RIWAYA-HUJUMA NZITO-PART 34
Leo nina huzuni kuliko kawaida, mwili wangu ni dhaifu na roho yangu imekuwa nyepesi sana. Nimempoteza kijana wangu mpambanaji Nathanieli ambaye alikuwa anafanya kazi kwa ukaribu zaidi na Bosi wako Newton Temba" alifungua mazungumzo Profesa akiwa anamhadithia Kachero Manu bila kufahamu huyo anajua kila kitu na ndio mhusika wa kifo cha Nathanieli kupitia pacha wake Yasmine.
Kisha Profesa akaendelea, machungu ninayoyapata ni kama siku kijana wangu Hamza Bendelladji wa Algeria alipokamatwa". Alipofikia hapo kwenye maelezo yake ya kumtaja Hamza, Kachero Manu alipigwa na butwaa na kuachwa mdomo wazi kwa sekunde kadhaa akiwa haamini kumbe Hamza, mhalifu nguli alipikwa kiuhalifu na Profesa.
Huyu Hamza Bendelladji ni mhalifu aliyefanikiwa kuiba pesa nyingi zaidi za mabenki kwa njia ya mtandao. Alikuwa ni kijana mdogo sana (25) raia wa Algeria, ambapo miaka kadhaa iliyopita alihukumiwa kifungo cha miaka 15 gerezani kwa uhalifu wa kuiba zaidi ya Bilioni 500 (Tsh) kutoka kwenye benki 217 za Ulaya na Marekani. Mashirika yote ya habari duniani kuanzia televisheni mpaka redio yaliripoti taarifa zake kijana huyo.
Kachero Manu akaanza kuomba kimoyomoyo Mwenyezi Mungu aweke baraka zake wamtie mbaroni Profesa ili dunia nzima iweze kujua kuwa Tanzania ina mashushushu bobezi kama wale waliopo katika mashirika makubwa kama CIA, FBI, MOSSAD, KGB na mengineyo yenye heshima ya kutukuka duniani.
"Hongera sana Profesa na sisi tunatakiwa tujue mbinu ulizompika nazo Hamza tukazitumie Tanzania" alijitia kupongeza kinafiki Kachero Manu huku akimtia shemere azidi kufunguka.
"Ha.. ha... ha...! Ahsante umenifurahisha sana kwa sifa unazonipa, mimi Tanzania kwa uwezo wangu wa kiakili wakati nafundisha Chuo Kikuu ilitakiwa niwe na eskoti ya ving'ora kunipeleka Chuoni na kunirudisha nyumbani, lakini hata heshima tulikuwa hatupewi.
Afadhali kidogo sasa hivi wasomi wenzangu wanakumbukwa na wanasiasa wanapewa vyeo vya kuteuliwa" alicheka kwa majigambo na majivuno bila kujua kuwa Kachero Manu ni popo, yupo nao kimagazigazi tu kuwapekenyua taarifa zao nyeti.
"Yule Hamza alikuwa na akili za kuzaliwa, kwanza alikuwa anaitambuka mashine husika ya ATM, kisha kwa kutumia "boot CD" ama "boot flash" anaathiri mfumo mzima wa mashine, hii ni diski maalumu yenye uwezo wa kutunza mafaili makubwa sana kwa kufanya mashine isinzie kwa muda. Baada ya hapo kirusi kiitwacho 'Tyupkin' kinaingizwa kwenye mfumo huo wa ATM, kazi ya kirusi hiki ni kukata mawasiliano ya kimtandao kati ya mashine ya ATM na seva za benki.
Baada ya hapo mfumo wa mashine unaanza kufuata masharti ambayo mtumiaji anaamuru na si maelekezo ya benki tena. Mpaka Hapo sasa unaweza kuingiza namba za siri ambazo zimetegeshwa tangu awali na kukupa uwezo wa kupakua kiasi chochote cha pesa kilichopo katika mashine. Njia hii huiba pesa zilizopo kwenye ATM mashine bila kuathiri akaunti za benki za mtu mmoja mmoja.
