Riwaya: "Hujuma Nzito"

HUJUMA NZITO-PART 15

Asubuhi hiyo alikuwa ameitwa kuja kusaidia upatikanaji wa risiti za safari feki ya nchini Uingereza, dili ambalo alitegemea litampatia zaidi ya milioni moja taslimu, halafu hapo hapo inaunganika na dili lingine lililoungwa juu kwa juu toka ofisi yake ya kupigia pesa ya "JUAKALI GENERAL SUPPLIES".

Moja kwa moja alipotua maeneo yale akaelekea kwenye ofisi aliyoitwa kwa ajili ya tenda hiyo chafu. Huko akakaa kama saa moja na dakika kadhaa, ndipo akawa amemalizana nao wapigaji wenzake. Alipotoka tu akaanza kuipiga namba ya simu ya Yasmine aliyotumiwa.

"Hellow...sistery, upo wapi mbona sikuoni?...usiulaze usiku mapema mapema, wakati ni ukuta..hapa sasa hivi nimepigiwa simu Ikulu kuna issue natakiwa nikarekebishe huko....Oooh OK. Sawa nisubiri hapo hapo nje !!" akakata simu yake.

Alikuwa anafanya mawasiliano na Kachero Yasmine huku akimtia ndimu kuwa ameitwa Ikulu wakati ni uzushi mtupu, lengo ni kujionyesha yeye ni mtu wa thamani sana anasakwa kila kona kama lulu vile, ili akikutajia dau lake usichomoe.
Yasmine hakutaka wakutane ndani ya jengo la Wizara, alitaka wamalizane nae nje ya jengo. Hivyo akamfahamisha yupo nje ya jengo kwenye kiduka cha Mangi anapoza koo kwa kujiburudisha kwa soda.

"Habari Aisee, Salaamu aleikum Bibie hongera kwa kupendeza.....!!" ilikuwa ndio salamu yake kwa Yasmine mara tu baada ya kuonana uso kwa uso. Tayari sura ya mrembo Yasmine ilishamchanganya, kumvuruga na kumkoroga vilivyo. "Vitu vya rangi ya Mtume ndio ugonjwa wangu huu....!!" alijiwazia kichwani mwake "Muddy Comp" huku wakipeana mikono ya salamu na Yasmine.

"Mie habari yangu ni nzuri, yaani nimefurahi sana kukutia machoni mjuba wewe. Maana ulivyo adimu kama mguu wa sisimizi uliodumbukizwa kwenye mchuzi wa rosti" alijishebedua Yasmine mbele yake na kumfanya Muddy ajione ni mtu wa thamani sana, kumbe anampaka mafuta kwa mgongo wa chupa.

"Acha tu mrembo, kwanza hapa nikitaka nipige chini dili lako maana Ikulu nasumbuliwa sana, kuna Afisa mmoja ananisumbua sana, namdanganya foleni kali. Alikuwa tayari atume gari zao zile na eskoti juu ya polisi ili mradi tu niwahi kufika, lakini wale JUAKALI naheshimiana nao sana nikaona sio vizuri kumuangusha yule Mkurugenzi" alizidi kujifagilia na kujikweza matawi ya juu.

"Jamani ahsante kwa kujali, Mungu atawalipa kwa upendo wenu, sasa tunaweza kwenda kuzungumzia ndani ya gari?" alibadilisha mada Yasmine sasa akimvuta taratibu kwenye lengo lake mahususi analolikusudia.
Nalo ni kumchukua "Muddy Comp" mpaka nyumbani kwake Mbweni. Alitaka ampeleke akamsulubishe, na kumpa mfueni vilivyo mpaka aropoke kila kitu pesa alizokuwa anapokea toka "Nyasa Empire Supporters" (NES) zilikuwa na madhumuni gani haswa. Kama zilikuwa ni mahari ya binti yake, au mchango wa matibabu atapike kila kitu anachokijua juu ya pesa zile kodi ya walalahoi, wavuja jasho wa Tanzania.

"Hamna shida tena itakuwa bora maana jua limeanza kunoga huko angani Malaika msimamizi wake hatuonei huruma, yeye analichochea tu makali yake" alijibu Muddy huku anamfuata sako kwa bako Kachero Yasmine kuelekea kwenye gari lake.

"Kaka yangu, mimi nafanya kazi Benki Kuu sasa kuna dili fulani inabidi ifojiwe saini ya Rais wa Benki Maendeleo ya Africa "ADB" ndio liweze kukamilika, naomba sana msaada wako kuna chambichambi ya kutosha usiwe na hofu na mgao wako..!" alizungumza kwa sauti ya kubembeleza huku amemlegezea macho "Muddy Comp", kwa mtindo wa kurembua.
Akajitia kushusha pumzi ndefu, kuonyesha amepewa mtihani mzito kuukabili. Kisha akaa kimya kitambo kifupi anajifanya anatafakari, halafu akafungua mdomo wake.

