Maisha ya Ndoa ya Binti wa Mtume
Mtume rehma na amani ziwe juu yake alikuwa na mabinti wanne ambao ni Zainab, Ummu kuluthum, Ruqaiya na Faatwimatu (Fatuma) . Wote waliolewa, isipokuwa hao watatu yaani Zainab, Ummu Kuluthum na Ruqaiya walifariki kabla ya mtume.
Fatuma Peke yake alifariki baada ya Mtume (s.a.w) miezi sita baada ya Mtume kufariki naye ndio akafuata.
Kwahiyo hapa binti ambaye tunaangalia maisha yake ya ndoa ni Fatuma.
MAISHA YA NDOA
kuoa ni mfungamano wenye nguvu unaowakusanya mwanaume na mwanamke katika kivuli cha maisha ya ndoa kisheria. Mtume rehma na amani ziwe juu yake amesema "kuoa ni sunna yangu na asiyetumia sunna yangu huyo hana shirika nami (yani hajashirikiana na mtume kwa jambo lolote).
Allah anasema Katika Quran 30:21
"Na katika ishara zake za kuonyesha ihsani zake juu yenu ni kuwa amekuumbieni wake zenu katika jinsi yenu ili mpate utulivu Kwao. Na amejaalia mapenzi na huruma baina yenu, bilashaka katika haya zimo ishara kwa wanao fikiri "
Kwahiyo kwa maana hiyo kuoa ni njia ya uchamungu na usafi na ni hifadhi ya afya na ni hifadhi ya tabia njema katika jamii, na ni kinga ya shari na magonjwa.
KUPEWA HABARI YA UCHUMBA
sheria ya kiislamu haikumnyima mwanamke rai yake ya kumchagua mchumba anaye mtaka, mwanamke amepewa haki ya kufanya hivyo na si kuchaguliwa mchumba na watu wengine bali yeye mwenyewe atafanya uamuzi wake.
Kipindi cha Mtume rehma na amani ziwe juu yake, alijiwa na binti mmoja bikra, akilalamika kuwa baba yake amemuoza kwa mwanaume ambaye yeye anamchukia kwa maana nyingine hamtaki huyo mumewe. Basi Mtume akampa uhuru wa kuchagua ama aondoke au abakie katika ndoa yake.
Na mfano mzuri wa uhuru wa mwanamke kuchagua tunauona kwa Bi khadija alipomchagua Mtume pamoja na kwamba walikuwepo watu wenye fedha na wafanyabiashara na wenye vyeo katika jamii ya makuraishi lkn aliamua kumchagua Mtume (s. a. w).
Je bibi Fatuma katika Uchumba wake na Sayidina Ally ilikuwaje?
Ifahamike hawa wawili waliishi nyumba moja, ulipo fika wakati wa kuolewa bibi Fatuma,baada ya sayidina Ally kuomba posa kwa Mtume rehma na amani ziwe juu yake. Mtume aliingia chumbani kwa bibi Fatuma akamwambia "Ewe binti yangu hakika mtoto wa baba yako mdogo Ally amekuchumbia sasa unasemaje?
Bibi Fatuma akalia kisha akasema "Ni kama kwamba ewe baba yangu umeniweka akiba kwa malofa wa kikuraishi" Mtume akamwambia binti yake kuwa "Namuapa Allah aliyenituma kudhihirisha haki sikuzungumza chochote katika habar hii, mpaka alipo nipa idhini Mwenyezi Mungu kutoka mbinguni juu jambo hili " Bibi Fatuma akasema kuwa "Nimeridhika na yale aliyoyaridhia kwangu Mwenyezi Mungu
na Mtume (s. a. w).
Kwahiyo hapa tunaona bibi Fatuma katendewa haki ya kusikilizwa rai yake na uamuzi wake. Na kigezo alichotumia Mtume kuchagua mchumba sio mali wala hadhi au cheo cha mtu bali aliangalia dini na tabia njema. Na mwanamke vile vile anatakiwa amchague mtu mwenye dini na tabia njema.
