RIWAYA- HUJUMA NZITO-PART 25
Moja ya lengo la Nyasa Empire Supporters (NES) lilikuwa ni kuweka kituo cha utapeli huo kwa ajili eneo la Afrika Mashariki na Kati. Jukumu la kwanza lilikuwa ni kuhakikisha pesa zilizoibwa na kutoroshwa kwenda kufichwa kwenye Mabenki katika Mji wa Sandton City zinarudi Tanzania kinyemela na kufanya lengo husika lililokusudiwa. Lengo la pesa hizo lilikuwa ni kutumika kwenye Uchaguzi Mkuu wa Rais, Wabunge na Madiwani kwa kuhakikisha wapiga kura wanahongwa ili wakichague na kukiingiza madarakani kwa kishindo chama cha upinzani cha National Movement Party (NMP) kinachoongozwa na Dr Patrick Ndomba.
Kwa muda wa siku tatu tu Kachero Manu alizoishi katika Mji huo akagundua kitu kimoja, kwamba kuna asilimia kubwa sana ya vijana wadogo kiumri wanaishi hapo Sandton City, na wengi walikuwa ni watu wenye asili ya Afrika Magharibi kuanzia Naijeria, Cameroon na Ghana.
Walikuwa na maisha mazuri mno, wengi wao wakionekana maeneo ya kula bata wakiwa na magari ya thamani sana na kufanya vitu vya anasa. Cha kushangaza hawa vijana hawakuwa na kazi wala biashara yoyote ya maana, hawakuwa na michongo yoyote ya kueleweka hadharani. Lakini waliweza kumudu maisha ya Sandton na anasa za hali ya juu.
Mfano mwenyeji wake Mr.Okworonko alikuwa anamkodishia Kachero Manu kila siku gari la kifahari aina ya 'Rolls-Royce Phantom' kwa gharama ya R4000 kwa ajili ya kumzungusha kwenye mizunguko yake ya mjini kila siku na kumrudisha mahali alipofikia.
Ilipofika siku ya tano, akiwa tayari ameshaanza kuiva na kufundwa mbinu mbalimbali za ukwapuaji wa pesa kwenye Mabenki, siku moja usiku wa majira ya saa 4:00 Kachero Manu akaitwa na Mr.Okworonko sebuleni kwake, wakaketi kwa ajili ya mazungumzo yao ya faraghani yaliyohitaji utulivu mkubwa baina yao.
"Kesho Asubuhi ndio nakupeleka kwa Professor Potchefstroom..!!" alifungua maongezi yake Mr.Okworonko kisha akaweka kituo akawa anajimiminia maji kwenye glasi yake na kuanza kuyagida mfululizo, kisha akaendelea. "Mimi nilichoagizwa nikufundishe nimeshamaliza kazi, Yeye ndio ataenda kukupa mbinu za mwisho namna pesa zitakavyotoka hapa na kurejea kwenu Tanzania.
Onyo ninalokupa ni kuwa Professor Potchefstroom hataki ubabaishaji, usaliti wowote dhidi yake ujue kifo kinakuita. Ana mtandao mpana Afrika nzima mpaka katika bara la Amerika. Una bahati sana kuonana na yeye, mimi nipo hapa nchini Afrika ya Kusini mwaka wa 10 sasa sijabahatika kumuona uso kwa uso zaidi ya kupokea maagizo toka kwa wakubwa zangu waliopo nchini Naijeria ambao nao Bosi wao ni Professor Potchefstroom.
Nikutakie kila la kheri kwenye safari yako ya kurejea nyumbani kwenu Tanzania". Yalikuwa ni mazungumzo mafupi yenye kutoa zaidi maelekezo ya upande mmoja badala kufungua mjadala.
Kachero Manu alikuwa anasikiliza tu kwa umakini mkubwa huku moyoni akifurahia kwenda kukutana na mzizi wa tatizo. Mtu ambaye ndiye aliyehandisi uhaini na ukwapuaji huo mkubwa wa pesa katika mabenki Tanzania, uliotikisa nchi nzima.
Wakatakiana usiku mwema huku kila mmoja akielekea kwenye khurfa yake kulala, tayari kwa Kachero Manu kujiandaa na safari ya kesho yake kuelekea kwa Professor Potchefstroom.
