Mtumiaji wa Mtandao wa TikTok anayetumia jina la Leonard Clasic (User4692412178624), Julai 3, 2023 mchana, aliweka video moja kwenye ukurasa wake pasipo kufafanua chochote.
Video hiyo inamuonesha Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan akikemea baadhi ya watendaji wa Serikali wanaoingia mikataba mibovu na kusababisha hasara kubwa kwa taifa.
Video hii inahusianishwa na Sakata la uwekezaji wa Bandari unaotarajiwa kufanywa na Kampuni ya DP World ya Dubai, imeendelea kusambaa sehemu mbalimbali huku baadhi ya watu wakimpongeza Rais Samia kwa kutoa kauli hiyo.
Video hiyo inamuonesha Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan akikemea baadhi ya watendaji wa Serikali wanaoingia mikataba mibovu na kusababisha hasara kubwa kwa taifa.
Video hii inahusianishwa na Sakata la uwekezaji wa Bandari unaotarajiwa kufanywa na Kampuni ya DP World ya Dubai, imeendelea kusambaa sehemu mbalimbali huku baadhi ya watu wakimpongeza Rais Samia kwa kutoa kauli hiyo.
- Tunachokijua
- Juni 10, 2023, Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania lilipitisha Azimio la kuunga Mkono Mkataba wa Uwekezaji wa Bandari kati ya Tanzania na kampuni ya DP World ya Dubai.
Pendekezo hili lenye lengo la kuanzisha Ushirikiano wa Kiuchumi na Kijamii katika uendelezaji wa Maeneo ya Bandari Nchini lilisomwa na Waziri wa ujenzi na Uchukuzi, Prof. Makame Mnyaa Mbarawa ambapo pamoja na mambo mengine alidai kuwa Serikali iliamua kutia saini ushirikiano ili kuongeza ufanisi Bandarini, ambapo ndio lango kuu la uchumi.
Kupitishwa kwa Azimio hili kuliongeza ukubwa wa Mjadala uliokuwepo hata kabla ya kupelekwa Bungeni. Mathalani, Juni 8, 2023, Mdau wa JamiiForums aliweka andiko lenye kichwa cha habari "Aibu: Bandari yakiri kusaini Mkataba na Wadubai"
Hii inaonesha kuwa aina hii ya mijadala ilikuwepo hata kabla ya kupitishwa kwa Azimio la kukubali uwekezaji huo Juni 10, 2023.
Kauli ya Rais Samia kuhusu Mkataba wa DP World
Juni 7, 2023, Mwenyekiti wa CHADEMA (Taifa) Freeman Mbowe alitoa kauli kwa niaba ya chama chake iliyopokelewa kwa mitazamo tofauti.
Pamoja na Mambo mengine, Mbowe alihoji kwanini Bandari za Zanzibar hazikuwepo kwenye Mkataba huo, na kwamba Rais Samia na Waziri Mbarawa wanatoka upande wa Zanzibar, iweje kama mkataba huo una manufaa makubwa wakuu hawa hawakuiingiza Zanzibar?
"Katika msingi huohuo ndugu zangu watanzania, katika mazingira haya, Watanganyika wana haki ya kuhisi kwamba Wazanzibari hawa wawili wanagawana mali za Tanganyika kwa wageni kwa faida zao binafsi wakati wakilinda mali zao wenyewe katika nchi yao ya Zanzibar"
Katika hali inayohusianishwa na kujibu kauli ya Freeman Mbowe, jioni ya Juni 12, 2023, akiwa Jijini Mwanza, Rais Samia alisema;
“Baada ya kusema hayo jioni imeingia, na ninaambiwa wapo wengine wengi kule nilitaka tu niwasalimie, lakini salamu moja kubwa ni kwamba Mama huyu ni Mtanzania. Atafanya kila analoweza kufanya Tanzania iendelee. Na Tanzania ni moja, haigawanyiki wala haiuziki. Kwa hiyo ndugu zangu mama ni Mtanzania, maendeleo yetu ndio muhimu. Kila linalofanyika ni kwa maendeleo ya Watanzania”
Tangu siku hiyo, Rais Samia hakuwahi kusikika akitoa kauli yoyote inayohusiana na Mkataba wa uwekezaji wa DP World nchini.