KUMTAZAMA MCHUMBA
Swala la kumtazama mchumba katika uislamu limeruhusiwa ila sharti lazima awepo ndugu wa karibu wa huyo mchumba, hakuna kizuizi cha kukaa nae na kuzungumza nae iwapo atakuwepo maharimu wake,yaani ndugu yake, kaka au mwingine katika familia.
Mtume rehma na amani ziwe juu yake alimwambia Mughira wakati alipokuwa amemchumbia mwanamke, je umemtazama? Mughira akasema hapana. Mtume akasema nenda na umtazame hakika kumtazama kutapelekea kukubaliana na kutengemaa maisha ya ndoa. Hapo mwenye kuchumbia atajua mchumba wake yukoje, kiakili na mtazamo wake kimaisha, si uzuri wa mwili tu bali uzuri wa fikra na ukunjufu wa moyo.
BIBI FATUMA NA SAYYIDINA ALLY WACHUNGUZANA
Sayyidina Ally alipofikia umri wa miaka ishirini na moja alikuwa hajaoa. Naye bibi Fatuma alikuwa amefikia umri wa miaka kumi na nane. Siku moja bibi Fatuma alimuambia Sayyidina Ally kuwa mimi nakushinda mimi ni mkubwa kuliko wewe. Wakati huo huo alifika Sayyidina Abbas akasema "ewe fatuma hakika umezaliwa wakati maquraishi wanajenga kaaba na Mtume akiwa na umri wa miaka 35 ama wewe Ally ulizaliwa kabla ya hapo kwa miaka mingi.
Lakini yote hayo yanaonyesha jinsi walivyotaka kufahamiana vizur kabla ya kuoana. Hivyo usikubali kuoa au kuolewa bila kujua unaolewa na nani.
MAHARI YA FATUMA
Sheria ya kiislamu haikuweka mipaka juu ya mahari ambayo anatoa mume kumpa mkewe. Bali sheria imeliacha jambo hilo kuwa ni maridhiano ya pande mbili.
Mtume rehma na amani ziwe juu yake amesema "hakika wanawake wenye baraka zaidi ni wale wenye mahari nyepesi "
Basi wakati sayyidina Ally alipotaka kumuoa bibi Fatuma, Mtume alimuuliza sayyidina Ally, je una chochote cha kutoa ambacho kitakua ndiyo uhalali wako wa kumuoa Fatuma? Ally akasema hapana. Mtume akamkumbusha vazi la kivita alilompa zawadi ambalo thamani yake haizidi dirhamu nne. Ally akasema lipo , Mtume akasema basi Fatuma iwe ndiyo mahari yake.
NASAHA KWA MAWALII NA WENYE KUOA
Mtume rehma na amani ziwe juu yake ni kiigizo chema kwa wazazi na wenye kuoa katika jambo hili la mahari. Sayyidina Umar al Faaaruq anasema "eleweni kama jambo la kuzidisha mahari lingekuwa ni jambo la kuheshimika katika dunia au la uchamungu mbele ya Allah, mbora wenu juu ya hilo angekuwa nabii Muhammad, hakutoa mahari kumpa mwanamke katika wake zake, wala hakupewa mahari mwanamke katika binti zake zaidi ya waqia kumi na mbili. Hivyo eleweni kwamba mahari sio thamani ya mwanamke mpaka iwe sababu ya wazazi kufanya ghali"
Uislamu umefanya njia kuwa nyepesi, na Mtume kaonyesha njia kwa maneno na vitendo.
Hali ilivyo hivi sasa wazazi wengi wameshikamana na desturi za kijahili na mila zilizo mbali na uislamu, wanazidisha mahari na kukataa kuwaoza mabinti zao mpaka mume atoe maelfu ya fedha. Wamegeuza kana kwamba mwanamke ni bidhaa inayouzwa na kufanyiwa biashara. Kutokana na hayo wanawake wanakuwa hawaolewi na hivyo kufanya mambo machafu kwasababu vijana wanashindwa kuoa na wanabaki kufanya zinaa.