[emoji3586][emoji3586][emoji3586][emoji3586][emoji3586][emoji3586][emoji3586][emoji3586][emoji3586][emoji3586][emoji3586][emoji3586][emoji3586][emoji3586][emoji3586]
Mama Catherine alikuwa tayari ameshawasili katika viunga vya shule ya sekondari ya wasichana-Kilakala iliyopo takribani kilometa 5 kutoka stendi kuu ya Mabasi ya Msamvu, ndani ya Mji kasoro Bahari, Morogoro.
Ujio wake pale shuleni ulitokana na barua ya wito toka shuleni ukimtaka afike mara moja bila kukosa tarehe 30/07/1970 saa 4:00 asubuhi. Ni barua ambayo ilizua taharuki kubwa katika mioyo ya wazazi wake Catherine Mushi, mwanafunzi wa Kilakala. Kwani binti yao alikuwa hajamaliza hata wiki tatu tokea aripoti shuleni hapo kwa ajili ya kuanza durusu za kidato cha 5.
Catherine alikuwa ni binti yao wa pekee katika ndoa yao ya zaidi ya miaka 20. Alichaguliwa kujiunga na shule ya wasichana Kilakala akitokea sekondari ya Korogwe Girls baada ya kuongoza kitaifa kwa upande wa wasichana katika matokeo ya mtihani wa kidato cha 4 kwa mwaka 1969. Alipata alama 'A' kwenye kila somo alilofanya mtihani wake, likiwemo mpaka somo la ufahamu wa maarifa ya Biblia.
Hivyo mtoto wao huyo wa pekee walimuona kama ni nyota ya baadae kwa Taifa la Tanzania hasa ukichukulia kipaji chake pekee cha kiakili alichojaaliwa na Mwenyezi Mungu na maadili ya hofu ya Mungu waliyomlea.
Mama Catherine alikuwa amekaa pamoja na wazazi wenzake watatu chini ya turubai maalumu lililowatenganisha wao na watoto wao likiwa nje ya ofisi kuu ya walimu. Ndani ya ofisi hiyo kulikuwa na kikao cha bodi ya shule inarindima huku vigogo wote wa bodi na uongozi wa Mkoa wa Morogoro ukiwa ndani ya kikao hicho. Mabinti hao walikuwa wanaitwa mmoja mmoja ndani ya kikao hicho kuhojiwa.
Wazazi wote walikuwa kama wamechanganyikiwa hawajui maswahibu gani ya kinidhamu yamewakuta watoto wao, hasa baada ya kuona kila binti akitoka kwenye mahojiano hayo anaangusha kilio kama amepewa taarifa za msiba.
Majira ya alasiri wazazi wote wakaitwa ndani ya kikao cha bodi hiyo kupewa nia na madhumuni ya wito wao. Walikabidhiwa rasmi barua za kuwajulisha kuwa watoto wao wamefukuzwa kwa kosa la kinidhamu la kukutwa na mimba.
Katika utaratibu wa kawaida wa shule wa kuwapima wasichana pindi wanaporudi toka likizo, ndio ukawanasa Mabinti hao wanne kuwa na mimba pamoja na Catherine nae akiwemo. Walitulizwa kwa kupewa ushauri nasaha wa kuishi nao kiustaarabu bila kuwanyanyapaa kuogopea wasije Mabinti hao wakachukua maamuzi magumu ya hata kujiua.
Baba Catherine, Meja Mushi alivyopata habari hiyo alicharuka kama mbogo aliyekoswakoswa risasi na jangili. Alitaka hata kumpiga risasi binti yake kwa aibu hiyo aliyoileta kwenye familia. Lakini ndugu, jamaa na marafiki wakafanya kazi kubwa ya kumshusha wahaka wake.
Mama Catherine bado nae akawa haamini anatafakari mwanawe kaipatia wapi mimba hasa ikichukuliwa maadili mufti aliyomkuza nayo bintiye. Jibu la mhusika wa mzigo huo likawa ni gumu kulipata wakabaki na giza zito kwenye mioyo yao.
