Hivi kweli tatizo ni viongozi tu ama tatizo ni jamii nzima ya waafrika? Inawezekanaje tukawa na viongozi wabovu katikati ya jamii ya watu waliostaaribika?
LOoo, hilo swali zito hasa ambalo linahitaji fikra pevu kulichambua. Huenda kukawa na siku tukalirejea, hasa tukiwa na wabobezi katika nyanja hizi. Sisi hapa tutapapasa tu kama watu waliogizani.
Kwa ufinyu wa mawazo niliyonayo, ningeanzia kwa kusema kwamba "Viongozi ni sehemu ya jumuia waliomo; lakini pia kutokana na hadhi ya huo uongozi wao ni sehemu mhimu ya ku-'shape' aina ya taifa wanalolijenga. Ni kiungo mhimu sana wanaolielekeza taifa na wananchi wako katika dira maalum waliyonayo viongozi hao.
Sasa sisemi hapa kuwa viongozi hao wanatakiwa wawe na kila kitu vichwani mwao, au mawazo yote yawe ni ya kwao tu; hapana. Lakini viongozi wenye dira huwakusanya viongozi wenzao ndani ya Taifa na kuweka mawazo yao pamoja yatakayoweka mwelekeo wa Taifa lao na jamii yao (wananchi) wanaowaongoza.
Na wala hata sisemi kuwa viongozi hao ni 'perfect',. Watakuwa na mapungufu kadhaa, lakini kiujumla wanakuwa ni viongozi walio na picha kamili wanakotaka kulielekeza Taifa lao.
Mimi sina shaka yoyote kichwani mwangu, kwamba kiongozi kama huyo tuliwahi kumpata hapa kwetu pamoja na uchanga wetu. Mwalimu Nyerere alikuwa ni kiongozi wa aina ya picha ninayoiona kichwani mwangu kuhusu hao uliyoyaandika hapo juu.
Na kama hakufanikiwa kulijenga Taifa hilo alilokuwa amelilenga, hilo pia ni jambo linalojadiriwa mara kwa mara; lakini tukumbuke tu hali ya uchanga wetu na mambo mengi yaliyokuwepo duniani wakati akijaribu kuijenga Tanzania aliyokuwa na picha yake kichwani akishirikiana na viongozi na wananchi wote kwa jumla.
Kuna mambo mawili kuhusu Afrika sikubaliana nayo hata kidogo. Kwanza sikubaliani kwamba tupo hivi kwa kuwa tulitawaliwa na wakoloni ambao waliturithisha elimu yao inayotufanya tusiiangalie Afrika Kiafrika. Miaka zaidi ya 60 tangu nchi ya kwanza Afrika kupata Uhuru bado tu tunashindwa kubadili mitizamo yetu kisa tu tulitawaliwa na wakoloni?
Wanaoendelea kuikumbatia na kuitumia dhana hii ni wachovu wa fikra.
Maoni yangu kuhusu uchelevu wetu wa kufikia huko tunakokutamani sote ni kwamba; tusiwe watu wasiokuwa na subira. Tunaweza kutazama mifano mbalimbali ya nchi zilizochukua hatua moja baada ya nyingine hadi kufikia hapo walipo leo.
Kwa nini sisi tunataka leo katika miaka 60 tuwe tumefikia hatua ya Korea Kusini? Tunajua waKorea walikotokea hadi wakafika hapo? Chukulia nchi kama Turkey. Imewachukua muda kiasi gani, pamoja na mizunguko yao miiingi kufikia hapo walipofikia? Kwa nini sisi tunataka leo tuwe kwenye hatua waliyofikia wao katika miaka 60 tu!
Sisemi kamwe kwamba nataka nasi tupitie mizunguko hiyo yooote waliyopitia nchi hizo, na muda waliouchukua kufika huko, La hasha. Kwani nyakati na teknologia zilizopo sasa ni tofauti. Sisi itatuchukua muda mfupi kama tutatuliza mawazo yetu na kuyalenga kwenye maendeleo tunayotaka tuyapate.
Lakini pia kuna upande wa pile wa picha hiyo, nchi kama Haiti, pamoja na kuwa huru miaka zaidi ya 100, wapo hapo walipo. Misri ndio wanaanza kuchangamka sasa, lakini wamechelewa mno!!. Nisingependa Tanzania nasi tuwe kwenye kundi la nchi hizi!
Hapa nataka nitoe mfano wa nchi kama Ethiopia. Kama hawa watatulizana vizuri na kuendelea kwenye kasi waliyonayo sasa hivi, Ethiopia katika miaka kumi ijayo itakuwa ni nchi tofauti sana na hii iliyopo sasa. Huu ni utabiri wangu, na ninaomba Mwenyezi Mungu aniweke nishuhudie utabiri huu.
Tanzania tulianza kuelekea huko, lakini Mh Magufuli nadhani atakuwa amezima breki kidogo kwa sasa. Sijui yajayo baadae.