Ravinder Kaushik ''Black Tiger'' : Jasusi mbobezi aliyefia jela ya ugenini

Ravinder Kaushik ''Black Tiger'' : Jasusi mbobezi aliyefia jela ya ugenini

Dumbuya

JF-Expert Member
Joined
Jan 23, 2014
Posts
596
Reaction score
878
Niseme ukweli nimekuwa mfuatiliaji mzuri wa mada mbalimbali katika jukwaa hili na
nikatamani nami kuleta bandiko moja ila kutokana na ratiba kuingiliana muda ukawa
hautoshi.
Kuna maneno nimekosa kiswahili chake fasaha na hivyo kutohoa au kutumia neno la kiingereza naomba tuchukuliane katika hilo.

Pia nimeona kabla ya kanuni za Mtandaoni hazijaanza kutugawa ni nafasi ya mwisho kupost ''Anonymously''.Hivyo baada ya kuisoma post ya ''Agent Provocateur'' nikahamasika kuimaliza makala hii. Karibu !!

Source ya taarifa :Ravindra Kaushik - Wikipedia na mitandao mbalimbali.


RAVINDER KAUSHIK

30spy1.jpg

Ni kijana aliyezaliwa kutoka familia ya kiPunjabi katika mji wa Sri Ganganagar uliopo karibu kabisa na mpaka wa India na Pakistan,jimbo la Rajasthan tarehe 11 April 1952.Ravinder alikuwa ni mtoto wa J.M Kaushik ambaye alikuwa mwanajeshi mstaafu wa kikosi cha anga (Indian Airforce).J.M Kaushik alikuwa akifanya kazi katika kiwanda cha nguo (Textile Mill) baada ya kustaafu.

Ravinder aliweza kusoma katika shule ya serikali na kufaulu vizuri na kuendelea na masomo ya juu katika chuo cha binafsi jimbo la Uttar Pradesh.Alikuwa ni kijana mtanashati,mwenye akili nyingi na kipaji kikubwa katika sanaa japo akiwa chuoni Lucknow alisomea shahada ya Biashara (B.com).Ravinder pia alikuwa kijana maarufu sana shuleni kutokana na kipaji chake cha kuigiza.

Ravinder alikuwa mpenzi wa sanaa za sinema na maonesho na hivyo ilivyofika siku ya mahafali yake mwanzoni mwa miaka ya 70 (1970's) alikuwemo kwenye kikundi cha maonesho siku hiyo.Ravinder alikuwa maarufu kwa kuwaigiza wapigania uhuru wa India na siku hiyoilikuwa ni nafasi yake ya kuigiza katika ngazi ya kitaifa kwani maonesho hayo yalikusanya watazamaji kutokea vyuo vya jirani na wengine mbalimbali.

Akiwa na umri mdogo wa miaka 21 aliweza kuteka mioyo ya watazamaji katika maonesho ya Sanaa pale Lucknow ambapo kwenye igizo hilo alikuwa ni shushushu wa India aliyekuwa akirubuniwa kutoa taarifa kwa vikosi vya China.Ukakamavu wake wa kuonesha uhimilivu wa hali ya juu pamoja na ustadi katika kuonesha uzalendo uliwafurahisha wote waliokuwepo na kumuweka katika orodha ya waigizaji waliokuwa bora mwaka huo.

Jambo ambalo Ravinder alikuwa halijui ni kuwa katika watazamaji walikuwepo maofisa wa Usalama wa India kutoka kitengo cha Utafiti na Uchambuzi (RAW yaani Reasearch and Analysis Wing) na maisha yake yalikuwa yanaenda kubadilika baada ya maonesho hayo.Zimebakia taarifa chache mno za kijana Ravinder Kaushik baada ya maonesho yale ila rekodi mbalimbali zinasema alifuatwa na maofisa wale wakiwa wamekunwa na kiwango cha ueledi,ushupavu na ujuzi alichoonesha akiigiza kama mwanajeshi wa India na kumshawishi kujiunga na kitengo hicho.
Ravinder hakuwa na pingamizi na inasemekana alikwenda nyumbani na kuaga kuwa anaenda New Delhi kwa ajili ya kufanya kazi ya kutumikia taifa pasi na ufahamu wa yanayo mngojea huko mbeleni.