Chanzo cha video inayosambaa Mtandaoni
JamiiForums imebaini kuwa video inayosambaa kwenye mitandao ya kijamii imekatwa kutoka kwenye mojawapo ya channel za YouTube zilizokuwa mbashara kwenye tukio la Upokeaji wa Ripoti ya Ukaguzi wa Hesabu za Serikali kwa Mwaka 2021/22 kutoka kwa CAG na Ripoti ya TAKUKURU ya mwaka 2021/22 kutoka kwa Mkurugenzi wa Taasisi hiyo Machi 29, 2023.
Tukio hilo liliripotiwa pia na JamiiForums ambapo sasisho la halfa hiyo lenye kichwa cha habari "Rais Samia apokea Ripoti za CAG na TAKUKURU za Mwaka 2021/2022" liliwekwa.
Kwenye muda wa 2:16:35 Rais Samia anasikika akisema;
"Mikataba mingine jamani, mikataba hii ina aina zake. Unajua kabisa mkataba wa aina hii hauwezi kuwa na vifungu hivi vikawa ndani ya huo mkataba. Lakini unaukuta mkataba wa aina hiyo na kuna kifungu cha ajabu ajabu kimo ndani ya huo kkataba, ambacho hakipaswi kuwemo kwenye huo mkataba. Lakini umepita kote, njia zote na mkataba ukaenda ukafanya kazi, sasa waliofanya kazi wanadai"
Anaendelea;
"Sasa unawapa watu wengine ebu someni huu mkataba wanasema huu mkataba mama haukupaswa kuwa na vifungu hivi. Sasa namuuliza ilikuwaje vikaingia, wanaangaliana machoni. Dhambi zetu sisi wenyewe, sisi wenyewe tunaua nchi yetu. Unaruhusu vifungu vya ajabu vinaingia kwenye mikataba visivyopaswa. Huko kwenye mikataba katazameni vizuri"
Maneno haya yanafanana na yale yanayosikika yakitamkwa kwenye video inayosambaa. Aidha, nguo alizovaa Rais Samia pamoja na Mandhari ya eneo husika ni yaleyale.
Hii inathibitisha kuwa video inayosambaa haina uhusiano na kauli ya Rais kuhusu sakata la Uwekezaji wa kampuni ya DP World kwenye Bandari ya Dar es Salaam.
Chanzo cha Mjadala wa DP World na yanayoendelea hadi sasa
Mjadala unaohusu uwekezaji wa Kampuni ya DP World nchini uliibuka Juni 6, 2023 kwenye mitandao ya kijamii.
Miongoni mwa watu waliotoa maoni yao ni aliyewahi kuwa Meya wa Jiji la Dar es Salaam, Boniface Jacob ambae aliweka andiko kwenye mtandao wa Twitter lenye kichwa cha habari "Hatimaye CCM waiuza rasmi Bandari yetu ya Dar es Salaam"
Chapisho hili liliambatana na Barua iliyotajwa kuwa ni azimio la Bunge lilidainkuwa Serikali ya Tanzania iliipa kampuni ya DP World kuendesha bandari ya Dar es Salaam kwa muda wa miaka 100.
Aidha, wananchi mbalimbali kwa nyakati tofauti wameshiriki kutoa maoni yao kuhusu suala hili akiwemo Mgombea urais wa CHADEMA (2020) Tundu Lissu, Profesa Issa Shivji na Balozi Mstaafu Dkt. Slaa.
Juni 19, 2023 yalifanyika maandamano yanayopinga uwekezaji huu na Julai 3, 2023, Mahakama Kuu kanda ya Mbeya ilianza kusikiliza Shauri lililofunguliwa na Wanasheria Boniface Mwabukusi na mwenzake wakitaka Mahakama iweke zuio kwa kampuni ya DP World kuhusu uwekezaji wake nchini hadi pale ambapo kesi ya msingi itakapomalizika.