Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais – Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Ridhiwani Kikwete amesema kuwa licha ya jitihada mbalimbali zinazofanywa na Serikali, Utumishi wa Umma bado unakabiliwa na changamoto kadhaa, ikiwemo kutokuzingatiwa kikamilifu kwa sheria, kanuni, taratibu, miiko na miongozo inayosimamia rasilimali watu katika kushughulikia masuala ya kiutumishi na kiutawala.
Akizungumza leo Juni 1, 2026 jijini Dodoma wakati wa ufunguzi wa kikao kazi cha viongozi wa utawala na usimamizi wa rasilimali watu serikalini amesema baadhi ya changamoto hizo ni matumizi mabaya ya madaraka na ofisi, huku Ofisi yake ikiendelea kupokea malalamiko kutoka kwa watumishi kuhusu upendeleo katika upatikanaji wa fursa mbalimbali zikiwemo maslahi, mafunzo pamoja na vitendo vya unyanyasaji wa kijinsia.