MAISHA NDANI YA RAW

RAW ni kitengo cha usalama cha India kinachojishughulisha na utafiti na uchunguzi wa mambo ya nje,kilianzishwa mwaka 1968 baada ya kushindwa kwa India katika vita ya mpaka wa Himalaya ambayo inapakana na nchi ya uChina.Kutokana na kushindwa vita hii na nyingine za mara kwa mara katika mipaka yake,India ilianzisha kitengo hiki katika jitihada za kutengeneza ubobezi katika kukusanya taarifa na kujenga uwezo wa kiintelijensia kuweza kutumia taarifa hizo kulinda usalama wa nchi.

RAW iliweza kufanikiwa kuwa kitengo maridadi kabisa kikanda (Asia) na kidunia katika ukusanyaji taarifa na kuweza kushiriki katika matukio mengi kama Uhuru wa Bangladesh na urudishaji wa Jimbo la Sikkim katika mipaka ya India.RAW imejikita katika kukusanya taarifa za nchi za nje,kupambana na ugaidi na kuishauri serikali ya India katika mambo yahusuyo sera za nchi za nje pamoja na usalama wa programu za nyuklia.Wadadisi wengi wanakichukulia kama chombo makini na wanakitambua kama moja ya taasisi nyeti na muhimu katika mhimili wa utawala wa India.

Baada ya kurudi New Delhi (yalipokuwa makao makuu ya RAW),Ravinder alianzishiwa mafunzo mara moja ili kumfundisha maarifa ya ujasusi ya kistadi na ya kitaaluma hasa katika udukuzi wa taarifa na uchunguzi wa maadui bila kusahau mafunzo ya ukakamavu wa mwili.Pia akiwa kama shushushu wa awali (Junior Spy) aliweza kufundishwa lugha ya Urdu na mafundisho ya dini ya kiislamu.Hii ilikuwa ni muhimu sana ukizingatia mission aliyokuwa ameandaliwa mbele yake.Na kutokana na jinsi India iliovyokuwa imejigawanya kidini ilikuwa ni lazima afisa usalama apitie mafunzo yote ya dini ili kumuwezeha kuishi katika jamii ya imani yoyote.

Kijana Ravinder pia aliweza kupewa mafunzo ya hali ya juu yahusuyo hali ya kijiografia ya India na maadaui wote wa nje (hasa Pakistan) ambayo kwa wakati huo ilikuwa ni tishio kwa India kutokana na mafarakano yaliyokuwa yakitokea mara kwa mara katika mipaka ya nchi hizo mbili.Akiwa katika mafunzo hayo ya ukachero Ravinder alitahiriwa pia.

Baada ya miaka miwili ya mafunzo ya hali ya juu Ravinder alikuwa tayari ameiva kwa mission yake na akiwa miongoni mwa vijana bora waliosajiliwa kwa ajili ya mafunzo katika kitengo cha RAW hasa kutokana na uwezo wake mkubwa wa kitaaluma na kuvaa uhusika pasipo kutambulika.


NABI AHMED SHAKIR – PAKISTAN

India ilikuwa imeshapigana na nchi majirani kadhaa,China na Pakistan zikiwa za karibu zaidi.Kwa muda sasa kitengo cha RAW waliweza kunasa taarifa za kiintelijensia kuhusu vita iliyokuwa inaandaliwa na Pakistan,hivyo kuhitajika hatua za haraka kuweza kuidhibiti ikiwezekana kuizuia kabisa.

Moja kati ya hatua mbalimbali ambazo India ilichukua ni kupeleka mashushushu kupeleleza na kudukua taarifa za kijeshi za Pakistan wakiwa kama maofisa wakazi (Resident agents).Kati ya maafisa waliochaguliwa katika mission hii,Ravinder Kaushik alikuwa mmojawapo ingawa yeye alikuwa na maagizo maalum ya kimkakati kwenda kuishi na kujipenyeza kwenye jeshi la Pakistan ili kukusanya na kutoa taarifa za kiintelijensia kwa RAW hatimae kuwawezesha kujipanga na kuzuia mashambulizi ya kutoka Pakistan.

