CCM mambo mazito
Waandishi Wetu, Dar na Dodoma Februari 6, 2008
Raia Mwema
HALI si shwari ndani ya Chama cha Mapinduzi (CCM) na Serikali yake na mji wa Dodoma sasa unatisha kutokana na dalili za wazi za kuwapo mgawanyiko mkubwa miongoni mwa viongozi na watendaji wa chama hicho tawala.
Mgawanyiko huo unatokana na wabunge wa CCM sasa kubaini kwamba chama chao kinakwenda mrama kutokana na kunyamazia uoza mwingi na masuala ya msingi yaliyoibua hoja kama za kampuni ya umeme ya Richmond na ubadhirifu ndani ya Benki Kuu (BoT).
RAIA MWEMA imefahamishwa kwamba pamoja na kuwapo vikao rasmi mjini Dodoma, vikao kadhaa visivyo rasmi vinafanyika usiku na mchana kujadili mipango na mikakati ya kuokoa jahazi.
Hali hiyo inatokea wakati wabunge wakitarajia kukabidhiwa leo ripoti ya Kamati Teule ya Bunge iliyochunguza kampuni ya Richmond na baadaye usiku baada ya kuahirishwa kwa kikao, wabunge wa CCM watakutana.
Pamoja na Rais Jakaya Kikwete kuwasili mjini Dodoma, juzi usiku kulifanyika kikao maalumu kilichowashirikisha mawaziri na manaibu mawaziri katika kile kilichoelezwa kuwekana sawa kuitetea Serikali ndani ya Bunge.
Mambo yanayoisumbua CCM na Serikali yake na ambayo yanatarajiwa kuibua mjadala na maamuzi mazito mjini Dodoma, ni uchunguzi wa kampuni ya Richmond na lile sakata la Benki Kuu ya Tanzania (BoT), linaloendelea kufukuta.
Aidha, kauli ya Rais Kikwete kwamba mawaziri na wabunge wanapaswa kuchagua kati ya biashara na siasa na uamuzi tata wa Spika wa Bunge, Samuel Sitta, kuahirisha safari yake ya kwenda Marekani ni ishara tosha kwamba hali ya kisiasa ndani ya CCM ni tete.
Wachunguzi wa mambo ya kisiasa mjini Dodoma wanasema hali ilivyo sasa haijapata kutokea katika historia ya CCM katika siku za karibuni na hiyo inazidishwa na misimamo ya kushitukiza ya Kikwete na hivyo kuonekana kama kiongozi asiyetabirika.
Wakati Spika Sitta anatangaza kwenda nchini Marekani kikazi, aliwaambia wabunge kwamba mambo yote mazito yatasubiri arejee, ikiwamo ripoti ya Richmond na ile ya ukaguzi wa BoT, sasa uamuzi wake wa ghafla kuahirisha safari hiyo na kurejea Dodoma unatoa mwangwi wa mtikisiko ndani ya CCM.
Taarufa zinasema Kamati Teule ya Bunge iliyoundwa kuchunguza mkataba wa kuzalisha umeme wa dharura uliokabidhiwa kampuni ya Marekani ya Richmond imekuwa katika shinikizo kubwa la kuiweka hadharani ripoti yake na hata baadhi ya viongozi wa juu wa Serikali hawajaiona ripoti hiyo iliyokabidhiwa kwa Spika Sitta.
Mwenyekiti wa Kamati hiyo teule, Mbunge wa Kyela (CCM) Dk. Harrison Mwakyembe na Makamu wake, Stela Manyanya, wamekua kimya tokea waikabidhi ripoti hiyo kwa Spika, lakini joto la ripoti hiyo limepanda na kuwafanya wabunge kuonyesha wazi kuwa wakali.
Mwishoni mwa wiki iliyopita, wabunge wote wakiwamo wa CCM walionyesha makali katika semina ya Wizara ya Nishati na Madini ambako walikataa kuchangia wala kusikiliza majumuisho kutoka kwa Waziri wa wizara hiyo, Nazir Karamagi na Naibu wake, William Ngeleja, wakisisitiza kupata kwanza ripoti ya Richmond.
Kitendo cha wabunge hao kilikua ni ishara tosha kuonyesha uwezekano wa wabunge wa CCM kushikamana kuwachukulia hatua mawaziri wake, katika mfululizo wa maamuzi mazito ndani ya chama hicho.
Awali Kamati Kuu ya CCM ilifanya maamuzi magumu ikiwa ni pamoja na uamuzi wa kutaka viongozi wasijihusishe na biashara lakini pia kutaka kuundwa kwa sheria ya kudhibiti matumizi ya fedha za kampeni, uamuzi ambao ulinukuliwa na Rais Kikwete katika hotuba yake ya mwisho wa mwezi Januari, 2008.
Katika kuonyesha mambo si shwari, Waziri Mkuu Edward Lowassa, anaelezwa kuitisha kikao cha kikazi cha mawaziri na manaibu wao mjini Dodoma juzi usiku, akiwataka kusaidia kuwaelimisha wabunge kuhusu nia njema ya Serikali katika kuileta kampuni ya Richmond.