Siku hazigandi hatimaye muda wa kujifungua ukatimu, akazaliwa mtoto dume. Mjukuu ambaye furaha yake ya kuzaliwa ikawasahaulisha aibu iliyoletwa na Catherine. Mjukuu akaleta neema ya upendo na umoja upya katika familia.
Babu yake akampa jina la 'Asante-Rabbi', akimaanisha Ahsante Mungu kwa zawadi ya mjukuu. Asante-Rabbi huyu Mziwanda wa Catherine ndio huyu Professor Potchefstroom kigogo mzito wa Nyasa Empire Supporters (NES) ya leo inayowatoa jasho na kamasi akina Kachero Manu na Kachero Yasmine na kuutikisa uchumi wa nchi.
Ndio huyo anayeheshimiwa na matapeli wote wa wizi wa mtandao kutoka nchi zote za Afrika Magharibi. Asante-Rabbi huyu alilelewa na kukuzwa kwa upendo na mahaba mazito na familia nzima, walikuwa wanamtunza kama mboni ya jicho. Kwa ujumla alikuwa mtoto wa Bibi na Babu.
Alipofikisha umri wa miaka 7, mwaka 1977 akaandikishwa darasa la kwanza. Kwa jina la Asante-Rabbi Mushi, babu yake hakutaka hata kulisikia jina la baba wa mtoto likitajwa. Alikuwa akitajwa mhusika jina lake anajisikia kichefuchefu.
Mhusika alikuwa ni Shamba-Boi wao aliyekuwa akijulikana kwa jina moja tu la Ngwenyama. Ambaye baada ya kupata penyenye kuwa Catherine kafukuzwa shule kwa sababu ya ujauzito, alilala mitini.
Alishajua ishu ikibumbuluka hawezi kubakia salama. Mchaga Meja Mushi wa jeshi la wananchi JWTZ asingemuacha salama, lazima angempiga risasi au kumtia kilema kwa kumuharibia binti yake.
Asante-Rabbi huko shuleni alipofika umri wa kusoma akageuka moto wa kuotea mbali kwa jinsi kichwa chake kinavyochaji darasani. Mtoto wa nyoka ni nyoka, kama mama yake mzazi Catherine alivyokuwa mtabe wa masomo darasani na yeye alikuwa hivyo hivyo. Matokeo ya kumaliza elimu ya msingi mwaka 1983 ndio yalimtangaza Asante-Rabbi Mushi mbele ya Watanzania wote kwenye redio na magazeti kuwa ni mshindi.
Aliongoza nchi nzima kwa kupata alama ambazo tokea baraza la mitihani ya taifa "NECTA" lianzishwe kulikuwa hamna mwanafunzi aliyewahi kupata alama hizo. Wapo waliomtabiria Asante-Rabbi mazuri, kuwa huenda akaja kuwa mmoja wa Wanasayansi wa kuheshimiwa dunia mfano wa akina Isack Newton, mwanafizikia bobezi.
Akachaguliwa kujiunga na shule ya sekondari ya wavulana, Mzumbe iliyopo Mkoani Morogoro. Shule ambayo ilikuwa ni maalumu kwa watoto wenye vipaji vya kipekee vya kiakili. Huko nako akauendeleza moto wake wa masomo ule ule aliouwasha tokea shule ya msingi.
Tokea kidato cha kwanza mpaka anahitimu kidato cha nne yeye ndio alikuwa kinara kwenye masomo. Maajabu ilikuwa kuna wakati mpaka wanafunzi wa kidato cha tano na sita walikuwa wakikwama kwenye somo la Hesabu na Fizikia, wanamuona Assante-Rabbi anawatatulia.
Ila chambilecho uzuri wa mkakasi ndani kipande cha mti, asiye na hili ana lile. Asante-Rabbi alikuwa mkimya na mpole kupitiliza, jongoo ana nafuu. Alikuwa ni mtu wa kujitenga hapendi kuchanganyika na makundi ya wanafunzi wenzake. Ni mwanafunzi mmoja tu shuleni pale ndio alizoeana nae sana, mpaka watu wakastaajabishwa.