Kabla ya kufika Kashmir (Pakistan) na kuanza mission yake,Rajinder Kaushik ilibidi kwanza abadilishwe utambulisho na identity yake pamoja na rekodi zake zote za nyuma kufutwa.Na katika zoezi hili akapewa jina jipya la Nabi Ahmed Shakir na kutengenezewa nyaraka zote za utambulisho zenye jina lake jipya la kiislamu ambalo lingemuwezesha kujichanganya kwenye jamii za Pakistan ambazo ni waislamu pasipo kuwa na shida ukizingatia kipaji na ujuzi wa kijasusi alionao kwa sasa.

Nabi Ahmed Shakir alishuka Pakistan akiwa na mission moja tu ; kudukua taarifa za kiintelijensia na kuzipeleka nchini kwake.Haikua kazi rahisi na kutokana na maelezo ya mission yake alikuwa na jukumu la kuingia katika jeshi na kujipenyeza ili kupata fursa ya kudukua taarifa za kiintelijensia.
Hatua ya kwanza kwa kijana Nabi aliyekuwa na umri wa miaka 23 kwa sasa ilikuwa ni kujiunga na Chuo Kikuu cha Kashmir akichukua masomo ya sheria (LLB) na mwaka 1975 alimaliza masomo hayo yote ikiwa ni katika kutengeneza historia nzuri pamoja na kupata nafasi ya kujiunga na jeshi la nchini humo.Kutokana na uwezo wake wa juu kitaaluma alifaulu vizuri na kufuatia utaratibu wa usajili wa jeshi katika vyuo kila mwaka alifanikiwa kujiunga na jeshi kwa ufaulu mzuri aliokuwa nao.
Akiwa afisa mwenye ukakamavu wa hali ya juu,Nabi Ahmed Shakir aliweza kupita mafunzo yote ya jeshi la Pakistan akiwa katika ngazi za awali (ukarani) na baada ya miaka michache aliweza kupanda vyeo mbalimbali ndani ya muda mfupi.

Nabi Ahmed Shakir pia aliendeleza maisha nje ya jeshi kwa kuoa mwanamke wa kipalestina Amanat ambaye alikuwa mtoto wa mmoja wa washonaji wa jeshi na kufanikiwa kupata mtoto mmoja.
Kutoka mwaka 1979,Nabi Ahmed Shakir alikuwa akipitisha taarifa mbali mbali za kimkakati na kijeshi toka Pakistan na kuzipeleka India na kuzidi kujitengenezea umaarufu mkubwa ndani ya RAW na vitengo vingine vya usalama kutokana na uhakika na ubora wa taarifa za kiintelijensia alizokuwa akitoa.Taarifa hizi ziliiwezesha India kuwa mbele kimipango na kimkakati katika kupambana na wapakistan na inasemekana aliweza kuokoa maelfu ya wanajeshi wa kihindi kwa taarifa zake muhimu na za kiintelijensia.Haikuchukua muda mrefu sana akapandishwa cheo na kufika ngazi ya Umeja katika jeshi la Pakistan na kupelekea kuzidi kwa umuhimu wake kwa RAW hata kutunukiwa jina la “Black Tiger'' (Chui Mweusi) na aliyekuwa waziri mkuu wa wakati huo Indira Gandhi ingawa kuna rekodi zinazosema ni waziri wa mambo ya ndani S.B.Chavan ndiye aliyempatia jina hilo.Mambo yalikuwa yanaenda vizuri kwa RAW na Ravinder Kaushik (Nabi Ahmed) lakini bahati yao ilikuwa inakaribia kufika tamati.


INYAT MASIHA NA MWISHO WA NABI AHMED SHAKIR

Mwishoni mwa Septemba mwaka 1983, raia mmoja wa India kwa jina la Inyat Masiha alikamatwa akivuka mpaka kuingia Pakistan.

