Rais, Makamu wa Rais, Waziri Mkuu wanawezaje kushitakiwa/kuwajibishwa?

Rais, Makamu wa Rais, Waziri Mkuu wanawezaje kushitakiwa/kuwajibishwa?

Parabolic

JF-Expert Member
Joined
Dec 3, 2013
Posts
2,922
Reaction score
3,252
Akizungumza Jumapili Agosti 24, aliyekuwa Balozi wa Tanzania nchini Cuba, Humphrey Polepole alipendekeza kuwepo kwa sheria ya kuwawajibisha viongozi kwa matendo wanayofanya wawapo madarakani.

Je, sheria za Tanzania zinasemaje kuhusu viongozi wa juu akiwamo Rais wa Jamhuri ya Muungano, Makamu wa Rais na Waziri Mkuu kushitakiwa?

Rais wa Jamhuri ya Muungano

Kwa mujibu wa Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Ibara ya 46(1), Rais wa Jamhuri ya Muungano ana kinga ya kutoshitakiwa, inasema: “Rais hatashtakiwa mahakamani kwa kosa lolote wakati akiwa madarakani.”
Kinga hiyo ni kwa kesi za madai na jinai.

Njia Pekee ya kumwajibisha, ikiwa pamoja na kumuondoa madarakani Rais ni kupitia Bunge la Jamhuri ya Muungano kwa utaratibu wa impeachment (Ibara ya 46A ya Katiba).

Hapo wabunge wanaweza kupendekeza hoja ya kumwondoa Rais kwa misingi ya kuvunja Katiba, kukiuka sheria za nchi, kutenda vitendo vya rushwa na kuendesha nchi kinyume cha maadili ya uongozi.

Shauri hili likikubalika bungeni, linapelekwa Mahakama ya Rufaa kuthibitisha tuhuma kabla ya Rais kuondolewa madarakani.

Makamu wa Rais

Kwa kujibu wa Katiba Ibara ya 50(2): Makamu wa Rais ana kinga sawa na Rais kuhusu mambo anayoyafanya kazini kwa mujibu wa Katiba. Hivyo, hawezi kushtakiwa mahakamani kwa mambo ya utendaji wakati akiwa madarakani.

Njia ya kisheria ya kumuondoa ni kupitia azimio la Bunge (kama ilivyo kwa Waziri Mkuu) kwa sababu ya uvunjaji wa Katiba, utovu wa maadili au kushindwa kutekeleza majukumu.

Waziri Mkuu

Anaweza kuwajibishwa bungeni (si moja kwa moja mahakamani) kupitia, azimio la kutokuwa na imani naye (Ibara ya 53(2) ya Katiba). Akituhumiwa kwa kosa la jinai binafsi (mfano kosa kabla hajawa Waziri Mkuu au nje ya majukumu rasmi), anaweza kushtakiwa mahakamani, lakini akihusiana na utendaji wa kazi za kiserikali, kinga iko pale pale hadi amalize muda wake.

Waziri, Naibu Waziri, na Viongozi Wengine wa Juu

Wanaweza kushtakiwa kwa vitendo binafsi vya jinai au madai. Lakini kwa mambo waliyoyafanya kwa ujumbe rasmi wa kiserikali, mara nyingi hutumia kinga ya kikatiba na kisheria.

Sheria ya BRADEA

Sheria ya BRADEA ni kifupi cha Basic Rights and Duties Enforcement Act, yaani Sheria ya Utekelezaji wa Haki na Wajibu wa Msingi.

Sheria hii ilitungwa mwaka 1994 ili kuweka utaratibu wa kisheria kwa wananchi wanaotaka kwenda mahakamani kudai au kulinda haki zao za kikatiba zilizoorodheshwa kwenye Ibara ya Tatu ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania (Ibara ya 12–29).

Kabla ya sheria hii, kulikuwa na utata juu ya namna wananchi wangeweza kufungua mashauri moja kwa moja wakidai haki za kikatiba.

Mambo muhimu

Inatoa utaratibu wa kufungua shauri ikisema shauri la madai ya ukiukwaji wa haki za kikatiba lifunguliwe kwanza Mahakama Kuu.

Mahakama Kuu ina mamlaka ya kusikiliza mashauri ya ukiukwaji wa haki za msingi na kutoa amri stahiki (mfano: amri ya kuzuia, kutengua sheria, kuamuru fidia n.k.).

