RIWAYA- HUJUMA NZITO-PART 23
Ghafla bin vuu akatulizana tuli kana kwamba kuna kitu amekikumbuka. Akaunda tabasamu pana la ushindi usoni mwake. Akashuka haraka chini ya gari na kwenda kufungua buti la gari kisha akashusha chini moja ya begi lake la safari. Begi ambalo lilikuwa na nguo na vifaa vya kazi vya akiba, kiasi kwamba akikurupushwa hata usiku wa manane kuhusiana na safari ya pande yoyote ya dunia anasafiri bila tatizo lolote.
Alifungua na kuanza kupekenyua ndani ya begi lake. Alikuwa anakitafuta kijitabu chake kidogo alichopewa na marehemu Babu yake mzaa mama siku alipompa taarifa za kuajiriwa kwake kama Afisa Usalama.
"Mjukuu wangu, nakukabidhi kitabu hiki kinaitwa Yasini Mubin ni kidogo lakini penda sana kukisoma kitakupa kinga dhidi ya wabaya wako, hata uchawi na mazingaombwe havitaweza kukudhuru ukikitumia ipasavyo. Mjukuu wangu kazi yako hiyo nzito lazima ujikomaze vilivyo kwa kuwa karibu na Allah Subhanahu Wata'ala" Yasmine alikuwa anayakumbukia maongezi yake na Babu yake siku alipokuwa anamkabidhi kitabu hicho alichokihifadhi ndani ya begi lake.
Bahati nzuri akafanikiwa kukifukunyua kitabu hicho mahali kilipojibanza. Sasa alikuwa tayari ameshakishika mkononi mwake kijitabu hicho, ambacho kimtazamo kilikuwa kimeanza kupoteza nuru kwenye kurasa zake kwa uchakavu wake uliokithiri.
Akafunga begi lake hilo na kulirudisha ndani ya buti na kurudi ndani ya gari yake. Kwa msaada wa mwanga wa ndani ya gari akaanza kuzitafuna nuni na jiimu za kwenye kitabu hicho maktubu kwa lugha ya kiarabu bulbu, kisicho na hata nukta ya kosa la kisarufi.
Ilimchukua kama nusu saa kukimaliza chote. Lakini maajabu kadri alivyokuwa anakisoma kijitabu kile kuna vitu mwilini mwake vilikuwa vinafunguka na mwili wake unaanza kuwa mwepesi na kurudia hali yake ya kawaida na uoga wote umemvuka. Akagundua kumbe alishaanza kufungwa na marogo ya kwenye nyumba ile.
Ghafla mvua nzito ile ya kidindia ikaanza kunyesha kwenye anga ile ya Sinza Mori huku sauti za radi zinalipuka angani mtindo mmoja mithili ya mabomu kwenye uwanja wa vita. Kachero Yasmine hakuwa na muda wa kupoteza ikabidi achomoe koti lake la kujikinga na mvua kutoka siti ya nyuma ya gari na kujivika mwilini. Baada ya hapo akateremka nje ya gari na kuvuka barabara kuelekea kiamboni kwa Man-Temba kwa mara ingine akiwa anatimua mbio.
Safari hii alipoingia tu ndani ya nyumba hiyo akawasha kurunzi yake, akamulika waa nyumba nzima na bastola yake ipo mkononi mwake. Nyumba nzima ilikuwa inavuja utasema imeezekwa na chujio mbovu. Alipoukaribia ule mlango wa bati, ghafla wakajitokeza tena paka wale wale watatu wanaanza kumcheza shere Kachero Yasmine Kama mwanzoni. Safari hii hakutana utani nao tena, akamlenga mmoja wao kwa bastola yake na kumfyatulia risasi moja iliyotua sawia kichwani mwa paka huyo.
Pale pale kiumbe kile kikadondoka chini na kuanza kupwiripwita kwa huruma mpaka kikata roho. Wale paka wengine kuona mwenzao anavuja damu wakatoka nduki huku nyayo zao zinalia pukutu pukutu kutokana na kuzidiwa kwa uzito wa miili yao.
Yasmine alipoumulika kwa kurunzi ule mzoga wa paka akakuta shingoni umefungwa bonge la hirizi nyekundu. Hapo hapo ule mzoga ukaanza kunuka fee fee harufu ya uozo. Hiyo ikazidi kuthibitisha kuwa yule hakuwa paka wa kawaida. Akaachana nao ule mzoga na kuendelea na kilichomleta kwenye nyumba ile.
Akalikorokochoa kufuli lile kwa funguo malaya mpaka likafunguka na kumuwezesha kuingia kwenye chumba kile. Alipokimulika mwangaza vizuri akakuta kuna tandiko moja tu, jembamba mithili ya ulimi wa ng'ombe. Hakukuwa na kitu kingine chochote kile cha thamani, jambo ambalo lilimstaajabisha sana Kachero Yasmine. Tandiko hilo lilikuwa limewekwa juu ya zulia chakavu lililoenea chumba kizima.