Kufuatia usaili wa awali,raia huyu alitia mashaka katika maelezo yake na hivyo kupelekwa katika kitengo cha Intelijensia cha Pakistan kuweza kubaini ukweli yakinifu.Kushukiwa kuwa ni shushushu wa India kulimweka Inyat kwenye usimamizi wa hali ya juu pamoja na shinikizo kubwa kutoka katika vikosi hivi vya Pakistan vikimtaka akiri na kusema ukweli juu ya utambulisho wake na dhima ya safari yake (misssion).Ni katika maongezi haya ndipo jina la Nabi Ahmed Shakir ''Black Tiger'' lilivyoweza kuibuka na kupelekea udadisi mkubwa zaidi hata kufikia mateso kwa Inyat na mwishowe kukiri kuwa ni ofisa usalama wa India na alitumwa kumpatia taarifa (maagizo) kadhaa mmoja wa maafisa wao aliyepo nchini humo.

Kutubu huku kwa Inyat ambaye alikuwa ni ofisa wa ngazi za chini kulipelekea uchunguzi mpana zaidi wa kuwepo kwa mashushushu wa kihindi katika ardhi ya Pakistan.Mateso zaidi yalimfata Inyat na kupelekea kutoa maelezo ya afis aliyekuwa anapelekewa maagizo hayo na kupelekea kumtaja Nabi Ahmed Shakir,ambaye kwa wakati huo alikuwa ni meja mwenye heshima katika jeshi la Pakistan.

Hii ilikuwa ni taarifa ya kushtukiza na yenye kuwaacha midomo wazi maofisa usalama wa Pakistan waliokuwepo.Ujumbe huu ulipitishwa kwa wakuu wa idara ya mambo ya ndani na jeshi la ulinzi na ikaagizwa kufanyika kwa uchunguzi mara moja kupata uhakika pasi na shaka yakuwa ni kweli Meja Nabi Ahmed Shakir ni shushushu wa India.

Mkakati ukapangwa wa kumtafuta Nabi na kuweza kumkamata kwenye tukio ''red handed''.Mkakati wenyewe ulikuwa ni Inyat Masiha kutumia lugha ya kijasusi kumpata Nabi kwa mawasiliano ya siri na kisha kupanga nae kukutana kwenye park ambapo maafisa wa Paskistan wangekuwepo kumkamata Nabi Ahmed Shakir.

Tukio hilo linapangwa na kuratibiwa katika umakini na uangalizi wa hali ya juu na baada ya kupokea ujumbe uliokuwa umeandikwa kwa kutumia lugha ya kiintelijensia (codes) ambazo ni wao tu wangeweza kuuelewa, Meja Nabi Ahmed Shabir alijikuta akiamuamini Inyat na kukubali kwenda kukutana nae katika eneo la mapumziko (park).Wakiwa tayari wamefika eneo la tukio,Meja Nabi Ahmed Shakir anakamatwa na kutiwa nguvuni mwa wanausalama wa Pakistan na kuanza safari yake mpya iliyojaa mateso,manyanyaso na ukatili wa hali ya juu.

Baada ya kukamatwa Nabi Ahmed Shakir sasa akiitwa kwa jina lake Ravinder,alipitia shuruba ya mateso makali na makachero wa pakistan kwa kipindi cha miaka miwili mfululizo katika kambi ya mahojiano Sialkot.Nabi Ahmed (Ravinder Kaushik) alifikishwa mahakamani na kuhukumiwa kunyongwa mnamo mwaka 1985.Hukumu ambayo baada ya rufaa aliweza kupunguziwa na kupata kifungo cha maisha jela.Hii ilikuwa mwaka 1990.