Hata hivyo, mwaka 2021, yalifanyika marekebisho kupitia Written Laws (Miscellaneous Amendments) (No. 3) Act, 2021, kifungu cha 4(2–5) kiliongezwa kikidai kuwa:

Marekebisho ya kifungu cha 4 cha BRADEA yaliweka masharti yenye utata, ikiwemo ulazima wa waombaji kuonyesha masilahi binafsi kupitia kiapo, sharti la maombi yote chini ya Ibara ya 26(2) kuendana na Ibara ya 30(3) ambayo ni kwa ajili ya uvunjaji wa haki binafsi, kifungu kilichoweka kwamba Mwanasheria Mkuu pekee ndiye anayeweza kushtakiwa katika kesi zinazohusu viongozi wakuu wa kikatiba, na sharti la kutumia njia zote mbadala kabla ya kufungua shauri la kikatiba.

Marekiebisho hayo yaliibua malalamiko kutoka kwa wadau wakiwamo wanaharakati wa haki za binadamu na wanasheria walipinga marekebisho hayo ya kutaka watu 30 wakafungue pamoja, wakidai yalizuia haki ya kila mtu mmoja mmoja kutetea Katiba.

Hoja yao ilikuwa: Katiba inatoa haki ya kila mtu binafsi kutetea haki zake, hivyo kizuizi cha watu 30 kilikuwa kinapingana na Katiba yenyewe.

Uamuzi wa Mahakama

Kupitia uamuzi wa Mahakama ya Rufaa uliotolewa Juni 13, 2025 ulitangaza kuwa vifungu vya kifungu cha 4 (2), (3), (4) na (5) vya Sheria ya Utekelezaji wa Haki za Msingi na Wajibu (BRADEA), kama vilivyorekebishwa na Sheria ya Marekebisho ya Sheria Mbalimbali (Na. 3), 2020, havina uhalali kikatiba.

Kesi hiyo, iliyofunguliwa na mtetezi wa haki za binadamu Onesmo Olengurumwa aliyewakilishwa na jopo la mawakili maarufu wakiwemo Profesa Issa Shivji, Mpale Mpoki, Dkt. Rugemeleza Nshala na John Seka, alieleza kuwa vifungu hivyo vilifuta kwa vitendo haki ya mashauri ya masilahi ya umma na kudhoofisha nafasi ya kikatiba ya Mahakama.

Mahakama ya Rufaa, kwa uamuzi wa pamoja ulioamuliwa na Majaji Levira, Rumanyika na Ngwembe, ilitoa maamuzi muhimu kadhaa. Ilisema kuwa sharti la waombaji kuthibitisha masilahi binafsi katika mashauri ya masilahi ya umma linapingana na roho ya Ibara ya 26(2), ambayo inamruhusu kila raia kuilinda Katiba.

Mahakama ilisisitiza kuwa Ibara ya 26(2) na Ibara ya 30(3) zina malengo tofauti—26(2) ni kwa masilahi ya umma na 30(3) ni kwa haki binafsi—na haziwezi kuunganishwa kitaratibu. Aidha, ilibaini kuwa kifungu kidogo cha (4) cha kifungu cha 4, kilichozuia kesi za moja kwa moja dhidi ya viongozi wakuu kama Rais na Jaji Mkuu, kilikiuka kanuni za uwajibikaji na usawa mbele ya sheria.

Sharti la kutumia njia mbadala lilionekana kuwa na utata na haliwezekani, hasa kwa kuwa hakuna njia mbadala zilizo wazi kwa waombaji wa mashauri ya masilahi ya umma. Mahakama pia ilifafanua kuwa kiwango cha uthibitisho katika mashauri ya kikatiba ni "uwiano wa uwezekano" (balance of probabilities) na siyo "bila shaka yoyote." Uamuzi huu ni hatua kubwa ya kurejesha haki ya kikatiba ya Watanzania kupinga uvunjaji wa Katiba bila kukumbana na vizuizi vya kitaratibu vinavyokwamisha upatikanaji wa haki. Mahakama imeelekeza Bunge kufuta vifungu hivyo ndani ya miezi 12, na iwapo halitafanya hivyo, vitakoma kuwa na nguvu ya kisheria.
 
Yameandikwa tu hayo jinsi ya kuwashtaki lakini hizo taratibu zote zipo chini yao, ni ngumu kushtaki
 
Back
Top Bottom