Mwanafunzi huyo akiitwa Newton Temba. Nae alikuwa na silka za kufanana na Asante-Rabbi. Mpaka watu wakawa wanajiuliza hawa hasa wanaunganishwa na kitu gani hasa ukichukulia ya kuwa Asante-Rabbi alimpita madarasa mawili Newton Temba.
Huyu Newton Temba ndio Man-Temba, ambaye ukubwani kwao waliunda tena uwili mtakatifu kati yake na Asante-Rabbi katika mawasiliano ya utapeli wa zile fedha zilizoibwa ndani ya Mabenki matatu makubwa nchini.
Basi pale shuleni wapo waliosema Asante-Rabbi anaringa kutokana na uwezo wa kiakili alio nao ndio maana hataki kabisa kujichanganya na wenzake anawaona vilaza. Wapo waliosema anajidai kwa kuwa anatokea familia ya kigogo wa Jeshi, Meja Mushi hivyo anajiona ni Mlalaheri na wengine wote ni Makapuku Bin Walalahoi.
Ili mradi kila mmoja alizusha lake, lakini hawakujua kitu ambacho kilikuwa kinamtafuna ndani kwa ndani mpaka kumfanya awe mnyonge kupitiliza kiasi hicho.
Kikubwa kilichokuwa kinamkosesha raha ni kitendo cha kutokumfahamu baba yake mzazi. Alishagundua kuwa Mzee Mushi ni Babu yake sasa Baba yake yupo wapi na kwanini hawaishi nae pamoja ndio kitu kilikuwa kinamkosesha sana raha.
Kila alipokuwa anajaribu kumchokonoa Mama yake mada ya kuhusiana na Baba yake mahali alipo, alikuwa anaitolea mbavuni hataki kuijadili hiyo mada. Ndipo ilipokuwa imebaki wiki tatu tu kumaliza mitihani ya kuhitimu elimu ya kidato cha nne, alipoamua kufanya kituko cha mwaka kushinikiza kumjua Baba yake mzazi.
Alitoweka shuleni bila ruhusa na kurejea nyumbani. Babu yake aliwaka akawa mkali kama pilipili mpaka anamtishia kumshushia kipigo kama asiporejea shuleni, lakini wapi hakuweza kufua dafu. Babu, Bibi na Mama yake mzazi walikuwa tumbo joto, wakijua pepo lililomtoa shuleni Catherine na kumkatiza masomo linataka kujirudia upya kwa mjukuu wao Asante-Rabbi, jambo ambalo waliapa kuwa hawatokubali wapo tayari wakeshe kwa maombi, kunuti na funga ili mradi pepo huyo amtoke mjukuu wao.
Licha ya juhudi zote za kumrai kuwa akamalize shule kwanza ndio wajadili jambo hilo kutokana na unyeti wake lakini wapi, walitoka kapa, Asante Rabbi aliwawekea kigingi, jibu lake lilikuwa ni moja tu, tena kwa kimombo "No Father-No School". Ndipo mama mtu akatwishwa mzigo wa kumpasulia ukweli mtoto wake.
Ndio siku miongoni mwa siku, usiku wa manane Catherine aligonga mlango wa ghulamu wake na kumualika kuwa ana mazungumzo ya faragha na yeye.
Wakaketi sebuleni wawili tu wakiwa na lepelepe la usingizi hamna mtu yoyote anayewashuhudia zaidi ya Mungu na Malaika wake. Fikra za Catherine zikarejea nyuma zaidi ya miaka 18 iliyopita akikumbukia hatua mpaka hatua kuanzia jinsi alivyopata mimba ya mziwanda wake Asante-Rabbi mpaka kujifungua kwake. Alikuwa hajasahau kipengere hata kimoja katika matukio hayo.
Alianza kukumbukia peke yake mawazoni mwake kuwa baba yake Asante-Rabbi, Ngwenyama alikuwa ni Shamba-Boi wao wa kazi za nje aliyetokea nchini Malawi kuja kutafuta kazi za nyumbani Jijini Dar es Salaam. Alikuwa ni kijana mtiifu, mwenye kujituma na mchapa kazi, hali iliyomfanya apendwe na kila mwana familia ya Meja Mushi. Kingine cha ziada alikuwa ni umbile lenye mvuto, ukichanganya na kazi zake za shuruba zikamfanya awe na umbo la kuvutia la kiuanamichezo.