NDOA YA BIBI FATUMA
Baada ya masuala ya uchumba kukamilika na mahari kulipwa, kilicho fuata ilikuwa ni ndoa. Mwaka wa pili baada ya Mtume rehma na amani ziwe juu yake kuhamia madina, na baada ya Mtume kurejea kutoka katika Vita vya badri, ilifanyika ndoa ya bibi Fatuma na sayyidina Ally.
Baada ya ndoa kufungwa, ukoo wa mutwalibu walifurahi upeo wa kufurahi, wakalisha watu Chakula cha harusi (walimatul-ars). Sayyidina Hamza akachinja baadhi ya ngamia wake na Saad r. a akachinja kondoo wake, na masahaba wa kiansar wakaleta vibaba vya mahindi wakawalisha watu. Kisha baada ya sherehe watu wakaondoka hali ni wenye furaha.
Hapa tunajifunza kuwa kusaidiana katika sherehe kama hii ya ndoa ni jambo zuri, utaona ni namna gani walichangia masahaba, mitwalib na wengineo kuhakikisha harusi ya binti wa Mtume inakuwa ya kupendeza.
MTUME AWAOMBEA DUA FATUMA NA ALLY
bibi Fatuma alipokwenda nyumbani kwa Ally r. a hakukuta nyumbani isipokuwa changarawe zilizotandikwa na mto wa ngozi uliojazwa majani, pamoja na glass moja na jagi moja.
Mtume rehma na amani ziwe juu yake akaomba apewe chombo chenye Maji, akaomba yale aliyokadiriwa kusema, akatemea mate ndani ya Maji hayo kisha akampaka Ally kifuani mwake na usoni mwake. Kisha akamwita Bibi Fatuma akamnyunyuzia maji yale na akamuombea kiasi alichojaliwa. Dua aliyowaombea ni hii :
"ewe Mwenyezi Mungu wabarikie ndani yao na nje yao na uwabarikie kizazi chao"
MATUMIZI KATIKA NDOA
mwanamke anatakiwa apate matumizi yake kutokana na uwezo na ni juu ya mwanaume kuishi na mkewe kutokana na uwezo wake. Ajiepushe na kila chenye kuharibu maisha ya mkewe. Na ni juu yake kumletea chakula anachokihitaji, na amuondolee taabu ya kwenda huku na huko nje ya nyumba yake, ili aweze kutekeleza wajibu wake kwa namna iliyo nzuri. Basi matumizi ya mume kwa mkewe yasiwe ya fujo wala kwa ubakhili.
Anasema Allah:
"Mwenye wasaa agharimu kadri ya wasaa wake na yule ambaye amepungukiwa riziki yake, atoe katika alichojaaliwa na Mwenyezi Mungu. Mwenyezi Mungu hamkalifishi mtu yoyote kwa kadri ya alichompa, atajaalia Mwenyezi Mungu baada ya dhiki faraja"
Na amesema Mtume:
"Mwogopeni Allah muwatendee wema wanawake, hakika nyie mmewachukua kwa amana ya Mwenyezi Mungu na mmehalalishiwa tupu zao kwa maneno ya Allah, basi wanayo haki kwenu kuwalisha na kuwavika kwa wema"
Huu ndio uislamu. Tugeuke nyumbani kwa Sayyidina Ally hali ilikuwaje?
Kama tulivyoona huko nyuma hali ya sayidina Ally kiuchumi haikuwa nzuri, wanandoa hawa waliishi maisha magumu na ya dhiki, siku ile ya kwanza hapakuwa na kitanda cha sita kwa sita wala tandiko la sita kwa sita tofauti na tulivyozoea sisi,lakini bibi Fatuma hakuona tabu.