Kipindi chote cha kukamatwa,kuhojiwa na kustakiwa kwa Ravinder Kaushik ''Black Tiger'' ,kitengo cha RAW hakikusema wala kufanya lolote na idara ya
ulinzi na usalama ya India ilikuwa kimya na haikuchukua hatua zozote kumuokoa mwana intelijensia wao aliyekuwa mikononi mwa adui katika ardhi ya maadui.Hata pale makachero wa Pakistan hali wakiwa na ushahidi juu ya Ravinder na Inyat walipojaribu kuanzisha majadiliano ya kimataifa bado walipinga kuwa siyo watu wao na kuwatelekeza bila msaada wowote.

Ravinder alipitia jela mbalimbali zikiwemo Sialkot,Kot Lakhpat na Mianwali ambapo aliishi kwa tumaini la kuwa ipo siku taifa alilolipigania na kulitumikia muda wote litakuja kumuokoa.Kutokana na uduni wa mazingira katika jela za Pakistan pamoja na kuhamishwa mara kwa mara ili kuondoa uwezekano wa mkakati wowote kupangwa kumtorosha,Ravinder alipata maambukizi ya ugonjwa wa kifua kikuu na baadae asthma katika jela yenye ulinzi wa hali ya juu ya Mianwali (New Central Jail Mianwali).

Mwaka 2001 takribani miaka 16 toka akamatwe,jasusi makini na hodari katika kazi yake,mwenye weledi na umakini wa hali ya juu alikuwa akipumua pumzi yake ya mwisho ndani ya kuta za jela ya Mianwali.Hakika kifo chake kilikuwa cha kusikitisha na chenye maumivu ya kutisha.Alifariki akiwa mpweke na mwenye kuelemewa na magonjwa.Kutokana na kukataliwa na taasisi za usalama za India,Kaburi lake likajengwa palepale Mianwali nyuma ya jela aliyofia.

Akiwa katika kitanda chake cha mauti,Ravinder alipata kuandika barua kadhaa na kuzituma kwa siri kwa baba yake ambayo moja wapo kuna nukuu ya maneno "Kya Bharat jaise bade desh ke liye kurbani dene waalon ko yahi milta hai?" akimaanisha ''Je haya ndiyo malipo ya mtu kutoa maisha yake kwa kulitumikia taifa la India?''.

Barua hizi za siri zilimfikia baba yake Ravinder,kaka yake na mama yake wa miaka 72.Baba yake alifariki kwa mshtuko wa moyo,na barua mbalimbali za kuomba serikali iingilie suala hili tokea mwaka 1987 ziliishia katika masikio yaliyozibwa.Hazikuzaa matunda zaidi ya majibu kadhaa ya wizara ya mambo ya nje kuwa suala hilo linashughulikiwa nchini Pakistan.
Kipande cha barua mojawapo kutoka kwa mama yake Ravinder kwenda kwa waziri mkuu A.B. Vajpayee kilisomeka , “Had he not been exposed, Kaushik would have been a senior army officer of the Pakistan government by now and (continued in) the coming years (serving India secretly).” yaani ''Kama mwanangu asingebainishwa,angelikuwa katika ngazi za juu kabisa katika jeshi la Pakistan na kuendelea kulitumikia taifa lake la India.''

Familia hii haikupata stahiki zozote kutoka serikalini,ila baada ya kifo cha Ravinder ilianza kupokea fedha za kujikimu kiasi cha Rupees 500 za kihindi na baadae kuongezwa hadi Rupees 2000 na kisha kusitishwa kabisa baada ya kifo cha mama yake Ravinder.

Maswali mengi yaliulizwa kwa Vyombo vya usalama vya India ambavyo vilikuwa kimya katika suala hili,kwa nini hawakuweza kumuokoa jasusi wao namba moja nchini Pakistan ???

1.Je,ni kwa sababu ya kulinda usalama wa makachero/mashushushu wake waliokuwepo nchini Pakistan ???
2.Je,ni kulinda heshima na uadilifu wa taifa (National Intergrity) ??

Moral of the story :
''There is a price to pay for being a patriot '' - '' Kuna gharama za uzalendo''

Dumbuya.
2018.
 
Kwanini majasusi wengi huishia kufa kifo kibaya hivi??
 
Back
Top Bottom