” “ Ndiyo mheshimiwa rais” “ Sawa ngoja nikazungumze na daktari nimpe maelekezo akuruhusu uondoke leo” akasema rais na kutoka nje ya kile chumba akazungumza na daktari .Wakati akiendelea na maongezi na daktari ,Evans akatokea ,akaongea pembeni na rais “Mzee ,mama Janet tayari amefika nimemuweka kule mgahawani anakusubiri” “ Ahsante sana Evans,Naelekea huko sasa hivi” akasema rais na kumalizia maongezi na daktari kisha akongozana na walinzi wake hadi katika eneo la mgahawa wa hotelini hapo .Watu wote walikuwa wameondolewa pale na Janet alikuwa peke yake.Rais akamfuata akavuta kiti na kuketi.Walinzi wakasogea mbali na kuwaacha rais na Janet peke yao waongee “ hallo janet habari za asubuhi” akasema rais “ Habari nzuri Ernest.Vipi wewe unaendeleaje? “ Naendelea vizuri Janet japokuwa niko katika kipindi kigumu lakini naendelea vyema.Kila kitu kitakaa sawa” “ Pole sana” “ Ahsante.Monica anendeleaje? Akauliza rais “ Anaendelea vyema.” Akajibu Janet na ukimya mfupi ukapita,wakatazama kisha Ernest akasema “ Ulinistua kwa simu ile uliyonipigia .Kuna tatizo gani? Akauliza rais. “ Samahani kwa kukustua na kukupotezea wakati wako Ernest .Kuna jambo ambalo nisingeweza kukueleza simuni.Dakika kama kumi hivi kabla ya kukupigia simu ile nilikuwa na Mukasha” “ Mukasha? Ernest akastuka “ Ndiyo.Nilikuwa na Mukasha.Alinipigia simu asubuhi ya leo akanitaka tuonane ana maongezi nami ya muhimu.Tulikutana na kitu alichoniitia kilinistua na kuniogopesha ndiyo maana nikalazimika kukupigia simu” akanyamaza kidogo akamtazama rais kisha akaendelea “Mukasha alitaka nimueleze siku ile tulipokutana hotelini tuliongea nini? Anasema kwamba ana wasiwasi na maisha yako kwa hiyo anataka akusaidie.Anadai kwamba chanzo cha mabadiliko haya yote yaliyotokea ghafla ndani ya siku chache katika serikali ni yale maongezi yetu ya siku ile.Akasisitiza kwamba baada tu ya mimi na wewe kukutana siku ile ulimtaka akutafutie kijana mahiri katika mambo ya uchunguzi na akakutafutia kijana mmoja anaitwa Austin.Hafahamu huyo Austin umempa kazi ipi .Anasema huyo kijana Austin amepigwa risasi usiku wa jana na watu wasiojulikana” Janet akanyamza akamtazama Ernest “ Ulimjibu nini ? akauliza Ernest “ Nilimjibu kwamba mambo tuliyoongea mimi na wewe ni binafsi na hapaswi kufahamu chochote kwani hayamuhusu.Sikutaka maongezi zaidi nikaondoka zangu ndipo nilipoamua kukupigia simu.Mukasha ameniogopesha sana kwa maswali yake.Ni vipi endapo atachunguza na kugundua kwamba Monica ni mwanao? Ninaanza kuwa na wasiwasi na Monica naona yuko katika hatari kubwa.Kwani huyo Austin umempa kazi gani hadi Mukasha awe na wasiwasi namna hii? Akauliza Janet “ Janet kwanza kabisa ahsante sana kwa kunipa taarifa hii.Pili nakuomba uwe na amani.Si Mukasha au mtu mwingine yeyote atakayetishia maisha yako au ya Monica.Nitamshughulikia Mukasha kwa hiyo usihofu” akasema rais “Ernest nayaamini maneno yako lakini namna nilivyomuona Mukasha kuna kitu anakitafuta na hatachoka hadi apate anachokitaka.Hatachoka kuchunguza huyo Austin umempa kazi gani” akasema Janet “Janet nimekwisha kuhakikishia kwamba hakuna yeyote katika nchi hii atakayetishia maisha yako wewe na Monica.Naomba uniamini katika hili.Mukasha hatapata anachokitafuta na safari hii amegusa sehemu mbaya” akasema Ernest “Ahsante Ernest.Vipi kuhusu huyo Austin umempa kazi gani kiasi cha kumfanya Mukasha ahangaike namna hii kutaka kufahamu? “Austin ni kweli kuna kazi nimempa lakini sintaweza kukueleza kwani ni mambo ya kiserikali .Kuhusu tatizo lililompata la kupigwa risasi halihusiani kabisa na kazi niliyompa aifanye.Hata hivyo nashukuru Mungu Austin anaendelea vyema na afya yake tayari imeimarika” akasema Ernest “ Sawa Ernest ni hilo tu nililotaka kukutaarifu na ninashukuru umelipokea na kuahidi kulifanyia kazi.Mchunge sana Yule Mukasha si mtu mzuri “ “Tayari ninamfahamu kwa hiyo usiwe na shaka naye nitamshughulikia.Nitamuelekeza kamanda wa polisi Dar es salaam aimarishe ulinzi nyumbani kwenu na kwa Monica pia.Nataka kuwe na ulinzi wa askari wenye silaha kwa saa ishirini na nne” “ Hapana Ernest usifanye hivyo.Kwa sasa Monica hafahamu chochote kuhusu wewe kuwa baba yake na ukifanya hivyo utamuogopesha sana.Mdhibiti Mukasha kwanza na endapo kutatokea kitisho chochote basi nitakuomba ulinzi lakini kwa sasa hakuna haja ya ulinzi wowote.Vile vile ukiweka askari wa kutulinda Ben atajiuliza maswali mengi na inaweza kuleta mtafaruku mwingine kati yetu kwani atajua mimi na wewe bado tunaendeleza mahusiano yetu.Sitaki matatizo yoyote na Ben kwa sasa” akasema Janet “Janet ni jukumu langu kama baba wa Monica kumlinda na kuhakikisha anakuwa salama.I wont forgive myself if anything bad happens to Monica” akasema rais “Ernest usiwe na haraka.Haya mambo yanakwenda taratibu .Ukienda haraka haraka utaharibu kila kitu.Lipe nafasi suala hili na wakati ukifika kila kitu kitakuwa wazi na utafurahi na mwanao” akasema Janet “ Janet uko sahihi lakini nina hamu sana ya Monica afahamu kuwa mimi ni baba yake mzazi ila nitafuata ushauri wako na nitasubiri.Lakini tafadhali naomba kama kuna jambo lolote lonalomuhusu Monica unalodhani ninapaswa kulifahamu usisite kunitaarifu” “Nitakujulisha Ernest.Una haki ya kufahamu kila kitu kuhusu mwanao.” Akasema Janet
******************