Kitanda alicholalia ilikuwa ni ngozi ya kondoo na mto ni ngozi ambayo imejazwa majani,shuka la kujifunika ni dogo haliwatoshi. Wakijifunika juu kichwa miguu inabaki wazi na wakijifunika miguu vichwa vinabaki wazi, je wewe binti wa leo ungeweza kuvumilia maisha haya?
BIBI FATUMA AOMBA MSAADA KWA BABA YAKE
kama tulivyoona maisha sayyidina Ally hayakuwa mazuri kiuchumi hivyo alishindwa kumuajiri mfanyakazi wa kumsaidia mkewe shughuli mbali mbali kama kuchota maji, kutwanga, kupika mikate na mengineyo. Mume huyu alipata sana tabu kuona mkewe kipenzi anachoshwa na kazi za nyumbani,akadhoofika na kukonda kwa mawazo. Lakini hana namna ya kuiondoa hali hiyo ili apate kumfariji mkewe kwa kumletea mtumishi.
Basi akamgeukia mkewe Fatuma akamwambia " nimebeba maji ya kuwanywesha ngamia toka kisimani ewe Fatuma mpaka kifua kinauma, na Kwa hakika Allah amemletea baba yako (mtume s. a. w) mateka, basi nenda umuombe akupe mtumishi "
Bibi Fatuma naye akasema "na mimi namuapa Allah nimetwanga mpaka mikono yangu imevimba na inalengalenga damu "
Basi Fatuma alipoenda kwa baba yake aliona haya kusema shida, kisha akarudi, mumewe akamuuliza vipi imekuwaje? Akajibu nimeona haya kumuomba.
Basi Ally Akamwambi mkewe basi twende wote kwa Mtume rehma na amani ziwe juu yake, walipofika na baada ya kusalimia, bwana Ally alisema
"Ewe Mtume wa Allah, namuapa Allah nimechota maji ya kuwanywesha ngamia mpaka kifua kinauma " Bibi Fatuma naye akasema "Nimetwanga mpaka mikono imevimba na kulengalenga damu, na kwa hakika Allah amewaleta mateka kwako na wepesi basi tupe mtumishi "
Mtume rehma na amani ziwe juu yake akasema
"Namuapa Allah sitakupeni mtumishi halafu niwaache masufi wakifunga matumbo yao kwa njaa kwani sina cha kuwalisha, nitawauza hao mateka kisha niwalishe hao masufi kutokana na thamani ya hao mateka. "
Basi sayidina Ally na mkewe wakarudi bure nyumbani,mpaka hapa tunapata mafunzo mengi, kwanza mke na mume wanatakiwa kusaidiana katika maisha pale inapobidi, kama dereva na utingo pale gari linapo kwama husaidiana kulisukuma ili safari iendelee.
Pia kushauriana ili kupata mbinu mbadala ,kama kwa wazazi wa mmoja wao kuna hali nzuri, basi si vibaya kuomba msaada, na ni juu ya wazazi kuwasaidia watoto wao ili wajikwamue kimaisha.
Tatu kama hali inaruhusu mume amtafutie mke Mtumishi ili aweze kutimiza majukumu yake mengine barabara. Mwisho akija kwa wazazi, kwanza aulizwe kilichomleta kisha ndio afanyiwe mambo mengine.
MTUME AWAELEKEZA NJIA BORA ZAIDI YA KUFANYA BADALA YA MTUMISHI
Mtume rehma na amani ziwe juu yake hakuwaacha hivi hivi baada ya kuwaambia kuwa mateka wale atawatumia kwa kuwasaidia masufi, alitafuta njia mbadala. Alikwenda nyumbani kwao na akakuta kweli wana hali mbaya, shuka wajifunikayo haiwatoshi, ukifunika kichwa miguu inabaki wazi na ukifunika miguu basi kichwa kinabaki wazi.
