Ripoti kuu ya Mwaka ya Ukaguzi wa Miradi ya Maendeleo ya Mwaka wa Fedha 2022/23

Ripoti kuu ya Mwaka ya Ukaguzi wa Miradi ya Maendeleo ya Mwaka wa Fedha 2022/23

Roving Journalist

JF Roving Journalist
Joined
Apr 18, 2017
Posts
3,984
Reaction score
13,760
Taarifa ya Jumla ya Mwaka kuhusu ukaguzi wa miradi ya maendeleo imetolewa kwa mwaka wa fedha 2022/23 kwa mujibu wa Ibara ya 143(4) ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977, na Kifungu cha 34 cha Sheria ya Ukaguzi wa Umma, sura ya 418.

Taarifa hii inawasilisha matokeo ya ukaguzi na kupendekeza hatua za kuboresha ambazo zinalenga kukuza uwajibikaji katika ukusanyaji na matumizi ya rasilimali za umma.

MUHTASARI

Ripoti hii ina sura 15 zinazojumuisha ukaguzi wa fedha na ukaguzi wa kiufundi uliofanywa katika sekta mbalimbali kwa mwaka wa fedha wa 2022/23. Maeneo yafuatayo yamejadiliwa kwa kina katika ripoti hii:

Hati za Ukaguzi

Kati ya hesabu 299 zilizokaguliwa, 296 (99%) zilipata hati inayoridhisha sawa na mwaka uliopita. Hata hivyo, taasisi moja 1(1%) iliyopo katika sekta ya kijamii imepata hati isiyoridhisha kutokana na taarifa yao ya fedha kuwa na matumizi pungufu.

Pia, uchambuzi wa uzingatiaji wa sheria za ununuzi na usimamizi wa bajeti kwa taasisi 299 ulihitimisha kuwa taasisi 130 zilifuata sheria za ununuzi na ripoti 69 zilikuwa na upungufu; vivyo hivyo, taasis 251 zilifuata sheria ya bajeti, wakati taasisi 48 zilifuata sheria zikiwa na mapungufu machache.

Utekelezaji wa mapendekezo ya miaka iliyopita

Uchambuzi wangu wa taarifa 299 za usimamizi wa miradi ya maendeleo kuna jumla ya mapendekezo 2,982. Kati ya hayo, 40% yalitekelezwa, 26% yalikuwa yanaendelea kutekelezwa, 29% hayakutekelezwa, 9% yamerudiwa, na 6% yalipitwa na wakati.

Utendaji wa kifedha na usimamizi wa matumizi

Uchambuzi wa taarifa 299 za fedha za mwaka 2022/23 ulionesha kuwa jumla ya fedha za miradi wa Sh. trilioni 6.50 zilipokelewa. Kati ya hizo, Sh. trilioni 4.19 zilitumika, na kuacha bakaa ya Sh. trilioni 2.31 hadi kufikia tarehe 30 Juni 2023.

Katika usimamizi wa matumizi, nilibaini kuwa katika mwaka wa fedha 2022/23, Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia (MoEST) ilikopa Sh. 4,549,015,746 kutoka katika miradi ya SEQUIP na LANES II, ambazo bado hazijarejeshwa. Pia, nilibaini kuwa TANROADS, MOEST na TASAF hawakutoza kodi ya zuio yenye thamani ya Sh. 1,118,230,367, wakati taasisi mbili (TASAF na TANROADS) zilitoza lakini hazikuwasilisha kwa Mamlaka ya Mapato Tanzania Sh. 5,216,572,492. Jumla kodi za zuio ambazo hazijatozwa na hazijawasilishwa kwa Mamlaka ya Mapato Tanzania ni Sh. 6,334,802,859.

Aidha, nilibaini kuwa miradi sita—mitano iliyotekelezwa na TANESCO na mmoja wa AUWASA—haikulipa fidia ya Sh. bilioni 13.69 kwa watu 567 walioathirika. Miradi mitano inadaiwa Sh. bilioni 12.67 na Mradi wa Maendeleo ya nishati ya jua ya Tanzania ulikuwa na nyongeza ya makadirio ya deni la Sh. bilioni 1.02 kama fidia. Licha ya kukaribia kukamilisha miradi (97% hadi 100%) bila malipo ya fidia kwa waathirika.