Taarifa za ndani ya kikao hicho zinasema katika kikao hicho, lugha kali zilitolewa ikiwa ni pamoja na maonyo kwa mashabiki wa masuala ya Richmond badala ya kuitetea Serikali.
Hata hivyo mawaziri hao wanaelezwa kusita kuitetea Serikali kwa kitu ambacho hawajakiona na wengi walisema watafanya uamuzi wa kuitetea Serikali baada ya kuiona ripoti ya Richmond kwa maana inaweza kuwa na mapendekezo ama maoni ya kuisaidia Serikali badala ya hofu iliyopo kwamba huenda kamati itaikandamiza Serikali.
Mawaziri hao walielezwa pia kwamba ripoti hiyo ya kamati haitawasilishwa kwenye kamati ya wabunge wa CCM pekee na badala yake itawasilishwa kwa wabunge wote ili kuepuka kuonekana kwamba kuna nia ya kulindana uamuzi ambao uliungwa mkono na mawaziri wote.
Hata hivyo, uamuzi wa Spika kutangaza kwamba ni lazima mambo hayo yajadiliwe akiwamo ni kutokana na yeye kuwa ndiye pekee aliyekaa na ripoti hiyo kwa muda mrefu na kuisoma na hivyo kuwa rahisi kwake kusimamia mjadala wake tofauti na Naibu wake, Anne Makinda.
Kitendo cha yeye kurejea Dodoma kwa haraka akitokea Dar es Salaam alipofika tayari kwa safari, kunaelezwa kutokana na shinikizo kutoka kwa watu walio karibu naye, akiwamo Rais Jakaya Kikwete, ambaye waliongozana kwa safari ya Dodoma waliko sasa.
Wabunge karibu wote wa CCM sasa wameungana na wenzao wa upinzani katika kuhakikisha wanawawajibisha mawaziri wanaoonekana kuwa mzigo kwa wananchi na chama chao, kwa kile kinachoelezwa kwamba ni moyo waliopewa na Rais Kikwete.
Habari zaidi zinaeleza kwamba Naibu Waziri mmoja amekuwa akitangaza hadharani kwamba waziri mmoja anayatejwa kuhusika na sakata la Richmond, anataka kuondoka na mtu kwa hiyo wabunge wasimsikilize na badala yake waitetee Serikali.
Sasa anapotuambia tuitetee Serikali halafu anamtaja waziri mmoja na kumuacha mwingine ana maana gani? anasema Mbunge mmoja wa CCM aliyetembelewa na Naibu Waziri huyo jana.
Wakati Richmond ikisumbua vichwa vya viongozi wa Serikali, uchunguzi unaoendelea kuhusiana na kashfa ya Akaunti ya Fedha za Madeni (EPA) ndani ya BoT, nao unaendelea huku wanasiasa wanaotajwa kuhusika wakiendelea kuhaha kuhakikisha kwamba hawahusishwi.
Katika juhudi hizo benki moja nchini imehusishwa na kuficha nyaraka muhimu zinazomhusu mwanasiasa mmoja anayetajwa kuhusika na sakata hilo bila kujua kwamba nyaraka hizo zimekwisha kuchukuliwa na vyombo vya dola hata kabla ya kuundwa kwa timu ya wachunguzi.
Kwa mujibu wa habari hizo, benki hiyo inatuhumiwa kuwa katika hatua za mwisho za kuharibu ushahidi wa kadi ya kufungulia akaunti ambayo RAIA MWEMA limethibitisha kuwa na picha na saini ya mwanasiasa mmoja maarufu ambaye anatumia nguvu kubwa kuhakikisha hafahamiki.
Kamati inayoongozwa na Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Johnson Mwanyika, imekuwa ikifanya kazi usiku na mchana ikiwa na vijana wenye utaalamu na mahesabu na nyaraka kutoka Ofisi ya Mwanasheria Mkuu, Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) na Polisi.
Vijana hao wanaelezwa kukabidhiwa vifaa na magari pamoja na mamlaka yenye nguvu za kufanya upekuzi na uchunguzi kwa mtu yeyote wakiwamo maofisa wa Serikali na wafanyabiashara wenye nguvu kubwa.
Kwa mujibu wa habari hizo, tayari mmoja wa watuhumiwa ambaye hajawahi kutajwa popote amekwisha kuhojiwa kwa saa kadhaa na ameonyesha kuchanganyikiwa kutokana na ushahidi uliopatikana kumhusu.
Kiongozi mmoja mwandamizi ameiambia RAIA MWEMA wiki hii kwamba, pamoja na misuguano yote inayotokana na matukio ya Richmond na BoT, Rais Kikwete ndiye anayeweza kuhitimisha kwa kufanya maamuzi mazito ili kuweza kuwaonyesha Watanzania kuwa ana nia ya dhati ya kuisafisha serikali yake na pengine chama.