Akawaambia "Tulieni hapo, je nikupeni habari iliyo bora kuliko mtumishi mliyemuomba?" wakasema ndio ewe Mtume wa Allah. Mtume rehma na amani ziwe juu yake akasema: Ni maneno aliyonifundisha Jibril (huyu ni yule malaika mkuu ambaye hushusha ufunuo kwa manabii na mitume)
Semeni subhanallah mara kumi kila baada ya swala, alhamdulillah mara kumi na allahu Akbaru mara kumi, na mtakapotaka kulala semeni subhanallah mara 33,alhamdulillah 33 na Allahu Akbaru mara 34.
Sayyidina Ally r. a anasema kulwa, namuapa Allah sikuacha kuyatumia maneno hayo aliyonifundisha Mtume. Hapa tunajifunza kuwa wazazi wajitahidi kwa kila namna iwezekanavyo kuwasaidia watoto wao waliomo katika ndoa. Mfano kama Baba wa binti ana uwezo asione vibaya kumsaidia mkwe wake, kwani kumsaidia mkwewe ni kumsaidia binti yake.
KUISHI NA MUME KWA WEMA
Msingi wa maisha ya ndoa ni upole na uvumilivu na kuyafumbia macho matatizo madogo madogo ambayo yanatokea kwa mmoja wa wanandoa kuteleza. Na katika mambo yanayo dhihirisha wanandoa kuishi kwa wema ni mume kuingiza furaha kwa mkewe na hivyo hivyo mke kwa mumewe. Mume aheshimu utu wa mkewe na awe awe mkunjufu wa Sura usoni kwa mkewe (aonyeshe tabasamu). Wakeze Mtume rehma na amani iwe juu yake walikuwa wakimfanyia maneno yenye kumuudhi, wanakaa mpaka usiku bila kumsemesha, lakini Mtume alivumilia kwasababu ya kuwafanyi upole na ukarimu.
Allah anasema:
"Na kaeni nao kwa wema, na kama mkiwachukia basi (msiwaache) kwani huenda mkakichukia kitu, na Mwenyezi Mungu ametia kheri nyingi ndani yake "4:39
Kwa mujibu huu tunaona maisha ya bibi Fatuma na mumewe yalivyokuwa mazuri wakipendana, wakishirikiana katika taabu na raha na hivi ndivyo wanavyotakiwa kuishi wanandoa. Lakini je waliishi tu bila mikwaruzano?
UGOMVI WAZUKA BAINA YA BIBI FATUMA NA MUMEWE
Maisha yalikwenda vizuri katika nyumba hii tukufu na kuishi kwa furaha na amani, huku wakizungukwa na mapenzi na huruma. Lakini mambo hayaendi siku zote katika mpango wa namna moja.
Tabia ya Ally r. a ilikuwa ya ukali na udhibiti wa mambo, na bibi Fatuma alikuwa mwepesi, mpole anayeweza kuvumilia tabu na anayehitaji upole toka kwa mumewe.
Siku moja sayyidina Ally alidhihirisha ukali kwa mkewe, bibi Fatuma akasema "Namuapa Allah nitakushitaki kwa Mtume " Fatuma akaenda kwa Mtume na kushitaki ukali wa mumewe, huku mumewe nae alimfuata nyuma, baada ya Mtume rehma na amani ziwe juu yake kusikia mashtaka yale, akakaa kimya kitambo kidogo kisha akasema
"Ewe binti yangu, sikia na upende kusikia (ukiambiwa) hakika hawi mwanamke wa maana,mwanamke ambaye hatekelezi matakwa ya mumewe,na mume akabakia kimya (lazima acharuke).
Basi Mtume aliwasuluhisha hao wanandoa na mambo yakerejea katika hali yake ya awali.
BIBI FATUMA AJIFUNGUA WATOTO
Siku ile ya ndoa Mtume rehma na amani ziwe juu yake aliwaombea dua hii "Ewe Mwenyezi Mungu wabarikie ndani yao na nje yao na uwabarikie kizazi chao"
Basi akawarudhuku watoto wanne, wawili wa kiume na wawili wa kike, wa kwanza Hussein, wa pili Hassan, Zainab na wa mwisho ummu kulthumu.