msovero
JF-Expert Member
- Jun 30, 2019
- 863
- 1,534
Dodoma. Baraza Kuu la Chama cha Walimu Tanzania (CWT) limemsimamisha rais wa chama hicho, Leah Ulaya kwa madai kuwa ameshindwa kuwaunganisha walimu na kueleza changamoto zinazowakabili.
Kwa uamuzi huo, Leah atasubiri hatima yake katika mkutano mkuu wa CWT utakaofanyika mwaka 2022 ili kujua kama atarudi katika nafasi yake ama la.
Akizungumza na Mwananchi Digital kuhusu uamuzu huo uliotolewa leo Jumatano Septemba 15, 2021, Leah amesema, "ni kweli mpendwa, mambo ya siasa ni magumu sana, nafasi za kuchaguliwa ni changamoto kubwa."
Makamu wa rais wa CWT, Dinah Mathaman ndiye aliyesimamia mkutano huo na shughuli ya upigaji kura ya wajumbe baada ya kuwasilishwa hoja ya kutaka asimamishwe na kisha yeye kupewa nafasi ya kujitetea.
Taarifa zinaeleza kuwa utetezi wake haukuwashawishi wajumbe kubadili nia zao ingawa wachache walionyesha kumtetea.
Mkutano huo umefanyika jijini Dodoma na kutawaliwa na usiri mkubwa ingawa taarifa za vuguvugu za sakata la kiongozi huyo wa juu wa CWT kusimamishwa zilivuja.
Akitangaza matokeo hayo, Mathamani amesema kura zilizopigwa zilikuwa 177 ambapo kura 42 zilimtaka aendelee na wadhifa wake, kura nne ziliharibika na kura 131 zilitaka asimamishwe.
"Kwa matokeo haya rais wa CWT, Leah Ulaya anasimamishwa mpaka hapo mkutano mkuu utakapoitishwa ili kupitia tuhuma zake na kujiridhisha," amesema Mathamani.
Katibu wa CWT, Deus Seif amekataa kuzungumzia jambo hilo akisema ni maamuzi ya wajumbe na kwamba yeye si msemaji.
Ulaya alichaguliwa Mei mwaka 2020 katika mkutano mkuu uliofanyika uwanja wa Jamhuri jijini Dodoma.
credited: mwananchi