MK254
JF-Expert Member
- May 11, 2013
- 32,408
- 50,809
Mzee aliyewashambulia kiongozi wa Cord Raila Odinga na gavana wa Kwale Salim Mvurya kwa bakora wakati wa mkutano Kinango, Kwale Septemba 29, 2014. Picha/FAROUK MWABEGE Na FAROUK MWABEGE
Imepakiwa - Monday, September 29 2014 at 16:54Kwa Mukhtasari
Kizaazaa kilizuka leo katika mkutano wa Cord eneo la Kinango kaunti ya Kwale baada ya mwanamume mmoja kumshambulia Raila Odinga na gavana Salim Mvurya kwa bakora.
KIZAAZAA kilizuka katika mkutano wa CORD eneo la Kinango kaunti ya Kwale baada ya mwanamume mmoja kumshambulia Raila Odinga na gavana Salim Mvurya kwa bakora.
Mwanamume huyo alijitosa uwanjani wakati wawili hao walipokuwa wakijiburudisha na ngoma ya kitamaduni ya Sengenya na kuwacharaza kwa bakora migongoni.
Tukio hilo lilitokea kwa kasi mno kiasi cha kuwapata walinzi wa viongozi hao katika hali ya mshangao kwa sababu hawakulitarajia.
Kitendo hicho kilizua patashika ambayo iliwalazimu walinzi kumbeba mwanamume huyo hobela hobela huku wakiwa na nia ya kumuadhibu.
Hata hivyo Bw Mvurya aliingilia kati na kuwarai walinzi hao wasimpige jamaa huyo aliyekuwa ametaharuki si haba.
Baada ya kuponea chupu chupu mwanamume huyo alitimua mbio na kabla ya wanahabari kumfikia na kumdadisi.
Punde waliporudi jukwaani Bw Odinga na Bw Mvurya walionekana kuwa wenye maumivu makali ila walijikaza kisabuni na kuendelea na mkutano huo.
Mbali na jamaa huyo kutoweka duru za kuaminika ziliarifu Taifa Leo kuwa alitenda kitendo hicho kutokana na kughadhabishwa kwake na hatua ya wawili hao kusakata ngoma na mkewe.
Wakazi hao ambao hawakutaka kutajwa walisema kuwa mkewe jamaa huyo alikuwa miongoni mwa wanamitindo waliokuwa wakisaka ngoma katika mkutano huo.
Hata hivyo ilikuwa vigumu kuthibitisha taarifa hizo kwani wengine wao walisikika wakisema kuwa jamaa huyo alikuwa amepagawishwa na ngoma hiyo ya kienyeji iliyokuwa imetia fora.
Baraka
Mkutano huo uliendelea kama kawaida ila baadaye kisa kisichokuwa cha kawaida kilitokea tena pale ajuza mmoja alipomjongelea Bw Raila na kumbusu mkono.
Walinzi waliokuwa macho walitaka kumkamata mwanamke huyo mkongwe ila Bw Odinga alitaka wamuachilie.
"Mwacheni mama aje kwangu hizi ni baraka kutoka kwa mungu na ishara tosha kuwa mola yuko pamoja nasi," Bw Odinga alisikika akisema.
Mwanamke huyo aliyembusu zaidi ya mara tatu alisikika akimwambia Bw Odinga "Tuokoe baba! Tuokoe mwanangu! Taifa hili linakuhitaji!"
Last edited by a moderator: