RIWAYA-HUJUMA NZITO-PART 31
Ngo...Ngo..Ngo....Ngo..., hodiii...hodiii...hodi humu ndani..!" aligonga kwa nongwa haswa ili hasimu wake asiendelee kumfaidi Yasmine. Kimya kizito cha ghafla kikatawala pale sebuleni kama vile hamna mtu. "Ngo..Ngo...Ngo..", "Karibuuu...!" sauti ya kiume ya kiunyonge ilijibu baada ya kusikia mlango unagongwa tena kwa mara ya pili. Baada ya sekunde kadhaa mlango ukafunguliwa.
"Karibu Mzee, Shikamoo" aliongea yule kijana aliyefungua mlango huku akiwa ametawaliwa na wasiwasi usoni mwake. "Ina maana Yasmine anakamuliwa na Kiben-10, kweli huyu hamnazo" aliwaza Nathanieli baada ya kumuona kijana mwenyewe anayemlaki mlangoni hapo hata kwenye kiganja cha mkono hajai. "Marahaba Yasmine nimemkuta hapa kwake?" alijitutumua kuuliza swali la jambo lililomleta.
"Hapana, hayupo, Bosi Yasmine toka jana hajarudi nyumbani sifahamu alipo, akija nimwambie nani alikuja?" alijibu kwa sauti ya hasira akionekana hajapendezwa na ujio wa mtu aliyekuja kumkatia stimu ya starehe zake huku akionekana anajiandaa kufunga mlango, hataki usumbufu. Nathanieli fikra zake zilimtuma Yasmine yupo ndani ila anataka kufichwa kitu, akaupiga kikumbo mlango na kujilazimisha kuingia kwa kushtukiza.
Hamadi...! Akamkuta binti mdogo tu yuko pale ukumbini ana sura ya wasiwasi, uso umejaa soni kwa aibu tele ya kufumaniwa. "Shikamoo..Baba..!" alisalimia kwa aibu yule msichana huku ameinamisha kichwa chake chini. Nathanieli hakujibu kitu, alishagwaya kwa sababu alichokikuta ni kinyume na matarajio yake. Hapa kilichokuwa kinaendelea ni paka akitoka panya hutawala, picha ikionyesha kuwa ni kuwa Shamba-Boi wa Yasmine alimvuta dada wa kazi wa jirani kujivinjari nae kimapenzi.
Nathanieli hakuitikia salamu aliyotunukiwa zaidi ya kuondoka eneo lile kwa hamaki bila hata kuaga. Ingawa aliondoka shingo upande kwa kutomkuta Yasmine, lakini hisia zake kuwa Yasmine ni kirusi cha Makachero kilichopandikizwa ofisini kwao zikazidi kustawi na kumea akilini mwake.
Dalili zote zilionyesha ile nyumba sio ya kifamilia kabisa hamna cha baba mdogo wala mama mdogo anayeishi pale. Pia mashaka yalizidi zaidi inakuwaje mtu mgonjwa asishinde nyumbani apite kuzurura tu mpaka nyumba yake inageuzwa danguro.
"Kuanzia sasa namuwekea vijana wa kumwinda na kumfuatilia nyenzo zake, kifo ni halali yake kwa mikono yangu" alijiapiza nafsini mwake huku anaondoka na gari lake maeneo yale. Tayari alishahukumu kuwa Yasmine sio mtu anayestahili kuendelea kung'ara sura yake katika mgongo wa dunia.
Kwa upande wake Yasmine akiwa hana hili wala lile, aliingia nyumbani kwake majira ya saa 3:30 usiku akitokea hospitali ya Taifa ya Muhimbili kwenye matibabu. Majibu huko ya daktari wake yalikuwa ni mazuri sana. Hakugundulika kuwa na matatizo yoyote makubwa ya kiafya hivyo alitakiwa tu auguze jeraha lake la kichogoni.
Alipofika nyumbani kwake kijana wake, Shamba-Boi alionekana kama ana wasiwasi na kama vile ana kitu anataka kumuambia lakini anaficha. Yule kijana alikuwa anataka kutoa taarifa za ujio wa mtu pale nyumbani, lakini alikuwa anahofia huyo mtu atakapoongea na Bosi wake Yasmine atamueleza kila kitu kuhusu yeye kuingiza ghashi ndani ya nyumba ya Bosi wake itakuwa msala kwake. Yasmine alishamsoma kisaikolojia kuwa kuna kitu anamficha.
