Lakini hebu tuulizane maswali
Iconoclastes hivi una uhakika leo huyo Hassan na kundi la viongozi wenzie wa IEBC wakiondolewa ndio hili zogo litakua limeisha?
Ninachojua ni kwamba Afrika, labda Yesu mwenyewe ndiye asimamie uchaguzi ndio uwe wa huru asilimia mia kwa mia. Wizi wa kura Kenya hutendeka tu kwa vyoyote vile, na huwa unatendeka hata kwa upinzani, unakuta hata maeneo ya upinzani wanakua na takwimu zinazidhihirisha wizi umetendeka huko.
Ilmradi viongozi wanashindana kila mtu anataka aongoze nchi, pamoja na wapambe wao, lazima panakua na mvutano wa shika nikamate, pasua kichwa. Hata kule Tanzania tulishuhudia unyanyasaji wa hali ya juu haswa pale Zanzibar, japo wao huwa waoga na serikali ilijaza huko askari wa JWTZ hadi jamaa wakanywea tuli. Ikizingatiwa Waswahili walivyo waoga hata kuinua kichwa ili walalamike hawakuthubutu, japo watakuambia eti ni kwasababu Nyerere aliwafanya wakawa wastaarabu, na ndio maana ukiwa Tanzania wakati wa kampeni, TV huonyesha hotuba za Nyerere sana. Yaani watu wasihoji sera maana Nyerere alisema wawe wastaarabu, Zanzibar iliwalazimu Marekani ndio wahangaike kuwatetea.
Hapa Kenya kwa sasa kitakachowaokoa upinzani ni kuhamasisha wafuasi wao wajisajili kwa mamilioni, yaani hadi hata kura zikiibiwa bado waibuke washindi. Lakini hizi vurugu wanazozifanya zitazidi kuwazika kwenye kaburi la sahau, maana tayari wafuasi wa upande wa serikali wameingiwa na taharuki, hivyo watajitokeza hadi wazee, wagonjwa, walemavu kujisajili kwa nguvu zote ili wazuie upinzani.
Tusipokua makini, 2017 patachimbika maana utakua ni ushindani wa kubanana shingoni na kwenye pua, kila upande watajitokeza kupiga kura kiasi cha kutisha.