"Mie kweli ni mpigaji madili kama ulivyoelekezwa pale "JUAKALI GENERAL SUPPLIES" lakini dili sampuli hiyo unayonieleza ya kufoji saini za watu nimeachana nazo kitambo kirefu sana. Nilishawahi kupata matatizo na vyombo vya dola siku za nyuma ilibakia chupuchupu nikanyee mtondoo gerezani" alijitia kubadilika na kuipanjua dili hilo hadharani mchana kweupe.

Kachero Yasmine alipomuangalia "Muddy Comp" wakati anajieleza aligundua fika kwa kumuangalia uso wake, kuwa anaongopa mchana kweupe, ni ndumilakuwili tena mnafiki mkubwa hasa kutokana na elimu yake ya saikolojia ya wahalifu wanayofundishwa katika Vyuo vya Ukachero.

"Jamani weweeh...kaka yangu Muddy nisaidie kwa leo tu mara moja mwenzako..chonde chonde tafadhali" alizidi kubembeleza Yasmine huku sasa akiwa amekifumbata kiganja cha mkono wake wa kushoto kwenye mkono wa "Muddy Comp". Kitendo cha kushikwa kiganja cha mkono tu, akaanza kulainika kama siagi kwenye uji wa moto, huku anajichekesha chekesha tu kama mwehu.
Jinsi Kachero Yasmine alivyo mjanja akawa anamchezea vidole vyake huku anambembeleza kwa maneno matamu yenye kumtoa nyoka pangoni. Mawazo mwake Muddy alishakubali waondoke alitamani sana wapite nae maskani Magomeni walau awaongopee rafiki zake kuwa leo kaopoa kifaa kipya.

"Daah..majaribu haya unaniletea binti, jela inaniita hivi hivi nitakuwa peke yangu ujue, huku wewe unakula mbwanda na familia yako uraiani" aliongea kwa sauti ya chini, akiwa ameshagandishwa ulimi kuonyesha yupo tayari kuifanya hiyo kazi.
Baada ya mazungumzo mafupi wakakubaliana na kufikia muafaka yupo tayari kufanya kazi hivyo waelekee huko Mbweni akakabidhiwe mchongo mzima. Kachero Yasmine alikuwa anaendesha gari lake kwa mtindo wa halambe halumbe.

Mara amekosa kugongana na gari hili, mara kamkosa kumgonga mtu ili mradi tafrani njia nzima. Alishavurugwa tayari alikuwa anataka mambo yaende haraka haraka. Walishakuwa wapo nyuma ya muda kuwatia mbaroni wahalifu wa "Nyasa Empire Supporter" (NES).
Muddy alikuwa muda wote ana furaha ghaya, akiona kabisa anaenda kupiga pesa ndefu na huenda akikomaa akang'oa kabisa mtoto wa Kizenji, Yasmine. Kumbe hakujua anaenda kupata suluba na kalinyekalinye za kufa mtu mpaka atajuta kuzaliwa.
[emoji3586][emoji3586][emoji3586][emoji3586][emoji3586][emoji3586][emoji3586][emoji3586][emoji3586][emoji3586][emoji3586][emoji3586][emoji3586][emoji3586]

Ratiba ya Kachero Manu na rafiki yake Dr.Edson Nkube ilibidi ipinduliwe kichwa chini miguu juu. Mishemishe zao badala ya kuanzia kwenye ofisi ya "DNA Diagnostics Centre" (DDC) walipopeleka sampuli ya mwili unaodhaniwa wa marehemu Dr.Pius Chilembwa, kwa ajili ya uchunguzi wa vinasaba vya marehemu, wakabadilisha kibao wakaamua waanzie kwanza mizunguko yao mtaa wa "Adolf Goertz Street", kule dukani kwa Mhindi "Bhatti Shop".

Sababu ya mabadiliko hayo ya ratiba yalitokana na taarifa walizopokea toka kwenye vyanzo vyao vya Kiintelijinsia. Penyenye ziliwafikia kuwa kuna ghasia na machafuko yanayotarajiwa kuanzia kurindima nchi nzima ya Afrika ya Kusini.
Wazawa walikuwa wanataka kuandaa maandamano kushinikiza serikali yao kuwafukuza Wafanyabiashara wa kigeni ambao ndio wamekamatia asilimia 80% ya Uchumi wa Afrika ya Kusini. Wakileta madai ya kuwa wageni hao wamekimbia nchi zao zenye hali ngumu za kimaisha wamekimbilia nchini Afrika ya Kusini, nchi yenye neema ya asali na maziwa.