Kijasho chembamba cha juu ya pua zake kikaanza kumvuja bila kupenda. Alijiona kama vile Amechezewa kanya boya ya hatari, kuliko mategemeo yake. Fikrani mwake alihisi huenda kitakuwa ni chumba ambacho kimesheheni vifaa vizito vya kazi kama ishara ya meseji alizokuta nyumbani kwa Nathanieli zilivyoashiria.
Akakifanyia speksheni chumba kizima kwa umakini mkubwa, mpaka sehemu za ukutani labda atakuta unafunguka popote, akatoka patupu. Baada ya taftishi ya zaidi ya nusu saa akaamua atimke zake ndani ya chumba kile hamna chochote cha maana anapoteza muda wake tu.
Alipoufikia mlango wa kuingilia anataka sasa ausukumize mlango ule wa bati atoke nje akasita kidogo. Akageuka nyuma na kumulika kurunzi pale kwenye tandiko kwa sekunde kadhaa kama mtu aliyegundua kitu. Akaamua arudi tena mahali ambapo limewekwa godoro. Alipofika akalipiga teke kwa kutumia viatu vyake vya raba vya ngozi, likasogea pembeni lile godoro. Akaanza kumulika kwa umakini mkubwa eneo lote pale sakafuni lililokuwa limezibwa na godoro lile.
Kuna kitu akakigundua katika taftishi yake hiyo. Aliona kuna mkato wa duara juu ya lile zulia katikati ya pale palipozibwa na godoro. Mkato huo ulionekana kuungwa kiustadi mkubwa na sehemu nyingine ya zulia hilo. Akafanya maamuzi ya kuvuta kwa nguvu sehemu hiyo ya zulia kwa bahati ikanyofoka na kuacha eneo wazi la sakafuni lililozibwa na mfuniko wa shaba.
Akajibidiisha kuuvuta huo mfuniko kwa nguvu zake zote, lakini akaukuta umeng'ang'ania ng'ang'anu hauchomoki kirahisi. Akaendelea kujibidiisha mtoto wa kike kwa nguvu zote kuuvuta mfuniko huo bila kukata tamaa mpaka ukakubali kufunguka. Ukalia mlio wa sauti buuuh..! mfuniko ule baada ya kukubali kuachia.
Sasa usoni mwake furaha yake ilikuwa sheshe isiyo na kifani, huku kijasho chembamba cha juhudi kikimtiririka mashavuni mwake. Alipoangalia saa yake ilikuwa inasoma saa nane na robo ya usiku wa manane. Pia huko nje, mvua ilishakata kunyesha kabisa kitambo kirefu.
Alipopiga chabo ndani ya shimo, kulikuwa na kiza totoro kiasi kwamba kurunzi ilikuwa haitoshi mwangaza wake. Akapiga moyo konde na kuanza kuteremka kuelekea chini ya shimo lile huku akiurudishia vizuri mfuniko ule juu, akijipa moyo wa liwalo na liwe. Muda wote alikuwa anawaza huyu mkazi wake hii nyumba, Man-Temba yupo wapi mpaka sasa.
Akaanza kuteremka ngazi moja baada ya ingine kuelekea chini ya shimo. Kadri anavyoshuka chini ndio hali ya hewa inazidi kumchefua chefu chefu, lakini akazidi kupiga moyo konde aendelee na msafara wake bila kusalimu amri.
Alishuka kama mwendo wa dakika 10 hivi ndipo akakiona mbele yake chumba kimoja kizuri ila kidogo sana chenye uwezo wa kuingiza watu wasiozidi watatu tu.
Kwa bahati mlango wake chumba hicho ulikuwa umebugazwa tu. Akausukuma na kuingia ndani mzima mzima. Ndani ya kichumba Kulikuwa na meza ndogo juu yake kuna kompyuta mpakato ndogo na mzinga mkubwa wa konyagi.
Alipomulika zaidi kwenye chumba kile akaona swichi ya umeme na kiyoyozi mle kwenye kijichumba. Akaelekea ukutani na kuwasha batani hizo, kufumba na kufumbua nuru ikaenea chumba kizima na kiyoyozi kikaanza kuleta hewa nzuri ya kuvutia ndani ya chumba kile na kulifukuza kwa kasi joto lililokuwa limeshitadi ndani ya chumba kile.
Akavuta kiti kisha akaketi juu yake na bila kupepesa macho akaanza kuhangaika kuiwasha kompyuta hiyo. Wakati Kompyuta inajiweka sawa kwa ajili ya kuanza kupiga kazi, akavuta droo ndogo ya upande wa kushoto wa meza hiyo, akashtuka kidogo.
Alikutana na lundo la ATM-kadi za benki tofauti tofauti za ndani na nje ya Tanzania na mishumaa isiyopungua mitano. Kadi hizo zilikuwa ni mali za benki mbalimbali za Congo, Gambia, Afrika ya Kusini na nchi nyinginezo. Akakumbuka wameshawahi kupewa mafunzo namna pesa zinavyoibwa kwenye mashine za benki, enzi ATM-Mashine zimeanza kutumika nchini Tanzania kwa mara ya kwanza.
