RIWAYA-HUJUMA NZITO-PART.38
"Tumebakiza mwezi mmoja tutimize azima yetu ya kuibadilisha Tanzania kuwa Dola ya Nyasa kupitia sanduku la kupigia kura. Dola ambayo itakuwa huru na kutambua mchango wa Wanyasa wote katika harakati za kupigania uhuru wa Tanganyika. Leo mashujaa wetu kama Oscar Kambona, Denis Phombeah na Wanyasa wenzetu waliopigania uhuru huwezi kusikia wakitajwa wala kuandikwa kwa wema katika historia ya mapambano ya uhuru wa Tanganyika.
Wanyasa kwa ujumla ndio waasisi wakubwa katika kuanzisha vuguvugu la ukombozi wa bara la Afrika. Katika harakati za ukombozi wa Afrika, mashariki na kusini mwa bara hili, ni Wanyasa ndio waliokuwa juu zaidi kuliko watu wa makabila mengine ingawa ka nchi ka Malawi asili ya mababu zetu ni kadogo na idadi ya watu wake ni ndogo ikilinganishwa na wengine.
Afrika hii nani asiyekumbuka Katika mwaka 1925 kiongozi wa ICU- 'Industrial and Commercial Worker Union'- chama cha wafanyakazi viwandani kule Afrika ya Kusini, ambaye alikuwa ni Mnyasa, Clement Kaadalie, akihutubia ktk mkutano uanzishwaji wa chama hicho alitamka wazi kuwa Waafrika wanachotaka ni milki ya mali zao katika bara lao na serikali ya 'aboriginals' yaani watu wa asili wa bara hili. Huyu alikuwa Mnyasa akiwa nchini Afrika ya Kusini.
Nchini Zambia, Kenneth Kaunda, ambaye ni Mnyasa aliyehamia nchini humo akiwa na mama yake, naye alianzisha harakati za ukombozi katika taifa hilo. Hapa kwetu, kuna orodha ndefu sana ya Wanyasa ambao walioshiriki katika ukombozi wa taifa hili, wakiwemo kina Kambona, Michael Kamaliza, hata Karume sisi tunadai ana asili ya kwetu Nyasa.
Kwa hiyo ndugu wajumbe mkitafakari kwa makini utaona kuwa 'Nyasaland', pamoja na kuwa ka nchi kadogo, haina bahari na uchache wake wa malighafi kuliwafanya watu wake kutoka kwenda nje ambako walijiendeleza na kushiriki katika mapambano ya harakati mbalimbali za ukombozi wa Afrika kuliko watu wengine waliotokea kwenye nchi kubwa na zenye rasilimali nyingi.
Narudia, ni "Nyasaland" zaidi na si nchi nyingine katika bara la Afrika ilitoa watu walioshiriki katika ukombozi sehemu nyingi barani Afrika. Ingawa Rais wao wa kwanza, Hastings Kamuzu Banda, alikuja kuuasi mtazamo huu mpana wenye lengo la kuikomboa Afrika na kuwakumbatia makaburu wa Afrika ya Kusini baadae". Mkutano huo wa kusisimua uliokuwa na malengo ya kuisimika rasmi Dola ya Nyasa ulikuwa unaendelea katikati ya bahari ya Hindi, katika moja ya Hoteli ya kisasa inayoitwa 'The Pride of Indian Ocean' iliyojengwa baharini na mwekezaji wa Kiitaliano.
Ilikuwa ina vyumba vya kulala 300 vilivyopo chini ya bahari na kumbi za kisasa za mikutano na starehe mbalimbali. Kupata nafasi kwenye Hoteli hiyo ulitakiwa uweke oda si chini ya miezi 6. Na gharama ya kulala chumba kimoja kwa siku ilikuwa ni zaidi ya milioni 3 za Kitanzania. Nyasa Empire Supporters (NES) walilipia Hoteli nzima kwa ajili ya huo mkutano wao maalumu wa kihistoria.
Mtaalamu wao wa propaganda katika chama hicho Dr Mathew Chirwa, aliyepata digrii yake ya kwanza mpaka ya uzamivu ya mambo ya propaganda nchini Urusi alikuwa ndio anawalisha sumu ya hatari wajumbe hao. Sumu ya ukabila na kuwafanya wajione wao ni kabila tabaka a'ali sana katika jamii ya Kitanzania kuliko makabila mengine yote.
Wataalamu wa mambo ya propaganda wenyewe wanakiri kuwa Dr.Chirwa alikuwa na uwezo wa kumtia ndimu hata mgonjwa mahututi aliyelazwa Hospitali ya Taifa ya Muhimbili kuwa ana uwezo wa kupambana na bondia mkali kama Tyson au Mohammed Ali na mgonjwa huyo akajikuta anaamka kitandani na kukunja ngumi tayari kwa mpambano.
Siku ya mkutano huo wa siri Ilikuwa ndio siku ya uzinduzi rasmi wa kampeni za Uchaguzi Mkuu wa Rais, Wabunge na Madiwani, Tanzania nzima. Huku chama tawala wakizindulia kampeni zao katika uwanja wa Taifa, Jijini Dar es Salaam, chama cha upinzani cha "National Movement Party" (NMP) cha Dr Patrick Ndomba kilikuwa kinajimwayamwaya katika viwanja vya Jangwani. Maajabu ni kwamba mpaka saa 10:00 jioni kadamnasi ya wafuasi wa chama tawala walikuwa hawazidi hata watu elfu ishirini (20,000) katika uwanja huo wenye uwezo wa kubeba watu elfu sitini (60,000) huku wafuasi waliohudhuria mkutano wa chama kikuu cha upinzani cha NMP walikuwa ni zaidi ya laki moja (100,000).