Iliwachukua kama nusu saa tu wakiwa na usafiri binafsi, kuwasili dukani kwa Mr.Bhatti. "Good Morning Mr.Bhatti, How are you?" alianza kusalimia Kachero Manu kwa uso wa bashasha, akafuatia Dr.Nkube nae kusalimiana naye huku wanapeana nae mikono ya salamu.

"Habari yangu nzuri sana iko karibuni sana" alijibu salamu kwa lugha ya kiswahili jambo ambalo liliwafanya Dr.Nkube na Kachero Manu waangaliane usoni na kutabasamu wakiwa hawamini kama Mhindi yule anaweza kuongea Kiswahili fasaha kiasi chake.

"Nashangaa nini, mimi meishi Tanzania miaka zaidi ya 20, wazazi iko kule wekeza zamani kiwanda cha kusindika nyanya, Dumila-Morogoro. Hivyo najua swahili na mlipoingia dukani nilikusikieni naongea swahili nikafurahi sana, nikajua nyie ni dugu zangu toka nchi ya Nyerere" alijieleza Bwana Bhatti wapi alipojulia lugha ya kiswahili.

Baada ya mazungumzo ya hapa na pale, wakajitambulisha kuwa wao ni waandishi wa habari wa kimataifa wa kujitegemea. Wapo nchini Afrika ya Kusini kutafuta habari za kichaa aliyepotea kwenye mazingira ya kutatanisha anayetafutwa kwa udi na uvumba na ndugu zake. Mr.Bhatti kwanza alionekana kuhuzunishwa sana na taarifa kupotea kwenye mazingira ya kutatanisha kwa majinuni huyo. Pia alionyesha kufurahishwa na ujio wa Wanahabari wale ili huenda Kichaa huyo akaonekana.

"Van-Dubbe kama alivyokuwa anajiita mwenyewe alizoea sana hapa mtaa wa Adolf Goertz Street. Tazunguka huku na kule lakini lazima rejee hapa. Menyewe penda jiita Rais wa Mtaa". Alifungua utangulizi wa mahojiano baina yao Mr.Bhatti kwa kuelezea namna alivyokuwa anamjua Majinuni aliyetoweka Van-Dubbe. Kachero Manu akafungua rasmi mahojiano baina yao.

Kachero Manu: "Kwanini alikuzoea wewe na sio wana mtaa wengine?, maana hata taarifa ya SABC-News ilionyesha polisi wamekuja kukuhoji wewe! "

Mr.Bhatti: "Swali zuri, watu wa huku roho baya sana, sasa mie iko mpa yeye chakula, maji na hata mavazi ndio maana Van-Dubbe iko hakauki hapa dukani kwangu! "

Kachero Manu: "Je siku chache kabla hajapotea, kuna mienendo yoyote ya hatari dhidi yake ulinusa hasa kutokana na ukaribu wenu?"

Mr.Bhatti: "Eeeh...iko watu wageni jitokeza ghafla jifanya nampenda sana kuja hapa nunulia mikate, soda naondoka nae kisha namrudisha, karibia wiki zima hivi..!!". Jibu la Mr.Bhatti likawafanya Dr.Nkube na Kachero Manu waangaliane usoni na kupeana ishara kuashiria kuwa hao watu huenda ndio wahusika wakuu.

Kachero Manu: "Unaweza kutuonyesha video zilizorekodiwa na CCTV-Camera ya hapa dukani kwako za wiki za mwisho mwisho kabla hajapotea?"

Mr.Bhatti:"Hamna shida mie CCTV yangu natunza matukio mpaka miezi tatu kisha nafuta, twende mkaone" alisema yule Mhindi huku wakisimama kuelekea nyuma ya duka lile, pembe za chaki kabisa, wakimuacha mtumishi wake mmoja Mr.Bhatti kuendelea kutoa huduma kwa wateja wake wachache waliokuwa wanaingia na kutoka hapo dukani.
ITAENDELEA

Sent from my TECNO CC6 using JamiiForums mobile app
 
RIWAYA-HUJUMA NZITO-PART 16

Walikaa kwenye mtambo wa CCTV-Camera kwa zaidi ya dakika 45 wakichambua picha na video hizo kwa umakini mkubwa mpaka wakafanikiwa kumgundua mtu mmoja kati ya washukiwa wa mauaji ya Kichaa Van-Dubbe.

Kwanza Kachero Manu alivyomuona tu Van-Dubbe taswira yake ikamjia moja kwa moja ndio ile maiti iliyozikwa kule Kijijini Kwembe. Mwili wake Van-Dubbe na mwili wa anayedhaniwa ni marehemu Dr.Chilembwa ulifanana sana.