Usimamizi wa Ununuzi

Nilibaini kuwa MWAUWASA ilitumia viwango vya ushindani vya kitaifa badala ya zabuni ya ushindani wa kimataifa katika upatikanaji wa huduma zenye thamani ya Sh. bilioni 3.55 kwa ajili ya ujenzi wa bwawa la maji katika Mji wa Kisesa, Mkoani Mwanza, unaotekelezwa chini ya Mradi wa Maji na Usafi wa Mazingira wa Ziwa Victoria (LVWATSAN). Hii ilipunguza ushiriki wa wazabuni wengine na kuzuia ununuzi kwa bei shindani.

Pia, nilibaini kuwa Mradi wa SEQUIP chini ya OR-TAMISEMI ulilipa Sh. 1,528,253,924 kwa mafundi ujenzi kwa ajili ya ujenzi wa majengo ya shule za sekondari katika Halmashauri ya Manispaa ya Lindi, Halmashauri ya Wilaya ya Mtama, na Halmashauri ya Wilaya ya Kilwa bila ya kusaini mikataba.

Mkataba na utendaji wa miradi

Niligundua kuwa Mradi wa Maji Safi na Usafi wa Mazingira Mjini wa Arusha ulikamilisha visima virefu 15 vilivyogharimu Sh. bilioni 9.16, ambavyo vilikamilika Mei 2023. Pamoja na kukamilika huko, hakuna miundombinu ya usambazaji maji inayounganisha visima hivyo kwa watumiaji wa mwisho. Upungufu huu umeufanya mradi huo kutokufanya kazi.

OR-TAMISEMI iliagiza ujenzi wa shule za awali za mfano awamu ya I na II, ambapo Sh. 12,252,675,000 zimetengwa kwa shule 197 katika halmashauri 160 chini ya mpango wa LANES. Katika ziara yangu mwezi Agosti 2023, niligundua kuwa majengo yaliyokamilika yenye thamani ya Sh. 1,395,600,000 katika halmashauri 25 hayakutumika kutokana na kutokuwapo kwa samani muhimu na huduma ya maji kwa ajili ya vyoo vya shimo vilivyojengwa.

Aidha, muundombinu wa Awamu ya 2 ya Mabasi Yaendayo Haraka (BRT) unaotekelezwa na TANROADS ulikuwa na gharama ya ziada ya Sh. bilioni 28.05 kutokana na mabadiliko ya muundo, upembuzi yakinifu usiotosheleza, na mapitio ya usanifu kabla ya kuanza kwa mradi.

Aidha, nilibaini tozo za riba kiasi cha Sh. bilioni 3.08 kutokana na kucheleweshwa kwa malipo ya wakandarasi na kutotumika kwa mkopo.

Uchambuzi wangu ulionesha kuwa TANESCO ilitozwa Sh 2,129,506,978 (69%) kwa ucheleweshaji wa kutumia mkopo wa Mradi wa Tanzania Zambia (TAZA), na TANROADS ilitozwa Sh. 874,996,553 (28.4%) kwa kuchelewesha malipo kwa wakandarasi na kwa kushindwa kutumia fursa za mkopo.

Wizara ya Maji na Wizara ya Maliasili na Utalii zilikabiliwa na tozo za kuchelewesha malipo Sh. 25,004,367 (0.8%) na Sh. 47,851,268 (1.6%) mtawalia. Tozo hizo zinahusiana na kuchelewa kulipa madai ya wakandarasi katika utekelezaji wa Mradi wa Pili wa Sekta ya Maji na Mradi wa Usimamizi wa Rasilimali za Asili kwa ajili ya Utalii na Ukuaji mtawalia.

Ukaguzi wa Kiufundi

Ukaguzi wa kiufundi ulifanywa katika maeneo yafuatayo:

Udhibiti wa gharama

Wakala wa Barabara nchini (TANROADS) uliingia gharama kubwa ya Sh. bilioni 130.51 katika miradi sita ya barabara kutokana na mapungufu katika upembuzi yakinifu, dosari katika usanifu, usimamizi wa mikataba na kucheleweshwa kwa malipo. Taarifa za upembuzi yakinifu zisizotosheleza ndiyo sababu kuu iliyopelekea Sh. bilioni 44.97 (34.5%) la ongezeko gharama, kwani hali za maeneo muhimu kama vile topografia, udongo na haidrolojia hazikupimwa kwa usahihi, na hivyo kuhitaji marekebisho makubwa wakati wa utekelezaji wa mradi.