Mara tu baada ya kuoga zake akaingia kwenye chumba cha CCTV-Kamera, kuangalia mienendo ya pale nyumbani kwake wakati hayupo. Yule Shamba-Boi alikuwa hajui kama matukio pale yote yanarekodiwa masaa 24. Kwa mshangao mkubwa sana akamuona Nathanieli amekuja nyumbani kwake na kaingia mpaka ukumbini kwake akawa anazungumza na Shamba-Boi wake.
"Amekuja kunifanyia taftishi, kanishtukia tayari kama nimewadukua?", Kamwambia Shamba-Boi wangu Hans asiseme ujio wake, mbona kakaa kimya?" ni baadhi ya maswali lukuki aliyokuwa anajiuliza Yasmine bila kupata majibu.
Mambo mengine aliyoyashuhudia kwenye CCTV-kamera ya Hans kumleta dada wa kazi wa nyumba jirani ndani ya nyumba kuu hakujali sana. Ulikuwa sio wakati wake kujadili upuuzi ule kulikuwa na mambo makubwa zaidi mbele yake ya kufuatilia kwanza.
"Zege halilali, nitakwenda usiku huu nyumbani kwake kumuuliza alifuata nini kwangu mchana kweupe kama sio mwanga ni nini sasa, kifo ni halali yake kwa mikono yangu..!" Yasmine alijiapiza huku akibadili nguo zake za kulalia na kuvaa za kazi ili aingie tena mzigoni. Alipanga akirudi huko kwa Nathanieli ndio atafanya mawasiliano na Kachero Manu ili wapeane taarifa wapi wamefikia katika taftishi zao za kuisambaratisha “Nyasa Empire Supporters (NES).
Akaingia kwenye gari lake na kupiga honi ishara ambayo ilimkurupusha kijana Hans chumbani kwake kuja kufungua geti ili kumruhusu Bosi wake atoke. Yasmine alipotoka tu akapita kama nyumba tatu hivi ya nne kutoka pale kwake kulikuwa na Baa maarufu tu katika mitaa ile.
Baa hiyo tayari ilikuwa imejaza watu lukuki wanafurahia maisha kwa namna wanavyoona wao inafaa kuyafurahia.
Akasimama mbele kidogo ya eneo hilo na kushuka nje ya gari, baada ya kujikuta amebanwa na kiu na hajabeba maji. Nyuma kidogo tu ya pale alipoegesha gari lake kulikuwa na gari nyingine aina ya 'Subaru-Forester' rangi nyeupe imeegeshwa kwa kujitenga kidogo na gari zingine.
Akaizunguka gari hiyo huku akimuona kijana mmoja akiwa amevalia fulana nyeupe na miwani nyeusi akiwa ameegemea kwa nje, mlango wa upande wa kushoto, kiti cha abiria anavuta sigara macho yote yapo uelekeo wa nyumba ya Yasmine. Yasmine hakumjali akampita lakini akiwa tayari ameshaikariri namba ya gari hilo kichwani mwake na kuelekea moja kwa moja kwenye njia ya kuingilia pale Baa akaenda mubashara mpaka kaunta.
Akazungumza na muuzaji baada ya sekunde kadhaa akakabidhiwa chupa kubwa ya maji. Akailipia na kuondoka zake huku akiifungua chupa hiyo njiani na kuanza kuinywa kabla hata hajafika kwenye gari yake. Alipotoka nyumbani alijigundua hajanywa maji ya kutosha, na kutokana na hali yake ya kiafya ilikuwa inamlazimu afanye hivyo kila anapopata wasaa.
Alipoingia kwenye gari yake, kabla hajaanza kuondoka, akawasha taa ya ndani ya gari kwa lengo la kukagua kilemba chake cha kichwani kama kimefungwa vizuri kusitiri jeraha lake lililozingushiwa bendeji. Akajiridhisha kuwa yupo sawa. Akaanza kuliondoa gari lake toka eneo hilo kwa mwendo mdogo mdogo na kutimka kuja maeneo ya Bamaga anapoishi Nathanieli.