Pia alikuwa ni mcheshi sana mwenye kupenda utani na kila mtu katika nyumba ile. Sasa Catherine alipomaliza shule mwaka 1969 akiwa nyumbani anasubiria matokeo ya kidato cha nne, ndipo majaribu ya Ibilisi yalipoanza. Alijikuta ghafla tu anampenda Ngwenyama toka moyoni. Na kwa kuwa alikuwa ni mtoto wa getikali hamna kuzurura ovyo kama mbwa koko wa uswahilini hivyo mwanaume wa maana kwake aliyemzoea machoni mwake ni Ngwenyama.
Kila dalili alizozionyesha kwa Ngwenyama kuonyesha amekufa na kuoza kimapenzi juu yake, hazikufua dafu. Akabakia anateketea moyoni kwa moto mkali wa huba. Mila za Kiafrika zilikuwa haziruhusu msichana kumtakia mvulana kuwa anampenda minghaili wazungu wao kwao ni kitu cha kawaida tu mtu kuelezea hisia zake.
Fursa ya pekee aliyokuwa anaisubiria Catherine ikajitokeza, baba yake Meja Mushi na mkewe walipata safari ya ghafla kuelekea Rombo-Moshi. Kulikuwa na msiba umetokea Kijijini hivyo walipaswa kwenda kuzika. Mzee Mushi akawausia waishi vizuri ndani ya hizo siku tatu, kuanzia Ijumaa mpaka jumatatu watakaporejea safarini.
Sasa nyumba ikabakia watu watatu, dada wa kazi, Catherine na Ngwanyama. Ijumaa ile ikapita salama mpaka Jumamosi. Tatizo lilikuwa kwa Catherine hawezi kumuambia hisia zake asije akaonekana yeye ni ghashi wa mahonyo. Siku ya Jumapili ndipo mpango wa Ibilisi kuwadondoshea Catherine na Ngwanyama katika dhambi ya zinaa ukatimu.
Ilikuwa ni kawaida ya Catherine kila ifikapo siku ya Jumapili kwenda kusali kanisani misa ya kwanza. Hivyo alikuwa anaondoka saa 12:30 shapu kuelekea kanisani, atakaa huko na kurejea nyumbani saa 3 asubuhi. Ratiba ya kazi ya Ngwanyama siku ya Jumapili ilikuwa ni kusafisha madirisha ya nyumba nzima.
Hivyo alipenda kuanza na madirisha ya chumba cha Catherine ili akirudi kanisani awe huru kujimwayamwaya kutumia chumba chake bila usumbufu. Lakini kumbe siku hiyo Catherine alichelewa kuamka hivyo akapanga aingie kanisani misa ya pili.
Hivyo wakati anaoga bafuni Ngwenyama yupo dirishani anafuta vumbi la madirisha habari hana. Hamadi weeh Ghafla bin Vuu, Catherine akawa anatoka kuoga akiwa amevaa kanga moja tu nyepesi ya Mombasa huku imemnatia mwilini na kulichora vilivyo umbile lake lenye mvuto wa aina yake.
Alikuwa ana umbo lenye kumtetemesha kiimani hata yule Mchamungu mwenye vilemba saba kichwani kama tu atakubali pepesi na tashwishi ya macho yake kushuhudia maajabu ya uumbaji wa Mwenyezi Mungu.
Catherine alikuwa hana hili wala lile amejitawala chumbani mwake, anajikausha maji mwilini sasa akiwa mtupu kama alivyozaliwa akiwa amelipa mgongo dirisha analosafisha Shamba-Boi wao huku akitikisa makalio yake yenye umbile la kifuu cha nazi kimadoido.
Ngwenyama alibaki mdomo wazi huku ameganda pale dirishani kama amenaswa na umeme. Macho yake aliyakodoa upeo wa mwisho wa kuyakodoa bila kufumba macho asije akapoteza fursa hiyo adhimu na ya bure ya kutalii mwili wa mtoto wa Kibosile wake, Catherine.
ITAENDELEA
Sent from my TECNO CC6 using
JamiiForums mobile app