Na pia ni njia inayoitaji ujuzi wa juu sana wa Kompyuta. Njia nyingine aliyokuwa anaitumia kuwaliza wazungu wa Ulaya ni kuvamia ulinzi wa Kompyuta za benki za wale wa madirisha ya wateja na maofisa wao, kisha akawa anarusha kirusi cha 'Spying software'.
Kirusi hiki kinaunganisha taarifa zote za maafisa wa benki na wewe mvamizi ikiwemo namba za siri kadhaa, hivyo kumpa uwezo wa kuendesha mifumo ya benki kama afisa wa benki husika. Baada ya hapo sasa mvamizi anaweza kuhamisha pesa kutoka kwenye akaunti za watu wengine na kuweka kwenye akaunti yake binafsi. Na hii njia ya pili ndio tumeitumia sana kwa hizi pesa zilizopo hapa nchini Afrika ya Kusini". Alizidi kufunguka Profesa akiwa sasa ameanza kupata uchangamfu tofauti na mwanzoni walivyoanza maongezi yao.
Baada ya maongezi hayo Kachero Manu akakabidhiwa rasmi nywira za siri za kuwasiliana nae pindi atakapokwama akiwa kazini. Huku akiahidi kuwa watakutana Tanzania siku chache zijazo mara pesa zitakapokuwa zimefika. Pia usiku aliahidiwa kuwa atasaini mkataba rasmi wa kuhakikisha Dola ya Nyasa inasimamishwa na akifanikisha malengo yake aliyopewa atapewa nyadhifa gani kwenye hiyo serikali mpya.
Pia alipewa jukumu la kutafuta wataalamu wa kufoji nyaraka 'Cobbler' watakaowatumia sana wakati wa kuhamisha pesa taslimu kuirudisha Benki kwenye akaunti za VICOBA na SACCOS. Wakaagana Kachero Manu akarudi chumbani kwake kupumzika.
Wakati amejipumzisha chumbani kwake, akaamua kuingia kwenye barua pepe yake akakutana na taarifa za kupendeza kutoka kwa rafiki yake Dr.Edson Nkube.
Vipimo vya DNA vya mama mzazi wa mwendawazimu, marehemu Van-Dubbe vilishatolewa huku vikithibitisha pasina kuacha mashaka kuwa Van-Dubbe ndio aliyezikwa Tanzania na ndio mtoto wake. Hivyo akataarifiwa kuwa tayari leo mchana Mama yake Van-Dubbe anasafirishwa kwa ndege kuelekea nchini Tanzania tayari kwa ajili ya kutoa ushahidi mahakamani pindi mambo yakikamilika.
Akafurahishwa na kazi nzuri na ya kutukuka iliyofanywa na Dr.Edson Nkube, Afisa Usalama wao wa siri ambaye hata ndani ya usalama wenyewe wengi wao hawamjui "Deep Cover". Hasa akikumbukia namna alivyomuokoa kwenye hatari alipotegewa mtego kwenye nyumba ya kulala wageni siku ya kwanza kukanyaga nchini Afrika ya Kusini.
Kachero Manu baada ya kuperuzi jumbe mbalimbali alizotumia, akaanza kupanga namna ya kuwatumia kwenye sakata hili raia wa Tanzania wanaoishi Jijini Johanesburg na kulipwa na kitengo cha Usalama Tanzania, hasa kuchunguza nyendo za namna hizo pesa zitakavyosafirishwa kwa njia ya barabara.
Taarifa alizopata ni kuwa Jijini Johanesburg pekee kulikuwa na Maafisa Usalama Waliolala "Sleeper Agents" zaidi ya 20, wanaolipwa mshahara na serikali. Ambao wengi wao kati ya hao 20 walikuwa wanakula shushu hawajawahi kupewa kazi yoyote toka waajiriwe.