Aina hii ya kuiba pesa kwa kutumia nta ya mshumaa, hii ni mbinu ya kizamani kidogo lakini bado kwa nchi zinazochechemea kiteknolojia ilikuwa inaweza kufanya kazi kwa asilimia kadhaa. Akaachana na kadi hizo huku akiweka umakini kwenye kompyuta aliyoiwasha punde ili kujitafutia kilichomleta ndani ya chumba hicho cha maajabu..
Kompyuta sasa ikawa imefunguka, akaanza kuyaperuzi mafaili ndani yake kadri atakavyo. Mafaili yote yaliyohifadhiwa ambayo aliyaona yana manufaa kwake alikuwa anayafowadi kwa Kachero Manu kwenye baruapepe yake na kuyahifadhi pia kwenye flashi yake. Alipanga akayasome vizuri nyumbani kwake atakaporejea maana tayari kichwa kilishachoka.
Ghafla wakati anajiandaa kuifunga ile kompyuta ikaja meseji kwenye mesenja yake Man-Temba, anaulizwa swali, "Pesa zinakaribia kusafirishwa wiki ijayo, tunasubiria mtu toka Tanzania atakayesindikiza magari hayo kutoka nchini Afrika ya Kusini kama ulivyoahidi". Ujumbe uliandikwa kuwa umetoka kwa Professor "Potchefstroom". Kachero Yasmine akashtuka na kubaki ameduwaa mdomo wazi kwa sekunde kadhaa kama zuzu hajui atoe jibu gani pale.
"Mbona hutoi jibu haraka, tukichelewa pesa zitagandishwa tushindwe kuzitoa kwa wakati, tekeleza makubaliano yetu kwa kumtuma mtu makini kama ulivyoahidi, hatuna muda wa kupoteza..!" ujumbe mwingine ulitumwa papo kwa papo kwa mtindo wa bandika bandua.
Yasmine akili yake ikachakata mambo kwa haraka sana, ikabidi ajiongeze tu kwa kujibu kwa kubahatisha tu."Sawa ameshafika mtu wetu, mpe mawasiliano namna atakavyokupata.!". Kimya kirefu kikatawala bila majibu yoyote toka upande wa pili mpaka akaanza kuingiwa na wasiwasi Kachero Yasmine kuwa huenda ameshtukiwa kuwa ni mdukuzi.
Mara akaona yule mtu anayejiita Professor Potchefstroom anachapa maneno ya kujibu. Uso wa Yasmine ukarudiwa tena na bashasha mpwitompwito na uchangamfu wake ulioanza kupotea. "OK... atapokewa na Mr. Okworonko, Sandton Gautrain Station kesho saa 6:00 mchana. Akifika ampigie kwa namba +27 83 347 21143. Tusiwasiliane tena kuanzia sasa mpaka siku mzigo wa kwanza unatua Dar es Salaam, Bye..Tchaooo..!!" jamaa akatoka kwenye mtandao.
Kachero Yasmine bila kufanya ajizi akatuma taarifa zote kwenye barua pepe ya Kachero Manu ikiwa na maelezo ya kina ya kumtaka ajifanye yeye ndio wakala aliyetumwa na Man-Temba nchini Afrika ya Kusini kufuatilia fedha. Alipotaka kuifunga kompyuta hiyo hakutaka kuiacha salama. Akairushia moja ya virusi wabaya wanaotafuna mafaili yote yaliyohifadhiwa.
Kirusi hicho kibaya ni Kachero Yasmine pekee ndio angeweza kuyarudisha mafaili hayo pindi akiyahitaji. Baada ya kufanikisha lengo lake hilo akajikuta anaunda tabasamu la ushindi, huku alijiapiza kiwa siku za wanaokula njama za uhaini kukamatwa zinahesabika kwa vidole.
Wakati anajiandaa kuondoka kwenye chumba kile akiwa tayari ameshasimama wima, akahisi kitu kama ubaridi usio wa kawaida juu ya sikio lake la kushoto. Alipogeuka tu akakutana na mdomo wa bastola unamsalimia. "Mrembo karibu kiamboni kwetu, jiskie huru..!" alikaribishwa na sauti nzito, yenye mikwaruzo ya mtu aliyekuwa amejifunika sura yake na kuachia macho yake tu huku akiwa tayari ameitwaa silaha ya Kachero Yasmine iliyokuwa pembeni ya meza yenye kompyuta.
Kachero Yasmine alipigwa na butwaa asijue la kufanya huku akijilaumu kwa uzembe wake wa kupitiliza uliomfanya afumaniwe kiwepesi sana. Nafsini kwake alikubali kabisa kuwa hakuchukua tahadhari ya kutosha. Uso wa Kachero Yasmine ulipigwa na taharuki, fedheha na soni isiyomithilika, akiwa ameishiwa mipango
ITAENDELEA
HAYA KACHERO YASMINE, KASHAINGIA KWENYE 18 ZA MAN-TEMBA
[emoji1787][emoji1787][emoji1787][emoji1732][emoji1732][emoji1732][emoji91][emoji91][emoji91]
Sent from my TECNO CC6 using
JamiiForums mobile app