Aidha, ucheleweshaji wa malipo ulisababisha limbikizo la riba la Sh. bilioni 42.8, wakati ucheleweshaji wa kukamilika kwa miradi ulihitaji kuwafidia wakandarasi Sh. bilioni 29.87 na washauri elekezi nyongeza ya Sh. bilioni 18.88. Pia, kiasi cha Sh. bilioni 3.99 kililipwa kwa Kitengo cha Ushauri wa Uhandisi (TECU) cha TANROADS bila mkataba rasmi. Ongezeko hili linaonesha hitaji la dharura la TANROADS kuboresha itifaki zake za upembuzi yakinifu, michakato ya mapitio ya usanifu, usimamizi wa mikataba, na mifumo ya malipo ili kupunguza kasoro za masuala haya ya kifedha katika siku zijazo.

Ujenzi wa barabara

Uchambuzi wangu wa udhibiti wa gharama kwa barabara zinazotekelezwa na TANROADS na TARURA ulibaini kuwapo kwa ziada ya gharama ya Sh. bilioni 66.06. Gharama hiyo ya ziada ilitokana na mabadiliko makubwa ya miundo wakati wa utekelezaji wa mradi. Mabadiliko hayo yalisababishwa na upungufu katika upembuzi yakinifu ambao haukuweza kuonesha hali halisi za maeneo kama vile topografia, udongo, na haidrolojia.

Pia, nilibaini ucheleweshaji wa malipo ya wakandarasi katika miradi minne ya barabara na TANROADS na mradi mmoja wa TARURA, hivyo kusababisha riba jumla ya Sh. bilioni 44.25, ambapo Sh. bilioni 42.57 kwa miradi ya TANROADS na Sh. bilioni 1.68 kwa mradi wa TARURA.

Ujenzi na ukarabati wa vivuko

Ukaguzi wangu ulibaini kuwa injini za kivuko cha MV Kilindoni zilikuwa zinapata joto kupita kiasi zinapokuwa katika mwendo wa mizunguko 1800 kwa dakika (rpm). Licha ya matakwa ya kimkataba kwa TEMESA kukagua bidhaa kabla ya usafirishaji na kanuni za sekta zinazohitaji uthibitisho wa vipimo kwenye injini mpya, wataalamu wa TEMESA hawakushiriki katika jaribio la kupima injini ya kivuko iliyofanyika nchini Korea. Kwa hivyo, utendaji wa mfumo wa injini ya baharini haukuthibitishwa, kinyume na matakwa ya kabla ya usafirishaji.

Vilevile, majaribio yaliyofanyika katika karakana ya kutengeneza kivuko cha Kigamboni yalikosa kiwango kinachokubalika cha ubora wa majaribio. Ingawa mradi uliripotiwa kuwa umekamilika kwa asilimia 100, hakuna cheti cha kukamilisha kilichotolewa, na Sh. bilioni 5.07 kati ya jumla ya mkataba wa Sh. bilioni 5.31 za mkataba zililipwa. Aidha, TEMESA ilishindwa kumuagiza mkandarasi kurekebisha tatizo la injini kuongezeka joto licha ya kupata taarifa ya tatizo hilo kutoka kwa wahandisi wa TEMESA wakati wa majaribio ya baharini mwezi Aprili 2023 ambapo ilithibitishwa tatizo la kuongezeka kwa joto kupita kiasi inapokuwa katika mwendo wa mizunguko 1800 kwa dakika (rpm).

Aidha, nilibaini kwamba ujenzi wa MV Kilindoni na kivuko kipya kati ya Nyamisati na Mafia ulihitaji idhini ya TASAC, huku vipimo muhimu vya udhibiti wa ubora havikuzingatiwa. Aidha, mabadiliko katika muundo wa ukarabati wa kivuko cha MV Nyerere hayakuwasilishwa kwa idhini ya TASAC.

Ujenzi wa vihenge vya kuhifadhia nafaka na ujenzi wa majengo ya VETA

Nilibaini kuwa NFRA ililipa Sh. 315,812,546 kwa mkandarasi kwa kazi za ujenzi ambazo hazikutekelezwa. Kazi hizo ni: ujenzi wa kuta, kazi ya zege, ufungaji wa nondo, na uchimbaji na ujenzi wa mfumo wa maji taka katika miradi ya Songea na Shinyanga.