"Huyu ni Mrakibu wa Polisi Makao Makuu Bwana Samson Komba, namjua fika tumeshakutana nae vikao vingi vya utendaji, kumbe ni mshenzi namna hii ameungana na wahalifu, kuzipiga shoka mali za serikali!" alijikuta Kachero Manu anaropoka kwa kujisahau kuwa pale amejitambulisha ni Mwandishi wa habari wa kujitegemea.

Alikuwa amepigwa na butwaa haamini kama kigogo mzito kama Samson Komba kuja kushiriki kumpoteza kichaa Van-Dubbe. Bahati nzuri, Mr.Bhatti alikuwa ameitwa dukani mara moja na mtumishi wake hivyo hakutilia maanani maneno ya Kachero Manu.

Huyo Mrakibu wa Polisi Bwana Samson Komba ndio kule kwenye genge la "Nyasa Empire Supporters" (NES) ndio akijulikana kama "Chew Master", Afisa Mkuu wa mambo yote ya Ulinzi. Ghafla bin vuu...Mhindi akarejea kwa kasi pale walipokaa Kachero Manu na rafiki yake huku anahema kwa uoga, kama vile amepatwa na kihoro.

"Mtaani kuna vijana fanya fujo navunja maduka naiba bidhaa nataka funge duka haraka sije filisi mtaji wangu, samahani sana" alizungumza huku anatetemeka.

"Bila samahani ahsante sana kwa ushirikiano wako, tunaomba anuani za wale ndugu zake Van-Dubbe kama unazo..!" Alizungumza Kachero Manu huku akiwa na furaha sheshe ya kupata taarifa muhimu alizokuwa anazihitaji sana.

Mr.Bhatti Akaanza kupekua kwa haraka haraka kwenye mafaili yake yaliyohifadhiwa kwenye mtoto wa meza, huku vidole vyake vinamtetemeka kwa hofu ya kukutwa na waandamanaji. Punde tu akakiona anachokisaka, kisha akachomoa kikaratasi fulani akampa Kachero Manu.

Akakipokea kikaratasi hicho na kukipitia kwa haraka haraka kisha akakisunda mfukoni mwake. Wakaelekezwa na Mr.Bhatti watokee mlango wa uwani, tayari duka lilishabugazwa na mtumishi wake kutokana na kuhofia vurugu zilizoanza kushamiri kwa kasi mitaani.

Walipofanikiwa kuwa kwenye eneo salama, wakaamua kugawana majukumu ya kazi kwa mkupuo hakuna tena kupiga ubwete kutokana na muda kwenda sana.
Kachero Manu akabeba jukumu la kufuatilia majibu ya vinasaba (DNA) vya mwili wa Marehemu Dr.Pius Chilembwa kwenye ofisi za "DNA Diagnostics Centre" (DDC), huku Dr.Edson Nkube akienda kufuatilia gari alilopata nalo ajali ya moto Dr. Chilembwa kujua mmiliki wake ni nani.

Walikubaliana kama majibu ya DNA yatakuwa ni tofauti na vipimo vya DNA ya Dr. Chilembwa, itabidi Kachero Manu aelekee kitongoji cha Soweto kwa wazazi wa Van-Dubbe ili awalainishe wakubali kupima kipimo cha DNA.
Kama DNA zao zitaowana na kipimo cha DNA ya sampuli aliyokuja nayo Kachero Manu, basi itathibitika pasina kuacha mashaka kuwa Van-Dubbe ndio maiti iliyozikwa kisanii kama Dr.Chilembwa.

SURA YA TISA

Bwana Molefe Thobakgale anasakwa na Dr.Nkube

Dr.Nkube alikuwa ndio kwanza anaegesha gari yake katika ofisi za kampuni ya kukodisha magari ya "Avis-Car Rental" iliyopo Jijini Johanesburg. Katika video za CCTV walizoziona dukani kwa mhindi, Mr.Bhatti walionekana baadhi ya watu walioambatana na majinuni Van-Dubbe wakiwa wamekodisha gari yenye pleti ya kampuni hiyo.

Lakini kama hiyo haitoshi, Dr.Nkube kwa kutumia watu wake wa intelijinsia waliomo ndani ya jeshi la polisi Jijini Johanesburg wakampatia taarifa nzima ya aina ya gari lililotumiwa na Dr Pius Chilembwa wakati anapata ajali na pleti namba zake.

Kupitia kwenye mtandao wa usajili wa magari nchini Afrika ya Kusini, alitafuta mmiliki wa gari hiyo mpaka akajua kuwa linamilikiwa na kampuni ile ya Avis, tawi la Santon, Jijini Johanesburg. Ndipo kiguu na njia akafanya maamuzi ya kwenda kumfanyia mahojiano mmiliki huyo wa kampuni ya magari ili kuweza kuunganisha nukta ya matukio haya mtawalia.