Hawa mashushushu walikuwa wanajichanganya mitaani hawajulikani na watu shughuli zao halisi. Wengine walikuwa wanafanyakazi saluni za kiume za kunyoa nywele, wengine wakiuza matunda mitaani, na shughuli kedekede zilizokuwa zinatumika kuwapoteza maboya watu wasiwajue kazi zao.
Walikuwa wamewekwa kama akiba ya kutumika siku wakihitajika. Na sasa wakati ulifika wa kutumika ambapo jukumu lao litakuwa ni kuchukua ushahidi wa kutosha uwe na video au picha wakati pesa zinatolewa mlundi kwa mlundi na kupakizwa kwenye magari.
Mawasiliano yake yote wakati yupo kwenye jumba hilo la Profesa gwiji wa Kompyuta alikuwa anayafanya kwa kutumia simu yake yenye programu maalumu ya kuzuia udukuzi. Hakutaka kabisa kugusa Kompyuta za ndani ya jumba lile, akiogopea 'Carnivore Computer', ambazo ni kompyuta maalumu zinategeshwa kwa ajili ya kufukua taarifa za mtumiaji.
[emoji3586][emoji3586][emoji3586][emoji3586][emoji3586][emoji3586][emoji3586][emoji3586][emoji3586][emoji3586][emoji3586][emoji3586][emoji125][emoji125][emoji125]
Majonzi na huzuni vilitawala msibani, nyumbani kwa Nathanieli. Ndugu, jamaa wa karibu na majirani walikuwa wamefurika kwenye kilinge cha nyumba hiyo. Askari polisi tayari walishaiondosha maiti ya Nathanieli. Wafanyakazi wenzake wa Benki Kuu nao hawakujivunga, walikuwa mstari wa mbele pale msibani kuhakikisha mambo yanaenda sawia bila kuharibika. Kila mtu alikuwa anasema lake pale msibani.
Penyenye za nguvu zilizoenea ni kuwa amevamiwa na majambazi usiku wa manane akauliwa. Wengine wakavumisha ni kifo kinachotokana na kisasi cha ugoni. Wakanyetisha kuwa alikutwa chumbani na mke wa mtu ndio mwenye mke akajichukulia sheria mkononi. Wakatilia nguvu nadharia yao kwa kuwa marehemu kakutwa yupo na chupi tu mwilini mwake, huku boksi kadhaa za kondomu zikifumwa chumbani mwake.
Hizi habari za uzushi zilikuwa zinaenezwa kwa kasi pale msibani na mitaani na vidinga popo na wale habari kuuzwa. Bila wenyewe kufahamu kuwa hizo habari zote ni propaganda zilizopikwa na kusambazwa na watu wa kitengo, mashushushu ili mradi kuwapoteza maboya mahasimu wao na pia ndugu, jamii na marafiki ili wasije kuharibu ushahidi wakati muda umekwenda matiti.
Maneno hayo ya ndarire yalizaa matunda chanya yaliyokusudiwa hasa ile dhana ya pili ya kushikwa na ugoni ndio ilishika kasi na kuaminiwa na wengi pale msibani. Huku dhana hiyo ikichagizwa na maisha binafsi ya Nathanieli ya kuishi bila mke wala kuwa na mtoto hata wa kusaga mkungu.
Vikundi mbalimbali vya kwaya vilikuwa vinatumbuiza nyimbo za maombolezo pale msibani. Kachero Yasmine nae alikuwa yupo pale msibani sako kwa bako na shoga yake kipenzi wa kazini Flora Tarimo. Alikuwa anawachora tu, huku akikumbukia vuta n'kuvute, patashika nguo kuchanika ya usiku wake alipokuwa anapambana na marehemu Nathanieli.
ITAENDELEA
Sent from my TECNO CC6 using
JamiiForums mobile app