Alikuwa anakwenda tu kwa mwendo wa wastani mpaka alipofika maeneo ya Tegeta Kibaoni eneo la mataa, wakati anasubiri taa za kijani zimpe ruhusa ya kuendelea kuitumia barabara hiyo ya Mwai-Kibaki alipotupa jicho kwenye kioo tu, akashtuka kidogo.
Gari ya tatu yake kutoka nyuma yake ilikuwa ni “Subaru-Forester” nyeupe ile ile aliyoitia machoni pale Baa ya jirani na kwake, na namba zake za gari ndio hizo hizo. Huku dereva ni yule yule jamaa aliyevalia fulana nyeupe aliyekuwa ameegemea mlango anajiburudisha na sigara.
Taa ziliporuhusu magari yanayoelekea Mwenge, Kachero Yasmine akachomoka nduki kwa spidi ya hatari akitaka kuwapima kama kweli wanamfuatilia yeye au wapo kwenye safari zao tu. Akajithibitishia bila mashaka kuwa wanamfuatilia yeye kwa sababu kila akiongeza kasi nao hawa hapa, akipunguza nao wanapunguza.
Walipovuka eneo la Bondeni tu, Kachero Yasmine akaongeza kasi huku akiwa yupo upande wa kulia wa barabara kuonyesha kama anaelekea Mwenge halafu ghafla tu akahamisha gari kuja kushoto na kukatiza kwa haraka sana kuja njia ya Kawe.
Kitendo hicho cha ujanja wa hali ya juu, kiliwachanganya wale maadui zake walijua anawatoroka. Nao wakatamani wahamie upande wa kushoto ili wamfuate njia ya Kawe. Dereva wao akakosa umakini alipohama hakupiga mahesabu vizuri akajikuta anakula dafrao kutoka kwenye Lori la nyuma yao lililosheheni mzigo wa makabichi likitokea Wilayani Lushoto, Tanga.
Ilikuwa ni moja ya ajali mbaya kuwahi kutokea kwenye eneo lile. Yasmine haraka haraka akaegesha gari kwenye miti pembezoni mwa barabara na kuja kushuhudia kwa macho yake, dafrao hiyo ya kutisha. "Wawaishwe hospitali haraka hawa huenda wakapona hao" yalikuwa ni baadhi ya makelele ya mashuhuda wa ajali ile.
Yasmine alipowaangalia vizuri wale majeruhi, akawakuta wapo watatu, lakini mmoja wapo ambaye hali yake ilikuwa nafuu alivunjika miguu yote, ila wale wengine walikuwa wamepata majeraha mazito ya kifuani na usoni kiasi kwamba wakati wowote walikuwa wanarejea akhera kwa Mola wao.
"Nisaidieni huyu mmoja kumpakiza kwenye gari yangu nimuwahishe Muhimbili" alipayuka Yasmine kwa sauti ya juu akijifanya ni msamaria mwema akiomba msaada wa raia wema kusaidiwa kumbeba yule mwenye nafuu kati yao. Yule jamaa kumuona Kachero Yasmine ambaye ni hasimu wao, yupo mbele yake ndio anataka kumpa msaada, akaanza kupiga kupiga kelele za kuwa wasimpeleke kwenye gari ya Yasmine.
Wale raia wema ndio kwanza hawaelewi kitu wanajua majeruhi akili zake zimefyatuka kidogo maana katika hali ya kawaida utakataaje msaada wa kuokoa uhai wako. Kumbe yule majeruhi alitambua kuwa ameshaingia choo cha kike mikononi mwa adui yake ambaye hana jema hata chembe na yeye.
Alivyopakizwa tu yule majeruhi, Kachero Yasmine akaliondoa gari lake kwa kasi akijifanya anamkimbiza hospitalini huku akiwa anatabasamu. Alikuwa akielekea kutafuta sehemu tulivu akambinye kwelikweli mpaka aropoke katumwa na nani amfuatilie.
ITAENDELEA
Sent from my TECNO CC6 using
JamiiForums mobile app