Aliposhuka tu kwenye gari kitu cha kwanza macho yake yakatua kwenye kidonda chake mkononi, majira yalikuwa yanasoma saa 7:05 adhuhuri, ikiwa ni saa mbili tokea wameachana na sahibu wake wa chanda na pete, Kachero Manu.

Akafanya haraka kupita geti la walinzi ambapo alisainishwa katika kitabu cha wageni. Akaandikisha taarifa za uwongo kuanzia jina lake mpaka namba ya kitambulisho chake. Baada ya kumaliza taratibu hizo za awali hapo getini akaruhusiwa kupita. Kwenye uwanja ule wa wazi wa pale kwenye kampuni kulikuwa na magari zaidi 100 ya kifahari, ya anuwai mbalimbali yakiwa yameegeshwa uwanjani yakisubiria wateja.

Akatembea umbali mfupi kama wa meta 10 akakutana na mlango mkubwa ambapo kulikuwa na mlinzi mwingine ambaye alimkagua tena kwa mara ya pili kuhakikisha haingii na silaha ofisini. Kwa bahati nzuri bastola yake alikuwa ameamua kuiacha kwenye gari lake.

Akaruhusiwa kuingia ndani ya ofisi hiyo ya wakala wa kampuni ya Avis. Baada ya kujieleza nia na madhumuni ya ziara yake kwa Katibu Muhtasi wa ofisi.
Akapewa maelekezo ya kutulia kitini, Mkurugenzi amekwenda kutekeleza ibada ya sala ya adhuhuri. Akitoka kuabudu ana mkutano kwa njia ya mtandao na wadau wake wa kibiashara kisha baada ya hapo ndio atakuwa huru ofisini kwake.
ITAENDELEA

Sent from my TECNO CC6 using JamiiForums mobile app
 
RIWAYA- "HUJUMA NZITO"-PART 17

Mkurugenzi wa Ofisi hiyo ya wakala Bwana Jamaly Ashrafy alikuwa ni mtu wa khamsa salati kipindi hakimbanduki msikitini. Swaumu za sunnah za Jumatatu na Alhamisi zilikuwa hazimkosi.

Dr.Nkube aliamua iwe isiwe, iwe mvua iwe jua lazima aonane na Bwana Ashrafy hivyo akakata shauri kumsubiria.

Baada ya kupita kama saa tatu, Bwana Jamaly akawa amesharejea Ofisini kwake. Alikuwa amevalia kanzu nyeupe kama theluji haina hata nukta ya doa la uchafu. Kichwani alikuwa amevalia balaghashia mufti kabisa yenye rangi ya kahawia ya kufumwa kwa mkono.

Miguuni alivalia makubazi ya rangi ya kaki yenye kuachia sehemu kubwa ya miguu yake. Mkononi alikuwa amekamatia tasbihi yake, vidole vyake vina kazi kubwa ya kuchezesha kete za tasbihi katika harakati za kumsabihi Mola wake.

"Karibu kitini Bwana Edson jisikie upo huru, samahani kwa kukuchelewesha, maana nimeambiwa upo muda mrefu sana ila ndio majukumu tena" alifungua maongezi baina yao baada ya kumkaribisha mgeni wake ofisini mwake.

Bwana Jamaly Ashrafy alikuwa na asili ya Tanzania Visiwani, aliyezamia nchini Afrika ya Kusini akiwa ghulamu mdogo tokea alipomaliza kidato cha nne katika sekondari ya Fidel Castro iliyopo kule Zanzibari. Tokea hapo baada ya kula msoto mitaani kwa kujishughulisha na kazi mbalimbali za sulubu, mwishowe ndipo akaibukia kwenye mafanikio kama wakala wa kampuni ya Avis.

Sasa maisha yake yalikuwa pambe sana, alichomoka kwenye kundi la Walalahoi na kuingia kundi la Walalaheri, chambilecho mchumia juani hulia kivulini. Mahojiano ya kirafiki zaidi baina yao yakaanza rasmi baada ya kuwa tayari alishajitambulisha hapo mwanzoni.

Dr.Nkube: "Kama nilivyojitambulisha kwako mwanzoni kuwa natokea chombo cha habari cha "SABC" ujio wangu ni kupeleleza juu ya tukio zima la gari yenu aina ya "Rolls-Royce Phantom" kupata ajali ya moto na kusababisha kifo cha Mkurugenzi wa fedha wa Benki Kuu ya Tanzania Dr.Pius Chilembwa" akaweka kituo kidogo cha maongezi yake, akameza mate kidogo, kisha akaendelea na mazungumzo yake. "Kwanza nikupeni pole kwa hasara mlioipata, lakini ningependa kufahamu Dr.Chilembwa alikodisha mwenyewe gari kwenu au kuna muwakilishi wake alikuja kwenu?"