Dalili ya mvua ni mawingu, kama uchaguzi ungekuwa unafanyika siku hiyo chama tawala kilikuwa kinadondoka madarakani asubuhi na mapema tu, habari yao kwisha kabisa. Walikuwa wanapumulia kwa kutumia mipira ya gesi kwenye chumba cha wagonjwa mahututi. Mkutano wa chama tawala ulipooza kama mkojo wa ngedere na wananchi walitokea tu kukichukia ghafla chama tawala kutokana na ukwapuaji wa mabilioni ya pesa katika mabenki uliofanyika.
Wizi ambao ulisababisha baadhi ya mabenki kufunga matawi yao nchini na kuhamia nchi za jirani. Hali ambayo ilisababisha ugumu wa maisha kwa walalahoi kutokana na ukosefu wa mikopo midogo midogo kwa wajasiriamali wa kipato duni. Wajasiriamali ambao mabenki hayo ndio yalikuwa mkombozi wao.
Chama cha upinzani cha "NMP"' wao walikamatia hapo hapo kwenye nukta ya ufisadi. Wao walishikilia ajenda hiyo hiyo tu, hawakubali kutolewa nje ya mada.
Kampeni zao na porojo zao kutwa kucha zilikuwa zinazungumzia ufisadi wa ukwapuaji wa zaidi ya bilioni 560 uliotokea katika mabenki. Huku wakipayuka kwenye maspika ya uwanjani hao waziwazi kuwa zimeibwa na vigogo wa chama na serikali ya chama tawala, ndio maana mpaka sasa hamna mtu aliyetiwa mbaroni.
Wakati mkutano wa hadhara wa chama cha Dr Patrick Ndomba unaendelea kurindima, huko katika viwanja vya Jangwani, nyuma ya pazia huko baharini kulikuwa na kikao haramu kinaendelea. Kikao ambacho kina mkono wa chama cha NMP bila wananchi kufahamu chochote. Nyasa Empire Supporters (NES) walikuwa ndio washika dau wakuu wanaotaka kuingia madarakani kupitia mgongo wa chama cha siasa cha National Movement Party (NMP).
NES ndio walikuwa wanalipa mishahara na marupurupu ya waajiriwa wote wa chama cha NMP, walifadhili ujenzi wa makao makuu ya kisasa ya chama hicho, na kugharamia gharama zote za kampeni nchi nzima za chama hicho.
"Pindi ukiisha tu uchaguzi na chama chetu pendwa cha NMP kushika hatamu ya madaraka, jambo la kwanza ni kubadili jina la chama, nalo ni kutoka 'National Movement Party' na kuwa 'Nyasaland Movement Party' (NMP). Aliposema hivyo ukumbi mzima ukaripuka kwa shangwe, mayowe na vigeregere.
Pili kitakachofuatia kwa kutumia wingi wa Wabunge wetu bungeni tutabadili katiba ambayo sasa itamfanya Waziri Mkuu awe ndio mwenye mamlaka ya juu ya kiutendaji kuliko Rais. Kwa mnasaba huo Rais mtarajiwa Dr Patrick Ndomba atakuwa pale juu kama nyoka la kibisa 'Figurehead'. Kisha Professor Potchefstroom ambao wengi hamumjui wala kumfahamu kuwa ni Mnyasa wao wanajua ni Mchaga ndio atakuja kushika madaraka ya Uwaziri Mkuu. Hapo ndipo Tanzania itageuka kuwa nchi mfadhili maana huyo jamaa ana akili za kuzaliwa nao atawapeleka mpwito mpwito wababe wa kiuchumi wa dunia.
Jambo litakalofuata baada ya hapo ni kubadilisha makao makuu ya nchi kutoka Dodoma na kuhamishia Ruvuma, huku Kinyasa kikitangazwa rasmi kuwa ni lugha kuu ya mawasiliano na kufundishia mashuleni. Pia tutamtangaza rasmi Bwana Oscar Kambona kama Baba wa Taifa namba mbili baada ya Mwalimu Nyerere.
Tutamjengea upya kaburi lake linaloendana na hadhi yake huku tukiweka mnara mrefu sana utakaoangaza nuru yake mpaka kwenye ardhi ya Mababu zetu huko Malawi. Hatuishii hapo, bali jina la nchi nalo litabadilishwa na kuwa "Nyasa Empire", huku harakati na juhudi za kuziunganisha nchi ya Malawi na Tanzania zitafanyika ili kupata dola moja ya "Nyasa Empire" yenye nguvu.
Mikakati hatari na mizito ya uhaini ilikuwa inapangwa huku si Kachero Manu wala Kachero Yasmine aliyefanikiwa kuingiza pua yake kwenye mkutano huo. Walikuwa wamepigwa chenga kali ya mwili, wakatepeta tepetepe kama chapati za maji. Bado walikuwa wanahanjahanja kutafuta mbinu za kupenya waweze kuingia mkutanoni.
Huko Ikulu nako mambo yalikuwa mazito, ugali moto, mchuzi moto kwa Mkuu wa Idara ya Usalama wa Taifa Bwana Omega Mtanika. Mheshimiwa Rais alikuwa amempa masaa 24 ahakikishe watuhumiwa wote wanakamatwa na kufikishwa mahakamani vinginevyo kibarua chake kinaota nyasi mara moja.
ITAENDELEA
Sent from my TECNO CC6 using
JamiiForums mobile app