Ogah,
Ahadi ni deni. Nimerudi kutoa tathmini yangu kuhusu mkutano wa Houston.
Mimi nilikwenda kama mtazamaji (observer), unajua tena kwa jina kama langu sipendi kupitwa na kitu. Mgeni mwalikwa alikuwa rais Kikwete na nasikia mkutano uliahirishwa kutoka April hadi Oktoba ili kum-accomodate na kwa mujibu wa ombi lake. Kwa hiyo tulishangaa tulipoarifiwa kuwa ameamua kurudi nyumbani mapema kufungua mkutano wa bunge la Commonwealth Arusha. Baadhi tukajiuliza ni nani anayemtayarishia rais ratiba yake? Eniwei hayo yakawa beside the point.
DICOTA ni kundi la Watanzania wa fani mbalimbali waliojikusanya ili kuweza kuchangia na kushiriki katika uwekezaji na biashara nyumbani. Alihutubia Bernard Membe, waziri wa mambo ya nje akimwakilisha rais na pia kulikuwa na viongozi mbalimbali wa serikali ya Tanzania na idara zake kama vile Emmanuel Ole Naiko wa TIC, mwakilishi wa CRDB, Naibu gavana wa BOT, mfanyibiashara maarufu Elvis Musiba na Felix Mosha wa NICO. Wote walihimiza umuhimu wa Watanzania walioko diaspora kuwekeza nyumbani. Siyo lazima uwe na mtaji mkubwa lakini kama kuna Watanzania 10 na kila mmoja akichanga dola elfu moja tayari mnazo elfu kumi ambazo zinaweza kuwekezwa Bongo.
Mbali na uwekezaji na biashara, yalijadiliwa pia masuala ya dual citizenship, ambapo Membe aliwahakikishia wadau kuwa bado linashughulikiwa na yeye anaunga mkono kabisa kutolewa kwa duo citizenship kwa sababu, kama alivyosema, serikali inatambua mchango wa raia wake waliozamia nchi za nje kwa sababu kedha wa kadhaa, na wakati huo huo, kama wamechukua uraia wa nchi nyingine za kimaslahi basi wananyang'wanywa uraia wa Bongo. Hiyo aliiita kuwa ni "contradiction" ambayo serikali inapaswa kuishughulikia na wanalishughulikia. Suala la urasimu ambapo mtu anayetaka kuanzisha kampuni inamchukua hadi miezi sita kukamilisha taratibu pia lilijadiliwa. Suala la madini likagusiwa na inaonekana viongozi serikalini wanatambua kasoro zilizopo katika mikataba. Lakini tuliondoka bila kuhakikishiwa ni hatua gani zinachukuliwa kuondoa kasoro hizo. Niliondoka nikiamini kuwa serikali imepania kuwashirikisha na kuwasaidia raia wa Tanzania walioko nje wanaotaka kuwekeza nyumbani kwa kuondoa adha na kero wanazokumbana nazo wakati wanapotaka kuwekeza nyumbani. Tusubiri tuone kama zilikuwa ahadi hewa au la. Kama nilivyosema, nilienda Houston kama mtazamaji, lakini nimeondoka nikivutiwa na wazo na malengo ya DICOTA. Natumaini wata- update website yao ili sote tuweze kujionea kile wanachojaribu kufanikisha.