Bwana Jamaly: "Ahsante sana tumepoa, hakuja mwenyewe, tuliyemkodisha gari ni mwingine kabisa!"

Dr.Nkube: "Unaweza kunipatia jina lake na anuani yake huyo aliyekodisha kwenu? "

Bwana Jamaly: "Hamna shida utapata" alijibu huku ameshika kasa ya kompyuta yake ya mezani anafungua faili lenye kumbukumbu za wanaokodisha magari kwao. Dr.Nkube aligundua kitu toka kwa Bwana Jamaly Ashrafy, viganja vyake vya mikono vilikuwa vinatetema kwa uoga, kuonyesha sio mzoefu wa mahojiano.

Bwana Jamaly: "Huyu hapa aliyekodisha gari yetu..! " alisema huku anamkabidhi Dr Nkube karatasi iliyodurufiwa kwenye printa ndogo ya mule ofisini. Kisha mahojiano yakaendelea kwa muda mrefu, Bwana Jamaly alikuwa anafunguka tu bila mficho.

Dr.Nkube: "OK..Ahsante sana", akaipokea na kuiperuzi kwa umakini mkubwa ile karatasi kisha akaikunja na kuisweka kwenye dayari yake ndogo ya mkononi.

Mahojiano yakaendelea tena kwa muda mchache mpaka yakafika ukingoni.
Alichogundua Dr Nkube kwa haraka haraka ni kuwa Bwana Jamaly Ashrafy alikuwa mweupe kabisa hajui chochote katika njama za washirika wa "Nyasa Empire Supporters" (NES). Kila alichoulizwa kwa anachokijua alikuwa anaropoka tu bila breki wala konakona.

Ila alichokuwa hakijui Dr Nkube ni kuwa Katibu Muhtasi wa Bwana Jamaly alikuwa ni kibaraka wa "Nyasa Empire Supporters" (NES), akilipwa ngwenje za kutosha kila mwezi kwa ajili ya kuchunguza usalama wao dhidi ya vyombo vya dola.

Alipewa vifaa maalumu vya kurekodi kila mahojiano anayoyafanya Bwana Jamaly Ashrafy na watu atakaowahisi kuwa ni wapelelezi, kisha anayatuma kwa njia ya mtandao hayo mahojiano kwa waliomtuma wakayafanyie uchambuzi.

Dr.Nkube wakaagana salama salimini wakiwa wameongea vya kutosha. Akasindikizwa mpaka mlangoni kisha Bwana Jamaly akafunga ofisi yake na kumuacha Dr.Nkube aende zake, kila mmoja akishika hamsini zake.

"Tafadhali naomba kitambulisho chako niweke rekodi za wageni waliokuja kutembelea ofisini, nimesahau pale mwanzoni, samahani sana" alijieleza yule Katibu Muhtasi huku akiwa amesimama kwenye kiti chake na kusogelea dirisha la kioo katika ofisi yake ile iliyozungushiwa vioo tupu tayari kwa kupokea hicho kitambulisho.

"Bila samahani!" alijibu kwa ufupi na kumkabidhi kitambulisho hicho yule dada kwa kutumia mkono wake wa kulia baada ya kukichomoa toka kwenye pochi yake anayoitumia kuhifadhia pesa na vitambulisho mbalimbali. Alipokiskani tu akamrudishia kwa haraka na kuagana naye kwa mara ya pili kwa uso wenye bashasha mpwitompwito.

Katibu Muhtasi yule alikuwa anamuangalia Dr Nkube kwa sura ya kebehi alivyompa tu mgongo, akijua fika hana maisha marefu mbele yake kutoka sasa. Alikuwa hajui kiswahili vizuri ila kitendo cha mazungumzo yao kutaja namba za gari lile alilofia Dr.Pius Chilembwa alihisi moja moja huyu ni mpelelezi katika kesi hiyo. Hivyo alijua taarifa ya uwepo wa huyu mtu ofisini kwao itagombewa kama peremende ikifika kunako wanaomtumia.

Dr.Nkube akatoka nje ya jengo, majira ya magharibi ilishatimu kutokana na nuru ya jua angani kuanza kufifia kutokana na ghurubi ya jua hilo huku kiza taratibu kikianza kulivamia anga katika pande zake zote nne. Akawa anajongea kuelekea mahali alipoegesha gari yake ili apate kuondoka mahali hapo akaendelea na harakati zake nyingine.

Dr.Nkube akaangalia simu yake kama ametumiwa arafa yoyote na muhibu wake Kachero Manu, akakuta hamna ujumbe wowote aliotumiwa wala kupigiwa simu. Akafungua mlango wa gari yake kisha akaingia ndani. Bila kuchelewa akawasha na kutimkia zake mitaani akishika baraste ya kuelekea kitongoji cha "South Western Townships" maarufu kwa jina la ufupisho la Soweto.