Vilevile, NFRA ililipa dola za Marekani 4,853,039.42 (sawa na Sh. 10,856,249,183) kwa vifaa vilivyowasilishwa lakini bado havijafungwa kwa kuwa mkandarasi alitelekeza eneo hilo tangu Desemba 2020. Malipo yaliyofanyika hayakutoa ufafanuzi wa gharama kuonesha matumizi ya usambazaji, ufungaji, majaribio, na kukabidhi. Msimamizi wa mradi alithibitisha malipo bila ufafanuzi wa wazi.

Aidha, nilibaini ongezeko la gharama la Sh. bilioni 1.26 zilizolipwa na NFRA kwa wakandarasi kutokana na mabadiliko ya maeneo ya ujenzi Sumbawanga na Babati. Uamuzi wa kuhamisha eneo la Sumbawanga ulichangiwa na kuhamisha eneo la viwanda hadi Kanondo, wakati kwa upande wa Babati, kulikuwa na mwingiliano na laini ya usafirishaji wa umeme wa juu iliyopangwa na TANESCO.

Nilibaini kuwa michoro ya muundo wa vituo 25 ilionesha kuwa vifaa vya kuzima moto kama vile kengele za moto, vitambua-moto, na vitambua-moshi vilitakiwa kuwekwa jikoni na kwenye karakana. Hata hivyo, ratiba ya vifaa ilionesha kuwa, ni vifaa vya kuzima moto tu vilivyojumuishwa, lakini havikuwekwa katika vituo husika. Hii inamaanisha kuwa, hakukuwa na vifaa vya kuzima moto vilivyowekwa katika vituo 25 vilivyojengwa. Hii inamaanisha kwamba, Sh. bilioni 2.6 zilizowekezwa katika ujenzi wa kituo kimoja zitakuwa hatarini endapo janga la moto litatokea.

Miradi ya umwagiliaji na ubora wa maji kwa matumizi ya nyumbani

Nilibaini kuwa utafiti uliofanywa na Tume ya Taifa ya Umwagiliaji huko Eyasi, Lyamalagwa, Mkombozi, na Magulukenda-Sukuma ulikuwa na upungufu ufuatao: kutokuwapo kwa uchunguzi muhimu wa geoteknolojia kwa ajili ya kazi za msingi na mifereji; utafiti wa hali ya maji ulitegemea sana mifano ya miaka 50 bila uthibitisho wa data halisi ya utoaji maji; na utafiti wa awali juu ya uchunguzi wa udongo ulikuwa na upungufu wa taarifa na mapendekezo.

Pia, nilibaini upungufu katika ujenzi na usimamizi wa barabara za shamba ndani ya miradi ya umwagiliaji ya Mkombozi na Magulukenda kwa kuwa barabara zilijengwa kwenye udongo usiofaa, wakati barabara za mradi wa Magulukenda-Sukuma zilikosa mifereji ya maji. Upungufu huu umesababisha Barabara kuharibika mapema, hivyo kutoweza kupitika nyakati za mvua.

Chini ya usimamizi wa ubora wa maji majumbani, nilibaini kulikuwa na Mpango wa Ufuatiliaji wa Ubora wa Maji usioridhisha katika mamlaka za maji. Hii ni kwa sababu programu zilizopo hazikufuata kikamilifu miongozo ya EWURA, kwani hakukuwa na vifaa vya ufuatiliaji wa utendaji. Licha ya kufanya ufuatiliaji wa kiutendaji, bajeti ya kipengele hiki haikujumuishwa katika Mpango wao wa Ufuatiliaji wa Ubora wa Maji (WQMP). Aidha, nilibaini kati ya mamlaka nane za maji zilizokaguliwa, 88% zilishindwa kufikia viwango vya mabaki ya klorini.

Kutokana na hatari kubwa za afya ya umma zinazohusishwa na kutofuata viwango vya mabaki ya klorini, mwaka 2022/23 na 2021/22 DAWASA na MWAUWASA zilibainika na changamoto hizi baada ya idadi kubwa ya watu kukabiliwa na viashiria za hatari hizo.


Pia soma: CAG Kichere: Licha ya kupewa Ruzuku ya Tsh. Bilioni 31.55, ATCL imepata hasara ya Tsh. Bilioni 56.64, ongezeko la 61% kutoka hasara ya Mwaka 2021/22
- Ripoti 21 za CAG zatua Bungeni kwa ajili ya kuanza kujadiliwa
 

Attachments

Back
Top Bottom