Hii sasa ilikuwa ni lala salama kwao hakuna kulala tena kwenye samadari mpaka kieleweke. Wanatwanga kotekote, Kachero Yasmine bado anakaba beki Jijini Dar es Salaam wakati Kachero Manu na sahibu wake Dr.Edson Nkube wanashambulia mahasimu wao wa "Nyasa Empire Supporters" (NES) wakitokea Jijini Johanesburg.

Aliwasili mtaa anaoukusudia majira ya usiku mbichi ukiwa umetimu, kiza kimetanda kimtindo. Mbalamwezi pekee ilikuwa inajitahidi kuangaza lakini ilizidiwa na kiza hicho. Nia na madhumuni ya ujio wake katika kitongoji hicho cha Soweto ilikuwa ni kuja mtaa wa Vilakazi.

Huo ulikuwa moja ya mitaa yenye heshima sana nchini Afrika ya Kusini na duniani kwa ujumla. Umaarufu wake mtaa huu unatokana na kuwa ni mtaa uliotoa washindi wawili wa Tuzo ya Amani ya Nobeli, nao ni Mheshimiwa Nelson Rolihlahla Mandela na Askofu Desmond Tutu.

Pia maeneo jirani na mtaa huo, kipindi cha harakati za ukombozi dhidi ya Makaburu, ghulamu wa miaka 13, Hector Pieterson alipigwa risasi na kufa hapo hapo na askari wa Makaburu na kusababisha machafuko makubwa ya Juni 16, 1976.

Dr.Nkube aliegesha gari yake nje ya Klabu moja maarufu ya starehe. Aliposhuka nje ya gari tu, akachomoa simu yake ya kiganjani toka kwenye mfuko wa suruali yake ya dangirizi iliyombeba vilivyo. Akaanza kumtafuta hewani Kachero Manu, ili afanye nae mawasiliano muhimu ya kikazi. Majibu yaliyokuja upande wa pili ni kuwa simu ya Kachero Manu haipatikani, ajaribu tena baadae.

Kwa bahati mbaya sana bila kukusudia kikaratasi kidogo kilichokuwa kimekunjwa na kuwekwa mfukoni kilikuwa kimemdondoka chini bila kufahamu wakati anatoa simu mfukoni.

Lengo lake la kumpigia simu alikuwa anataka afahamu Kachero Manu yupo maeneo gani hapa Soweto ili kama amemaliza majukumu yake anayatekeleza, waende pamoja anapokusudia kwenda. Akarudisha simu yake mfukoni na kupiga moyo konde kuwa ataenda peke yake kwenye nyumba hiyo anayoikusudia kwenda.
ITAENDELEA

Sent from my TECNO CC6 using JamiiForums mobile app
 
RIWAYA-HUJUMA NZITO-PART 19


Nikupongeze sana kwa hatua ya upelelezi uliyoifikia mpaka sasa, ulibaki kidogo tu ungegusa kichwa chenyewe. Haya geuka nyuma tukupe zawadi yako ya kazi nzuri ukaisimulie huko jongomeo unakoelekea hivi punde tu" alipewa amri ya kuwapa mgongo akiwa tayari ameshavuliwa viatu, shati lake na sarawili yake amebaki na nguo ya ndani tu. Dr.Nkube hakutaka afe kirahisi kama mgonjwa kiharusi kitandani. Alijipanga lazima apambane nao.


Ghafla bin vuu..Dr.Nkube akasikia sauti ya kulalamika maumivu ya mmoja wa wale maadui. Hakutaka kulaza damu tena, akajirusha pembeni kwa nguvu kuchupia kitanda kama kipa anayechupia mpira kwenye lango lake. Alipotua juu ya godoro kutupa macho na yule adui yake mwingine nae yupo chali chini anagaragara maumivu makali anayoyasikia.


Haraka haraka akaamka pale kitandani na kushuka chini ya kitanda huku akiwa haamini kama kilichotokea ni uhalisia au ni muujiza. Akiwa bado anashangaa mle chumbani hajui ni muujiza gani umetokea akastukia mlango unapigwa teke na Kachero Manu anaingia na mkononi ameshika bastola yake inayofuka moshi yenye kiwambo cha kuzuia sauti.

"Asante Komredi, umeniokoa na kifo chupuchupu" alishukuru Dr.Nkube, huku akishusha pumzi ndefu, wakikumbatiana na Kachero Manu. "Usijali nimelipa kisasi cha wewe ulivyoniokoa kule "New Salama Lodge" kwa kumtuma yule kijana wako" alijibu Kachero Manu huku wote wanaangusha kicheko.


Wakafanya upekuzi wa haraka haraka nyumba nzima, hawakupata chochote kitakachowaisaidia. Kwenye upekuzi wa moja ya ile maiti wakakuta kivuli cha kitambulisho feki cha uanahabari cha Dr.Nkube kile alichompa Katibu Muhtasi wa Bwana Jamaly Ashrafy na kukiskani. Hapo hapo Dr.Nkube akang'amua aliuzwa na yule dada kwa maadui zake.


Ikabidi wote watoke ndani ya nyumba ile haraka haraka kabla hawajafikwa na matatizo toka vyombo vya dola. Wakatembea takribani kama mwendo wa dakika 10 hivi mpaka wakaifikia gari yao. Wakiwa kwenye gari wanarejea ndipo kila mmoja akaanza kumuelezea mwenzake hatua aliyofikia ya kazi tokea walipoachana majira ya dhuha, asubuhi.


Alianza Dr.Nkube kuelezea kuwa hapo Soweto pale alipokuja kuokolewa, alimfuata marehemu Molefe Thobakgale ambaye ndio kutokana na taarifa ya wakala wa Avis, Bwana Jamaly Ashrafy, alikodisha gari lililopata ajali ya moto iliyomuua anayesadikiwa kuwa ni Dr.Pius Chilembwa. Dr.Nkube baada ya kumaliza simulizi yake akashikwa na hamu sasa ya kujua Kachero Manu alinusaje mpaka kujua yeye yupo kwenye hatari ya kupoteza uhai wake.


Kachero Manu Alimhabarisha kuwa walipoachana alifanikiwa kuja Soweto na kumshawishi mama mzazi wa kichaa Van-Dubbe kwenda kupima DNA katika taasisi ya "DNA Diagnostics Centre" (DDC) ambapo majibu watayapata kesho yake. Hivyo akamrudisha nyumbani kwake majira ya jioni kwa kutumia gari la kukodi.


Wakati anataka kuondoka Soweto akaamua arudi mashimashi bila gari kutokana na umati wa washabiki wa mpira waliofurika mitaani. Katika tembea yake ndipo akalikuta gari lao limeegeshwa Klabu. Akadhania labda Dr.Nkube atakuwa Klabu anapata moja moto moja baridi, kumbe Lahasha wa kalla! hakuwepo.
Akashikwa na hofu kidogo na kuanza kulizungukia gari kuangalia usalama wake, ndipo akaokota kikaratasi chini ya ardhi kina anuani ya hapo alipomfumania.

Akaiwasha simu yake aliyokuwa ameizima muda mrefu na kukuta kuna ujumbe wake kuwa mara mbili mtawalia alitafutwa hewani na Dr.Nkube. Akaanza kupigia simu yake kumtafuta bila majibu yoyote, ndipo akaamua kuzitii hisia zake zilizomuelekeza amfuate kwenye nyumba ile ya mshukiwa wake.


Kwa bahati nzuri akamkuta amebananishwa almanusura wainyakue roho ya rafiki yake. "Vipi sasa majibu ya DNA ya mwili unaodhaniwa kuwa ni wa marehemu Dr Pius Chilembwa, majibu yake mbona umeyaficha huyaweki hadharani" Dr Nkube uzalendo ulimshinda aliona rafiki yake anakwepesha kwenye kiini cha upelelezi wao.


"Oooh...Sorry...nilipitiwa habari njema ni kuwa "DNA Disgnostics Centre" (DDC) wamethibitisha pasina kuacha mashaka ya kuwa ile sampuli niliyokuja nayo sio mwili wa Dr Chilembwa" aliongea Kachero Manu huku uso wake umebeba tabasamu kunjufu la ushindi.
"Kwa munasaba huo ninathibitisha pasina kuacha mashaka kuwa Dr.Pius Chilembwa yupo hai, ni jukumu letu sasa kumsaka kwa udi na uvumba popote alipo ajibu kesi yake ya kula njama na kukwapua mabilioni ya pesa za mabenki yaliyokuwa chini yake.

Majibu ya kesho ya DNA toka kwa mama mzazi wa Kichaa Van-Dubbe yatatupa picha halisi ya kuwa kule Tanzania tumezika mwili wa Mwendawazimu Van-Dubbe aliyetekwa na kuuliwa kwa makusudi kwenye ajali ya moto iliyotokea nchini Afrika ya Kusini".


Baada ya kama nusu saa ya msafara wao wakafika nyumbani kwa Dr.Nkube huku wakijipongeza kwa kazi nzuri waliyoifanya siku ya leo kila mmoja kwa kadri ya uwezo wake. Kachero Manu alipanga kesho kutwa yake arudi nchini Tanzania akamuongezee nguvu Kachero Yasmine kuwatia mbaroni wahusika wote.

ITAENDELEA...............................





Sent from my TECNO CC6 using JamiiForums mobile app
 
Cookies are required to use this site. You must accept them to continue using the site. Learn more…